Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia. Nami leo sitahangaika na mambo makubwa sana ya Kitaifa, bali nitaenda kwenye mambo ya kawaida ambayo yatatusaidia kusonga mbele kama jamii. Nakubali na naipongeza Serikali, na ninajua kinachoisukuma Serikali kwa sababu tunayo matatizo mengi, kwa hiyo, kila hatua inayofanyika ina ahueni upande fulani. Katika mpango, yale maeneo matano ya kujikita, kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na mwisho kabisa kuendeleza rasilimali watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa upana wake, huo ndiyo uhalisia wa yale ambayo tunayahitaji kama nchi. Tunachokikosa ndani, ni namna tunavyoweka vipaumbele. Hii nikawaida, ukiwa na matatizo mengi; kwa mfano, una njaa, wakati huo huo una kiu, wakati huo huo kichwa kinauma, wakati huo huo hujaoga, kila solution unaiona ni ya maana, lakini kuna solution ambayo ikija itasaidia hizo nyingine kuweza kushughulikiwa. Yaani kuna vile vipaumbele. Kuna mzungumzaji mmoja alisema tunakosa ufungamanishaji wa mipango ya Wizara moja na Wizara nyingine. Wengine wakaja mpaka na mpango wa kurudisha ile Big Result wengine wakasema tuwe na Tume ya Rais ya ufuatiliaji wa matokeo, lakini mimi naona haya yote ni mle mle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa namba 19 wa hotuba ya Waziri, ameongelea sekta binafsi ameweka na takwimu. Sote tunajua kwa hawa watu wote milioni 61 Serikali haijaajiri hata milioni moja. Kitu kinachoweza kuajiri watu wengi ni sekta binafsi. Sasa ni nini kifanyike kwenye sekta binafsi ili iajiri? (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, sasa kwenye sekta binafsi, ukiangalia leseni unazotakiwa kuwa nazo kufungua biashara, mfano biashara ya hoteli; kuna leseni sijui, kuna TALA kuna OSHA, kuna TRA hapo, kuna fire kuna NEMC, TFDA, TBS sijui huko halmashauri ukiacha leseni, kuna leseni za vileo, halafu zote unakuta mtu amezi-frame, ameziweka kwenye ukuta, hata nafasi ya kuweka decoration hakuna. Kwa nini usiwe na mfumo ambao unapoenda Manispaa, hivi vitu vingine vyote vimeunganishwa? Kwa hiyo, unalipia tu una-tick na inakuwa ndiyo precondition ya leseni kutoka badala ya kila mamlaka kujichukulia jinsi inavyotaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kubwa zaidi ni procedure ya kuzipata hizo leseni. Kwa mfano, NEMC yenyewe, process yake na gharama za ile Certificate ni shughuli hasa! Kuna baadhi ya Taasisi huelewi; wanakuja watu wa OSHA na Fire kwa pamoja, na wote wanaangalia mfumo wa umeme, wote wanaangalia uokozi kama ikitokea dharura, wote wanachukua hela na wote wanaongozwa na sheria tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, OSHA inatoa namna ya kupata leseni yao. Ukipata inasema, ulipe baada ya siku 30. Ila ukienda kwenye kanuni iliyotungwa na Waziri ni kwamba baada ya siku 30 kama hujalipa unachajiwa asilimia tano ya lile deni kila siku. Maana yake ni nini? Huyu mtu anayejipanga amechelewa kulipa unam-discourage kabisa hata kulipa, lakini je, hizi shughuli za OSHA zinafungamana moja kwa moja na uzalishaji wa hizi biashara tunazoziongelea, jibu ni hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha huu usumbufu kwenye biashara, ukienda kwenye Deni la Taifa ambalo tumeambiwa limefanyiwa auditing limeonekana tuna uwezo nalo, ni nini kinaelekeza Serikali ikope kiasi gani na kwa ajili gani? Hatuna, kwa sababu hatuna yale maeneo ambayo tumeyatenga. Kwa mfano, hivi kweli katika nchi hii ambayo tunataka