Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Mimi nitajikita zaidi katika ule ukurasa wa 32 wa hotuba hii ambayo imezungumzia juu ya wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka kwamba jambo hili tatizo kubwa la wafugaji na wakulima limekuwa ni janga la Taifa. Watu wameuana kwa ajili ya mipaka, wafugaji wakienda kulisha kwenye mashamba ya wakulima, sasa mimi naomba kwa vile Waziri Mkuu yupo hapa akihitimisha hotuba yake alitueleze hii Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, kazi yake kubwa ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua wazi kwamba nchi yetu ni kubwa sana yenye square kilometers 947,303 ukiondoa 61,500 unabaki na 885 ambayo ndiyo ukubwa wa ardhi yetu. Kwa sehemu ya kilimo amesema kwamba ni hekta milioni 44 ambazo zinafaa kwa kilimo, ingawa mpaka sasa hizi ni hekta 14.5 Milioni ambazo zinatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia yote haya ni kwamba nchi yetu haitilii umuhimu wa wafugaji, wanaona wafugaji ni watu tu wa kuswaga ng’ombe na kukimbia huku na huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka kwamba nchi yetu inaringa kwamba ni nchi ya tatu katika Afrika kwa kuwa na mifugo mingi Milioni 25, lakini hotuba ya Waziri Mkuu inaonyesha kwamba katika hizo ng’ombe Milioni 25 pato letu limekuwa ni Dola za Marekani Milioni 22,400. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikilinganishwa na wenzetu wa Kenya ambao wao wameweka msisitizo kwenye kufuga kisasa, zero grazing. Utakuta kwamba wao pato lao ni karibia Bilioni Moja za Marekani, wakati ng’ombe wao wanaofuga ni Milioni 21 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Milioni 25 ya ng’ombe wetu wa Tanzania asilimia 98 ni wa kienyeji na wanafugwa kienyeji. Ukiangalia nchi ya Denmark ambayo ina ng’ombe 1,500,000 wao wamepata Milioni 330 USD kutokana na mauzo ya ng’ombe. Kwa hiyo, tunachojiuliza ni kwamba hivi Tanzania tutangoja lini wananchi wetu waendelee kuuana, wafugaji na wakulima kwa ajili ya ardhi, wakati tuna ardhi kubwa lakini haijapangiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia unakuta kwamba takwimu zinaonyesha eneo la kulima ni kiasi gani, lakini takwimu hazionyeshi eneo la wafugaji ni kiasi gani. Swali ninalojiuliza ni kwamba hawa wataalam wetu wa ugani wa mifugo wao hawajui faida ya zero grazing wala hawajui faida ya cross breeding kiasi kwamba ng’ombe wetu wote ni wa kienyeji ni kiasi kwamba tuna ng’ombe lakini wasio na tija? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba Serikali yetu kwa vile imeunda Wizara nzima ya Mifugo, Wizara hii ije na mpango mkakati mzima wa kutuonyesha kwamba imetengwa ardhi kiasi gani ya wafugaji na wafugaji hawa wangapi wameshapewa maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wawekezaji wameweza kutengewa nafikiri Milioni 200 hectors, kwa nini wafugaji wetu wasitengewe maeneo ya kulima? Ni kwamba tunaamini kwa watu wa nje kuliko watu wetu wenyewe, hata fedha hizi ambazo Waziri Mkuu ameweka hapa kuonyesha kwamba ndiyo zimepatikana, naamini sehemu kubwa ni wafugaji wenyewe waliohangaika kuingiza pato hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali mara nyingi wanasema wafugaji wapunguze ng’ombe, lakini hawajaweka kiwango kwamba wapunguze kutoka kiasi gani ifikie kiasi gani, na wakipunguza wanawasaidia nini katika malisho yao na maji yao. Maana wafugaji wanafugaji wanafuga ng’ombe wengi wakijua kwamba hata nusu wakifa watabaki na nunu. Sasa Serikali unapoendelea kusema punguzeni mifugo bila kuweka idadi hujawasaidia wafugaji wala wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine hebu tuangalie hizi Ranchi zetu utakuta kwamba ukienda kama kwenye Ranchi ya Kongwa ina eneo kubwa sana ambalo limetengewa kufuga lakini productivity ya pale haiendani na eneo lile. Hawa ni watu wamewekwa pale wanalipwa mshahara, lakini production ni ndogo mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba kwa nini Serikali isiangalie haya maeneo nakuona kwamba kama hawa wanaoendesha hizi Ranchi hawawezi kwa nini wasiwape wafugaji wakafanya kazi hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeweza kuhamisha wafugaji kutoka Ngorongoro kwenda Handeni, kitu gani kinashindikana kuhamisha wafugaji wale wenye ng’ombe wengi na kuwapeleka kwenye maeneo ambayo wametengenezewa kwa ajili ya ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wenzetu wa huko Kenya tunasema kwamba wanaofuga ni wale ma-settlers lakini what does it mean, settlers ina maana wamefanya zero grazing na wanaweka miundombinu yote inayotakiwa, sisi tunashindwaje ku-settle wafugaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiona ni hapa kwamba Serikali ipo tayari kupeleka hela nyingi kwenye migodi tubaki na mashimo baada ya miaka 100 ijayo, kuliko kusaidia wafugaji wetu na kuwaweka mahali, wakawatengenezea biogas, wakawapandia majani, wakawasaidia ile slung ya biogas wakapandia kama mbolea ikasaidia katika kukuza majani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali mna kazi kubwa ya kufanya, hamjatu-impress kwenye upande wa wafugaji. Kwa ajili hiyo, hatuna haja ya kuringa kwamba tuna ng’ombe wengi maana wale ng’ombe wote wamechoka na wachungaji wamechoka hawana tija. Ahsante sana. (Makofi)