Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji. Kabla sijaingia kwenye mpango zaidi, niseme tu kwamba, lengo la nchi yote au mipango ya nchi yote ni kukuza uchumi wa nchi yake. Kwa hiyo masuala yote ya Mpango wa Maendeleo lazima yaendane na mipango ya muda mrefu. Wabunge wengi wameongea lakini bila mpango wa muda mrefu nchi yetu tutakuwa tunapiga marktime muda wote. Maana yake tutakuwa tunajenga na kubomoa. Nitoe mfano mmoja, ukiangalia wataalam wetu, ikiwezekana saa nyingine hawa wataalam wa mipango mirefu kama Watanzania wenzetu wanashindwa, basi tungetafuta hata consultant kutoka nchi za nje waje kutusaidia ili tusipate hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna mipango ile ya muda mrefu ya kuona mbali, tunaangalia hapa, kesho tunabomoa, tunajenga hapa, keshokutwa tukipata kipya tunabomoa kile tulichogharamia tunajenga kipya. Kwa mfano, wewe angalia barabara hata zile za pale Morogoro Road yaani mipango hata haijafika miaka 15 au 16 tayari imekuja mwendokasi, barabara nyembamba inang’ang’anizwa hiyo hiyo ili mradi tu daladala hizi za mwendokasi zipite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Sam Nujoma barabara haina hata miaka 10 limekuja lile daraja lile flyover, kuna madaraja pale yale mawili makubwa yalikuwa pale upande wa external nayo yamevunjwa tayari yaani tunapata gharama, tunavunja na kujenga. Sasa ukiangalia ni kwa kuwa hatuna mipango ya muda mrefu, yaani kwamba ujue kwamba mji huu utakuwa hivi, barabara hii itakuwa hivi, eneo hili litakuwa hivi. Kila siku tunajenga, tunapata hasara. Kwa hiyo tunatumia kodi za wananchi kwa kuvunja na kujenga upya kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija hapa Dodoma peke yake tunajua kabisa ndani ya miaka mitano nyuma kwamba kuna airport ya Msalato inakuja, lakini leo hapa tumeongeza runway tumelipa yale majumba, wakati tunajua kabisa tunajenga kule. Kwa hiyo tumeifanya Dodoma leo tumeigawanya katikati. Kwa nini hizo pesa tulizolipa wale runway ile tuliyojenga na zile fidia zile ingetosha kujenga kiwanja kidogo kama kile ili watu watue. Leo kule kwenye Uwanja wa Msalato kuna Marais watashuka pale, viongozi watashuka pale, uwanja mkubwa. Sasa palikuwa na haja gani ya kupoteza pesa wakati kuna mpango mwingine unakuja? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa watu wa mipango kwenye nchi hii ni shida, hawana mipango ya kuangalia mbele. Sasa hivi ukiangalia Bandari Kavu, tumepiga kelele bandari kavu imepelekwa pale Kwala pale Vigwaza, Bandari kila siku ya Mungu inafunguliwa kesho, inafunguliwa kesho, sasa hivi tayari imeishakuwa nayo ya kizamani, maana yake reli ya standard gauge itafika hapa Dodoma, kwa hiyo itakuwa nayo haina thamani standard gauge itafika pale Morogoro, sasa una haja gani tena kwenda kufuata mzigo Kwala badala ya kuweka Bandari Kavu Morogoro kwa ajili ya watu wa Kongo, watu wa Malawi na Dodoma ni kwa ajili ya watu wa Uganda na sehemu nyingine kwa kuanzia, kwani hatuna mipango ile endelevu? Hiyo Kwala imeishakula mabilioni ya pesa na aina kazi yeyote tena ya msingi kama itafunguliwa hii standard gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia barabara sasa hivi katika bajeti hii inayokuja lazima tukubali kwamba sasa hivi kwenye barabara lazima tutumie PPP. