Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, utangulizi; ninayo heshima kubwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2023/2024, pamoja na Mapendekezo ya mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapitia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa tukiwa na takwimu sahihi ya idadi ya watu na majengo kutokana na Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika tarehe 23 Agosti, 2022 ambapo idadi ya watu imefikia 61,741,120. Takwimu hizi zinatuwezesha kuandaa mpango jumuishi na unaotekelezeka. Maendeleo ni takwimu, hongera sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kusimamia vyema zoezi la sensa mpaka takwimu zimepatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze kwa dhati Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara Mheshimiwa Mama Anne Semamba Makinda na Kamisaa wa Sensa Tanzania Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Mohamed Haji Hamza. Hongera timu ya watakwimu wote walioshiriki, Makarani wa Sensa, Wenyeviti wa Vitongoji na wananchi wote kwa moyo wa kizalendo walioonesha katika kukamilisha zoezi hili muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchambuzi wa utekelezaji na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2023/2024. Deni la Serikali; takwimu zinaonesha kwamba deni la Serikali limeongezeka kutoka shilingi trilioni 60.72 kipindi cha Aprili, 2021 hadi shilingi trilioni 69.44 Aprili, 2022 hili ni ongezeko la shilingi trilioni
8.72 katika kipindi hicho ambalo ni ongezeko la 14.4%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwendendo wa ukuaji wa deni la Serikali; deni la Serikali lilikuwa kwa asilimia saba (2019/2020), asilimia 13.7 (2020/2021), asilimia 11(2021/2022) lakini pia takwimu zinaonesha kuwa Serikali ilipokea mikopo mipya kipindi cha miezi miwili, Mei na Juni, 2021 kiasi cha shilingi trilioni 3.799.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu hizi zinazua maswali mengi yasiyo na majibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kujiuliza kwa nini deni la Serikali liongezeke kwa shilingi trilioni 8.72 wakati katika mwaka husika wa fedha wa kuishia Aprili, 2022 deni lililipwa kwa zaidi ya shilingi trilioni 7.2 na wakati huo huo shilingi ya Tanzania iliimarika kwa wastani wa 0.03%. (sababu ya riba haiwezi kupandisha deni kwa kiwango hicho).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tafsiri yake Serikali ilichukua mikopo mipya yenye thamani ya shilingi trilioni 15.92 kinyume na kiwango kilichoruhusiwa na kupitishwa na Bunge cha wastani wa shilingi trilioni 10.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, deni la Serikali lilikuwa linakua kwa wastani wa asilimia nne lakini ghafla miaka ya 2020/2021 na 2021/2022 deni la Serikali limekua kwa wastani wa asilimia 12.33. Wakati deni la Serikali likiongezeka kwa kasi hiyo ukusanyaji wetu wa mapato ya ndani sio wa kuridhisha ambapo Tanzania inakusanya asilimia 11.40 ya pato la Taifa ikiachwa nyuma na nchi jirani za Kenya asilimia 13.70 na Rwanda asilimia 15.90 ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha Taarifa ya Kamati ya Bajeti ukurasa wa tano na sita kipengele cha 2.5 imeshtushwa na kasi ya ukopaji unaoendelea, nanukuu; ”Aidha imekuwa ni rai ya Kamati ya muda mrefu kuweka na kutumia kiashiria cha ukumo wa ulipaji wa deni la Serikali kwa mapato ya ndani (Debt Service to Domestic Revunue Ratio) ili kuhakikisha kwamba mapato ya ndani yana uwezo wa kugharamia shughuli zote za Serikali pamoja na deni la Serikali.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa kasi wa deni la Serikali wa namna hii ambao pia hauzingatii uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani usipodhibitiwa kuna hatari nchi yetu kuingia kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo na Serikali kukopa, lakini ni lazima mikopo inayochukuliwa na Serikali izingatie uwezo wa nchi kulipa madeni hayo na ukomo wa kukopa uliopitishwa na Bunge katika bajeti ya mwaka husika, na hii ni kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Katiba na Sheria za nchi (Sheria ya Fedha, Sheria ya Bajeti na Sheria ya Mikopo) zinaeleza bayana utaratibu wa namna ya kukopa na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, kwa nini Serikali ikope zaidi ya kiwango kilichoruhusiwa na Bunge?