Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe na mimi rambirambi za kutoka Musoma Vijijini kwa maafa na majonzi yaliyotupata, tunaomba wapumzike kwa amani. Vile vile katika mjadala wetu tunaoufanya sasa, nadhani tutakuwa tumejifunza na bajeti tunayoitayarisha, mambo yaliyotokea MV Bukoba na yaliyotokea juzi tutayaona kwenye mipango na bajeti ya mwaka ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala wetu ni lazima kwanza tujue malengo yetu. Mipango tunayoifanya iko ndani ya mipango ya miaka mitano ambayo inaisha 2025, ambayo malengo yake ni ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa ajira mpya na huduma bora kwa wananchi. Ndiyo maana kwa vyote hivi hatuwezi kukwepa pendekezo ambalo tumerudia mara kwa mara kulitoa, kwamba lazima tuwe na Planning Commission ambayo iko ndani ya Ofisi ya Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa malengo yetu ambayo yako kwenye hiyo document inasema kwamba, ikifika mwaka 2025 tunataka GDP per capita yetu iwe dola 3000. Hiyo inamaanisha kwamba ikiwa sasahivi tuko watu takribani milioni 62, kufika 2025 huenda tutakuwa milioni 68 lakini tunaweza tukafika milioni 70. Maana yake ni kwamba ukichukua GDP per capita ya dola 3000 kwa kila mtu kwa mwaka, tukifika 2025, tunapaswa kuwa na GDP isiyopungua bilioni 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi GDP yetu ni dola bilioni 62. Kwa hiyo huu mpango na bajeti yake ni lazima ituweke kwenye barabara ya kutoka bilioni 62 sasa kwenda kwenye bilioni 200; ni kazi kubwa kweli kweli. Na hapa lazima mipango yetu tuelezane ukweli, tuone kama hilo lengo la GDP per capita ya dola 3000 lilikuwa sahihi au tuliandika tu kwa haraka haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi sisi tukiwa na bilioni 62, GDP per capita yetu inakadiriwa mwishoni mwa mwaka kuwa dola 990. Kwa maneno mengine tumerudi chini, na hivyo tutaenda kwenye group la nchi masikini kufuatana na viwango vilivyowekwa na Benki ya Dunia tarehe moja Julai mwaka jana. Kwa hiyo tumeshuka, tusiongelee uchumi wa kati, hatuko huko tena, tumeshuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huohuo sisi tukiwa hivyo, wenzetu wa Kenya ikifika mwisho wa mwaka huu sisi tukiwa na GDP ya dola bilioni 62, wao watakuwa na GDP ya dola bilioni 107. GDP per capita ya Kenya, mwisho wa mwaka huu itakuwa ni dola 1,550, sisi tutakuwa ni dola 990. Kwa hiyo ukichukua yale ma-group yaliyotengenezwa na World Bank, Jirani yetu Kenya ambaye tunataka kumpatia na gesi yetu, yeye yuko kwenye Lower Middle-Income Country ambayo inaanzia dola 1046 mpaka dola 4095. Sisi tuko chini tuko dola 990, Kenya wapo dola 1,550. Kwa hiyo haya tunayoanza kuyajadili leo, mapendekezo yangu ni haya: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo yetu ni lazima tupunguze mfumuko wa bei (low inflation), mipango na bajeti yetu. Inflation August mwaka huu ilikuwa 4.6%, Septemba imepanda imekuwa 4.8%. Hii lazima tuipunguze, ndiyo tuyajadili, tushawishi Wizara ipunguze. Lengo la pili muhimu kwenye mambo tunayoyapanga na bajeti yake na inafanyika duniani kote, wanapunguza low inflation halafu wanapunguza na interest rates. Ikiwa inflation itapanda inamaanisha benki nazo zitapandisha riba zao za mikopo. Kwa hiyo huu mpango na bajeti yake lazima tulenge huko kwamba interest rates zisipande, zikipanda hata waliokopa nyumba, baiskeli na magari lazima zipande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho tunapaswa kukiongelea kwenye hii bajeti ni kuzuia Government Bonds (hatifungani) kutumika pasipokuwa na malengo sahihi. Maana yake ukiitumia, inflation ikiongezeka, utalazimika kutumia hii hatifungani. Ukishaitumia ujue sasa umeleta matatizo kwa uchumi wa nchi. Kwa hiyo hili nalo, hii bajeti ije itueleze namna ya kuzuia kukimbia kutumia Government Bonds, kututoa kwenye matatizo ambayo tungeweza kuyatatua kwa njia nyingine kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mipango tunayoijadili na uchumi wake, lazima ituelekeze ambapo wachumi wanatueleza. Unajua kuna wachumi wa aina mbili na inabidi uchague unapenda kumsikiliza nani. Kuna wale waliochukua econometrics kama akina marehemu Prof. Rweyemamu na kitabu chake cha miaka ya 1970; halafu kuna wale ambao ni political economist, hao maneno ni mengi na hesabu zao za kujumlisha na kutoa tu. Sasa inabidi sijui unataka kumsikiliza yupi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukichukua wataalamu wa uchumi kabisa wanasema duniani ukitaka kupunguza uchumi ni lazima uchumi wako ukue kwa zaidi ya 8%. Kwa hiyo hii mipango lazima itueleze, kwa sababu mwaka 2020 uchumi ulikua kwa 2%, mwaka jana kwa 4.5% na mwaka huu tunategemea kwenda kati ya 4% na 5%; na mimi takwimu zangu nazitoa kwenye vyanzo ambavyo dunia inaviamini. Unaweza kuwa na chanzo chako kama huko duniani hawakijui, sipendi kukitumia hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa China, ukisikia China kufanikiwa kiuchumi, kwa zaidi ya miaka 20 uchumi wao ulikuwa kwa kadiri ya asilimia 15 mpaka asilimia 20; kwa miaka 20 ndipo China ikafika hapo ilipo. Sasa sisi tunataka