Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa miradi mikubwa Wilayani Muleba katika nyanja za afya, elimu, maji, miundombinu, umeme na kadhalika. Kwa niaba ya Wanamuleba namshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake, namshukuru kwa mkutano wake alioufanya Wilayani Karagwe kwa ajili ya kuboresha bei ya zao la kahawa, hakika wakulima wa zao la kahawa wanatoa pongezi nyingi sana kwa kufuta tozo 42.

Mheshimiwa Spika, nachangia hoja ya Waziri Mkuu katika ukurasa wa 42 kifungu cha 75 kuhusu ardhi. Wilaya ya Muleba ina migogoro miwili mikubwa ya ardhi baina ya Kampuni ya Ranchi (NARCO) na wakulima katika Kata ya Rutoro na eneo la MWISA II. Nitajikita kwenye mgogoro wa MWISA II.

Mheshimiwa Spika, mgogoro wa MWISA II ulianza mwaka 2016 baada ya NARCO kuvamia eneo la MWISA II na kuanza kupima vitalu kwa ajili ya kukodisha wafugaji. Upimaji huo ulihusisha na kuathiri ardhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vimepimwa na kusajiliwa kisheria. Huu mgogoro unahusisha kata saba (Kyebitembe, Karambi, Kasharunga, Mubunda, Burungura, Ngenge na Rutoro) vijiji 12 na vitongoji 19. Upimaji huu unakiuka Sheria ya Ardhi ya Vijiji, kuna taaruki kubwa.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana mwezi Julai 2021, Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi alifika Muleba kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Baada ya mkutano na kwenda kujiridhisha na hali halisi, tulifikia maridhiano kuwa NARCO wasiingilie maeneo ya vitongoji na vijiji ambavyo vimesajiliwa kisheria. Hii ilikuwa faraja kwa wananchi wa vijiji hivyo 12 na vitongoji 19.

Mheshimiwa Spika, NARCO wameanza na wanaendelea kuingilia mashamba ya wananchi katika vitongoji vya Kabwensana na Mahigabili katika Kijiji cha Kakoma, Kata ya Burungura na kuanza kuhamisha watu kwa nguvu, kuwanyang’anya mashamba yao na/au kuwagawia watu wengine heka sita kwa kisingizio cha kupanga makazi. Kuna sintofahamu na taharuki kubwa sana. Kulingana na mila na desturi zetu, tunazika wapendwa wetu kwenye mashamba yetu karibu na nyumba zetu. Hamishahamisha hii haizingatii hata sheria ya kuhamisha makaburi ya wapendwa wetu “The Graves (Removal) Act, Act No. 9 ya 1969.

Naomba Ofisi ya Wazir Mkuu itusaidie kumaliza mgogoro wa MWISA II ambao unahusisha kata saba, vijiji 12 na vitongoji 19. Ni mgogoro unaohushisha eneo kubwa na watu wengi sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.