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama miradi yote iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 ilitengewa fedha na kuidhinishwa na Bunge, je, mikopo ya ziada iliyokopwa na Serikali imetekeleza miradi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba ufafanuzi katika kipindi cha kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023, bahati mbaya sana Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba hakutoa maelezo yoyote juu ya hoja hii. Ninaomba kushauri tena kama ifuatavyo; kwanza, Waziri wa Fedha na Mipango atoe maelezo ya kina kuhusu ziada ya mikopo ya Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, CAG afanye ukaguzi maalum wa deni la Serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 ili kuweka uwazi na kuondoa mkanganyiko kwa Watanzania kuhusu hali ya deni la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu mikopo iliyochukuliwa na Serikali izingatie uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kung’ang’ana na vigezo vya kimataifa ambavyo vinaweka rehani mustakabali wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo; hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango ukurasa wa 28 kipengele cha 35 ameainisha kuwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unatarajiwa kutekelezwa kwa kushirikisha sekta binafsi, lakini pia hotuba ya Kamati ya Bunge ya Bajeti ukurasa wa 13 kipengele 3.1.4.1 (c) naomba kunukuu; ”Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Serikali kutafuta njia nzuri ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo itazingatia manufaa mapana ya Taifa kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo ili kutekeleza mradi huo.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri huo wa Kamati ya Bajeti yapo maswali mengi ya kujiuliza kabla ya kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; kama Taifa tumeshafanya tathmini ya kina na kujiridhisha kuwa mradi wa Bandari ya Bagamoyo unaweza kutekelezwa kwa njia ya ubia na bila kuathiri uchumi wa ustawi wa nchi yetu, tutawezaje kulinda mifumo ya kiusalama ya nchi, mwekezaji binafsi anaweza kuamua kupandisha gharama za usafirishaji na uchukuzi wa mizigo bandarini wakati wowote tutawezaje kudhibiti mfumuko wa bei, tutawezaje kuwalinda wafanyabiasha na wawekezaji wetu wa ndani, tutawezaje kudhibiti mifumo ya ukusanyaji wa mapato nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili; Taifa hivi sasa tuna miradi mikubwa ya kimkakati ambayo iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na yenye mahitaji makubwa ya fedha, miradi hiyo ni pamoja na Reli ya SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bwawa la Kidunda, ujenzi na ufufuaji wa meli, uboreshaji wa bandari zilizopo, ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, ununuzi wa ndege mpya na kadhalika. Je, kama Taifa tunao uwezo wa kiuchumi na kimapato kwa sasa kuweza kubeba gharama za mradi mpya wa Bandari ya Bagamoyo wakati tuna miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea maeneo mbalimbali nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; tumejiandaaje kulinda haki za Watanzania katika mkataba huo kwani uzoefu unaonesha mikataba mingi ya ubia tuliyoingia kama Taifa ni ya upigaji na mifano dhahiri ipo na wote tunakumbuka kama Symbion, Richmond, IPTL, TRL, City Water, Aggreko na kadhalika, mikataba ambayo imelitia hasara kubwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne; Kamati ya Bajeti imeonesha mashaka yake kwa chanzo cha fedha kilichopendekezwa na Serikali cha ubia na ndio maana ikashauri itafutwe njia nzuri ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ambayo itazingatia