Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa kupata nafasi ili niweze kutoa mchango wangu. Kwanza nianze kwa kupongeza Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. Vilevile kipekee kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba anawapatia maendeleo Watanzania. Nimpongeze sana kwa kampeni yake ambayo ameianza ya kuwapanga wamachinga ili waweze kupata maeneo bora kwa ajili ya kuweza kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Spika, nikupongeze pia wewe mwenyewe binafsi pamoja na Bunge lako. Wewe na Bunge lako mmekuwa mstari wa mbele sana katika kuhakikisha kwamba mnasimamia masuala ya usawa wa kijinsia ndani ya Bunge. Bunge lako linazo Kamati mbalimbali na katika hizo Kamati pamoja na Wabunge mbalimbali hakuna Kamati hata moja ambayo Mbunge wa Viti Maalum anazuiliwa kuingia ndani ya Bunge hili. Wabunge wa Viti Maalum wanaingia mpaka kwenye Kamati ya Bajeti, lakini katika hali ya kusikitisha iko shida kubwa sana katika halmashauri zetu Wabunge wa Viti Maalum tunakatazwa kuingia kwenye Kamati ya Fedha. Kamati ambayo ndiyo inapanga mipango yote ya maendeleo ya halmashauri zetu, Kamati ambayo ndiyo inayopanga hata zile asilimia 10, kwa maana nne kwa ajili ya akinamama, nne kwa ajili ya vijana, lakini asilimia mbili kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, hali hiyo inasikitisha sana na sisi kama Wabunge na nakumbuka kwa sababu mimi ni Mbunge wa kipindi cha pili sasa, tumekuwa tukizungumza sana hata Bunge lililopita tuliongea, lakini mpaka sasa hivi hakuna ambalo limefanyika.

Mheshimiwa Spika, kazi nzuri na kazi kubwa ya Mbunge ni kusimamia maslahi ya watu anaowaongoza. Kwa hiyo na sisi Wabunge wa Viti Maalum tumeaminiwa na wanawake wa mikoa yetu. Mimi Shonza ni Mbunge wa kipindi cha pili, nimeaminiwa na wanawake wa Mkoa wangu wa Songwe ili niwasimamie maslahi yao na namna ya kusimamia maslahi yao ni Bungeni na kule kwenye halmashauri zetu, ambapo huko ukiingia Mbunge wa Viti Maalum wanasema kwamba sheria inakataza Mbunge wa Viti Maalum kuweza kuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha. Sasa matokeo yake fedha hizo ambazo zinatolewa ni nyingi lakini fedha hizo zimekuwa hazirejeshwi. Aliongea hapa juzi Mheshimiwa Festo kwa uchungu mkubwa sana, fedha zinazotolewa ni nyingi lakini shida ipo kwenye marejesho, kwa sababu sisi ambao ndiyo viongozi ambao tunakaa na hao watu tunajua changamoto zao…

SPIKA: Mheshimiwa Shonza, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Leah Komanya.

T A A R I F A

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa hata kwenye kukabidhi fedha hizi katika mkoa mmoja sehemu moja anakabidhi Mkuu wa Mkoa sehemu moja anakabidhi Mbunge, kwa hiyo kunakuwa na double standard lakini makundi yale ya jamii hayashirikishwi katika ule mwongozo uliopewa, kazi hii tungeachiwa Wabunge kwa sababu tunawajua wananchi ili vijiji vyote viweze kutendewa inavyotakiwa.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Niseme kwamba nakubaliana kabisa na taarifa ambayo amenipa na maelezo ambayo umeyatoa.

