Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Mapendekezo ya Mapendekezo ya Mpango ulioletwa hapa mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nami nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa maandalizi mazuri yaliyoanza na uwasilishwaji wake mzuri. Ila naomba nirejee jambo ambalo nimewahi kusema humu ndani. Sioni tuna shida gani ya kukubali kupokea ushauri mpya. Mipango hii tunayoendelea nayo na utaratibu tunaoutumia wa kuandaa kwa kipindi cha miaka mitano, tunaandaa mwaka mmoja mmoja, hatuwezi kufikiria kusogea mbele zaidi? Nilishauri hapa tuwe na mipango ya miaka 50, itakuwa na tija ili vitu vyetu tunavyovipanga, vikamilike kwa ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa dhima yetu inayotuongoza inasema, kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya Taifa. Sasa kama tunazungumza viwanda, hii ni process ya muda mrefu. Naomba Waziri anapokuja, hizi dhima zilizopita huko nyuma, angalau arejee basi kutupa tathmini, walifikia malengo kwa kiwango gani? Ili michango hii tunayoitoa hapa, iwe na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalisema kwa utangulizi tu. Tunapotoa mawazo hapa, wakubali kupokea vitu vipya; na hili litatuondoa kwenye hii hali ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea. Wakiambiwa nendeni mkaandae mpango, wanarudi kwenye laptop zao, wanabadilisha mwaka na figure pale, wanatuletea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Mheshimiwa Waziri, hebu wakati unapokuja mwaka mwingine, fikirieni namna ya kutuletea mpango wa kutumia watu wetu wenye akili. Mindset za watu tuone, wote tuna akili ndiyo, lakini wapo watu wenye uwezo mkubwa kuliko sisi. Hata huko kwenye Wizara zenu mna watu ambao wana uwezo mkubwa lakini bahati mbaya hatuwatumii kwa sababu hatuna mpango wa kuwatumia hawa watu. Sasa shida tuliyokuwa nayo ndiyo hii tunayokutana na watu ambao kazi yao ni kujaza maboma, yaani yuko pale Wizarani, anatuma taarifa ana-edit, anatuletea. Tuwape watu uwezo wa kufikiri waje na vitu vipya, kama hivi ambavyo nasema tuwe na mipango ambayo itatekelezwa kwa kipindi cha miaka 50, miaka100 na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa namna ambavyo kwa kweli Wizara ya Kilimo imepokea mawazo yetu na imeanza kufanya kazi. Nimefurahi kuona kwenye mpango huu tumeanza mashamba maalum kwa ajili ya kulima mbegu zetu, nipongeze sana. Nimpongeze pia Waziri wa Kilimo, kwa kweli kwa hili anatupa heshima sana. Wametenga hekta 853 na mchakato uko kwenye tathmini. Sasa nikawa najiuliza, ina maana tangu tumepata uhuru ndio tunaanza kutengeneza mashamba yetu ya mbegu? Basi kwa kuwa tumeanza, niombe sana Mheshimiwa Waziri kwa kweli aongeze speed ili tuwe na mbegu sahihi za kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishauri Bunge lililopita kwamba, hili suala la mbegu lichukuliwe kama suala la

