Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa wachangiaji. Kwanza naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania akisaidiana na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wetu Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa Kassim. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nampongeza sana Waziri wa TAMISEMI pamoja na wasaidizi wake wote wawili na Katibu Mkuu na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya hasa ya kwenda kusimamia miradi ya fedha nyingi ambazo tumezipata kwenye Halmashauri zetu. Hongera sana Waziri na timu yako, tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawaomba wananchi wako wa Jimbo lako watusaidie kuendelea kukuombea, nasi tunakuombea kwa kazi unayoifanya pamoja na wasaidizi wako kuwaletea maendeleo Watanzania. Hongera sana Mheshimiwa Waziri wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza CEO wa TARURA kwa kazi nzuri anayoifanya kusimamia kitengo hiki cha TARURA. Kwa kweli mimi nasema Waheshimiwa Wabunge wenzangu, anafanya kazi nzuri na tunaomba sasa aongezewe fedha maradufu ili aweze kukamilisha kwenye Halmashauri zetu kufanya kazi nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, pale upande wa afya, pale Mawande; Kijiji hiki cha Mawande ni kikubwa sana. Kina wakazi wengi sana, lakini hatuna zahanati. Wananchi wale wametoa eneo lao, wamesomba mawe, mchanga uko pale, naomba tupate fedha ili wananchi hawa waweze kujengewa zahanati ili waweze kupata huduma iliyo karibu zaidi, itapendeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile katika Kata ya Utengule eneo la Ikelu nao pia wamekusanya mawe mengi, wamekusanya mchanga, wametengeneza barabara mpaka kwenye eneo lilotengwa kwa ajili kujenga Kituo cha Afya. Naomba tupatiwe fedha ili wananchi hawa weweze kujenga Kituo cha Afya ili huduma iweze kuendelea kutolewa pale.

Mheshimiwa Spika, pia katika Jimbo langu la Makambako, Kata ya Mjimwema, katika bajeti hii tunayokwenda nayo, naomba sana tupewe fedha za kujenga sekondari katika Kata ya Mjimwema. Eneo wanalo, walishatenga, hawana fedha. Nakuomba sana tupewe fedha za kuanzia au za kutimia timu nzima ya kujenga madarasa ya shilingi milioni 600, utakuwa umetusaidia sana katika Kata yetu ya Mji Mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzangu wameongelea habari ya Madiwani, niliongea kipindi kilichopita, nirudie tena nami kusema. Madiwani hawa ndio wanaosimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao, wakisaidiana na Wenyeviti wa Vijiji, ndiyo mafiga yanakuwa yamekamilika. Tunaomba sana katika mipango ya Waziri, tunaishukuru Serikali kwa kuwapa Bima ya Afya, ni jambo jema, wamefanya jambo jema zuri sana. Sasa mkae, muone namna ya kuwasaidia kuongeza posho za Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji ili timu hii iweze kusimamia vizuri fedha za maendeleo zinazopelekwa huko katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, na hili naomba Waheshimiwa Wabunge mnisikilize vizuri. Sipendi kugombana na taasisi za dini. Kuna mtu mmoja nilimsikiliza juzi juzi hapa akielekezea namna ambavyo amesema kinapofika kipindi cha uchaguzi, CCM tunaiba kura. Nadhani wote mlilisikia hilo. Sasa nasema kwa uchungu mkubwa, mimi nimeshinda kwa kishindo, siyo kwa kuiba kura; na Waheshimiwa Wabunge wote hapa wameshinda kwa kishindo, siyo kwa kuiba kura na Rais alishinda kwa kishindo siyo kwa kuiba kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu aliyozungumza maneno haya, anataka kutugombanisha na wananchi. Tumeshinda, ndiyo maana hata Jimbo la Sumbawanga tumeshindwa, ameshinda CHADEMA.

MBUNGE FULANI: Nkasi.

MHE. DEO K. SANGA: Nkasi, ameshinda CHADEMA. Kwa hiyo, kuelekezea jamii kwamba CCM wanaiba kura, siyo kweli. Tunashinda kwa kishindo. Watu wanakubali kwa sababu ya haya yanayotekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hivi kwenye maeneo yetu, Rais amepeleka miradi mingi, amepeleka fedha nyingi za maendeleo, watu wanakubali kwa kazi zinazofanyika, ndiyo maana wanatupa kura nyingi. (Makofi)

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Haleluya!

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, ndiyo maana juzi wakati nachangia, nikasema Rais akakope tena fedha ili zifanye kazi ya kujenga nyumba za walimu; za watumishi, vyoo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ndiyo nilisema siku ile hapa, ASAS wa Iringa ameunga mkono jitihada za mama, na ndio amesema anajenga darasa moja pale Makambako. Mbunge wa Mbarali naye akaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais, anajenga darasa moja pale Makambako. Haya ndiyo yanayofanya watu watuchague kwa sababu ya kazi zinazofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mitandao, watu wameelezea jambo ambalo unashangaa. Wanasema, unaona Mama sasa anaongozwa Mheshimiwa Kikwete. Hivi ni kweli! Kwani Mheshimiwa Kikwete hakufanya kazi nzuri katika nchi hii? Awamu ya Nne Mheshimiwa Kikwete ndio watu walisema fedha zilijaa kwa wananchi, hakufanya Mheshimiwa Kikwete? kwani Mheshimiwa Kikwete ana matatizo gani? Tumwache apumzike vizuri kule Msoga. Tuache habari za kwenye mitandao, tuache Mama afanye kazi ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Nimeona niliseme hili kwa hisia kali na kwa sababu watu wanataka kupotosha watu... (Makofi)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Sanga naomba ukae kidogo. Mheshimiwa Halima, Kanuni. (Kicheko)

KUHUSU UTARATIBU

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ambacho nakushukuru Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na timu yako kama nilivyosema, hakikisha wananchi wa Mawande wanapata zahanati; hakikisha Kata ya Utengule eneo la Ikelu wanapata Kituo cha Afya kutokana na kazi ambazo zimefanyika. Diwani wa eneo hili anafanya kazi nzuri sana pamoja na Madiwani wote wa Halmashauri ya Makambako.

Mheshimiwa Spika, naunga mkona hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)