manufaa mapana ya Taifa kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu mimi Mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni mradi mzuri na una manufaa makubwa kwa Taifa letu, lakini tujipe muda kukamilisha miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa maeneo mbalimbali nchini na pia kujipa nafasi ya kutafuta fedha za kugharamia mradi huo bila kuathiri uchumi na ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP – MW 2,115); kuhusu utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP – MW 2,115) kama ilivyotolewa taarifa kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2023/2024 kipengele (b) ukurasa wa 19 na Taarifa ya Kamati ya Bajeti kipengele 3.1.3.1 ukurasa wa 9 na 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikushauri hapa Bungeni kuunda Kamati Teule ya Bunge na nikasema utanishukuru. Leo hii unashuhudia mkanganyiko mkubwa uliobainishwa na Kamati yako ya Bajeti ambayo imeshindwa kupata taarifa za uhakika juu ya kinachoendelea katika utekelezaji wa bwawa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Arab Contractors ya Misri umeongezwa na Serikali bila sababu za msingi, bila kufanya tathmini na bila kubainisha gharama za ongezeko la muda wa mkataba (variations cost) zitabebwa na nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, muda ulioongezwa katika mkataba baina ya TANESCO na Mkandarasi Arab Contractors haujulikani hadi sasa kwamba ni miezi 12 au miezi 24, TANESCO inaonesha kwamba mkandarasi ameongezewa muda wa miezi 12 yaani hadi tarehe 15 Juni, 2023 lakini mkandarasi na Wizara ya Nishati wanasema muda ulioongezwa ni miezi 24 hadi Julai, 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, huku tunaelezwa mradi umefikia 75% ya utekelezaji, lakini mkandarasi ameongezewa muda mrefu wa miaka miwili kumalizia mradi ulibakiza 25% tu ya utekelezaji hali inayoleta mashaka makubwa juu ya ukweli wa hatua za utekelezaji zinazowasilishwa na Serikali Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, mara tunaletewa maelezo hapa Bungeni kuwa TANESCO na mkandarasi wanavutana bila Bunge kuelezwa wanabishania nini. Ni hatari sana kuingia kwenye mabishano huku mradi ukiwa umefikia 75% ya utekelezaji na malipo yakiwa yamefanyika zaidi ya 70%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, sababu hazitolewi za kwa nini malipo halali ya kimkataba ya CSR kiasi cha shilingi bilioni 260 haijatolewa licha ya Serikali kuendelea kufanya malipo kwa mkandarasi yaliyofikia zaidi ya 70% ya madai yote ya mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Kampuni ya Arab Contranctors inapaswa kulipa gharama za ucheleweshaji wa mradi (variations cost) kwa muda wa miaka miwili kiasi
cha shilingi trilioni 1.3 kwa mujibu wa mkataba ambayo ni 10% ya gharama za mradi kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti,si Wizara ya Nishati wala TANESCO iliyodai fedha hizo kwa mkandarasi ambaye hivi sasa ameshalipwa madai yake kwa zaidi ya 70%. Kwa nini Serikali iendelee kumlipa mkandarasi bila kukata fedha za CSR na faini ya ucheleweshaji? Madai haya ni haki ya Watanzania kwa mujibu wa mkataba na sio hisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchelewa kwa mradi huu wa Bwawa la Julius Nyerere kumeliingiza Taifa kwenye hasara kubwa ikiwemo kuwepo migao na katakata ya umeme isiyoisha, migao ya maji, Mradi wa SGR kutokufanya kazi baada ya kukamilika, kukosa wawekezaji kutokana na nchi kutojitosheleza kwa umeme, hasara na ajira kuyeyuka kwa shughuli za uzalishaji zinazotegemea umeme, nchi kushindwa kuuza umeme nje ya nchi na Taifa kukosa mapato na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha Wizara ya Nishati kuendelea kuwasilisha taarifa zenye mkanganyiko Bungeni kuhusu utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, kuongeza muda wa mkataba kiholela na kushindwa kudai madai halali ya kimkataba ya shilingi trilioni 1.56 yanaleta mashaka makubwa na kuashiria kuwepo kwa mianya ya rushwa, uwezo mdogo wa Wizara