Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia fursa nami kuchangia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwenye maeneo makuu mawili, ambayo migogoro ya ardhi pamoja na uwekezaji wa tija kwenye malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba wananchi wanakuwa wanatwaliwa maeneo yao aidha na mwekezaji au na idara mbalimbali za Serikali. Tumeshuhudia, mathalani mimi tangu niko Bunge la Kumi hapa naongelea mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wananchi wa Bugoth na Kenyambi kule Tarime.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara ya mwisho Wizara ya Fedha iliandika barua kwenda kwa Halmashauri ya Mji wa Tarime Novemba 18 ikiwaeleza kwamba wameshapokea tathmini kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kwamba wanaenda kutoa fedha takriban bilioni 2.5 kwa ajili ya maeneo ya Tarime, Usule kule Tabora na eneo la Nyangurunguru Mwanza; ambapo kwa Tarime ni takriban bilioni 1.6. hata hivyo mpaka leo, walienda wakafanya tathmini na uhakiki wa mwisho na wakawaambia kufikia Februari watakuwa wamepeleka hela.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kufuatilia kwa Katibu Mkuu Hazina na hata kwa mama yangu pale, Mheshimiwa Stergomena Tax, tukahakikishiwa kwamba kufikia Machi hela zitaenda, lakini mpaka leo wananchi wa Tarime, Bugosi na Kenyambi hawajapatiwa hela na wanapata adha kubwa. Kama mnavyowajua, wenzetu wa Jeshi la Wananchi, ukikatiza kwenye maeneo yale unapigwa unapewa adhabu kubwa. Ng’ombe wakijitokeza wakiingia wanapigwa faini kubwa, mpaka laki tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba, kwamba hawa Watanzania ambao wamezuiliwa kufanya uendelezaji wowote ule; kuanzia mwaka 2010 mpaka leo, walipwe fidia ili waende maeneo mengine wakafanye uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa ninasema hapa, kwamba kama wameshindwa kulipa fidia basi Jeshi hili lirudi kule Nyandoto ambako kulikuwa na kambi yake ili wale wananchi nao waendelee na uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kuhusu uwekezaji wa Barrick. Kuna maeneo ambayo walifanyia tathmini kule Nyamongo, maeneo ya Nyamichele na kwingineko. Kwa mfano Nyamichele pale zaidi ya wananchi 2,000 mpaka leo waliwakatia mazao yao wakaonesha kwamba wanaenda kuwalipa lakini hawajawalipa mpaka leo, wale wananchi wanasubiria hawajaweza kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba, tunapokuwa tunatoa hizi ardhi basi tuhakikishe tunalipa fidia kwa stahiki kwa mujibu wa sheria inavyosema; msiendelee kuwatia umaskini, hawajiendelezi hamuwalipi hela wanakaa tu; ili waweze kwenda sehemu waweze kuzalisha na kuweza kuongeza tija kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ni uwekezaji wa tija kwenye malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ambayo yanaanzia mwaka sifuri mpaka nane. Sote tunatambua kwamba mtoto hata ubongo wake unakuwa kwa asilimia 90 katika umri huu. Na nimesema niongelee hili hapa kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu ndio waratibu na wasimamizi wa program jumuishi ya miaka mitano ambayo mmeianzisha, na ambayo ndiyo ya mama; sasa nikasema niongee na nitanabaishe changamoto ambazo tunakutana nazo na ni vipi tutazitekeleza. Tusiishie kuwa na document tu, tuna document nzuri tunai-document lakini kiuhalisia (in practiclal) unakuta haifanyiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba watoto hawa umri wa miaka sifuri mpaka nane ni takriban milioni 16.5, ambao ni kama 30% ya population tuliyonayo. Katika program hii inaeleza kwamba kumsaidia mtoto katika kumlea, kumlinda, kumuhudumia kupata elimu bora ya awali, kuwa na afya bora, lishe bora kuhakikisha kwamba hadumai na mengineyo. Kuanzia kwanza mama akiwa mjamzito mpaka anazaliwa anafikisha miaka nane.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa Tanzania ni tofauti kabisa. Sote tunatambua kabisa kwamba kama Serikali ingefanya uwekezaji wa tija kwenye eneo hili ina maana umeshamjengea huyu mtoto foundation, tunakuwa na rasilimaliwatu yenye tija ambao wanaenda kulijenga taifa kwa baadaye. Tusipowekeza katika foundation ya umri huu ina maana tutaendelea kuwa na Taifa ambalo kwa kweli hatutaona hata huo uchumi unatamalaki. Tutajiegeza aidha kwa kutegemea ma-experts kutoka sehemu nyingine; kwamba, hatutakuwa na watu ambao ni analytical, watu ambao wamepevuka na ubongo wao umekuzwa vizuri, hawajadumaa, hawajashambuliwa na magonjwa mbalimbali, wamepata elimu ya awali vizuri na wanaweza kuwa hivyo. Kwa hiyo ni lazima tuwekeze.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti mbalimbali zimefanyika na zinaonesha kwamba leo ukiwekeza dola moja kwa huyu mtoto au katika hizi program za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto faida yake au uzalishaji wake ni dola 17 za kimarekani. Lakini pia umeona kwa Watanzania zaidi ya asilimia 43 ya hao watoto hawafikii ukuaji timilifu, hawapati haya malezi kama yanavyotakikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia ukatili, mathalani nitatoa mfano kwenye ukatili tu, maana tunatakiwa tuwekeze kwenye lishe, elimu ya awali, kwenye kuhakikisha mtoto anahudumiwa vizuri na tuwekeze kwenye kumlinda; na naangalia hapa kwenye kumlinda na usalama wa huyu mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matukio ya kikatili dhidi ya watoto kwenye taifa letu ambayo yamekuwa ni mwendelezo. Nita-site tu mfano ambao nimeshuhudia kwa wiki moja tu hii, na nitaanza jana kwenye Jimbo la Shinyanga Mjini la Waziri Patrobas pale. Kuna mtoto wa mwaka mmoja na miezi 18 amebakwa na baba wa kambo au baba yake mlezi. Amepelekwa hospitali Kambarage pale, wakapelekwa Government Hospital wakasema wakampa referral kwenda Bugando. Yule mtoto ameharibiwa kwa kutobolewa kote, mbele na nyuma. Inasikitisha sana! Inasikitisha sana! Mtoto wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja!

