Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami nianze kuchangia kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake yote kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM na utekelezaji mzuri wa bajeti hii ambayo tunaendelea nayo. Pia nawapongeza Mawaziri na TAMISEMI wote kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata tukiwapongeza hapa, kutokana na muda wetu hatutakamilisha shukrani kwa sababu kwa kweli TAMISEMI katika bajeti hii wamefanya vizuri sana. Nimepitia utekelezaji kwa kuona kwa macho yale yote ambayo tuliyaomba, bajeti hii tunayoendelea nayo kwa kweli asilimia karibu 99 wameyatekeleza na miradi inaendelea kutekelezwa kwenye Jimbo langu kwenye Kata zote. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika bajeti hii inayoendelea, naomba mambo machache; moja, ni kwamba kuna shilingi milioni 130 zile kwa ajili ya ile Sekondari ambayo tunaendelea kuijenga. Pale kwenye Jimbo langu ile Sekondari ni kama imekamilika kwa sababu Naibu Waziri wa Elimu alipita juzi akaelekeza tuanze usajili. Kwa maana hiyo aliridhika na kiwango cha ujenzi wa ile Sekondari, na ninawakaribisha mje mwone namna watendaji wamepambana, ile Sekondari imekamilika na natarajia tuanze kuitumia mwezi wa Saba. Kwa hiyo, ile shilingi milioni 130 tunaomba ije kwa wakati ili tuweze kukamilisha katika kipande chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upande wa bajeti hii tunayoendelea nayo, tunashukuru Serikali ilitupa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara mbili katika kila Sekondari, lakini tukumbuke kila Sekondari ina maabara tatu. Sasa tunamalizia majengo mawili na bahati nzuri huwa yanafuatana, linabaki moja. Kwa hiyo, tunaomba zile za ukamilishaji wa maabara ya tatu katika Sekondari na zenyewe zifanyiwe kazi mapema ili watoto wetu waweze kusoma kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika bejeti hii tunayoendelea nayo, tatizo la walimu ni kubwa, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza lakini sasa hapa nina ushauri kwamba, hebu wale walimu ambao wapo tayari mashuleni wanajitolea, wawe ni wa kwanza kuajiriwa kwa sababu unakuta wale walimu ambao wapo mashuleni na wamejitolea kufundisha wanakosa ajira lakini anapewa ajira mtu mwenye elimu, lakini kipindi hicho chetu usikute yuko kwenye maeneo tofauti ya kutafuta riziki, tunawaacha wale ambao wamejitolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukianza na wale, maana yake hata shule zetu zitakuwa hazina upungufu wa walimu kwa sababu walimu wataona tukijitolea itakuwa ni kipaumbele katika kupewa ajira. Kwa hiyo, tujitahidi katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya kwenye TARURA, nadhani tumefanya vizuri, lakini maeneo yetu ya mijini ambayo tunaratajia huo mradi wa TACTIC, ni vyema sasa nasi tukawahishwa. Tumepewa shilingi milioni 500, lakini maeneo mengine wamepewa shilingi bilioni moja kwa sababu tunatarajia tutapata huo mradi wa TACTIC kwa ajili ya barabara zetu za mijini; lami pamoja na taa na ujenzi wa stendi. Sasa tunatamani wananchi wajue, tunawaeleza kwamba tuna mradi huu utakuja, lakini sasa tufafanuliwe ni lini hasa tutaanza mradi huu katika Halmashauri zetu za Miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipitia bajeti hii ambayo sasa tunakwenda kuipitisha, nimeona yale ambayo mmetuwekea, tunashukuru na tunaona ni katika yale yale ambayo ni matarajio ya Wabunge pamoja na wananchi wanaowawakilisha. Hapa naomba Mheshimiwa Waziri alinukuu jambo hili liwe kama dharura kwake. Tuna Shule ya Msingi inaitwa Iboni. Nimeona hapa kuna fedha kwa ajili ya kukarabati shule zilizochakaa, lakini shule hii imechakaa over kuchakaa. Leo hata ukiwa na feni tu ukasema upulize kwa kasi kubwa, bati zote zile zinang’oka. Shule ile imejengwa miaka mingi sana; wamesoma babu zetu na baba zetu. Sasa hii siyo tu ku-repair, hii inahitaji madarasa ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu special zaidi, shule hii ina wanafunzi wa kawaida, lakini pia ina wenye mahitaji maalum na ndiyo shule pekee yenye watoto wenye uhitaji maalum. Pale wapo wasio na usikivu, wasioona, wenye mtindio wa ubongo. Bahati mbaya madarasa yao