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ufanye kila aina uwezavyo leo hii accident nyingi zinauwa mpaka Viongozi wengi hapa Maprofesa, Madaktari, kwa mfano yule wa SUA. Kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ile barabara ni foleni si ya kawaida, kutoka Morogoro mpaka hapa panaitwa Makunganya foleni si ya kawaida, kutoka hapa Dodoma Mjini kwenda mpaka pale Ihumwa foleni si ya kawaida. Hivyo leo, au ninyi kwa sababu wengine mnapitapita humu kwenye vinanii nanii humo hatuonani huku vizuri, tuangalieni sisi tunaokaaa foleni! Ndiyo maana hata saa nyingine kila mtu anajiwekea king’ora na vile vitaa, mnasema ahaaa! anayeruhusiwa hapa ni kuanzia Waziri Mkuu, watu kila mtu anaweka ili apige mkwara apite, kwa sababu barabara hazipitiki, kwa hiyo tutumie mpango wa PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kila Mbunge hapa akipiga kelele mnampa kilometa tano, yule mwingine karuka sarakasi, pamoja na sarakasi kapewa kilometa ishirini mpaka barabara ije ifike kwake ni miaka kumi. Sasa hatuwezi kumaliza barabara zote. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale panaitwa nini; Mlima Nyoka pale Mbeya kila siku accident lakini ukiziangalia zote zinasababishwa na barabara, pale panatakiwa four-way, six-way akija huyu Waziri wa Ujenzi, anasema tunao mpango, lakini ukiangalia ule mpango wa muda mrefu hatuwezi kujenga wenyewe, Dunia nzima inajenga kwa PPP na kama PPP hatupati? Basi kopeni, kukopa siyo dhambi. Mimi mtu anaponiambia kama mnasema wenyewe deni himilivu kopeni! Kama Inyala pale kila siku watu wanakufa kopeni, hapa Dar-es- Salaam-Morogoro na siyo hapo sehemu nyingi hata huko Mwanza barabara nyingi hazipitiki. Kopeni halafu wekeni mpango wa road tall nyinyi Serikali wenyewe badala ya kutumia PPP mtakuwa mnachukua road tall, mtu anataka kupita pale atapita kwa road tall mtarudisha ile mikopo siyo shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unapokopa kitu unapokopa kitu, maana yake mimi sitaki kuwa mnafikimnafiki wananchi huko nje.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyeki, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, taarifa.

T A A R I F A

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa Kaka yangu Mheshimiwa Shabiby, kwamba hata hizo kilometa 25 nilizopigia sarakasi bado hazijatangazwa mpaka sasa. (Kicheko/Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, endelea.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa naipokea na nilijua kwa sababu nafanya research na nipo Kamati ya Miundombinu. Ni kweli. Bila PPP huwezi kupata Mheshimiwa Mbunge.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, subiri. Waziri wa Fedha na Mipango.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza kuongea ni mtani wangu, lakini Mheshimiwa anaechangia, anachangia vizuri lakini nilitaka niweke kumbukumbu sawa kwamba moja naunga mkono mchango wake, anachangia vizuri Mheshimiwa Shabiby.