ya Nishati kusimamia utekelezaji wa mkataba na ni dharau kubwa kwa Bunge lako tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka mwanzo nilishauri kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ili kuchunguza ukweli wa jambo hili na leo ninashauri mambo mawili yafanyike ili kuunusuru Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere na kuepuka hasara inayoweza kutokea mbeleni ya kupoteza matrilioni ya fedha za Watanzania na mradi kuishia njiani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, iundwe Kamati Teule ya Bunge kubaini ukweli na chanzo cha mkanganyiko wa taarifa zinazotolewa na Wizara ya Nishati na kupendekeza hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Bunge liiagize Wizara ya Nishati na TANESCO kukata fedha zote za CSR na gharama za ucheleweshaji wa mradi kwa Kampuni ya Arab Contractors kiasi cha shilingi trilioni 1.56 katika malipo yatakayoendelea kutolewa kuanzia sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maeneo ya kupewa kipaumbele; Serikali imeweka vipaumbele vingi ambavyo ni ngumu kuvitekeleza kwa ufanisi na ikumbukwe kuwa kupanga ni kuchagua. Ni vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ukafanyika kwa awamu kulingana na uwezo wa rasilimali zilizopo. Nimepitia maeneo mbalimbali ya mapendekezo ya mpango na naomba kushauri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naipongeza Serikali kwa hatua ya kupata mkandarasi na kusaini mkataba wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda hali itakayopelekea kumaliza tatizo la maji la muda mrefu linaloikabili Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu, Serikali itekeleze kwa vitendo mradi ulioahidiwa kwa muda mrefu wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Mkoa wa Simiyu ambao maji yatasambazwa katika Wilaya za Busega, Bariadi, Itilima, Meatu na Maswa. Wananchi wa Jimbo langu la Kisesa wanausubiri mradi huu kwa hamu kubwa ili kutatua matatizo ya maji ya kunywa, kilimo, mifugo na shughuli nyingine za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwenye mipango ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji, msitusahau wakulima wa Jimbo la Kisesa na Mkoa mzima wa Simiyu kwa kuwa tunayo maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mpunga, pamba, mahindi, mbogamboga na kadhalika na Serikali itenge fedha za kutosha katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Serikali itenge fedha za kutosha kuwezesha utafiti kufanyika nchini katika taasisi zake za kama COSTECH, TARI, TALIRI, TAFIRI, TAWIRI na kadhalika ili kuwezesha kupata taarifa muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ujenzi wa madaraja ya Mwamhuge katika Mto Sanga (mpakani mwa Meatu na Maswa), ujenzi wa daraja la Sanjo (mpakani mwa Meatu na Itilima), ujenzi wa Daraja la Mwabuzo (linalounganisha Meatu, Kishapu na Igunga) pamoja na maombi haya naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TARURA na TANROADS kwa utekelezaji mzuri wa ujenzi wa barabara na madaraja jimboni kwangu Kisesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu; uUjenzi wa zahanati kila kijiji na ununuzi wa vifaa muhimu vya kitabibu, madaktari na wauguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, Serikali itenge fedha za kutosha kwa uboreshaji wa bandari zote katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutafuta masoko ya mazao nje ya nchi hongera sana. Tumeshuhudia mkiwezesha kupata masoko makubwa ya mazao kama korosho, soya, parachichi, pamba, choroko, dengu, mabondo, samaki, nyama na mazao ya mbogamboga, lakini kupata masoko ya nje ni suala moja na kumudu mahitaji ya soko ni kitu kingine. Kama Taifa tunapaswa kuwekeza vya kutosha katika kuhudumia masoko ya kimataifa ili kuhakikisha tunazalisha kwa wingi na kwa viwango vinavyohitajika na masoko husika. