Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kidogo kwenye huu mpango. Kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ameniwezesha kunipa afya njema na kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyotoa mwongozo kwamba unaweza ukasema ametangulia kusema Mheshimiwa Muhongo profesa, Mheshimiwa Kimei na mimi hapa darasa la saba naomba nitoe mchango wangu, pamoja na kwamba wamenitangulia hawa vigogo. Mpango huu kwanza nianze kumpongeza Waziri wa Fedha kwa Mpango mzuri ambao ameuweka hapa mbele tuweze kuujadili. Nitakuwa na yangu machache sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kama atakumbuka huwa nalalamika kila mara, kila Bunge linapofikia kipindi kama hiki kwa kumwambia kwamba upotevu wa fedha kwenye maeneo mbalimbali ni upotevu mkubwa sana ikiwa kwenye maeneo hususani kwa wafanyabiashara. Hili pato ambalo tunalizungumzia limekua, lingeweza kukua zaidi iwapo tutaendelea kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yetu ya watu wanaofanya biashara. TRA ina upungufu kidogo pamoja na kwamba inafanya kazi vizuri, lakini kuna wafanyakazi au watumishi wa (TRA) ambao siyo waaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kwenye Jiji la Dar-es-Salaam kwa sababu naishi hapo, ukweli ukizunguka kwenye maeneo mbalimbali ya wafanyabiashara, hususani kwenye maduka unakuta watu wengi wananunua bidhaa na hawapewi risiti. Hili lipo kwa asilimia mia moja linafanyika, kama wanatoa risiti basi ni kwa asilimia kumi ama kumi na tano na hao wanaotoa risiti, umenunua mali ya shilingi milioni moja, unapewa risiti ya shilingi laki moja. Hawa wafanyabiashara wanapata wapi hicho kiburi? Mheshimiwa Waziri wa Fedha, naomba hili ulichukue ukae na hicho kitengo cha (TRA) wajaribu kuangalia huu upungufu watauzuia vipi, kwa sababu leo hii tuna mambo mengi ambayo tunahitaji yakafanywe kwenye maeneo yetu. Kama fedha haitakusanywa vizuri, haya maeneo yatafanyiwa vipi kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna maeneo mengine ambayo inabidi tuyaangalie. Kuna watu wanahitaji kulipa fedha za Serikali kupitia control number, unakuta mtu anafuatilia siku tatu nne mpaka wiki hajapewa control number, je, hiyo fedha aliyonayo mfukoni haitapata kazi nyingine? Suala hili nalo wajaribu kuliangalia sana kwa sababu watu wanaenda kuomba kulipa fedha ya Serikali, kuna tatizo gani kumpa siku hiyo hiyo control number? Inachukua mpaka wiki nzima, control number haijatolewa. Huu nao ni upungufu na unasababisha kupunguza mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia mpango wa Serikali, namna gani tuboreshe tuweze kukusanya pato la Taifa. Nizungumzie upande wa madini, wachimbaji wetu wa madini hivi sasa wanaongeza ama wanachangia pato la Taifa kutoka asilimia nne mpaka asilimia nane. Hata hivyo, watu hawa wachimbaji wetu ama sekta hii ya madini ikiwaboreshea vizuri wachimbaji kwa kweli Wizara hii ya Madini inaweza ikachangia pato la Taifa hata zaidi ya asilimia ishirini. Nitatoa mfano kidogo, wakiwezeshwa hawa wachimbaji wetu, mfano, STAMICO anafanya utafiti wa kufanya explorations ili kujua huyu mchimbaji anapata wapi madini na kwa kiasi gani ili aweze kupata mapato makubwa. STAMICO ama hawa GST wanafanya gharama zao kuwa ni kubwa sana, kiasi kwamba, hawa wachimbaji wadogo ama wachimbaji wa kati wanashindwa kumudu gharama za kufanyia explorations, matokeo yake wanakwenda kufanya uchimbaji ambao ni local. Kwa hiyo mapato hayapatikani kwa wingi, lakini wakiwezeshwa kwa kupunguziwa gharama za kufanyia explorations na pia kuwezeshwa vyombo vya kiuchimbaji vya kisasa, naamini kabisa Wizara ya Madini inaweza ikaongeza pato lake katika Mfuko wa Taifa kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukusanya mapato hayo, tunahitaji tufanyiwe mambo mengi. Hata hivyo tuangalie kwenye upande wa sekta ya kilimo, leo hii mvua zetu zimekuwa ni za rasharasha, lakini kilimo kinachangia kipato kikubwa sana. Leo hii katika maeneo mbalimbali tumekuwa na ukame, lakini mvua zinaponyesha kuna maji mengi yanapotea, kwa nini Serikali ama Wizara ya Kilimo isiweke mkakati mzuri wa kuweza kujenga mabwawa makubwa ili sasa kipindi chote cha mwaka kiwe ni kipindi cha kulima. Wakulima watakapopata mazao ina maana tunanyanyua pato letu la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano kidogo, kwenye maeneo kama vile Jimbo la Nyang’hwale. Jimbo la Nyang’hwale tuna maeneo mengi sana ya mabonde ambayo maji yanatiririka yanakwenda Ziwa Victoria. Yale maji yangeweza kutegwa na kuweza kumwagilia na kupata mazao, tungeweza kuchangia pato. Hilo ni eneo moja, je, ikiwa kwa nchi nzima? Kwa hiyo naomba hili nalo lichukuliwe liwe katika vyanzo vyetu vya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vyetu vya mapato tukivipata, basi Serikali isisahau basi kuweka mpango wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Busisi - Nyang’hwale kwenda Kahama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Ahsante sana. (Makofi)