Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Bakar Hamad Bakar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa zawadi ya uhai na uzima na kuweza kuniwezesha kusimama katika Bunge lako tukufu asubuhi hii. Pia, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii, lakini pia nikupongeze kwa namna ambavyo unaendelea kuliheshimisha Bunge letu ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kupambana na kutatua changamoto za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza hivi hali ingekuwaje kama Mama Samia asingekubali kuweka na kutoa zile bilioni 100 kila mwezi ambazo zinaenda kutatua na kupunguza changamoto ya mafuta. Najiuliza ingekuwaje kwa wakulima wetu kama Mama Samia asingekubali kuzitoa zile bilioni 150 kwa ajili ya kupunguza changamoto ya bei ya mbolea na bei ya mbegu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia huwa najiuliza, hivi bei ya unga na mafuta ya kula ingekuwaje kama kodi za bidhaa hizi pamoja na tozo zisingeweza kuondolewa na kuweza kuwawezesha wananchi kuweza kupata bei nafuu angalau kutokana na uchumi ambao kwa sasa hivi unaendelea duniani. Baada ya kujiuliza haya yote, niwaombe sana Watanzania tuendelee kumuunga Mama Samia mkono, tuendelee kumuombea dua ili aweze kuyatekeleza haya ambayo yanapangwa kwa umakini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango huu ambao tunaenda kuujadili pamoja na bajeti ya mwaka 2023/2024, mimi nitatoa mapendekezo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa kwamba kuna mwenendo wa sekta za kibenki, kwamba benki sasa hivi zimeanza kupata faida kubwa kupitia return on equity pamoja na return on asset. Hatuwezi kujisifia kwa kuwapa benki hizi kupata faida pekee yao. Kwa sababu ndani ya benki hizi zisingekuwepo kama si wawekezaji. Bado interval na difference kubwa ipo kwenye wawekezaji pamoja na benki hizi. Watu ambao wanawekeza fedha zao, fedha wanayoipata kama faida ni ndogo kulinganisha na pesa wanayoipata benki kama faida. Bado interest cost ambayo waomba mikopo wanaichukua, wanaomba na kupewa ni interest kubwa sana hadi sasa hivi, lakini ukiangalia wale wanaowekeza fedha zao ile interest income wanayoipata ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa hali hii utakuta kwamba benki zinatengeneza faida kubwa lakini wale wanaowekeza bado pesa wanazozipata na income wanayoipata ni ndogo sana. Kwa hiyo, hatuwezi kujisifia kwa jambo hili. Mimi niombe muongozo wa mpango na tutakapokwenda kutengeneza mpango basi angalau sasa tushushe riba ya mikopo lakini pia tuongeze ile interest income ambayo inapatikana kwa wawekezaji wanaowekeza kwenye benki zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge la Bajeti nilichangia kuhusiana na kuwepo kwa Islamic banking bado naendelea. Kwenye muongozo huu wa mpango ambao tunaenda kuuandaa pamoja na bajeti inayokuja naendelea kulisisitiza jambo hili. Kwa sababu kipindi kile cha bajeti halikuweza kutekelezeka lakini naamini kwa sababu tunaenda kutengeneza mwongozo, tunaenda kutengeneza mpango wa bajeti lakini pia tunaenda kutayarisha bajeti ijayo, naamini jambo hili Mheshimiwa Waziri kutokana na umuhimu wake unaweza kulichukua na kuweza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametuambia hapa kwamba mikopo chechefu imetoka kuanzia asilimia 9.3 mpaka sasa hivi ni asilimia 7.8. Mimi nipongeze kwamba inapungua lakini bado hiki kiwango ni kikubwa na ni kikubwa kwa sababu ile ambayo mwanzo niliizungumza, kwamba riba ya mikopo ni kubwa sana, lakini Islamic banking ndiyo ambayo inaenda kutatua changamoto hizi. Mifumo hii ya Islamic banking ipo hapa nchini tangia 2008 lakini tangu kipindi chote hicho inatumika kienyeji. Bado hakuna sheria, bado hakuna miongozo, bado hakuna kanuni ambazo zinaiongoza na kuisimamia Islamic banking ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe sana Serikali, ilichukue jambo hili, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuweka kile kipengele kwenye ile financing act ya kuondoa VAT kwenye mikopo ya mrabaha ambayo ni Islamic product. Kuondoa kipengele kile kuanzia mwaka huu 2022 lakini bado tunatakiwa tuwe na sheria ambayo inaongoza namna bora ya kuendesha hizi huduma za mikopo ya kiisilamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichangie jambo moja, nakuomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana naunga mkono hoja.