Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Salim Alaudin Hasham

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye mpango huu wa bajeti. Pia namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kufika hapa siku ya leo. Pia nisiwe mchoyo wa fadhila, bila kumshukuru Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuhakikisha anaiendesha nchi hii katika usawa na utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kama matatu ya kuchangia kwenye Bajeti. La kwanza nitagusa kwenye mambo ya barabara. Kwanza niwapongeze Wizara zote kwa kazi nzuri wanazozifanya. Pia nawapongeza Wizara ya Ujenzi inavyopambana, tumeona miradi mingi ambayo inatekelezwa, miradi ambayo imekamilika, lakini hatuwezi kurudi nyuma maana miundombinu ya barabara ndiyo chachu ya maendeleo ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana niliuliza swali hapa Bungeni kuhusu barabara zetu hasa kwenye Jimbo langu la Ulanga. Majibu ya Mheshimiwa Waziri yalikuwa ni mepesi, lakini sijui ni kwa sababu gani? Kikubwa, ninapozungumzia barabara ya kutoka Kilombero kwenda Ulanga ya kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa 67 ilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015, lakini iliingia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020. Bajeti zote; mwaka 2020/2021, 2021/2022 na 2022/2023 tumekosekana. Tuna imani labda bajeti ijayo tunaweza tukaingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu ya msingi kuombea barabara ile. Jimbo la Ulanga sasa hivi ni kitovu cha madini na pia ndiyo Mkoa wa Madini ambao Mheshimiwa Dotto alikuja kuufungua juzi. Tuna miradi mikubwa sana ambayo inakwenda kufanyika kwenye jimbo lile. Wawekezaji wanaenda kuweka zaidi ya Dola milioni 200. Sasa hivi wako kwenye mchakato wa kulipa fidia kwa wanakijiji ili kuweza kupisha miradi ile. Barabara zetu sasa hivi tunapitisha Noah tu; na gari kubwa inayopita ni Fuso, lakini ikinyesha mvua network inakatika kwa maana hiyo barabara haipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshajiuliza hivi hawa wawekezaji tusipowawekea mazingira mazuri, kesho wakianza kukafanya mobilization: Je, watawezaje kufanya kazi yao na biashara yao inafanyika masika na kiangazi? Inamaanisha adha kubwa itaenda kuwakuta wananchi wa Jimbo la Ulanga, na pia wawekezaji wale watakuwa kwenye wakati mgumu sana wa kufanya kazi yao. Hiyo ni kampuni moja nimezungumzia, Jimbo la Ulanga tunaenda kufanya makubaliano na kampuni nyingine mbili ambazo zinaenda kuchimba madini ya Kinywe. Madini haya yanaenda kubebwa kwenye magari makubwa. Barabara ile haitaweza kukidhi na kuwasaidia wawekezaji hawa kuweza kufanya kazi zao kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninapozungumza, nipo hapa na ndugu yangu Mheshimiwa Taletale anakuja, ametoka kunilalamikia suala la barabara. Nikamwambia mimi sio Waziri, Mheshimiwa Taletale, ongea na Mheshimiwa Waziri, mimi mwenyewe nina majanga yangu kibao jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu Mawaziri hawa wanatakiwa watupe kipaumbele sana. Sijui kama kuna mawasiliano katika hizi Wizara. Mheshimiwa Dotto ameshamaliza kazi yake kwenye upande wa madini, kwamba watu wanaenda kufanya kazi zao. Kungekuwa na mawasiliano basi, kwamba jamani, tumeshamalizana na hawa watu wanakuja kuwekeza, waende kwa Waziri wa Ujenzi, jamani, barabara zetu zikoje? Zinaweza kukidhi mahitaji ya wawekezaji? Au hospitali, kwamba watu wanakuja kuajiriwa zaidi ya 1,000, je, hospitali zetu zinakidhi mahitaji ya watu na kuwekeza? Siyo mradi mdogo, watu wanakwenda kuwekeza zaidi ya Dola milioni 200 halafu hamna barabara, hakuna hospitali za maana, tutaenda kuchekesha, na hata hao wawekezaji watatuona hatuko serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nirudi kwenye Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia. Ndugu yangu Mheshimiwa Francis hapa amesema, nami ilikuwa katika mpango wangu wa kuchangia leo; unamwambiaje mwananchi huyu? Kwanza unamwambia akinunua kifurushi cha siku, kwa wiki atatumia shilingi 10,000; akinunua cha wiki atatumia shilingi 5,000. Maana yake huyu mtu umemhamasisha kwamba anunue kifurushi cha wiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yetu coverage network yake ni mbaya, vijiji vingi havina network na maeneo mengi hayana network. Mkulima amejiunga kifurushi chake cha shilingi 5,000, ameenda zake shambani, baada ya siku nne anakuja mjini anaambiwa kifurushi chake kimeisha. Kifurushi chake kimeenda wapi? Hela yangu nani amekula? Tusijibizane majibu rahisi rahisi, ni lazima watu tujue kwamba hii ni dalili ya wizi watu wanaibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumlazimisha mtu anunue kifurushi cha shilingi 35,000 anatumia wiki mbili, wiki mbili nyingine unamwambia kifurushi chako kimeisha, mimi sioni kama ni sahihi na Waziri yuko hapa anatusikiliza. Tuna jambo la kufanya kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia sekunde thelathini.

MWENYEKITI: Hizo ni za mwenzio. Haya, malizia.

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye mawasiliano na teknolojia, tuone sababu za msingi za kufunga kamera kwenye miji yetu mikubwa kwa ajili ya Security. Wenzetu Kenya wameshafunga kamera miaka saba iliyopita, sisi population inaongezeka, uhalifu unaongezeka, tunawatuma askari wanaenda porini hawajui hata mhalifu yuko wapi? Hili ni jambo la msingi sana, miji yetu mikubwa ikafungwe kamera kwa ajili ya security. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)