kiusalama kwa sababu, bila mbegu sahihi hatuwezi kufanya kilimo kilicho sahihi na bila kilimo hatuwezi kuongeza uchumi wetu, kwa sababu unapoongeza uzalishaji ndio unakuza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kimenishangaza ni kwamba wameanzisha mashamba hizi block farming hapa Dodoma, lakini wameweka changamoto kwamba mashamba yametengwa lakini hakuna maji. Sasa niombe Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze kwamba katika hayo mashamba kuna maji ya uhakika, tuweze kupata kauli yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo pia wamefanya vizuri na ningependa kuchangia. Kwenye umwagiliaji wametenga fedha na kule Hai tunashukuru tumepata miradi mingi ya umwagiliaji. Sasa naendelea kumwomba Mheshimiwa Waziri atazame na pale Metrom tukipata ile tutafanya kazi kubwa sana ya kuinua uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni sambamba na masoko, tumeshaanza vizuri sana kuimarisha kilimo na tumewekeza huko. Hali ya masoko ikoje? sisi pale Hai na soko la Kwa Sadala limeshakuwa sasa ni kila siku nazungumza. Soko hili la Kwa sadala jamani sio tu la Hai, hili litahudumia kanda yote ya kaskazini na ni kama soko la kimataifa. Nilisema hapa ramani tuliyotengeneza siyo ya kawaida tumeweka vitu vingi humo ndani, kuna sorting industry, humo ndani kuna grading, kuna kufungasha. Hebu watutengenezee hela watuletee ili soko lile liweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri uwanja wa ndege ule wameshaukubali uwe wa kimkakati wa kilimo. Wameshatuletea fedha za kujenga common use facility pale. Kwa hiyo hili soko likijengwa litatusaidia sana kwenda sambamba na hiki ambacho tunakifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja kabla muda haujaisha. Sisi Mlima Kilimanjaro pale ni chanzo cha mapato. Mapato yale yanakusanywa kupitia Serikali Kuu lakini sisi tulioko pale, kama ilivyo maeneo mengine, watu walioko migodini humo wanakusanya service levy, lakini sisi pale hatupati. Niombe sana kwenye eneo hili la mipango Waziri atakapokuja hapa atuambie, kama ambavyo maeneo mengine wananufaika na sisi tunataka tupate walau service levy kutokana na Mlima Kilimanjaro. Hili naomba sana sana Mheshimiwa Waziri atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo natamani niseme hapa ni kuhusiana na NIDA. Kwenye taarifa NIDA ili waweze kutoa vitambulisho vya utaifa kwa wananchi wetu, wanahitaji bilioni 42.5 ambayo haijapelekwa. Sasa hapa tunapanga mipango mingi na tunatoa maelekezo mengi, mpaka tumesema ile asilimia 10 inayoenda kukopwa na vikundi, wale wanaoingia wanatakiwa wawe na NIDA. Sasa najiuliza, kama hawa hawana fedha hizi za kuweza kutengeneza vitambulisho, hali itakuwaje kwa wale wanaoenda kukopa? Hiki ni kikwazo. Kwa hiyo niombe sana hizi fedha zitafutwe na NIDA wapewe ili Watanzania wote waweze kuwa na vitambulisho vya Utaifa na waweze kupata huduma kama ambavyo tumezungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linafanana na hili ambalo nilikuwa nazungumza hapa, ni la kuanzisha Tume ya Mipango ya Taifa. Tunapozungumza hapa naona Wabunge wengi wamechangia, tuanze taasisi hii lakini kuwe na watu wenye uwezo, hili ni muhimu sana. Tumekuwa na mazoea tunaanzisha taasisi tunapeana, hapa twende na watu wenye uwezo ili watusaidie yaani kwa maana wenye akili sio tu wenye vyeo ndio namaanisha namna hiyo. Kwa sababu wengi kwenye utumishi wamo lakini wenye akili hawapati nafasi. Shida kwenye taasisi hizi mtu mwenye uwezo anafichwa chini chini. Ninyi ni mashahidi angalieni hata kwenye…

MHE. JANEJELLY J. NTANTE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. JANEJELLY J. NTANTE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba Serikali haiajiri watu wasiyo na akili. Watumishi wote wa Serikali wana akili sawasawa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, unapokea taarifa hiyo?

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya mama yangu, wala sina tatizo. Ninachokisema mimi, wote tuna akili siyo tu watumishi wa umma hata sisi wote tuna akili ila tupishana uwezo, ndio ninachokisema. Sasa wale wenye uwezo wapewe nafasi ya kutumika na ukitaka hapa Mawaziri hapa waite Wakurugenzi wao, Wakuu wa Idara, wawanyanganye simu, halafu wawape laptop mpya, waqambie tutengeneze mpango waone tutakachokipata. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wako kule wadogo ambao hawaonekani kwenye vyeo vyao, ndio wanaofanya kazi, hawa wana vyeo ndio, lakini uwezo wa kueleza humu hawana. Si huwa wanaingia kwenye Kamati, unauliza swali anauliza dogo unasemaje? Ndio anatoa majibu. Sasa tuwape madogo wakalie viti wafanye kazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)