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nitoe taarifa kwamba Serikali tayari imeishatoa tangazo la kazi la kupata watu wa kufanyakazi na wameandika barua kuonyesha nia, kwa utaratibu huu anaousema wa PPP tutajenga barabara inayotokea Kibaha mpaka Morogoro njia za kutosha kama za majuu kule. Pia kwa utaratibu ule ule kutokea Igawa mpaka Tunduma na Mbunge wa kutoka Songwe naye alisema hilo. Hii ni tayari ipo kwenye hatua ya taratibu za kimanunuzi, watu wameishaonesha nia kwa hiyo taratibu zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hii barabara ndefu anayosema pamoja na kupiga sarakasi siyo kwamba hajapewa, nayo pia zabuni zilishatangazwa na shortlisting imeishafanyika. Barabara ndefu kwenye historia inayoanzia Mbulu inakwenda mpaka Maswa kupitia Sibiti imeishatangazwa, barabara inayotoka Ifakara mpaka Lumecha kule na yenyewe imeshatangazwa kwa utaratibu uleule. Barabara inayotoka Handeni mpaka Singida na yenyewe imeshatangazwa, barabara inayotoka Arusha mpaka Kongwa imeishatangazwa, ile barabara ya kule Mtwango pamoja na Nachingwea inaunga mpaka inatokea somewhere Masasi inapita Wilaya tatu hizo zimeishatangazwa na shortlisting zimeishafanyika, zenye urefu wa zaidi ya kilometa 2,500 kwa utaratibu wa EPC+F. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na kwa hapa Dodoma tayari tulishaweka Jiwe la Msingi na ujenzi unaendelea wa ile by-pass ambayo ni zaidi ya kilometa
100 na ninaamini pia na yenyewe itatoa suluhisho hilo. Tukiishamaliza hii PPP ya kwanza na tunaleta Sheria Bunge linalokuja kurekebisha ile Sheria ili iweze kuweka urahisi wa kutekelezeka kwa sababu hilo ni dirisha ambalo tunaamini litapunguza Deni la Taifa pia litatoa space kwenye Bajeti ya Serikali ili Serikali iweze kutoa zaidi huduma za jamii ikiwepo Mikopo ya Elimu ya Juu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, hujazungumzia barabara za Dar-es-Salaam, tunaendelea Mheshimiwa Shabiby.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza dakika tatu naomba msimamishe muda. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijakataa, lakini nipo Kamati ya Bunge ya Miundombinu, hizo barabara alizozitaja zote tuna kilometa 25, kilometa 30, kilometa ngapi… za kuanzia, hata mkiangalia ile ya Kiteto kwani imepitishwa leo? Si ina miaka kama mitatu, minne? Ndiyo maana nimesema Serikali yeyote duniani haiwezi ikamaliza barabara kwa kupitia pesa zake. Ukienda nchi yeyote iliyoendelea unakuta kuna barabara zinalipiwa road tall kwahiyo tumieni PPP na mkishindwa kopeni pesa halafu zile barabara mzifanye za road tall ili hela ikusanywe kwa road tall ili Wabunge wote watapata hiyo pesa. Kwa sababu hao wanaonesha nia wanaonesha nia siku nyingi lakini hawapati majibu, maana yake mimi nipo kwenye Kamati ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme huko nje mitaani watu wengi wanaamini kwamba Serikali ya Awamu ya Tano iliacha pesa kwenye Serikali hii. Kwamba ilikusanya pesa mpaka zingine zimebaki, zipo na watu wanaamini kwamba miradi yote ilikuwa inafanya kama reli, kama Bwala la Mwalimu Nyerere bila mkopo pamoja na madaraja. Hata hivyo nataka niseme hakuna ukweli, kwamba hizo reli tunazojenga ni mkopo, hilo bwawa tunalojenga ni mkopo na watu lazima wafahamu kwamba hiyo Serikali ya Awamu Tano ilikopa kiasi kikubwa cha pesa. Hata tunapokuja hapa Serikali ya Awamu ya Sita, inapoanza kuingia kigugumizi wakitishwa kidogo mkopa sana hawakopi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakiambiwa tu ninyi mna kazi ya kukopa toka muingie mnakopa na wao kweli wanaingiwa woga hawakopi kweli. Nataka niseme hii reli waliyoipeleka mpaka Mwanza bila kukopa kufika Kigoma ni sawasawa na mtu umechukua mkopo, umejenga jumba linatakiwa likurudishie pesa hujalifanyia finishing, sasa utarudishaje hiyo