Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima na salama kwa leo kukutana hapa kujadiliana kuhusu bajeti ya ulinzi na usalama katika nchi yetu hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa neno moja; kule kwetu kuna ndege kwa kiarabu anaitwa bull bull, kwa Kiswahili anaitwa kasuku. Kasuku ukisema hodi, basi naye anasema vilevile hodi! Sasa kasuku yule ile hodi hajui kama maana yake ni nifungulie mlango. Kwa hiyo, imekuwa yeye ame-copy tu kwamba ndiyo amesema hodi. Nafikiri mmeshuhudia, watu wanazungumza ekari, halafu baadaye wanageuza maneno kwa sababu ni maneno ya bull bull. Anaondoka bull bull! (Kicheko/Makofi)
Mimi najikita zaidi katika kuongelea masuala ya maslahi ya wanajeshi wanapokuwa kazini na wale wanaostaafu. Nachelea kupoteza muda mwingi, nitakuwa consistency na wale waliochangia suala hili. Nitajaribu kuongelea kuhusu wastaafu wa Jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mawili; kuna watu waliingia kwenye mikataba huko katika majeshi tunafahamu, pengine watachukua kwa mkupuo au watakuwa wanapata pensheni. Badala yake wakaja wakataka ku-reverse, kuja kujirejesha tena upya. Kwa hiyo, hawa ilikuwa wazingatiwe jambo lao hili kwa sababu lengo ni kulinda usalama na amani ya nchi yetu na lengo ni kuwa na wanajeshi wa akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wote hawa walioingia kwenye mambo hayo mawili whether ya kuchukua kwa mkupuo au kupata pensheni, lengo letu kama Taifa sasa hivi ni kuwaweka kama askari wa akiba na tusiwe na wapinzani katika ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la kushukuru, watu wengi sana wameunga mkono hii bajeti. Hii bajeti imeungwa mkono kwa vitendo na watu wote, kwa hiyo, na mimi naiunga mkono bajeti hii na hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napata mashaka kidogo; inakuaje mtu umekaa ukimwona mwanajeshi unaanza kutetemeka, una nini wewe? Una kitu gani ulichoficha? Kuna ajenda gani? Kwa nini wewe uwe unaona taabu kukutana na majeshi ya ulinzi na usalama? Kwanza anza kujiangalia kutokea hapo, una mashaka gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kitu kimoja; Jeshi la Ulinzi na Usalama kazi yake moja ni kulinda mipaka yetu nje na ndani. Mimi ni shahidi, bomu la mwanzo kulipuka baada ya uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba pale Zanzibar lililipuka mbele ya Kanisa Anglikana Mkunazini, lililipuliwa na majeshi, tulitarajia aende nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, bomu la pili lililipuka round about ya Michenzani upande wa njia ya kutokea Bwawani. Likalipuka la kwanza pale, baada ya dakika 10 likalipuka bomu la pili; na mimi mwenyewe nilikuwa niko maeneo ya pale pale kwa sababu ni maeneo yangu ya kujidai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya mabomu ikiwa tunao maadui wa ndani, kwa nini Jeshi letu la ulinzi lisifanye kazi ndani? Mabomu mengine mawili yalienda kuteguliwa katika Kambi ya JKU Zanzibar Saateni. Yametegwa na haya mabomu, tunafikiri jukumu hili ya kutegua hayo mabomu akafanye nani? Jeshi la Wananchi wa Tanzania liendelee kufanya kazi zake ndani na nje ya mipaka yetu, kwa sababu bado tunao maadui wa ndani na nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu waliokuwa wanazungumza kwamba jeshi lilienda kuwatisha watu wasishiriki uchaguzi wa tarehe 20 Machi, wamemsahau aliyewatisha! Hivi dakika ile ile kiukweli wamesahau? Basi akili hizi zitakuwa za kuku, maana kuku ukimwinga, anaondoka. Baada ya dakika chache kuku anarudi pale pale. Itakuwa wana akili za kuku hawa, wameshahau aliyewaambia wasiingie kwenye uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli Jeshi la Wananchi ndiyo limeenda kusimamia kwamba watu wasiingie kwenye uchaguzi wa marudio? Mtu anazungumza maneno hayo hapa wakati anafahamu kwamba kiongozi wake ndiye aliyesema hayo maneno. Sasa leo wanakuja kuyaleta hapa, nashangaa sana! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo lilizungumzwa hapa na wengi kila mtu akikaa anasema kwamba anaunga mkono. Maneno yaliyozungumzwa na Kambi ya Upinzani, mimi namheshimu sana mzee wangu. Maneno aliyozungumza kwamba, demokrasia ya Zanzibar iliharibiwa na majeshi, nashangaa sana. Naweza nikasema, kuna mshairi mmoja anasema; “masikini roho yake, kioo kimemcheza.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli alijipima na akajiangalia kwamba yeye aje azungumze maneno hayo hapa, amewahi kuwa kiongozi wa ngazi za juu kabisa, maskini roho yake kioo kimemcheza!
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine unapoambiwa ufanye jambo, ujaribu kutazama, wenzako wanakutoea hao! Usiwe zumbukuku ulimwengu uko huku! Ni lazima ujiangalie huko katika hali gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niunge mkono hoja lakini kingine cha umuhimu kabisa katika kuangalia masuala haya ni hali ya uwiano katika ajira na utawala wa Jeshi la Wananchi, hili ni Jeshi la Wananchi wa Muungano wa Tanzania, ikiwemo Zanzibar na Tanzania Bara.
Kwa hiyo, hata katika utawala, leo wametajwa pale Majenerali nikasema na mimi nitasikia jina la kwetu sikulisikia, tuwe na uwiano katika masuala haya na kwenye ajira pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ni la msingi na kubwa zaidi, Jeshi letu litahusika na ulinzi wa mipaka katika bahari kuu. Hili liangaliwe kwa sababu ni jambo la kiuchumi na linahitaji zana za kijeshi, lakini pia kuzingatia uharamia unaofanyika katika nchi jirani ikiwemo Somalia lakini uchujaji uwe mzuri kwa sababu pia na wavuvi wetu nao huwa wanakwenda kuvua. Nilimsikia Mbunge wa Bumbwini aliuliza swali katika kipindi cha maswali na majibu kuhusiana na suala hili. Kwa hiyo, naomba masuala hayo yazingatiwe na yafanyike vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo ni muhimu, nimejaribu kupima hapa na nime-synthesis hoja nyingi sana…
(NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo, Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.