mawili yote yameanguka, leo wanasoma chini ya mikwaju, na hawa watoto ni maalum kabisa. Naomba jambo hili na lenyewe katika ile idadi ya madarasa, basi japo tupate madarasa yao mawili, ni muhimu sana kwa sababu watoto hawa ni wale wa uhitaji maalum. Kwa hiyo, natarajia Mheshimiwa Waziri atalichukua hili kwa msisitizo wake na tutawasaidia watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tena kuishauri Serikali kwamba sasa hivi tu-invest pia kwenye hosteli. Katika Halmashauri ya Mji, hatuna Sekondari hata moja yenye hosteli, lakini tunaona watoto wanashindwa kumaliza shule kutokana na mwendo wanaotembea. Wanaweza wakaanza shule watoto 60, wakamaliza 40, wengine wote wanaishia njiani. Kwa hiyo, nashauri, nami angalau pale Halmashauri ya Mji tupate japo hosteli, kuwe na sekondari japo moja yenye hosteli iliyokamilika, hasa hii sekondari mpya ambayo mmetuletea, ni shule ya kisasa sana, tukiijengea mabweni, kwa kweli itakuwa ni over shule; itakuwa ni shule zaidi ya shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nigusie kidogo kwenye upande wa Madiwani. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI hawa Madiwani wanatakiwa wote wapewe heshima inayofanana. Bahati mbaya, sasa sijui ndiyo maelekezo ya TAMISEMI, kuna baadhi ya maeneo ya Halmashauri Madiwani hawa wanakuwa hawapewi thamani kama ile thamani ambayo Madiwani wa sehemu nyingine wanapewa. Mfano, unakuta Diwani anatoka kilometa 30, anakodi pikipiki shilingi 15,000/=; kwenda na kurudi ni shilingi 30,000/=; akifika kwenye Kikao anapewa posho ya shilingi 40,000/=. Kwa maana hiyo, Diwani huyu kweli anawezaje kwenda kutekeleza majukumu yake kwa kupewa posho ya shilingi 40,000/=? Ukiuliza, tunaambiwa ndiyo mwongozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujue, ni kweli TAMISEMI mmewaongoza wao kuwalipa Madiwani posho shilingi 40,000 wakati Halmashauri nyingine wanalipwa kutokana na stahiki halali? Wengine wanalipwa posho shilingi 100,000/= na zaidi, lakini Halmashauri nyingine ikiwemo Halmashauri yangu, posho shilingi 40,000/= Diwani anatumia nauli kwenda na kurudi shilingi 30,000/=, itakuwa siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine utaona kwamba Wabunge wengi wamechangia kwamba Madiwani waongeze maslahi, ni kwa sababu mmepeleka fedha nyingi sana kule kwenye Kata ambazo zinasimamiwa na Madiwani, halafu Diwani unampa shilingi 40,000 au unampa shilingi 300,000 anakwenda kusimamia fedha nyingi, matokeo yake Madiwani wetu wanakata tamaa na wanakuwa hawafanyi kazi kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi sana nilitaka nielezee jambo moja. Kulikuwa na mchangiaji ambaye alizungumzia ujenzi wa stendi na soko la kisasa ambalo limejengwa Dodoma hapa; na wakasema yamejengwa mbali. Naipongeza Serikali na niipongeze sana TAMISEMI kwa kujenga yale masoko na stendi, kwa sababu leo soko kama lile na stendi kama ile, mjini hapa katikati unaweza ukalijenga sehemu gani ukalipata? Kujenga maeneo haya pembezoni mwa miji, maana yake mnakwenda kuutanua mji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi leo wakitaka kununua viwanja katika Dodoma hii, hawawezi kununua huku, wanakwenda kununua Mtumba na maeneo kama hayo. Maana yake ni nini sasa? Mji unakua na watu wanapata fursa. Hapa cha kusaidia ni kwamba, Jiji letu la Dodoma linapaswa viwanja vile vinavyozunguka soko na stendi wagawiwe wananchi wajenge ili lile soko na ile stendi iwe na thamani. Wasifanye tena vile viwanja vikawa ni kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya public. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwapongeze na niwape hongera; tumekwenda Nyamagana kule Ilemela, tumekuta stendi moja ya kisasa sana. Kwa hiyo, kama kuna mpango huu, hata Kondoa tuna uhitaji wa stendi, na tumeisogeza pembeni ili kuukuza mji. Nawaomba sasa Wizara ya TAMISEMI katika maeneo, na tunajua Kondoa ipo katikati ya Manyara na Dodoma. Kondoa ipo karibu na Makao Makuu ya nchi. Kwa maana hiyo, tukipata na ile stendi yetu ambayo tumeiandaa pale pembezeni mwa mji, mtasaidia kukua kwa mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, ninashukuru sana na ninawapongeza Wizara. Ahsanteni sana. (Makofi)