Mheshimiwa Spika, changamoto imekuwa kubwa kwa sababu fedha hizi kama ambavyo nimesema, huwa hazirejeshwi, kwa sababu hakuna intervention ya Wabunge kwenye kusimamia hizi fedha. Nitatoa mfano mmoja. Kwenye Jimbo la Tunduma ambalo anatoka Mheshimiwa David Silinde, Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuwa akizisimamia hizi fedha na tumeona juzi alitoa fedha nyingi sana; alitoa bodaboda, akatoa bajaji akatoa na zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya kusaidia makundi ambayo yapo kwenye Mkoa wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto kwenye Halmashauri nyingine na Majimbo mengine Wabunge hawashirikishwi. Nami kama Mbunge wa Viti Maalum, nilipigiwa simu na nikaambiwa kumbe ni kweli hizi fedha huwa zipo. Kwa sababu wengine wanaona kama ni historia, ni kitu ambacho hakipo, kumbe ni fedha ambazo zipo na Serikali inafanya kazi kubwa sana kutoa hizi fedha, lakini changamoto ni kwamba intervention ya Wabunge hakuna. Kwa hiyo, tumeona kwamba maeneo ambayo yamepata fedha hizi na kuna intervention ya Mbunge, mafanikio ni makubwa sana. Nampongeza Mheshimiwa David Silinde kwa sababu ni Waziri hawezi kusema, lakini mimi kama Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wake, ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni kwamba hizi fedha haziendi kwa wahusika, yaani unakuta kuna watu wanapata fedha lakini hawana vigezo vya kupata hiyo mikopo. Pia kuna maeneo mengine Wilaya moja ina vijiji 100, lakini kwenye kuzigawa hizi fedha utashangaa mgao ni shilingi milioni 100. Shilingi milioni 50 yote inakwenda kwenye Kijiji kimoja, kwenye kikundi kimoja. Kwa hiyo, bado unakuta kuna double standard kwenye kugawa hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema, kwa kweli wakati umefika, sisi kama Wabunge tukae, tujadili. Hili suala naomba lifike mwisho ili sisi Wabunge, wakiwepo Wabunge wa Viti Maalum wanawake, Wabunge wanaowakilisha Vijana na wa Majimbo, sisi ndio tuwe wasimamizi wa huu mfuko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijikite kwenye kutoa ushauri kwa Serikali. Kwa kuwa Wabunge kwa miaka mingi tumekuwa tukilalamika juu ya suala la Wabunge kutokuingia kwenye Kamati ya Fedha, naomba sasa, kwa sababu Mawaziri wapo hapa na wanatusikia, ni wakati muafaka sasa hili suala lifike mwisho, mtoe miongozo. Kama ni suala la kikanuni, basi hizo kanuni ziletwe humu ndani ya Bunge zibadilishwe; na tukishabadilisha humu ndani ya Bunge, hiyo miongozo ichukuliwe ipelekwe kule kwenye Halmashauri zetu ili tuweze kuondoa hii changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili; kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa sana kwamba sisi Wabunge Viti Maalum hatuna Mfuko wa Jimbo, Wabunge wa Viti Maalum vile vile hatuna miradi yoyote ambayo tunasimamia kwenye Halmashauri zetu; ukiwa Mbunge wa Viti Maalum, huwezi ukasema hata uende kukagua hospitali, haiwezekani. Utaulizwa, umekuja kukagua kama nani? Kwa hiyo, hatuna kazi specific ambayo Wabunge Viti Maalum tunapewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nitoe ushauri kwa Serikali, ninaamini kwamba Serikali inatusikia; naomba Serikali, ikiwezekana hii asilimia nne kwa ajili ya akina mama isimamiwe na Wabunge wa Viti Maalum. Kwa sababu ilivyo sasa hivi, asilimia nne kwenye hicho kikao, tena ikiwezekana iwe ni Mfuko wa Jimbo, kama ambavyo Wabunge wa Majimbo wana Mfuko ya Jimbo, nasi asilimia nne hii iwe ndiyo Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya Wanawake. Kwa sababu sisi ndio tunajua changamoto za wanawake, tunajua makundi gani ambayo yanapaswa kupatiwa mikopo na tunajua makundi gani ambayo hayana sifa. Kwenye hiyo Kamati, Mwenyekiti wake awe ni Mbunge wa Wanawake ili aweze kuisimamia vizuri hiyo asilimia nne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe unafahamu, kwenye chaguzi zetu huwezi kuwa Mbunge wa Wanawake kama siku ya uchaguzi hujajipanga vizuri kwenda kuwaeleza wanawake utawasaidiaje waweze kupata mikopo ya asilimia nne? Kwa hiyo, huwa tunaongea tunawaambiwa wanawake, lakini kimsingi hatuna instrument ya kuweza kuwasaidia waweze kupata hii mikopo. Malalamiko yamekuwa mengi, kikundi kina sifa zote, kinaomba mikopo zaidi ya miaka mitano, miaka kumi, hakipati, lakini vikundi vingine ambavyo havina sifa vinapata mkopo. Hii ndiyo sababu ambayo inapelekea hata marejesho yake yanakuwa ya kusuasua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho kwa Serikali; naomba, kwa sababu tumeshuhudia sasa hivi Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan ameanzisha kampeni nzuri sana ya kuwapanga Machinga ili waweze kupata maeneo mazuri, wafanye wafanye biashara zao kwa amani ili hizi fedha ambazo zinakopeshwa kwa Machinga ziweze kurejeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri, kwa sababu Halmashauri inatenga 10%, naomba Serikali iangalie uwezekano wa ku- top up angalau 3% kwenye ile 10% ambayo inatengwa na Halmashauri ili hiyo 3% iende ikaboreshe miundombinu kule kwa wafanyabiashara kwenye kujenga masoko, kujenga viwanda, ili Serikali inapotoa fedha kuweza kuwakopesha, basi hawa vijana, akina mama na watu ambao wana makundi maalum, waweze kuwa na sehemu ya kuzifanyika hizi kazi. Nakushukuru. (Makofi)