Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wetu ambao uko hapa mezani. Kwanza niishukuru Serikali yetu kwa kazi kubwa ambayo inaifanya chini ya Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan. Pia nimshukuru Spika wetu, dada yetu Mheshimiwa Tulia Ackson na wewe mwenyewe msaidizi wake kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge letu. Tumepata wakati wa kutosha wa kuchangia Mpango huu ambao naamini kabisa mchango wa Wabunge unaenda kuakisi katika ule Mpango Mkuu ambao utawasilishwa hapa kwenye Bunge la Januari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kawaida kwetu kuchangia huu Mpango wa Miaka Mitano na sasa tuko kwenye Mpango wa Tatu. Bado sijaona ni kwa jinsi gani maoni ya Wabunge ambao tunajadili hapa yanaakisi katika mipango hiyo. Nilipenda sana kuona Mpango unapowasilishwa uelezee waziwazi ukiainisha mchango wa Wabunge umechukuliwa kwa kiasi gani katika bajeti, lakini pia katika utekelezaji wa Mpango huu ambao unawasilishwa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuna maendeleo chanya, ukuaji chanya katika uchumi wetu. Kwa mfano, ongezeko la asilimia 5.4 katika mwaka 2021, kwa sasa hivi tumeenda zaidi ya ongezeko la asilimia 5.5. Hii ni indication nzuri kwetu, lakini tunaona kabisa ongezeko hili limetokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika maeneo ya maji safi na taka, ambao ongezeko lake ni asilimia 11.9, fedha bima asilimia 10, uchimbaji wa madini na mawe asilimia 8.5, huduma za jamii asilimia 8.5 na umeme asilimia 8.3. Tunaona kabisa hapa maeneo yote haya ambayo yametajwa yanagusa sekta binafsi ambazo katika Mpango Mkuu wa Miaka Mitano, sekta binafsi ilikuwa inatarajiwa kuchangia uchumi wa Taifa kwa takribani trilioni 9.8 na kati ya hizo trilioni 5.1 zilikuwa zinategemewa kuzalishwa na sekta binafsi za ndani wakati hicho kiwango kilichobakia kuchangiwa na sekta binafsi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa umakini ushirikishwaji wa sekta binafsi kwetu bado ni changamoto. Kwanza kabisa inaanza na definition ya sekta binafsi, sekta binafsi ni nini? Kwa sababu, inavyoonekana na jinsi tunavyoichukulia kiwepesi tunaona kabisa kwamba, sekta binafsi ni taasisi za watu binafsi ambazo hazina mahusiano na Serikali, lakini wenzetu walishaondoka huko, sekta binafsi ina mahusiano chanya na Serikali na sekta za umma. Sekta ya umma haiwezi kuendelea bila ya mahusiano chanya na sekta binafsi. Ndio maana wakati wenzetu wanajitahidi ku- out source kila kitu kushirikisha sekta binafsi, sisi tunakimbilia Force Account katika kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale Watanzania ambao walipata kufanya kazi nje wanafahamu. Kule wenzetu mpaka simu ya kampuni ambayo unatumia imekodishwa kutoka kwenye kampuni binafsi, computer unayotumia imekodishwa kutoka kwenye kampuni binafsi, photocopy ambayo unachapisha imekodishwa kutoka kampuni binafsi. Hivyo ndivyo wanavyoshirikisha sekta binafsi katika ukuaji wa Serikali, katika biashara za Serikali na ndivyo wanavyotengeneza matajiri wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kila kitu tunaenda kwenye Force Account. Sina hakika tutaishia wapi, lakini nina hakika kwamba, kama tunaweza tukafanya research kuna maeneo ambayo tunaweza kabisa kuona tumeshindwa. Wakati umefika sasa kuangalia ni jinsi gani tuna-engage watu wetu katika uchumi mpana wa nchi yetu katika kuwashirikisha aidha, moja kwa moja ama kupitia shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la sekta binafsi unaweza kuona kwamba, hata mikopo ambayo imetolewa kwa sekta binafsi, pamoja na kwamba, imeongezeka kutoka trilioni 20.6 mwaka 2021 mpaka trilioni 24.5 mpaka Juni, 2022, lakini tujiulize mikopo hiyo imekwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi kikubwa cha fedha ambazo zimekopeshwa sekta binafsi, asilimia 38 zimeenda kwenye shughuli binafsi. Unaposikia shughuli binafsi unashindwa kuelewa ni zipi katika uzalishaji. Hakuna kitu kinachoitwa shughuli binafsi katika uzalishaji. Asilimia 16 imeenda kwenye shughuli za kibiashara, asilimia 10.7 zimeenda kwenye viwanda, lakini ukienda kuangalia riba on average unakuta riba ni asilimia 16.