Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza na TARURA tumeona kuna ongezeko kubwa la bajeti ya TARURA, ukilinganisha kuanzia mwaka 2020/2021 bajeti ya TARURA ilikuwa bilioni 275, ikaja 2021/2022 ikapanda mpaka bilioni 722 na hivi sasa tunavyozungumza bajeti ya TARURA 2022/2023 ni bilioni 802. Hi ni hatua kubwa sana ambayo itasaidia kuboresha barabara zetu za vijijii. Napenda kuwaambia TARURA Mkoa wa Njombe, sisi wananchi wa Mkoa wa Njombe ni wazalishaji wazuri sana wa vyakula pamoja na zao la chai. Kwa kuwa tumekuwa na changamoto kubwa sana kwa wakulima wetu wa chai, chai kuharibika zinapotoka kule mashambani kwenda kwenye viwanda, zinafika zikiwa hazina ubora kutokana na changamoto za barabara.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi naamini kwa bajeti hii na kwa mwendo huu mzuri wa Serikali ya Rais Samia kuhusiana na suala zima la kuboresha barabara zetu za vijijini, naamini sasa barabara hizi zitakwenda kuwa mkombozi wa chai zetu kutoharibika na kufika kwa ubora na wakulima wetu wa chai wataweza kupata pesa nzuri wanapokwenda kuuza kule viwandani. Ushauri wangu kwa TARURA Njombe ni wakati sasa wa kufanya survey za barabara zetu mapema ili barabara zetu za vijijini ziweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie suala la afya ya msingi. Katika suala la afya ya msingi nimeona kwenye bajeti ya TAMISEMI wanaendelea kukamilisha ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali zetu, lakini sambamba na kupeleka vifaa tiba katika hospitali, zahanati na vituo vya afya ambavyo vimekamilika. Ni jambo zuri ni kazi nzuri wanayoifanya, lakini ushauri wangu nawaomba kuna changamoto kubwa sana ya wauguzi kwenye vituo vyetu vya afya, kwenye hospitali zetu, kwenye zahanati zetu na Mkoa wa Njombe kwa kweli tatizo hili limekuwa ni kubwa mno kwa Majimbo yetu yote sita ndani ya Mkoa wa Njombe na hata ukizungumza na baadhi ya Wabunge kwenye mikoa yao bado changamoto ya wauguzi ni kubwa sana. Kwa hiyo naiomba Serikali wajikite katika kuhakikisha kwamba wanamaliza tatizo la wauguzi, wakae pamoja na Wizara ya Utumishi ili waone namna gani wanaweza kuongeza wauguzi katika zahanati zetu, vituo vya afya na hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye elimu msingi; katika elimu msingi nataka nizungumzie masuala ya majengo, Walimu na wanafunzi na niseme jamani, kusema ukweli katika suala la majengo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameupiga mwingi. Ndani ya mwaka mmoja amejenga madarasa 15,000, madarasa 3,000 kwa ajili ya elimu ya awali na hii imesaidia watoto wetu wale walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda kufuata elimu sasa changamoto hii imekwenda kwisha.

Mheshimiwa Spika, vile vile tulikuwa na changamoto watoto hapa walikuwa wanaenda second selection madarasa 12,000 yamejengwa ajili ya shule za sekondari. Kwa kweli Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anahitaji pongezi nyingi sana haijapata kutokea ndani ya mwaka mmoja Serikali kujenga madarasa 15,000. Ushauri wangu sasa pamoja na kuwa tumejenga madarasa mengi 15,000 ndani ya muda mfupi, naiomba Serikali sasa iangalie umuhimu wa kuongeza walimu wa sayansi. Walimu wa sayansi ni changamoto sana kwenye shule zetu. Nashukuru juzi nimeona Waziri wa Utumishi ametoa kibali kwa ajili ya kuajiri Walimu naomba sasa Wizara hii ya TAMISEMI ikae na Wizara ya Utumishi ione namna ya kutoa kipaumbele kwa Walimu wa sayansi. Ukizingatia sasa hivi ulimwengu wetu huu ni ulimwengu wa sayansi tujitahidi tuajiri Walimu wa sayansi ili kusudi watoto wetu tuwaandae vizuri katika kukabiliana na ulimwengu huu wa sayansi.

Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kuna salamu zake kutoka Kata ya Igwachanya kwa Mheshimiwa Diwani Mawata. Tarehe 22 mwezi wa kwanza mwaka 2022 alienda pale shuleni, kuna changamoto ya bwalo. Bwalo lile limeanza kujengwa tangu mwaka 2012 kwa nguvu za wananchi pamoja na Serikali wameshajenga foundation wameweka na nguzo. Vile vile Mheshimiwa Jafo alipita pale mwaka 2020, akaahidi kwamba watawapa milioni 100 mpaka leo hawajawapa na kukamilisha ujenzi ule wa bwalo lile inahitaji milioni 275 tu, kwa nyie watu wa Kagera ni hela ya mboga tu. Naomba wajitahidi wapeleke pesa ili kusudi bwalo lile likamilike na Mheshimiwa Diwani aamini kweli alinituma na salamu zimefika.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwaomba sana pamoja na bima za afya ambazo wametoa kwa Madiwani lakini bado kuna umuhimu wa kuwaongezea posho Madiwani hawa kutokana na kazi kubwa wanayoifanya. Niwaombe sana sana katika hili.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, nilisahau kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa zile bilioni 1.5, kila Jimbo la mkoa wa Njombe za TARURA tulizipata, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)