Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nimepewa salamu na wananchi wa Kinondoni nimletee Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba wao wanafurahishwa sana na utendaji wako wa kazi. Wanakuona kila mahali kwenye migogoro kwenye utatuzi wakasema huyu Waziri Mkuu tulienaye anafanana sana kama ile timu iliyotengeneza gap ya point 10 haishikiki! Mimi naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu uendelee na kasi hiyo hakuna mtu atakayekugusa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Rais, alipokuja pale Kinondoni kwa ajili ya kuzindua yale majengo ya Magomeni Quaters ambapo wananchi 642 wamepata makazi mapya, hakika wananchi wa Kinondoni wamefurahia sana na sikuwa nimepata nafasi ya kuzungumza, lakini nataka nimwambie kupitia Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Rais wananchi wa Kinondoni wamefurahi sana na wanamuombea kila la kheri, Mwenyezi Mungu amjalie afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanasema haya kutokana na jinsi Serikali inavyofanya kazi yake kwenye eneo hili la Kinondoni, tunasubiri mradi ambao utaanza mwezi wa Julai inshallaah ambao ni mradi wa Mto Msimbazi, maeneo ambayo yalikuwa yanapata mafuriko kila wakati, maeneo ya Kigogo, maeneo ya Mzimuni, maeneo ya Magomeni, yanakwenda kupata sura mpya kwa mradi wa Shilingi Bilioni 240 na zaidi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wale wanachokiomba Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba hili uli-note, kwamba zitakapokuja taratibu za kulipa fidia basi zifanywe kwa wakati. Kwa sababu wana hofu na lile lililotokea katika Kata ya Magomeni, Mtaa wa Suna, Kata ya Hananasifu, Mtaa wa Kawawa na Mtaa wa Hananasifu yenyewe na Mkunguni, wananchi wamevunjiwa njia nyumba zao Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kipindi cha mwaka 2015/2016, Wizara ya Afya pamoja na watu wa mazingira walikwenda kuvunja zinazofikia 945 wananchi wale mpaka leo wanapata shida, hakuna wakuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, sitaki niyazungumze haya mengi nitaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu unipe nafasi nikutane na wewe ili nilete hiki kilio cha wananchi wa maeneo kwako na uone jinsi gani utaweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, Kinondoni tuna mtandao wa barabara za lami wa kilomita 165 na kwenye Jimbo langu barabara za lami ni kilomita 95.35 na hapa nataka nizungumzie kitu kinachoitwa spot maintenance ule ukarabati wa mashimo katika barabara. Eneo hili ni gray area Mheshimiwa Waziri Mkuu, linatisha.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu Serikali imetenga Shilingi Bilioni 5.6 kwa ajili ya kutengeneza mashimo. Najua Wabunge wengi waliomo humu ndani wanaishi Kinondoni au wanapita Kinondoni. Tuna barabara ambazo zinapata mashimo mara kwa mara, sasa fedha zinazotengwa ni fedha nyingi sana 5.6 billion Shillings ni hela nyingi sana kwa ajili ya kuziba mashimo.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nalileta suala hili mbele yako na mbele ya Waziri Mkuu ni kwamba mashimo yale kila siku yanakuwa ni yale yale, huu ni mradi. Leo likitengenezwa shimo lile baada ya miezi mitatu litatengenezwa tena shimo lile lile. Huu ni mradi, kwa sababu fedha nyingi kama zile zinamalizika namna gani? Kwa viraka vidogo vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka na naiomba Serikali kwanini isifikirie utaratibu wa kurudi kizamani angalau kwa majaribio katika Jiji la Dar es Salaam, tuna karakana kule Ilala, tuna karakana pale Mwananyamala pale Kinondoni, kwanini Serikali isitumie na kuwa na vifaa na mafundi wetu wa kutengeneza mashimo yale ili tukaondokana na huu utaratibu ambao sasa hivi watu wanatumia fedha nyingi kuziba mashimo yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano upo mzuri sana, ukitembea Kinondoni utaona, ukiweka alama pale kuna barabara inaitwa Tarimba Road ambapo napita kila siku, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kila baada ya miezi mitatu, lazima itatengenezwa eneo lile lile, hivi hatuoni? Kwenye hilo, nitakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu ulisimamie, kwa sababu yawezekana tunaweza tuka-save fedha nyingi kwa utaratibu ambao nimeupendekeza, kwa sababu zamani ulikuwepo utaratibu huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alichukue hili aweze akalifanyie kazi ili aweze kuliangalia, si vibaya ukafanya utafiti cost benefit analysis kuweza kujua kama tukiendelea na utaratibu wa sasa hivi ama tukiendelea na utaratibu wa kuwa na karakana zetu kipi kitaifaidisha Serikali na kuweza kuipa thamani ya fedha kwenye maeneo haya. (Makofi)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, taarifa!

