Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama ramani utaona nchi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nzuri kuliko zote duniani ni Tanzania; na si kwamba, ni Tanzania tu ambayo imejaliwa, Tanzania hiyo ni Tanzania ambayo inatoa mwanamke bora sana duniani anaitwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu...

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Nani, Mheshimiwa Jumbe kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamisi Taletale.

T A A R I F A

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, alipoimba nilikuwa nataka kuingia chini ya meza. Kwa hiyo, nimuombe asirudie tena kuimba nyimbo nzuri akiwa anatutisha, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa…

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa hiyo kwa sababu yeye ni talented sina haja ya kumbishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu kusisitiza kwamba, Tanzania hii ni nchi ambayo imebarikiwa sana. Inatoa mwanamke bora kabisa ambaye anaitwa Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Rais wa nchi hii. Ni nchi hii duniani ambayo inatoa Spika bora kabisa, a super woman, anaitwa Tulia Ackson. Ni nchi hii inatoa Mawaziri bora kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka tu niseme katika hali ya nchi kama hii ni lazima tufike wakati tujue kwamba, sisi tunaangaliwa na dunia nzima. Na tunapoangaliwa na dunia nzima ni lazima tuwe tunakubaliana kwamba, tumekuja hapa Bungeni kwa ajili ya hoja na si kutakiana ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hili kwa masikitiko makubwa. Jana mchangiaji Mheshimiwa Festo Sanga amechangia vizuri sana kuhusu suala la kuwatetea wananchi juu ya mambo ambayo yanaendelea Mbarali lakini matokeo yake imeonekana yeye hayupo kwa ajili ya kutetea wananchi bali ana maslahi yake. Sisi hapa tumekuja kwa ajili ya kuwatetea wananchi, hatujaja kwa ajili ya kufurahisha watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ameongea hapa Mheshimiwa Saashisha kuhusiana na suala la kutokutumia wataalam vizuri, tunatafutiana ajira. Nina mfano mmoja mzuri naomba niuweke hapa. Pale Bandari ya Tanga tulipokuwa tunasomewa taarifa hapa kulionekana kulikuwa kuna baadhi ya vitu ambavyo hazikuwa sawa. Aliyeibua mambo hayo nataka nikwambie, yupo mfanyakazi aliibua mambo hayo mpaka sasahivi hayupo kazini, alifukuzwa na hakuna mtu anayetaka kumjadili wala kuona kwamba anafaa kuendeleza bandari n ani mtaalam. Kuna jamaa mmoja anaitwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kumtaja jina kwa sababu, namfahamu na yeye ndiye aliyeibua uozo, walipoona anaibua uozo huo wamemfukuza kazi. Ninaomba wanaohusika wawatafute hao watu watatusaidia kwa mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongelea mambo ya kuanzisha Bandari ya Bagamoyo. Hivi bandari tulizonazo tumezitumia kwa uhakika?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA
UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Mlagila Jumbe kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali yetu inathamini sana misingi ya utawala bora, na kwa kuwa Serikali yetu imejipambanua kuhakikisha wkamba, inapambana na rushwa na inasimamia haki kwa watumishi wote wa umma ambao wamekuwa ni chanzo cha utendaji kazi bora, matumizi bora ya fedha na suala zima la maadili katika utendaji wa kila siku wa wawatumishi; kwa hiyo, kwa kuwa Serikali imejipambanua hivyo ninaomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge tuko tayari kumfahamu mtumishi huyo na kufuatilia kama iko misingi ya utawala bora imevunjwa kwa uadilifu na utendaji kazi uliotukuka kwa mtumishi huyo, Serikali itachukua hatua zaidi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe unapokea Taarifa hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri?

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Bagamoyo tunaisema sana hapa. Je, hivi Bandari ya Tanga tayari tumeshamaliza kazi zote zilizotakiwa pale, ili iweze kupokea mzigo? Ni kweli Bandari ya Dar es Salaam inafika wakati inaelemewa. Je, Bandari ya Mtwara ambayo ina kina ambacho ni natural, ambayo iko vizuri, Je, tumeitumia ipasavyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba Bandari ya Bagamoyo tusiiseme kama bandari. Tukisema industrial park itakuwa ni nzuri zaidi, lakini tukisema juu ya bandari ninaomba bandari tulizonazo tuweze kuzitumia ipasavyo, ili...

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jumbe inaonekana watu wameupenda sana uchangiaji wako. Kuna Taarifa kutika kwa Mheshimiwa Soud.

T A A R I F A

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba tu kumpa Taarifa mchangiaji kwamba, wakati tukiongelea kuhusu networking ya bandari, basi pia tuiweke pia Bandari ya Zanzibar umuhimu wake kwa sababu nayo pia ni sehemu ya nchi ya Tanzania. Na huduma itakapotoa itatoa kwa ajili ya nchi nzima. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Sawa. Mchangiaji anaweza akaweka huo mchango, lakini tusije tukachanganya mambo, tukaanza mambo ya muungano hapa halafu tukawa tumezalisha jambo lingine zito.

Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe.

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bandari ninaomba likae hivyo, lakini naomba nijielekeze pia kwenye barabara na mchango ambao tunachukua kwenye mafuta wa road toll. Tunakoelekea sasahivi ni kwamba tunaenda kwenye magari nyanayotumia gesi; na hapa yupo Dangote anatumia gesi. Tunakoelekea itatokea wakati huo mfuko ambayo tunatoa kwenye mafuta tutashindwa kuufikisha na utashindwa kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wataalamu watusaidie, nchi zote sasa hivi zimeacha ku-charge kwenye mafuta, tutumie teknolojia, tuangalie ni namna ambavyo tunaweza tukapata hiyo kodi kwenye magari baada ya kwenye mafuta. Kwa mfano, kuna Road Toll; tunao uwezo wa kutumia teknolojia, Wajerumani wame- advance sana, wana kitu kinaitwa MOT, gari linahesabika kwa jinsi linavyotembea barabarani ndivyo linavyolipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mkulima ambaye analima kwa trekta, anatembea shambani, diesel anayonunua analipa Road Toll, mchenjuaji ambaye yuko kule porini anatumia diesel kuendesha mtambo wake, analipa Road Toll kwa kununua mafuta. Hii siyo haki. Hebu tutafute njia sahihi ambayo itahakikisha kila mmoja analipa kwa haki. Gari lililobeba mafuta, limelipa Road Toll, halafu mtu anayeenda kutumia shambani, analipa Road Toll. Hata kuendeleza kilimo inakuwa ni shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, hebu tukae na wataalam wanaotakiwa, ambao wanaweza wakafanya haya mambo vizuri, watuhakikishie na watuongoze. Sasa hivi zipo taxi pale mjini, zote zimehamia kwenye gesi, hazilipi. Hakuna anayelipa tena mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba hebu tunapozungumza mipango hii twende kwenye irrigation. Tuna irrigation ambazo ni muhimu sana; kuna irrigation ambayo iko sehemu ya pale Malawi na Tanzania ambayo inasisitizwa lakini leo sioni Mpango ukiongelea hiyo, ambayo ni Songwe River Basin.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Haya, ahsante sana.

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)