Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoendelea kuchapa kazi na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kila uchao, niwaombe tu tuendelee kumuombea sana Mama yetu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kupongeza kazi nzuri zinazofanywa na ofisi ya Waziri Mkuu kwenye maeneo mbalimbali, naomba nitoe ushauri kwenye Wizara ya Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, hasa kwenye eneo la vijana.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwa mwaka wa fedha 2021/2022 fedha ya Mfuko wa Vijana iliyokuwa imetengwa ilitolewa yote Shilingi Bilioni Moja, lakini kwa masikitiko makubwa kwamba fedha hizo ambazo kila mwaka Waheshimiwa Wabunge walivyokuwa wanachangia huku tulikuwa tunasikia kwamba walikuwa wanaomba hizo fedha ziongezwe.

Mheshimiwa Spika, kwa bajeti ya 2020/2021 fedha hizo hazikuwa zimepatikana na mwaka huu ambao tunamalizia sasa Shilingi Bilioni Moja iliyokuwa imetengwa yote ilipatikana lakini matumizi yake kwa vijana ni Shilingi Milioni 205.

Mheshimiwa Spika, lazima kujiuliza na ukiuliza unaambiwa kwamba vijana wa Kitanzania waliokuwa wametengewa fedha Shilingi Bilioni Moja hawakukidhi vigezo vya kuweza kuitumia hiyo Shilingi Bilioni Moja. Sasa hivyo jukumu la kuwawezesha hawa vijana wakatumie fedha Shilingi Bilioni Moja iliyokuwa imetengwa na imepatikana ili waweze kujikwamua kiuchumi ilikuwa ni jukumu la nani?

Mheshimiwa Spika, ni jukumu la Serikali kuwajengea uwezo na hivyo vigezo vilivyokuwa vimewekwa na Serikali ni vigumu kiasi gani kiasi kwamba vijana wa Kitanzania hata wale wahitimu wa elimu ya juu na kati hawawezi kuvikidhi? Nilikuwa nadhani Serikali kupitia Wizara husika inayo sababu ya kuhakikisha kwamba hivyo vigezo vinajulikana lakini na kuweka utaratibu rahisi ili hao vijana waweze kutumia ama kupata hizo fedha ambazo kimsingi mwisho wa bajeti zitabaki na sijui kama hiyo itakuwa imekuwa ni lengo la kutengwa kwa hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa najaribu kuangalia kama jumla ya Shilingi Bilioni Sita imetumika katika program ya kukuza ujuzi kwanini isiwiane na Bilioni Moja iliyokuwa imetengwa kwa vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri iliyofanyika ya kutoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kwa vyuo 72 na mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu 2,215 nilikuwa najiuliza fedha hizo zisingeweza kutumika kwa mfano kwa vyuo vya maendeleo ya wananchi, vijana ambao wanahitimu kwenye chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Newala pale Kiduni, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi pale Mtwara – Mtawanya, ili vijana hawa wanapokuwa wamepata huo ujuzi ambazo wamekwenda kujifunza, wakapata mitaji ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi, kwa hiyo pengine kuna haja ya kuongeza ama kuweka mipango zaidi ya kuwawezesha vijana kutumia hizo fedha Shilingi 795,000,000 ambayo mpaka sasa haijaweza kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia taarifa ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi, imeonekana kwamba Milioni 25.9 ya Watanzania ndio wanauwezo wa kufanya kazi na kati ya hao Vijana ni Milioni 14.2. Hata hivyo, inaonesha ukosefu wa ajira kwa vijana ni takribani asilimia 12.2, hasa nikawa najiuliza hivyo kweli kama vijana asilimia hii 12 wenye umri wa miaka 15 mpaka 35 tunaamini wengi wao watakuwa wameshamaliza vyuo vikuu na vyuo vya kati, kwanini hii Bilioni Moja isiishe yote, ikawapatia ajira wakaweza kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Je, Maafisa Vijana tulionao kwenye Serikali za Mitaa kwenye ngazi ya Mikoa na Wilaya wanatimiza wajibu wao kuhakikisha hizo fedha zinatumika na vijana wanaweza kujiajiri?

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nadhani hapo kuna kazi ya kufanya ili tuweze kimsingi kuwawezesha vijana kiuchumi na hatimaye suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi liweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili nichangie kwenye eneo langu Mkoa wa Mtwara. Nilikuwa naangalia kwamba tunapoelekea sasa hivi tunaanza kuandaa mashamba yetu ya Korosho, lakini changamoto kubwa pamoja na mambo mengine ni ukosefu ama uhaba wa vifungashio kwenye zao la Korosho hasa magunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kwa vile tunajua Watanzania wote tunategemea kilimo na wananchi wa Mkoa wa Mtwara tunajitahidi kupambana katika kuhakikisha kwamba hicho kilimo cha Korosho kinatukwamua na umaskini, sasa hii changamoto ya mifuko ambayo kimsingi inaonekana kama haijapata tiba kwamba kila inapofika msimu kila mwaka kunakuwa na changamoto ya magunia. Je, hatuwezi tukapanga kabla, hatuwezi tukafanya maoteo ya kupata hayo magunia ili kuondokana na hivyo changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa na hiyo ingewezekana kama tungeweza kutumia viwanda vya ndani, kama kuna hiyo Mikao ambayo inalimwa zao la kimkakati Mkonge tunashindwaje kupata magunia ya kufungasha korosho na hivyo kupelekea Korosho kurundikwa chini na kukosa ubora kila msimu tunapokuwa tumevuna hizo korosho, ni imani yangu kwa mwaka huu na kwa vile Waziri wa Kilimo anafanyakazi vizuri ni imani yangu kabisa kwamba hiyo changamoto haitatokea tutakapokwenda kwenye msimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongeze pia na Mnyororo wa thamani tunaposema kwamba korosho lazima ibanguliwe ili bei yake iweze kupanda sasa hata vile viwanda ambavyo tumekuwa tukivilalamika kwamba viboreshwe na vile vilivyokufa vihuishwe, mpaka sasa hivi hatujaona hata kiwanda kimoja ambacho katika Mkoa wa Mtwara kilikuwa kimekufa kimeanza kuboreshwa, sasa huu mnyororo wa thamani hatutaweza kuufanya wala kufikia, kwa hiyo ninaiomba Serikali, naamini Serikali yangu ni sikivu sana.

Mheshimiwa Spika, sasa tunapokwenda katika bajeti ya mwaka huu Mheshimiwa Waziri Mkuu na unajua kabisa namna ambavyo wananchi wa Ruangwa Mkoa wa Lindi na Mtwara hatuna zao lingine zao letu sisi ni korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiimarisha kwenye eneo hili tunauhakika nyumba hizo za nyasi, sijui na nini, wananchi wote watakuwa wanaishi kwenye makazi ya kisasa na tutakuwa pia tuna uwezo wa kuhakikisha kwamba tumejikwamua na tupo kwenye maisha bora na salama.

Mheshimwia Spika, nakushukuru naomba niunge mkono hoja. (Makofi)