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchumi wa kisasa katika dunia hii ambayo tunaishi huwezi ukaenda kumlipisha riba mwananchi wako ya asilimia 16, ukategemea kwamba, inaenda kuchochea uchumi. Huwezi kwenda kumtoza riba mjasiriamali kwa asilimia 16, ukategemea kwamba, anaenda kuwa competent katika dunia ambayo inakimbia sasa hivi kwenye single digits. Ndio maana wawekezaji wote ambao wanatoka nje wanafanya vizuri sana hapa Tanzania ukilinganisha na Watanzania kwa sababu, taasisi zetu za kifedha hazijatimiza wajibu wake wa kuhakikisha kwamba, zinamwezesha Mtanzania katika kuhimili mikikimikiki ya kiuchumi, ya kibiashara na yeye anakuwa full participant badala ya kuwa subordinate wa wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ukweli kabisa, jukumu la kuwatengenezea mitaji wananchi ni la Serikali, ku-facilitate matajiri, kutengeneza matajiri ni la Serikali na jukumu hili hatuwezi kulikaimisha kwa watu. Tunatengenezaje mitaji? Kwa kuwapa mikopo ambayo ina nafuu, kuwatengenezea ruzuku, kutengeneza miundombinu ambayo unamwachia mwananchi nafasi ya kushiriki kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri sasa umefika wakati wa Bunge lako, hii michango ya Wabunge kuichukulia kikamilifu na umefika wakati wa kuanza kutafakari kuwa hata na Kamati ya Bunge ambayo kazi yake ni kufuatilia maazimio ya Bunge na utekelezaji wa Serikali. Tukifanya hivyo tutajua tumetoka wapi? Tuko wapi na tunaenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishindwa kufanya hivyo ndio utakuta kwamba, tunapanga bajeti ya mwaka huu ya fedha. Kwa mfano, pale Dumila kuna barabara imetengenezwa mpaka Kilosa, Kilosa pale tunaizungumzia Mikumi, kuna Kiduku pale ambacho hatujui lini kimeshakaa kwenye bajeti ya Serikali zaidi ya miaka mitano na hivi tunavyozungumza ipo kwenye bajeti ya Serikali na hatujui lini itatengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Mpango wa bajeti, tunazungumzia jinsi ya kutengeneza framework ambayo inaweza kwenda kusaidia kutengeneza fedha za Serikali kwa ajili ya kuhudumia jamii nyingine. Kuna uwekezaji mkubwa pale Ilovo, bilioni 571 zinaenda kuwekezwa pale Ilovo, lakini kuna SGR ambayo inapita Kilosa, lakini kuna reli ya TAZARA kutoka pale Kidatu kwenda Mlimba kwenda mpaka Zambia. Kipande cha reli kutoka Kilosa kuja Ilovo kimekufa na sasa hivi tunawekeza bilioni 571 pale Ilovo lakini hakuna mechanism ya kusafirisha sukari tukikamilisha kile kiwanda kutoka Ilovo kuja Kilosa kuungana na SGR kupeleka nje ya nchi na mikoani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili hatuhitaji mawazo ya wageni kuja kutuambia, linaonekana kwa macho, lakini hata ujenzi wa barabara ambayo itabeba bidhaa za sukari kutoka kwenye kiwanda hiki ambacho tunawekeza inahitaji kuingizwa kwenye mpango, sio tu kwa sababu, Mbunge amesema, lakini ni kwa sababu inaenda kwenye eneo la uzalishaji ambalo tunahitaji kwa ajili ya kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sasa inapaswa kujielekeza katika maeneo ya uzalishaji. Utalii Kusini ni jambo ambalo haliepukiki. Utalii kuunganisha Hifadhi ya Nyerere na Mikumi haliepukiki, kuna zaidi ya dola milioni 120 zimewekezwa pale, lakini ukiangalia nje ya zile hifadhi kuna uwekezaji gani ambao unaenda kusisimua wananchi kushiriki katika shughuli za kitalii, haupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, kuna zile bilioni 260 za CSR ambazo zinatokana na Bwawa la Mwalimu Nyerere…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili sisi hatuna la kusema zaidi ya kusema inna Lillah wa inna ilayhi raji’un. Ahsante. (Makofi)