Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Anton Albert Mwantona

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nami pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya aliyotupatia. Pia nimshukuru Rais wangu, Rais mpendwa Samia Suluhu Hassan kwa yale ambayo anatufanyia kwenye Majimbo yetu. Nimshukuru mdogo wangu Waziri Mheshimiwa Bashungwa, Manaibu wake Mheshimiwa Silinde pamoja na Mheshimiwa Dugange, nimshukuru pia Katibu Mkuu wa Wizara hii Shemdoe Profesa. Vile vile pia nimshukuru sana sana Engineer ambaye ni Mkurugenzi wa TARURA Ndugu Seif, lakini pia kwa namna ya pekee sana nimshukuru Engineer wangu ambaye yuko kule Jimboni kwangu au Wilayani kwetu Rungwe ambaye anaitwa Kamara, anafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, leo kwa sehemu kubwa nitakuwa nashukuru maeneo mengi, lakini nitakuwa na changamoto moja au mbili ambazo naomba Waziri ambaye ni Waziri makini sana aweze kusikiliza kwa makini na aweze kunisaidia katika Jimbo langu la Rungwe. Kwanza nashukuru sana kwa kupandisha bajeti ya Mfuko wa Jimbo kwa asilimia 45. Mfuko wa Jimbo una mchango mkubwa sana kwa maendeleo katika Majimbo yetu. Kwa hivi nashukuru sana kwa kupandisha hii bajeti kwa asilimia 45, ila nashauri kwamba hizi pesa za Mfuko wa Jimbo zifike mapema zaidi kwenye majimbo yetu kwa sababu ni muhimu kuchoche maendeleo kule Majimbo.

Mheshimiwa Spika, pia kwa sababu pesa itaongezeka, naomba hizi pesa zije hata kwa awamu mbili, ije awamu ya kwanza mwezi wa Saba, lakini baada ya miezi sita hizi pesa ziweze kuja tena kuchochea maendeleo. Kwa sababu muda mwingi utakuta unakaa mwaka mzima hizi pesa zinakuja mara moja kwa mwaka kiasi kwamba wananchi wanasahau kwamba kuna vitu vingine vinatakiwa kufanyika. Naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hilo, kwamba tuangalie kama tunaweza kupata hizi pesa kwa awamu mbili katika majimbo yetu ili majimbo yaweze kuchangamka mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, suala lingine la pili, nimeangalia kwenye utekelezaji wa bajeti ya mwaka jana kwenye TAMISEMI bado mapato ya ndani kwenye halmashauri zetu siyo mazuri sana. Mwaka jana nilisema na mwaka huu naongea tenah kuna chanzo kimoja cha mapato katika halmashauri zetu ambacho kipo very potential na kama tutakisimamia vizuri tunaweza tukaongeza mapato katika halmashauri zetu. Chanzo hicho ni service levy, service levy inakusanywa inafanana na Sheria ya TRA ambayo ni kodi ya mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama tukishirikiana na TRA vizuri, tukafanya assessment, TRA wanafanya assessment zao na service levy wakafanya assessment kwa pamoja kama parallel tunaweza tukaongeza mapato kiasi kikubwa sana kwenye service levy na tukaongeza mapato ya Halmashauri zetu kwa kiasi kikubwa.

Naomba hilo lizingatiwe na Waziri aweze kuli-note, washirikiane na TRA kuhakikisha wanapo-produce zile assessments za TRA kwenye kodi ya mapato wa-produce pia assessments za service levy katika halmashauri zetu ili kuongeza mapato katika halmashari zetu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo natoa pongezi kwa Wizara ni kuanzia mfumo wa kielektroniki katika kusimamia Mifuko ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. Hilo nawapa pongezi, naomba wakalisimamie kwa karibu kuhakikisha kwamba mambo yanayofanyika katika halmashauri zetu katika ngazi za TAMISEMI pia wanaweza wakayaona na wanaweza wakayashauri.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye afya. Mwaka huu wa fedha tumeletewa zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya Kiponjora, tumeletewa milioni 250 kwa pesa za tozo tunajenga Kituo cha Afya Ndanto, lakini tumeletewa bilioni 1.39 katika Hospitali yetu ya Wilaya Rungwe ambayo inaitwa Makandana. Milioni 300 ujenzi unaendelea, ilikuwa ni kwa ajili ya jengo la emergency, milioni 90 ujenzi unaendelea kwa ajili ya jengo la wafanyakazi, lakini bilioni moja kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo pale katika hospitali yetu.

Mheshimiwa Spika, nilivyokwenda kwenye kampeni mwaka uliopita walinisisitiza sana na walinitwisha jiwe kichwani ambalo linasema kuna matatizo makubwa ya kiutendaji katika Hospitali yetu ya Wilaya. Haya ni lazima niyaseme kwa sababu ni mwakilishi wa wananchi, matatizo ambayo nayapata katika maeneo yao lazima niyalete hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Naibu Shaka Abdul Shaka ambaye ni Mwenezi Taifa alikuja kutembelea pale kwetu, alitembelea kata tatu, alitembelea Kata ya Kiwira, Bagamoyo na Mpuguso, matatizo yote anayoelezwa ni matatizo ya service ya pale katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe. Kuna matatizo makubwa sana, mimi mwenyewe nimefanya ziara kwenda kushukuru kwa wananchi, akinamama ndiyo waathirika wakubwa na wengine wanaambiwa kabisa kwamba bwana nenda ukamwambie Mama Samia hapa hatuna madawa.

Mheshimiwa Spika, tunajua kuna matatizo MSD, tumeambiwa hapa Bungeni, lakini kuna lugha za kuwajibu wananchi, ili tuwaambie wajue kwamba Serikali inapitia matatizo fulani ambayo tunayajua MSD kuna shida. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwamba amebadilisha Mwenyekiti pamoja na Mkurugenzi MSD, hiyo napongeza sana kwa sababu tunategemea huko mbele ya safari tunapokwenda, tunakwenda kufanya marekebisho katika huduma zinazopatikana katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba kama hatutafanya marekebisho katika huduma zinazotolewa katika hospitali zetu nchi nzima, majengo tunayojenga ni bure, hayatatusaidia chochote, lakini kuboresha majengo na miundombinu mbalimbali inayofanyika katika hospitali zetu kwenye maeneo mbalimbali ni lazima yaende na elimu kwa watumishi wetu, tuwaambie wanatakiwa watoe service inavyotakiwa wananchi waweze kunufaika na matunda ambayo tunayapeleka katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu, wananchi watamlaumu bure Mheshimiwa Rais kwa sababu tu kwamba tunajenga majengo lakini hakuna service inayopatikana.

Kwa hiyo, naomba sana sana Waziri Mheshimiwa Bashungwa nafikiri nimeshamwona, waende wakafanye marekebisho kwenye Hospitali ya Wilaya ya Rungwe, tupate huduma zinazotakiwa kwa wananchi wa pale Rungwe ili tuondoe malalamiko ya wananchi ambapo kila siku wanalalamika kwamba huduma zinazopatikana hapa hazitoshelezi.

Mheshimiwa Spika, nimalizie upande wa barabara. Nimempongeza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)