wafanyabiashara, tunataka wawekezaji wa nje, bado maji ya kunywa ni shida kwa watu, maji ya kuoga ni shida kwa watu, bado umeme ni shida kwa watu huyu mwekezaji anakuja kufanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni nchi ambayo tuko katika Maziwa Makuu, tuna mito ya kutosha, tuna kila resource iliyoko karibu na sisi. Kwa nini hili Deni la Taifa tusiweke dheria ambayo inasema kwa miaka mitano mkopo wowote ambao tutachukua uelekezwe asilimia fulani kwenye maji na umeme kwa miaka mitano mpaka hilo tatizo liishe. Tujue kabisa kwamba umeme na maji sio tatizo tena kwetu ili tuwaite hao wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Ardhi, ni kweli tuna rasilimali nzuri sana ya Ardhi, nafikiri sisi tuko vizuri sana uki- compare na wenzetu wa Afrika Mashariki ukiacha Congo. Hata hivyo kwa jinsi tunavyotumia hii ardhi hatuna maeneo tuliyotenga kuendana na advantage za kijiografia kwa ajili ya matumizi fulani. Sehemu ya makazi iwe makazi, kilimo iwe kilimo, kila mahali wanafanya jinsi wanavyoona. Nitatoa Mfano Mkoa wa Kilimanjaro, eneo lililokuwa zuri zaidi kwa kulima kahawa ni kule chini pembezoni ya mlima lakini huko ndiko tumejenga zaidi. Eneo lile la tambarare ambalo hakuna mvua, hamna udongo wa volcanic tumepaacha ndiyo kwa ajili ya mashamba ambayo yatanyeshewa na nini? Kwa hiyo hakuna Mpango wa Serikali unaosema maeneo haya yatakuwa ni ya kilimo tu, maeneo haya yatakuwa ni ya kazi hii tu na mwisho wake tumebaki na EPZ zile ambazo tumeziweka kati kati ya miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna solution niliiongelea juzi, mikopo chechefu ndani ya nchi. Ile mikopo chechefu tunavyoiangalia sio kwa ajili tu ya zile biashara au zile benki kukosa hela, lakini inawapa watu umaskini. Mtu anakuwa na access ya kukopa kuliko uwezo wake wa kurudisha, maana yake ni kwamba atashindwa kui- manage ile hela, ataingia kwenye madeni, ndio unaona kila siku mikopo yetu hailipiki. Nilisema ni rahisi kuwa na system ambayo itai-connect TRA, mahesabu ya wafanyabiashara, lakini ita-connect NBAA kama Msimamizi Mkuu wa Mahesabu lakini na hizo benki, yaani kwamba ukiangalia tu mtu anataka kukopa bilioni moja, ukiangalia kodi zake anazolipa kwenye biashara zake ina- justify, ukiangalia mahesabu ambayo amepeleka NBAA yana-justify.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyo sasa hivi tunakuwa na vitabu vingi, yaani NBAA hao ambao ni certified account anatengeneza kitabu anaki-certify hicho ni kwa ajili ya TRA, anatengeneza kingine anaki-certify hicho ni kwa ajili ya benki na kingine hata ukitaka cha kwako cha nyumbani anakutengenezea. Sasa sio mfumo, hatuendeshi uchumi kwa namna inyotakiwa. Kwa hiyo nashauri sana hiyo mifumo iunganishwe ili iweze kuleta tija kwa hawa wafanyabiashara na hata hizo taasisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni huduma za uokozi, hii lazima tukubaliane. Ni kichocheo pia kwenye uchumi hasa kwa wawekezaji wa nje. Nakumbuka at one time Dubai waliendelea sana wakiwa na maghorofa makubwa, wakawa challenged na fire and rescue services waliyokuwa nayo. Hawakuwa na fire ambayo inaweza ikafika ghorofa ya 100 wakati wakiwa na hayo majengo. Sina hakika hata sasa hivi kama Dar es Salaam tuna gari la fire ambalo katika zile ghorofa tulizonazo pale, moto ukitokea juu kuna mechanism ya kuuuzima. Hiyo ni kichocheo cha namna ya kuwakaribisha wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda wangu umeisha, nakushukuru na naunga mkono hoja.