Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa mwisho na nitajitahidi niende kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wizara kwa juhudi zao hasa Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri wake kwa kweli wako field muda wote na nimekuwa nikiwafikia mara kwa mara. Niwashukuru pia watendaji, ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu na Dkt. Ntuli ambaye anashughulikia masuala ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee yale ambayo tumeshafanya hasa kwenye barabara ambapo sisi tuna mradi wa TACTIC kwenye Jimbo la Moshi Mjini ambayo ilichelewa kwa mwaka mmoja lakini tunategemea watalisukuma ili mwaka huu basi liweze kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye hospitali ya wilaya kuendana na jiografia yetu tulishapewa milioni 500, lakini kutokana na ufinyu wa maeneo sisi tunajenga gorofa, tumeleta ramani kwao wameshapitisha, tuliomba watuongezee ili fedha ya kuanza ili ile fedha ya kwanza kitu kitachowekwa pale kiweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kituo cha afya wametupa milioni 250, Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde alikuja aliona namna tunavyokwenda kwa kasi, tunaomba basi ile 250 ya kumalizia nayo iweze kufika ili tuweze kukamilisha kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwenye shule, ambayo tunaijenga kwenye Kata ya Msalanga, ile milioni 470 tumeifanyia kazi vizuri, tunaomba sana sisi tumejipanga kwa kutumia nguvu za wananchi, tuanze kuongeza mabweni. Sasa tunaomba juhudi hizo za wananchi zikianza, kwa sababu kati ile iko pembezoni, basi Serikali iangalie namna ya kutuongezea, ili basi tuweze kuwa na mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeenda kwenye suala la Wamachinga, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hatua aliyochukua kwa ile incident ya Mwanza. Nimwambie maeneo yote yenye Wamachinga kumekuwa na tabia hiyo ya kuwanyang’anya watu vitu na sidhani kama ni njia nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, kule Moshi, kuna watu walikuwa wanauza mabegi, walinyang’anywa na wanapofanya ile operation wananchukua maeneo yote. Sasa inapokuja kwenda kuwarudisha, vile vitu wanavyovichukua hawaandiki vitu gani ni vya nani? Tunawasababishia wale Wamachinga umaskini na sioni sababu ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu au mawazo yangu, ni vizuri wawatumie wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwenye hizo operation, wanawafahamu wale watu na vitu vyao ili vinapochukuliwa, baadaye itakapobidi kuwarudishia basi warudishiwe vitu vyao, lakini kuvichukua na kupotea, ni sawasawa kabisa na kusema Serikali inawanyang’anya wananchi mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye kuwapanga, naamini tukiweza kuwatumia Wenyeviti wa Serikali za Mtaa tunaweza kuwapanga vizuri badala ya kuwa na zile operation za kuwanyemelea kuvunja na kuchukua vitu na kuvipoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masoko mbalimbali, tumekuwa na incident za kuwaka moto masoko. Ninawazo ambalo nadhani linaweza likasaidia, kwa nini tusibadilishe mtindo wa ujengaji kwenye masoko haya ambayo siyo rasmi, badala ya kutumia mbao tutumie chuma ili kupunguza haya matatizo yanayotokana na moto ambao unajitokeza mara kwa mara. Kule Moshi umetokea lakini bado watu wanarudia kujenga kwa kutumia mbao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba hilo mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mradi wa kimkakati wa stendi pale Moshi, mradi ule umesimama kwa muda mrefu, ningeomba Mheshimiwa Waziri anapohitimisha aangalie namna ya kusaidia miradi hii ya kimkakati ambayo ilikuwa kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, stendi yetu ya Ngaka – Mfumuni imesimama na hakuna kinachoendelea.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Mtemvu, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji wakati anamalizia kuzungumzia juu ya masoko ya kimkakati, pamoja na stendi. Tunalo soko ambalo ni sambamba na stendi pale Mbezi Louis ya Magufuli, mpaka sasa tunatambua stendi ile inaingiza takribani bilioni 50 za Watanzania za ndani lakini bado haijakamilika, kwa sababu ya VAT na kadhalika baada ya kutokea kwenye jiji kuja ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo. Tunawaomba sana ili ile fedha za Watanzania zikatumike, zikawe na tija, basi ni vizuri mhakikishe stendi ile inakamilika ili iweze kuleta tija ahsante.

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea tu kwa sababu ni ndugu yangu huyu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba niende pia kwenye suala kupanga miji, hili linahusisha Wizara mbili, mfano wa Moshi, tulishafanya vikao na Wilaya ya Hai, pamoja na Moshi Vijijini kupanua maeneo. Sasa kwa sababu inahusisha TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ardhi, imeendelea kuwa na mkwamo mkubwa na matokeo yake ni nini yale maeneo ambayo tulikuwa tupanukie yameendelea kujengwa bila mpangilio, kwa sababu kule hakujawa mjini, kwa hiyo, kumekuwa na slums zinatokea kule na baadaye tukija kupanua mji, basi tunaenda kurasimisha maeneo ambayo hayatakuwa na miundombinu wowote. Sioni ugumu wa kuongeza yale maeneo ya kiutawala na iwe hivyo kwa miji yote ambayo inakuwa, tuwe tuna plan ahead, bada ya kuwa ya slum ambazo kila mara tunazirasimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo liko TAMISEMI, lakini linahusisha pia ajira, watu wa bodaboda. Bodaboda ni ajira rasmi na kama ni ajira rasmi ni vizuri wale watu waendeshaji ambao sio wamiliki na wale ambao ni wamiliki wanaendesha waweze kuingizwa kwenye mfumo wa WCF kwa kuwatumia TAMISEMI, kwa nini nasema hivyo? Hawa watu ndio wanapata ajali sana na wakipata ajali, wamekuwa ni mzigo kwenye matibabu yao, wangeweza kurasimishwa wakawekwa kwenye Mfuko ule wa WCF, wanaweza kutibiwa na kupata fidia pale wanapopata ajali badala ya hali ilivyo sasa ambao wanakuwa mzigo kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, pamoja na watu wengi kuongelea kuwaongezea posho Madiwani pamoja na Wenyeviti, hili ni la muhimu sana, lakini tuangalie kwa upana. Isipokuwa ningeomba pia suala la ajira hizi mpya tuangalie zile kada za Walimu pamoja na watumishi wa afya, hasa wale ambao tayari wanajitolea kule ili waweze kupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)