Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii. Pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yake kwa maandalizi mazuri ya hotuba ya bajeti ya ofisi yake, lakini pia kwa kuiwasilisha vizuri kwa umahiri mkubwa. Pia naipongeza sana Serikali yetu ya CCM ambayo inaongozwa na mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa njia jumuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia ujenzi wa uboreshaji wa miundombinu katika sekta ya elimu, sekta ya afya, sekta ya maji, barabara, na kadhalika, lakini hivi karibuni pia tumeshuhudia jinsi Maafisa Ugani ambavyo wamewezeshwa kwa kupewa vitendea kazi. Ni jambo jema na la kupongeza sana. Nampongeza pia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa kazi nzuri. Tumeona wakulima wamepewa matumaini makubwa sana ya kuwezeshwa kwa kupewa pembejeo kwa mfumo wa ruzuku, tunaishukuru sana Serikali yetu. Naomba nitoe ushauri kidogo tu kwa upande wa kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mwelekeo mzuri wa utekelezaji wa kiujumla katika sekta ya kilimo, nasi sote ni mashahidi, lakini pamoja na jitihada zote hizi, mkulima kwa mfano wa korosho anazalisha korosho, lakini utaona kwamba, korosho hii haitumii vizuri ipasavyo, pamoja na kwamba, ni mzalishaji wa korosho. Ninasema haitumii ipasavyo kwa sababu ulaji wa korosho kwa kweli kwa Mtanzania ni kidogo sana. Ukichukulia kwa mfano wa nchi kama ya India, ni ya tatu duniani kwa uzalishaji wa korosho. Inazalisha zaidi ya tani 700,000. Tanzania inazalisha zaidi ya tani 200,000, lakini ukiangalia kwa matumizi ya korosho, India inatumia korosho zaidi ya tani 300,000 wakati Tanzania sisi hatupo hata kwenye ramani ya utumiaji wa korosho. Tunatumia korosho kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutokutumia mazao ambayo anazalisha mkulima, hasa yale ya chakula, tutaona pia bei inashuka mara kwa mara na kwa kiasi kikubwa; na utakuta hata kila mwaka bei inashuka, lakini zaidi ya hapo, maisha ya mkulima yanaendelea kuwa duni. Hakuna tafsiri ya moja kwa moja ya uzalishaji wake na uboreshaji wa maisha yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitoe ushauri kidogo tu kwamba, Serikali ifanye integration ya kilimo na viwanda. Nasema hivi ili tuweze kupata multiplier effect. Kwa mfano, suala la ajira limezungumzwa sana hapa, tuweze kupata pia mapato, tuweze ku-regulate pia bei. Kwa mfano, bei ya korosho; tukiwa na viwanda vyetu vya korosho kwa ajili ya kusafirishwa nje ambayo ni ghafi, itapungua na hii itasababisha mvutano; demand and supply principle pale, bei itapanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya korosho vipo vingi sana katika nchi yetu, vipo. Kwa mfano watu binafsi wana viwanda 39 vya korosho; lakini ukiangalia ni viwanda 20 tu ndivyo vinavyofanya kazi. Sasa hii inashangaza. Utaambiwa kwamba, vile viwanda 19 ambavyo havifanyi kazi, havina changamoto ya mtaji, wala havina changamoto yoyote. Nami naiomba Serikali iangalie na kuchunguza ni kwa nini lile lengo la kubangua korosho ghafi 56,000 halikutekelezwa, inakuja kubanguliwa 9% tu? Inategemewa kubanguliwa korosho tani 4,900 kwa kipindi cha mwaka 2021/ 2022, tatizo ni nini hapa?

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali iliangalie hili kwa umakini kwa sababu suala la viwanda tumekuwa tukilizungumzia muda mrefu, hususan, viwanda vya korosho. Tumezungumza mara tumesema vibinafsishwe, mara vianzishwe viwanda, leo wanaanzisha watu viwanda 39 viwanda 19 visifanye kazi bila sababu yoyote ambayo inaelezwa hapa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilimo labda nimalizie tu kuiomba sasa Serikali ihimize utumiaji wa vile ambavyo tunavizalisha, hususan kwenye korosho. Korosho ina lishe, ina ubora mkubwa sana kwenye upande wa lishe, tutumie korosho Watanzania, ina manufaa makubwa sana hasa kwenye ku-control diabetes, pressure na magonjwa mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie kwenye upande wa afya. Tuna hospitali inajengwa kule Mtwara inakaribia kukamilika, hospitali ya rufaa ya Kanda ya Kusini ambayo iko Mitengo. Hii hospitali imekamilika kwa hatua za kwanza, lakini ina matatizo ya watumishi, inahitaji watumishi takribani 400 kwa hatua za kwanza ambapo ikikamilika itahitaji watumishi 1,200, lakini kwa sasa ina watumishi 46 tu ambapo madaktari bingwa ni wawili na madaktari wa kawaida ni watatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba maprofesa wale ambao wanastaafu na madaktari bingwa, waajiriwe angalau kwa mkataba katika hospitali hii na hata katika hospitali nyingine Tanzania, kwa sababu hili siyo tatizo la hospitali hii moja tu, ni katika maeneo mengi. Hata hivyo, naomba retirement age ikiwezekana iongezwe kwa sababu hili ni tatizo ili kusudi tuweze kukabiliana nalo. Mimi niko Kamati ya LAAC tunazunguka na tunaona shida ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee tu kidogo hapa kwamba, kuna tatizo pia katika hiyo hospitali. Maji yanayokwenda pale ni ya chumvi na wataalam wanasema itachukua muda mfupi sana vifaa kuharibika; na hakuna bajeti tena ya kutoa maji katika mradi mwingine. Kuna chanzo cha Mchuchu pale Mikindani kina maji baridi.

Sasa naomba Waziri wa Maji aangalie uwezekano wa kutoa maji ya baridi kutoka chanzo cha Mchuchu ili kusudi kupeleka pale kuzuia tatizo ambalo linaweza likajitokeza la kuharibika kwa vifaa katika ile hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa kuomba uboreshaji wa miundombinu ya maji uende kwa kasi kubwa zaidi ya hivi ilivyo sasa, uende kwa kasi kubwa ambayo itazidi ongezeko la watu…

(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: …kwa sababu hili ni tatizo kubwa. Kwa mfano, Kisasa kule maji hatupati, tunachukua wiki mbili kupata maji.

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)