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuiunganisha Tanzania na dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikishwaji wa Watanzania na upatikanji wa ajira; mpango lazima uzingatie ushirikishwaji wa Watanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini, lakini yapo mambo yanayoendelea ambayo yanakinzana na hii dhamira njema ya Serikali, mifano; moja, wafugaji wa mifugo ya asili wa kijiji cha Ilunde B, Kibondo Mkoani Kigoma kila leo wanafukuzwa kwenye maeneo yao ikidaiwa kuwa ni eneo la Hifadhi la Pori la Akiba la Kigosi Muyowosi. Wananchi hawa wameiomba Serikali kufika na kuhakiki mipaka ili kubaini ukweli bila mafanikio badala yake operation za kuwafukuza zinaendelea kila uchao kufukuzwa, kuchomewa moto makazi, kutaifishwa mifugo, kupigwa faini na kupigwa na kuumizwa kinyume na haki na misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kusitisha operation zinazoendelea katika Kijiji cha Ilunde B, Wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma na badala yake ufanyike uhakiki wa mipaka ambao utashirikisha wananchi wote na Serikali ya eneo husika ili kuondoa utata wa mipaka uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wananchi wa vijiji 33 vya Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kufukuzwa kwenye maeneo ya makazi na kilimo kwa kisingizio kwamba wako ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula amepiga marufuku shughuli za kilimo kuendelea katika maeneo hayo ambayo kwa muda mrefu wamekuwa wakiyatumia kwa shughuli za kilimo cha mpunga ambapo mchele huo umekuwa ukiuzwa ndani na nchi jirani za Uganda, Malawi, DRC, Zambia, Visiwa vya Komoro, Sudani Kusini, Kenya na Rwanda ambapo linapunguza tatizo la upungufu wa chakula nchini, kuingiza kipato kwa wananchi na kupata fedha nyingi za kigeni kutokana na mauzo ya mchele nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu wameiomba Serikali kufika eneo hilo ili kupitia na kuhakiki mipaka baina yao na hifadhi lakini badala yake limetolewa tamko la kuondolewa bila kusikilizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya Waziri ambayo yanalenga GN No. 28 inayolalamikiwa na wananchi kila sehemu ambapo imetanua mpaka bila ushirikishwaji wa wananchi na kwa sehemu kubwa haina uhalisia kwa kuwa ramani haijafanyiwa uhakiki wa mipaka na kutoa tafsiri ya ramani chini ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wananchi hawa waachwe waendelee na shughuli zao za kilimo na Serikali iende ikakae na wananchi hao ili kufanya uhakiki wa mipaka na pande zote kujiridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, TANESCO kuingia mkataba na kampuni binafsi ya kutoa huduma ya kuendesha kituo cha huduma kwa wateja (callcenter) ambapo TANESCO ina otusource uendeshaji wa kituo chake cha huduma kwa wateja kwa kampuni binafsi kazi iliyokuwa ikifanywa na vijana wa Kitanzania 279 waliokuwa na mkataba na TANESCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za kukasimu shughuli za uendeshaji wa kituo cha huduma kwa wateja kwa kampuni binafsi hazijawekwa wazi. Vijana 279 wanaachishwa kazi kumpisha mtu binafsi kuendesha huduma hiyo, haya ni mawasiliano nyeti yanayofanywa na wateja kupitia callcenter ya TANESCO inakuwaje yaendeshwe na mtu binafsi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu TANESCO isitishe uamuzi wake wa kubinafsisha vituo vya kutoa huduma kwa wateja (callcenter) na badala yake iimarishe kitengo hicho na kiendelee kuendeshwa na shirika hilo huku ajira za vijana 279 zikilindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, wafugaji walioshinda kesi Mahakamani zaidi ya ng’ombe 6,000 lakini Serikali imekaidi kurejesha mifugo yao, licha ya wananchi hawa kushinda kesi Mahakamani miaka zaidi ya mitatu iliyopita mifugo yao haijarejeshwa na Serikali hali inayopelekea familia hizo kuingia kwenye lindi kubwa la umasikini. Sababu za kutorejesha mifugo hiyo hazitolewi na hili sio jambo zuri kwa nchi inayofuata misingi ya sheria ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iwarudishie wananchi mifugo yao au kiasi cha fedha kinacholingana na thamani ya mifugo iliyoshikiliwa kama Mahakama zilivyoamua. Nawasilisha.