Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi. Vilevile nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi yake nzuri anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nachukua nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kumaliza uchaguzi wao kwa salama na amani na kuhakikisha CCM imeshinda kwa kishindo kikubwa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Ulinzi kwa hotuba yake nzuri na bajeti yake nzuri inayoashiria mafanikio makubwa sana, ahsante sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia na nitagusia kuhusu majengo ya makazi ya askari. Makazi ya askari imekuwa bado ni changamoto kubwa. Namwomba sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi aweze kujitahidi kufanya kazi yake kuhakikisha kwamba askari wetu wanapata makazi bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya kikosi hicho wamo mafundi wazuri sana wenye uwezo wa kufanya kazi zao kwa uhakika, wenye ujuzi mzuri katika Jeshi letu la Tanzania. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kutumia vijana hawa ili kuleta maendeleo ya nchi yetu hata yale majengo yanayojengwa na Jeshi letu la Kujenga Taifa, basi waweze kujenga mafundi hawa kutoka ndani ya Jeshi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie sasa suala la majengo. Nimefurahi sana kusoma katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri kuwa kuna majengo takribani 5,000 ambayo anaendelea kuyajenga. Basi naomba sana kila ukiendelea kuyajenga majengo hayo, basi aweze kuwatumia wanajeshi hao kuhakikisha kwamba tunapunguza matumizi makubwa kuliko kuwapa wakandarasi wa nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kusimamisha majengo hayo kwa upande wa Unguja, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie kwa upande wa Unguja, wanajeshi wetu kule Unguja wanahitaji majengo haya na mpaka sasa wanakaa katika majengo ambayo siyo mazuri. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ufanye jitihada zako binafsi kuhakikisha kwamba na upande wa Unguja unapata majengo mazuri. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, atakapokuja hapa ndugu yangu, Mheshimiwa Mwinyi, alieleze Bunge lako hili, kwa upande wa Unguja ni lini wanajeshi wetu wataanza kujengewa nyumba mpya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea na kuchangia mchango wangu huu, niongelee kuhusu uchukuaji wa vijana na kupeleka JKT. Mheshimiwa Waziri, naamini kama Serikali ina nia nzuri ya vijana wetu kuwaajiri na kuwapa ajira. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri anapotaka kuchukua vijana hawa kuwapeleka ndani ya JKT, kwanza aangalie uwezo wake wa kuchukua vijana hawa. Vilevile achukue vijana wenye uwezo wa kuajiriwa na sifa za kuajiriwa. Mheshimiwa Waziri vijana hawa kuwachukua na kuwapeleka ndani ya JKT, watakuwa wamepata mafunzo. Vijana hawa wanakosa ajira na baadaye wanarudi mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana kaka yangu, wanaporudi mitaani vijana hawa, basi inakuwa ni tatizo. Tunajijengea uadui sisi wenyewe. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, unapotaka kuchukua vijana, jipime na uwezo wako wa kuweza kuajiri pasipo na kuwabakisha kurudi mitaani tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar tuna kikosi chetu cha JKU. Hiki kikosi ni imara, kizuri, kina mafunzo mazuri. Mheshimiwa Waziri nikuomba sana, hiki kikosi kinafanana na kikosi cha JKT. Nakuomba sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, kaka yangu mpendwa, uweze kuendeleza ushauri pamoja na Wizara husika ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha vijana hawa unawachukua na kuwaweka pale ndani ya kikosi cha JKU, baadaye vijana hawa ndiyo uwachukue katika ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri vijana hawa ukiwaweka pale, basi nafikiri unaweza ukapata mafanikio mazuri na naamini utapata vijana wazuri wa kuwaajiri. Siyo kuwapeleka JKT na baadaye ukawarejesha tena Zanzibar. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, naamini Waziri wewe ni Waziri msikivu, mchapakazi, maoni yangu utayachukua kwa kina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa ajira kwa upande wa Zanzibar. Bado hali siyo nzuri kwa utoaji wa ajira, vijana wetu ambao wanachukuliwa mpaka sasa ni vijana 300 tu. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana kaka yangu, ajira ambayo imetoka takriban watu 5000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa upande wa Zanzibar nakuomba sana at least tupate vijana 500 angalau ifike asilimia 10 ya vijana ambao wanachukuliwa kutoka Zanzibar kwenda kuajiriwa ndani ya vikosi hivi vya Muungano. Mheshimiwa Waziri, bado hali siyo nzuri katika kuajiri hawa vijana, bado idadi yetu ni ndogo. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulione ili kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la Jeshi la Tanzania kutumika Zanzibar. Zanzibar ni kati ya sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilishangaa sana, kuna Wabunge wanasema wanashtushwa na Kikosi cha Jeshi kutumika upande wa Zanzibar. Hili ni Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; likifanya kazi Zanzibar, Tanzania Bara, likifanya kazi Dodoma, linafanya kazi kwenye Katiba. Hili linaruhusiwa kufanya kazi popote kwa sababu hili ni Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lina uhalali wa kufanya kazi mahali popote bila kupingwa na yeyote, ni kutokana na Katiba inayowaruhusu kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Wabunge wenzangu tuliachie Jeshi letu pendwa, Jeshi letu makini, Jeshi letu zuri liendele kufanya kazi zake kama ipasavyo. Tuliachie Jeshi, tusiliingilie katika kufanya kazi katika matakwa yake ya kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchaguzi wa Zanzibar umeshamalizika tarehe 20 Machi, 2016 hautarudiwa tena, kilichobaki ndani ya Bunge hili tuje kuchangia mambo mengine; tuchangie bajeti ya ulinzi kuliboresha Jeshi letu kuendelea kufanya kazi, siyo ku-discuss masuala ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia.