Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nakupongeza sana kwa namna ambavyo unaendesha mjadala huu kwa kutoa elimu ya namna ya kuujadili mjadala huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze vijana wangu wa Singida Big Stars, leo katika uwanja wa nyumbani wameendelea kutunza heshima ya uwanja ule na kuwafanya watani zetu Simba kushindwa kufurukuta. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sima, kanuni zetu zinasema, mchango wako ujadili jambo ambalo lipo kwenye Meza. Hoja ya hapa ni Mipango (Kicheko/Makofi)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea maelekezo yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana nizungumzie sana eneo la elimu. Kwenye elimu vision ya 2025 inataka tuwe na jamii iliyoelimika, ikiwa na maana ya well educated and learning society ambapo tunataka tuwe tumefikia kwenye high level of quality education. Serikali imefanya kazi kubwa sana. Nataka nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kwa dhati kuanzia chekechea mtoto anaanza shule mpaka kidato cha sita anasoma bure, Elimu Bila Malipo. Hili ni jambo kubwa sana. Naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo, imeongeza enrolment, watoto wengi sasa wameingia shule na ninaamini mwakani wengi wataingia, na Serikali imeboresha miundombinu. Hivi tunavyozungumza, Serikali imetoa fedha nyingi za kujenga madarasa, na kujenga shule. Hili ni jambo jema sana, naipongeza sana Serikali kwa kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hapa tunazungumzia elimu. Elimu ina pande mbili; kuna elimu nyoofu na elimu ya kati (alternative). Leo mahitaji yetu ni nini kwenye Mpango huu? Elimu nyoofu maana yake, tunatarajia mtoto akianza darasa la kwanza, mpaka anamaliza Chuo Kikuu. Leo chukulia shule ambayo ina watoto wasiopungua 1,000 mpaka 4,000, wote hawa tunatarajia wamalize. Huko mbele wanakoendelea, maana yake watakuwa wanaenda wachache, wengine watabaki mtaani. Sasa Mpango unatuelekeza nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maelekezo ya Mpango, tumezungumzia hapa kuhuisha; naomba nisome hapa; mpango umesema, “kuhuiwisha mitaala ili iendane na soko la ajira.” Hapo lazima tufike mahali tuelewane. Kwanza, kuhuisha mtaala uendane na soko la ajira. Maana yake kuna tatizo hapa ambalo Serikali haijalibanisha moja kwa moja, nami nataka niwakumbushe, kuna ile Tume ya Mipango, iliyotoa taarifa hii mwaka 2014. Nilisema, Mwenyekiti wa wakati huo alikuwa Mheshimiwa Dkt. Mpango ambaye ni Makamu wa Rais wa leo. Sasa kama tunatambua kwamba Tume ya Mipango ilifanya kazi nzuri, tuna kila sababu ya kuihuisha ile tume ili ifanye kazi hii na kutuletea matokeo yaliyo chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa nataka niongeze jambo moja jepesi sana. Kuanzishwa mtaala ni jambo moja, lakini kuhuisha ni jambo lingine. Hapa tuzungumzie mtaala ambao unaongelea practical oriented. Hatuwezi kuwa na mtaala ambao hauongelei suala la practical. Tunahitaji elimu yetu iwe practical zaidi. Sisi ambao tulimalizia malizia kusoma zamani, kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari tulikuwa na karakana na shule za ufundi. Shule zote hizi zilimwezesha Mtanzania aliyemaliza shule aweze kukabiliana na maisha yake ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiishie hapo. Tunapotaka kujenga ujuzi na umahiri wa mwanafunzi ili aweze kukabiliana na maisha yake, tusiishie hapo. Mtaala huu lazima uzungumzie michezo (sports and games). Una wanafunzi 4,000 kwenye shule moja, hawa wote wanatarajia kwenda kidato cha kwanza, hawa wote wanatarajia kwenda kwenye elimu nyoofu, tunahitaji na wengine waingie kwenye michezo waweze kujiajiri. Hatuwezi kufanana wote tukawa wataalam, wapo wengine wanaweza kuwa sehemu ya michezo, na tumeona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Wizara ya Michezo, imefanya kazi nzuri sana. Vijana wetu wamefanya vizuri sana, wa kike na wa kiume. Sasa mpango huu hasa kwenye eneo la mitaala, lazima kuanzia shule ya msingi tuanze na utaratibu wa kuanzisha michezo na michezo hii tuajiri walimu wa michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu walimu tumewakabidhi kujumu zito sana, jukumu ambalo ni la kimaadili. Mbali na kufundisha, ndiye ambaye anakaa muda mrefu na mtoto, na huyu mwalimu kwa kiasi kikubwa anaweza kuathirika kisaikolojia kwa sababu anahangaika na kundi kubwa la Watoto, lakini ukishakuwa na michezo, tayari unaweza ku-manage hili eneo la maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiomba Serikali, suala la walimu la kwanza ni ajira, lazima tuongeze ajira ya walimu. Jambo la pili ni motisha kwa walimu. Kazi kubwa wanayoifanya pamoja na kujenga madarasa na vitu vingine, wanafunzi ni wengi mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa ambalo tumelizungumza kwenye elimu, tumezungumza udhibiti ubora wa elimu. Hii ndiyo ngao kubwa. Hawa ndio wanaokagua ubora wa elimu yetu. Tukizungumzia elimu bora, ni hawa wadhibiti ubora wa elimu, lakini humu tulichozungumza tumesema kuimarisha mifumo. Mifumo ni jambo kubwa sana, lakini nataka kuishauri Serikali, tuimarishe mifumo ya online, yaani mifumo ya mtandao ili unapotaka kujua taarifa za udhibiti ubora kwenye shule yako, maana yake ni rahisi tu kuingia kwenye mtandao na kujua taarifa ya shule badala tu yakuzungumza mfumo. Mfumo unaweza ukawa umetufunga, nasi tutashindwa ku- access vizuri, lakini ukizungumzia mfumo wa mtandao (online) utakuwa umetusaidia ku-access vizuri maendeleo ya shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wadhibiti ubora, wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Haya mazingira magumu ndiyo yanaweza kusababisha tusipate takwimu nzuri ya kuzungumzia quality education kwenye nchi yetu. Jambo kubwa ambalo naiomba Serikali, fedha inayotoka Hazina badala ya kwenda TAMISEMI, iende shuleni, hii fedha itoke moja kwa moja iende kwenye Wilaya zao. Wadhibiti ubora wana ofisi kwenye kila Wilaya, fedha yao iende kule ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu huo huo, ipo miradi inakuja mingi sana na miradi hii inafadhiliwa na World Bank, kwa mfano TACTIC. Mradi wa TACTIC una component kubwa. Una masoko, barabara, na kadhalika. Singida ni sehemu katika miji 45; tangu mradi umekuja, tumebaki kupiga danadana, lakini mradi huu ndiyo suluhu ya matatizo yetu, ndiyo utatusaidia kuongeza kipato katika kukusanya mapato na utasaidia kuongeza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuiomba Serikali, tunapoweka Mpango wa Maendeleo, uendane na miradi mikubwa ambayo inaleta tija kwenye jamii. Hatuwezi kuishia kuzungumza tu, tuna mradi TACTIC, Miji 45, inabaki kuwa ni hadithi. Tufike mahali miradi hii ikija ndiyo miradi tunatakiwa tuisimamie ili ituwezeshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida pale tuna uwanja mzuri wa Ndege, na sasa tunafahamu; nami nimekuwa nikiuliza swali mara nyingi, lakini bado majibu yanakuja yale yale. Kwenye Mpango huu hatujazungumza habari ya kuboresha viwanja vya ndege kikiwemo kiwanja cha Singida. Singida ni Mji unaokua, tuna bidhaa nyingi, mazao ukizungumza hapa mpaka kesho asubuhi na mikoa mingine hawana. Sisi tuna karanga, tuna alizeti, tuna samli, tuna kila kitu. Naiomba Serikali iweke mpango endelevu wa kukarabati viwanja vya ndege kikiwemo kiwanja cha Singida, na hili jambo litatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna suala la renewable energy. Tuna umeme wa upepo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.