Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehrma ambaye ameniwezesha leo hii kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nampongeza sana Waziri Mkuu na watendaji wote wa Ofisi yake ambao wameshiriki kwa njia moja au nyingine kufanikisha bajeti hii. Naomba nijielekeze katika Kilimo. Mimi natoka Jimbo la Nanyumbu. Ndani ya Jimbo langu, Korosho ndiyo uti wa mgongo wa wananchi wa Jimbo langu. Karibu asilimia 95 ya wananchi wanategemea zao hili la Korosho, hivyo naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri mwenye dhamana na Kilimo kwa kazi nzuri anayoifanya kuhakikisha kwamba zao hili la Korosho linasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2021 sisi ni mashahidi, Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ilitoa pembejeo bure kwa wananchi wote wanaolima zao la Korosho. Wananchi wa Jimbo langu walinufaika sana, kwa hili nashukuru sana. (Makofi)

Mheshmiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, mwaka huu Waziri mwenye dhamana ametangaza kwamba wananchi wote watakaolima Korosho ndani ya Jimbo la Nanyumbu watapata pembejeo bure kama ilivyo mwaka 2021. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili naipongeza sana Serikali kwa kuhakikisha kwamba Maafisa Ugani walioko ndani ya wilaya yetu wanapewa vitendea kazi. Sisi ni mashahidi, karibu pikipiki 7000 zimetolewa na naamini kabisa lengo ni kuhakikisha kwamba kilimo kinasonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, tumeona Serikali imeongeza mitaji katika Benki ya Kilimo, Benki ya Kilimo iliyoanzishwa mwaka 2012 ilikuwa na mtaji na bilioni 60, Serikali imeongeza karibu bilioni 208, lakini Mfuko ule wa Ufaransa wa Maendeleo umeongeza karibu bilioni 210. Kwa hiyo kuna fedha nyingi ndani ya benki hii ambazo zina lengo kubwa la kuhakikisha kilimo chetu kinasonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio haya naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye korosho ili tuweze kuzalisha zaidi sio suala la pembejeo na viatilifu peke yake, kwa sababu ili korosho uweze kuvuna unahitaji kupalilia korosho. Katika hali ya kawaida, mkulima wa kawaida, hana uwezo wa kupalilia hekari 10 yeye mwenyewe kwa hiyo lazima ataajiri vibarua.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika korosho ili uweze kupata tija kupata mavuno mazuri, lazima upulizie korosho, unahitaji mabomba ya kupulizia, mafuta ya petroli, vibarua wa kukusaidia kupulizia, kwa sababu korosho una amka kati ya saa 8 usiku na saa 10 alfajiri kwenda kupulizia korosho, kwa hiyo lazima uajiri watu wa kukusaidia kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ili upate mavuno mazuri lazima uwe na vibarua wa kuokota korosho zako, debe moja la korosho tunaokota kwa sh.1,500, lakini pia korosho unahitaji watu wa kukusaidia kuhamisha kutoka shambani na kupeleka nyumbani.

Kwa hiyo vitu vyote hivi vinahitaji fedha. Sasa Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa kwamba kuna benki ambayo ya kumsaidia mkulima, naomba nitoe ushauri, wakulima hawa wapewe mikopo haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuwapa mikopo hii pembejeo na viatilifu itakuwa kazi bure kwa sababu mikorosho itakuwa porini watashindwa kupalilia, watashindwa kupulizia, watashindwa kuokota, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe benki zetu CRDB, NMB, zinatoa mikopo kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa wingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana kwa utaratibu huu huu wananchi walizalisha na Mheshimiwa Waziri ni shahidi, zaidi ya tani 26,000 zilizoongezeka, lakini bei ya korosho ilikuwa ndogo kuliko miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha aeleze ni mambo gani yaliyosababisha bei ya korosho kuteremka na je, wananchi wanaambiwaje kuhakikisha kwamba msimu ujao bei itakuwa nzuri. Mambo haya tusipoyafanya tunaweza kuwavunja nguvu wakulima wetu, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, hili ni jambo ndani ya wilaya yangu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri aliliingilia kati lakini bado halina ufanisi. Msimu umefungwa wakulima wa jimbo langu bado wanaidai Serikali, bado wanavidai vyama vya MAMCU zaidi ya sh.26,000,000, korosho wameuza, wamepeleka mnadani, mnada umefanyika, lakini wakulima bado hawajalipwa fedha zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ametoa agizo kwamba walipwe ndani ya wiki moja. Nashukuru tutafuatilia kwa pamoja kuhakikisha wakulima wale wanalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ahadi ya viongozi wakuu; viongozi hawa wetu wanapokuja katika majimbo yetu wanatoa ahadi. Naomba sana ahadi hizi ziwe documented lakini zitekelezwa kwa muda husika. Nina ahadi kule tangu ya Awamu ya Pili ya Mzee Mwinyi mpaka leo haijatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Kijiiji cha Mikuva Mheshimiwa Rais Ali Hassan Mwinyi aliahidi kujenga Kituo cha Afya mpaka leo haijatekelezwa, Waziri Mkuu 2018 aliahidi kujenga barabara za lami kilometa tano ndani ya jimbo langu, mpaka leo haijatekelezwa. Mama yetu Samia Suluhu Hassan wakati anainadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi aliahidi kutengeza barabara ya lami kutoka jimboni kwangu kupitia Selous hadi Morogoro mpaka leo haijatekelezwa na sijui itatekelezwa lini. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aeleze hizi ahadi za viongozi zitatekelezwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni kuhusu maji; maji ni uhai na ndani ya jimbo langu Mradi wa Maji kutoka Mto Ruvuma kuja Mji wa Mangaka ndio uliopo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Mheshimiwa Waziri alipokuwa anajibu hoja asubuhi alisema alisema hivi karibuni, sisi wananchi wa Jimbo la Nanyumbu tunataka kujua lini mradi huu wa maji wa Miji 28 utaanza kutelezwa lini tupate time, kwa sababu ukimpa mtu muda unampa matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tumenunua ndoo shilingi 2,500, mwananchi wa kijijini anapata wapi uwezo wa kuzalisha hiyo hela akanunua maji. Kwa hiyo naishauri sana Serikali, mradi huu ni mzuri na wa maana sana tuambiwe lini mradi huu utaanza ili wananchi wangu waweze kuwa na imani na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni la mawasiliano, tumeelezwa hapa Mkongo wa Taifa umeshafika Mtambaswala na umeunganishwa na Msumbiji, lakini nataka nikwambie kuna mambo ya ajabu sana ndani ya mkongo ule. Tulielezwa Mkongo wa Taifa faida zake kwamba, gharama za kupiga simu zitapungua, sidhani kama zimepungua. Tulielezwa mawasiliano yatakuwepo, mawasiliano mpaka sasa ni magumu, lakini pale Mtambaswala…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja naomba Serikali itekeleze hayo yaliyoelekezwa. Ahsante sana.