SPIKA: Mheshimiwa Tarimba kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mpembenwe.

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba anachokisema ni kitu sahihi kwa sababu hata pale katika barabara ya Msimbazi kuna wawakilishi ambao wanaiwakilisha nchi mashindano ya kimataifa, barabara pale siyo nzuri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Tarimba, malizia mchango wako.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa sababu hii taarifa siwezi nikaipokea kwa sababu sijapita hiyo barabara bahati mbaya niko Kinondoni.

Mheshimiwa Spika, jingine ambalo ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu tuliseme ni usimamizi wa miradi ambayo Serikali inawekeza fedha nyingi sana. Pale Kinondoni, kuna maeneo ambayo yanapata sana mafuriko wakati wa mvua. Kata za Dugumbi, Kata ya Tandale, Kata ya Makumbusho, Kata ya Magomeni, Kata ya Mwananyamala na Kata ya Hananasifu, kuna Mto ambao unaanzia Sinza kwa Mheshimiwa Profesa Kitila, ule mto unakuja unapita unaitwa Mto Ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, Serikali mwaka 2019 ilipata Mkandarasi anaitwa CHICO kampuni moja ya Kichina, kwa thamani ya Shilingi Bilioni 32.5. mpaka tunavyozungumza mradi huu ulitakiwa umalizike mwaka 2019 ambapo ndiyo umeanza na umalizike Desemba, 2020.

Mheshimiwa Waziri Mkuu mradi huu haujamalizika, Mkandarasi hayupo katika eneo la kazi na ameshalipwa shilingi bilioni 20 kati ya zile Shilingi Bilioni 32. Kazi iliyofanyika ni asilimia 76 na ameongezewa muda mpaka mwaka jana tarehe 31 Desemba, 2021 bado hakuna kinachofanyika, mvua zinaweza zikaja, wananchi hawa wakaendelea kupata matatizo, ninaiomba Serikali iingilie kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiyumkiniki Kinondoni mahali ambapo kuna watu wengi, mahali ambapo pana shughuli nyingi na wananchi wale wanaendelea kupata shida katika mafuriko wakati Serikali ilishatenga fedha na ilishalipa fedha asilimia zaidi ya 76.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, Wananchi wa Kinondoni wameniambia, Serikali Sikivu kama hii na hasa wewe ambaye uko tayari kwenda kila mahali penye matatizo. Juzi ulikuwa Bukoba, kwenda kutatua matatizo ya kilimo ninakutarajia siku moja uibukie pale Kinondoni, ulione hili suala. Naamini kabisa ukionesha rangi yako tunayokujua, siyo rangi ile nyekundu hapana! Rangi yaani kwa maana your true colors za uchambaji kazi naamini kabisa wasimamizi wa miradi hii wataona naam! Sasa Serikali iko serious. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuomba kwa sababu pale tulio wengi ni wacha Mungu, tukiomba dua mara nyingi Mwenyezi Mungu anasikia. Tunataka tukuombee Mungu katika eneo hili kwamba na ninyi mnuse nusu fainali, hebu tufanyie hii kazi. Mkitufanyia hii kazi sisi tutakwenda kukesha msikitini tarehe 17 Mwenyezi Mungu awajalie mambo yenu yawe mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unajua mimi ni ‘Walii’ nikizungumza niko katika swaumu basi mambo haya Mwenyezi Mungu atakwenda kuwajalia, mimi ni mtu mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kukupongeza kwa mara nyingine pamoja na Serikali zima kwa kazi nzuri unayofanya na niwatakie kila la heri, Mwenyezi Mungu atujalie, kwa wale ambao wanafunga, Kwaresima Karim, basi Mungu awajalie kila jema na wale walio katika mfungo wa Ramadhani Mwenyezi Mungu awajalie. Hizo ndizo salamu kutoka Kinondoni, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja hii. (Makofi)