Mheshimiwa Naibu Spika, na haya matukio ni mengi, mengine yanakuwa reported mengine si reported. Kama taifa huyu mtoto hata akipona atakuwa affected kisaikolojia. Sasa wako wangapi kama hawa kwenye taifa letu? Tunachukua hatua gani dhidi ya haya yanayoendelea?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tena nilikuwa naangalia taarifa ya habari juzi kule Songea Shule ya Msingi Tembo Shujaa sijui kijana wa miaka 19 amebaka na kulawiti watoto wa Shule ya Msingi zaidi ya nane, wadogo! Lakini kuna siku tulikuwa tunapata semina hapa, dada yangu Jesca hayupo leo, kule Iringa watoto wadogo wamelawitiwa na kubakwa! Sasa what are we doing? Mnafanya nini? Yaani tunafanya nini kama taifa? Kwa sababu hata hizi sheria tunazoziweka mimi naona kama vile zinakuwa loose. At a time unafikiri hata hao watu wawe wanahasiwa kabisa or even you remove that part ili jamii iweze kukaa vizuri, kwa sababu its unbecoming kabisa kwa taifa; its unbecoming.

Mheshimiwa NaibU Spika, kwa hiyo we end up documenting these things lakini hamna implementation so ever. Inaumiza sana! Inaumiza sana kama taifa; na kama mzazi kwa kweli naumia; kwa sababu pia nina watoto wadogo wa kiume na wa kike huwezi kujua huko wanafanyiwaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumeshuhudia watoto hawa wananyanyasika wanauawa majumbani; yaani kuna mambo mengi sana. Mimi nafikiri tutafute approach nzuri ya kuhakikisha kwamba tunatatua hili tatizo. Tutafute the better approach.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri yafuatayo; moja; Serikali kama imedhamiria kutekeleza huu mpango itenge bajeti ya kutosha na katika hizi bajeti najua kuna settle means ziko huku katika kila Wizara ihakikishe ina kifungu kidogo cha bajeti kwenye Wizara husika; Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya TAMISEMI yenyewe pamoja na Wizara ya Elimu Sayansi ya Teknolojia ili sasa tuweze kutekeleza kwa ukamilifu kwa kila mtu pale inapomgusa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tuhakikishe basi kunakuwa na uratibu na usimamizi wenye tija kuhakikisha kwamba hawa watoto tunawalinda na wanakua kwa ktimilifu, yaani tusiishie ku-document ndugu zangu! naongea kwa ku-bold! Tukiishia ku-document hizi paper hatutafika popote pale tutakuwa na taifa ambalo limekuwa affected kisaikolojia, tutakuwa na taifa ambalo haliwezi kuzalisha kwa tija…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho dakika moja tu kwenye elimu ya awali ili watoto waweze kupata hizi elimu mbadala walimu ni wachache...

NAIBU SPIKA: Haya, sekunde moja.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaleta kwa maandishi ahsante sana.