pesa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni lazima wakope, wafikishe hii reli Kigoma, lazima wakope, wafikishe hii reli Kalimwa hadi Kalema, bila hivyo hii Reli ya Mwanza bila kushirikisha nchi ya Uganda na nchi ya South Sudan reli ya Mwanza itakuwa haina faida yeyote katika Serikali hata tone, kwa sababu utakwenda Mwanza treni utarudi na nini? Hakuna chochote. Lazima ukienda Mwanza unaporudi upate mzigo wa kwenda South Sudan, upate mzigo wa kwenda Uganda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii reli ya Kigoma ndiyo ambayo italipa zaidi kwa sababu leo hii pale wanayo machimbo ya nickel ambayo kila siku itakuwa inasafiri kutoka Burundi kuja Dar e Salaam. Leo hii Kalemi kuna Shaba nyingi sana inatoka kule inakuja Tanzania lakini inashindwa kwa ajili usafiri wa reli haupo na Serikali imetoa bilioni 48 kwa ajili ya kujenga ile bandari lakini bandari imekaa haina faida yeyote ile kwa sababu ya ukosefu wa reli.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nataka nizungumzie ni kuhusu mazingira. Mazingira nchi hii tunakazi ya kuzungumza tu. Maji, tuchukue maji ya bahari tuchuje, mara tuchimbe mabwawa, hivyo mlishawahi kujiuliza Wabunge huko yanakotoka maji kuna mtu alienda kupanda mti hata mmoja? Tuna kazi ya kusema tu tabianchi.

Mimi kwangu pale Gairo kule Tarafa ya Nongwe kuna Mito Minne, Mto Msowelo, Mto Ludewa, Mto Mvumi, Mto Mkondoa ambayo inaenda Dakawa, inaenda Mto Wami. Ukienda kule mpaka Mbunge ufanye kuhemea uweke watu wawafukuze watu wasikate miti. Vyanzo vya maji vinakufa lakini hakuna Mamlaka yeyote inayoweza kupanda hiyo miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalalmika tabianchi, ukiangalia ukienda kwenye Wizara ya Maji wanamabonde, kuna Bonde Wami, Ruvu, kuna Bonde siijui la Kanda gani, ukija huku Mazingira wanatoa hela mpaka zawadi Million 50, lakini mtu anaepewa hizo zawadi za Million 50 na Mazingira wamepanda miti kwenye nyumba za gorofa mbele mijini, kule kwenye vyanzo vya mito hakuna! Ukienda TFS wapo, wanasimamia misitu. Basi waungane hawa kati ya maliasili, mazingira na hawa watu wa maji na hizi pesa wanazopewapewa za kupanda miti itafutwe Taasisi moja isimamie vyanzo vyote vya maji hapa Tanzania, zaidi ya hivyo tunapiga kelele! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapiga kelele Mto Ruvu, lakini Mto Ruvu chanzo chake ni kule Morogoro Kusini, nenda kaangalie kila kona kuna ng’ombe! Ng’ombe peke yake wamemaliza ile miti yote, wamekula kila kitu, wamekata kila kitu, ukienda si ng’ombe tu wakulima wamefanya mashamba mpaka ile mbuga ilikuwa inaitwa Gode yote, sasa maji yatatoka wapi? Mnatafuta vyanzo vingine wakati mlivyonavyo tunashindwa kuvitunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana hawa Maliasili, Wizara ya Maji na Wizara ya Mazingira wakae pamoja waangalie kama nikumkabidhi TFS wamkabidhi TFS kwa sababu sasa hivi yeye ana Jeshi atunze ile misitu na apange ile miti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni barabara ile ya kutoka Gairo kwenda Kilindi ya lami ambayo inaenda kukutanika na ile barabara ya kutoka Handeni mpaka Tanga kwenda mpaka Minjingu, ile Barabara ina ahadi ya Marais watatu, Rais Kikwete, Rais Magufuli lakini mpaka leo haijawekwa kwenye mpango naomba ikae kwenye huo mpango, kwa sababu ni barabara nyepesi kabisa. Ahsante sana. (Makofi)