tu tufike 8% growth. Kwa hiyo mapendekezo yangu ni kama haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji ili uende kasi, ndugu zangu lazima tuwe na bidhaa nyingi na mpya kwenye soko, siyo kuongeza tozo. Tozo na kodi hazikuzi uchumi. Kinachokuza uchumi ni bidhaa kwenda kwenye soko la ndani na soko la nje. Kwa hiyo hii bajeti, mipango yetu na bajeti, tueleze hivyo, halafu lazima itueleze ajira mpya. Hili neno mpya, siyo zilezile. Ajira mpya ni zipi na kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, itueleze mzunguko mkubwa na mpana wa fedha kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, tufanye yafuatayo: mimi nina mapendekezo yangu kwa wataalamu kwamba twende kwenye kilimo, kwani kina asilimia 30 ya GDP yetu. Hebu tupigane tufikishe asilimia 40. Sasa sitaki kurudia, haya nilishayaongea. Mazao ambayo ni lazima tuyawekee mkazo ni yale ambayo tunatumia ndani ya nchi na nje ya nchi yana soko, ambayo ni mahindi, mchele, ngano, mihogo, matunda na mbogamboga. Haya yote matumizi yake duniani kila siku ni kati ya asilimia 40 na 60 ya watu waishio duniani, twende huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, uvuvi na ufugaji. Samaki watoke ziwani, watoke baharini, tuongeze nyama na maziwa. Hapa uvuvi na ufugaji tukazane tuchangie angalau 5% ya GDP yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, madini. Tuendelee na Tanzanite, Gold na Diamond. Pia kama nilivyowahi kuwaeleza hapa, kuna madini ambayo ni muhimu na yana thamani kubwa kuliko haya. Haya ni lazima mipango na bajeti hii itueleze inavyoiwezesha geological survey. Haya madini yatapatikana kwa kutumia geological survey, siyo Tume ya Madini. Tume ya Madini inasimamia, sasa utasimamiaje huna kitu kipya? Tuwapatie geological survey waendelee kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna madini ya electronics industry, yanayotumika kwenye electronics kama Palladium, Lithium, Copper, Tin, Nickel, Gold na Aluminum. Computer zozote tulizonazo zina Lithium, Cerium, Europium, Samarium, Neodymium na madini mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ugomvi mkubwa sasa hivi unaendelea wa microchips kati ya Marekani na China kama mnafuatilia. Kwa sababu hizi hata simu zenu zote zina microchips. Computers zote na electronics zote madini yanayotakiwa humo ni Sillicon na rare earth element 17, niliwahi kuyataja humu, sina haja ya kutaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya madini, atakayetusaidia kuyapata ni geological Survey, wawekeze wafanye utafiti, watafute madini mapya yanayohitajika duniani, yanaitwa technology metals. Sasa hapa madini tujipige mpaka tufikishe asilimia 15 ya GDP; wanakaribia 10, lakini uchumi wetu uwasukume twende kwenye 15% of our GDP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ni muhimu na ukiona katika mapendekezo yangu nimeanza ajira ya watu wengi naenda napungua kilimo, uvuvi, ufugaji, mining na sasa uchumi wa gesi. Yote hayo yalitushinda tukadhani uchumi wa gesi, ndiyo utatutoa, lakini tukaamua kuweka kapuni. Sijui kama tutasalimika tusipotoa huko kapuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba uchumi wa gesi una vitu vitatu muhimu; tutazalisha umeme mwingi wa bei nafuu na ujenzi wa mitambo yake ni wa haraka. Halafu umeme wa gesi hauna jua, hauna ukame, tuta-export LNG tunayotaka kuijenga pale Lindi, ni biashara kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu muhimu kabisa, ni petrochemical industrials. Hapa kabla hatujamuuzia mtu yeyote jirani yetu tunayeshindana naye gesi, lazima tujiulize: Je, tukimpa gesi yetu, atakuja na viwanda haraka atuuzie bidhaa zinazotokana na gesi yetu? Hilo ni suala la muhimu sana. Petrochemical industries mfano wake ni mbolea, plastics zote, viti vyote mnavyokalia, vyote ni gesi; sabuni, detergents nyingine, drugs, madawa ya wadudu, rangi na insulating materials. Viwanda ni vingi sana vya gesi. Kwa hiyo, napendekeza hapa hii gas economy ituchangie kati ya 15 na 20% ya GDP. Huu mpango…

MWENYEKITI: Profesa, hiyo ni kengele yako ya mwisho, nakuongeza dakika tatu.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wewe Mwenyekiti ni mwema bwana. Nyingine ya tano ni tourism. Kufika Aprili mwaka huu 2022, tourism imeingiza dola bilioni 1.5. Sasa jamani, tujitahidi tourism tujitahidi ituletee 12% ya GDP yetu, hapo uchumi utakuwa mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, nimeandika, sports, games, music na culture vitupatie GDP mbili. Mwisho ni climate change. Tunataka kuiona hii bajeti inaongelea hili, maana yake matatizo yamekuwa mengi. Sasa hivi Carbon dioxide emission za Tanzania per Capita; tunavyochafua mazingira kwa kila mtu kwa mwaka. Kwa mwaka 2020 ilikuwa 0.18 metrics tons a person per annum. Mwaka 2019 ilikuwa 0.21 metric tons per person per annum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutengeneze mpango na tuje na bajeti. Ndiyo maana kwa kumalizia ni kwamba haya yote niliyoyataja hatuwezi kuruhusu Wizara moja inayapanga yote, mengine hayapo kwao ndiyo maana tunahitaji Planning Commission. Ahsante sana. (Makofi)