Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai wa kuweza kuchangia siku hii ya leo. Pia, namshukuru sana Rais wetu kipenzi mama Samia Hassan Suluhu kwa kazi yake nzuri aliyoifanya. Amemwaga fedha nyingi sana kwenye sehemu zetu za kazi kwa ajili ya afya na elimu. Tunamshukuru sana Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali zetu za Mkoa wa Lindi zimechakaa sana na zinakatisha tamaa. Kuna hospitali za wilaya ukifika pale huwezi ukaamini kama ni hospitali ya wilaya, hospitali zile ni kongwe na zimechakaa sana. Hospitali hizo zina matatizo mengi, kwanza hazina vifaa tiba, zina matatizo ya watumishi, wataalam mbalimbali hakuna. Kuna tatizo lingine la kukosekana kwa umeme, unazimika mara kwa mara. Tunaomba wapatiwe hata solar kwenye zile sehemu muhimu katika Hospitali hizo. Zaidi kwa mfano kuna Hospitali ya Nachingwea tunahitaji kupatiwa solar kwenye jengo la mama na mtoto, pia kuna tatizo la taa ile kubwa ya theatre hakuna kabisa kwenye hospitali ile. Ni Hospitali ya Wilaya lakini haina hicho kitu, taa ile kubwa ya theatre hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la ambulance, Wilaya nzima kuna ambulance moja ambayo iko kwenye Kituo cha Afya Kilimalondo, ni mbali sana kutoka pale Wilayani Nachingwea. Tunaomba sana sana tupate ambulance kwa sababu, kuna Ambulance ambayo ni mbovu zaidi ya miezi sita na haitengenezeki. Tunaomba sana watuangalie kwa jicho la pili tupate ambulance kwenye hospitali hiyo. Hakuna ukumbi wa mikutano, asubuhi kunakuwa na ile morning report, hakuna ukumbi wa kufanyia kile kitu, wanasimama tu wanapeana ripoti. Tunaomba watusaidie tupate ule ukumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wodi ya wanaume imechakaa sana, inakatisha tamaa. Hakuna kichomea taka kulingana na uwezo wa hospitali ile. Incinerator iliyopo ni ndogo sana tunaomba watusaidie tupate hiyo incinerator. Uzio wa Hospitali ya Nachingwea ule unakatisha tamaa, ni mbovu mbovu, mbovu mno. Tunaomba watusaidie tupate matengenezo ya hospitali hiyo. Pia, hakuna dental chair kwenye hospitali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna Hospitali ya Liwale, katika hospitali hiyo tunashukuru wametuletea X-Ray, lakini X-Ray hiyo kuna mtaalam mmoja tu, akiumwa au akiwa na dharura yoyote au akienda likizo, hakuna huduma inayoendelea pale. Tunaomba tuongezewe wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, kuna hizi barabara. Barabara zinakatisha tamaa sana, kuna barabara ya kutoka Lupota kwenda Chingunduli, huwezi kupita imekufa ile barabara, inakatisha tamaa. Tunaomba watusaidie tutengenezewe hizi barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi niliuliza swali kuhusu barabara ya Nanganga – Nachingwea – Masasi – Liwale, lakini bahati mbaya nimejibiwa jibu la Mkoa wa Mtwara barabara tofauti kabisa. Naomba sana tupate jibu la msingi baadaye kabla hawaja-wind up Wizara husika, hizo barabara tupate majibu ya msingi ili tujijue na sisi tuko katika sehemu gani. Wananchi wa kule tangu tumezaliwa na wengine mpaka wamekufa, hatuijui lami jamani, hatuijui lami, inasikitisha na barabara hizo ni za mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana watuangalie kwa jicho lingine, kwa jicho la huruma, barabara zinakatisha tamaa. Akinamama wajawazito wanajifungua njiani kwa kukosa barabara. Barabara na madaraja hakuna, tunaomba sana watusaidie, tunaomba sana TAMISEMI waangalie hilo suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la watumishi naomba niongee kidogo nieleweke. Watumishi wengi wanaoajiriwa wanaopelekwa Mkoa wa Lindi, wanakwenda kuchukua check number, then wanaomba uhamisho wanageuza. Matokeo yake kule kwetu kunakaa hakuna watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa hivi, kuna vijana wengi wanajitolea, kuna wanaojitolea nafasi za ualimu na nafasi zingine. Tunaomba sana wapewe kipaumbele wazawa wa kule kwa sababu wamezoea mazingira ya kule. Wakiajiriwa watu wa kule watakaa. Inasikitisha sana wanapoajiriwa watu wengi tunasema tuna watumishi, lakini baada ya muda mfupi watumishi wote wanakuwa wameshaondoka. Sijui ni kwa nini, sijui kunaonekana vipi kule kwetu. Tunaomba sana hili suala lipewe kipaumbele. Watumishi wakiajiriwa waanze kuajiriwa wazawa wa kule. Kwanza wana uchungu na kwao; pili wamezoea mazingira magumu watakaa. Naomba sana, haya masuala yaangaliwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nalirudia ni barabara, jamani barabara, barabara jamani, barabara za kwetu zinasikitisha. Tunaomba jamani watufikirie kwa barabara za kwetu na sisi wenzao ni binadamu pia, tunaomba. Barabara za kwetu ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini nasisitiza kuhusu suala la barabara. (Makofi)