Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Na mimi naomba nichangie Muswada huu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Sengerema kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza Wabunge wenzangu wakichangia kuhusiana na suala la mafuta na kulalamika bei ambazo zinavyopanda sasa hivi bei zimefikia katika kiwango cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia ya nchi hii. Naomba nirejee kidogo kwa ajili ya kuweka hansard ikae sawa.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1982, 1983 na 1984 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata tatizo (crisis) ya mafuta ikabidi kutumia mafuta ya furnace; lakini wakati huo yalikuwa ni masuala ya kiuchumi, ambapo Mheshimiwa Hayati Julius Kambarage Nyerere ilimlazimu sasa kwa kutumia TPDC alikwenda Algeria, Saudi Arabia na kwa wenzetu Kuwait wakakubali kutupa mafuta hali ikaja ikawa nzuri.

Sasa hali inavyokuwa mbaya kama kwa sasa hivi ambako tunakoelekea ni suala sasa la Mheshimiwa Rais tunamuomba, mama yetu Samia Suluhu Hassan sasa ni wakati wa kwenda mwenyewe mahala ambapo kuna hali ngumu kama hii mama asafiri yeye mwenyewe Rais wa nchi akazungumze na hawa wazalishaji wa mafuta ili tuweze kupata mafuta ya gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, huu mfumo wa PPBA mimi nakumbuka ulianzishwa kama si 2012 ni 2014, na leo hii mfumo huu una miaka 10. Si vibaya kama nchi kuangalia, kwamba je, mfumo huu bado uko sahihi tuendelee sisi kama nchi kuutumia? Sisi kama nchi mfumo huu je, una madhara gani na una faida gani kwetu?

Mheshimiwa Spika, faida ya kwanza iliyopo kwenye mfumo wa PPBA ni kwamba tunaweza kutathmini na kutabiri kodi yetu ya mapato kwa miezi miwili, kwa sababu kuna mafuta yatakuwa yameagizwa kwa miezi miwili tunajua kodi yetu tunayokuja kuikusanya hiyo ni faida kubwa ya kwanza. Ya pili ni kupata uhakika wa kuwa na mafuta katika miezi miwili inayokuja

Mheshimiwa Spika, lakini yako madhara sasa ambayo yanaletwa na taasisi hizi mbili, PPBA pamoja na EWURA. Taasisi hizi ni kwamba ziko chini ya Wizara ya Nishati. Hawa wenzetu wa EWURA mguu mmoja wako Wizara ya Maji, mguu mmoja wako Wizara ya Nishati; na hao ndiyo wanaokuja kupanga bei ya mafuta, hao, kwa mamlaka ambayo iliyopitishwa na Bunge, ndio wanaokuja kupanga bei ya umeme. Sasa hii EWURA iangaliwe iwekwe wapi kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na hili suala la PPBA, ni kwamba yeye ndiye anayepokea zabuni za mafuta, zabuni za uagizaji wa mafuta na zabuni za utangazaji wa bei ambazo yeye anajua sasa kwamba fulani ameshinda kutokana na hali hii.

Mheshimiwa Spika, tunalo Shirika letu la Mafuta (TPDC) Shirika hili a mafuta wakati wa marehemu Rais Julius Kambarage Nyerere pale Tipper aliwekeza yeye pamoja na wenzetu wa CALTEX kutoka Italy, Tanzania ikawa na asilimia kama sijasahau 51 au 49; lakini nafikiri ni 51 CALTEX wana asilimia 49. Hata hivyo, Baba wa Taifa hakuishia pale, ni kwamba tukawa na shirika letu la BP. Katika BP Serikali ikawa ina asilimia kule 51 na BP wakawa na 49. Hii inaonesha namna gani Baba wa Taifa alikuwa amejiandaa kukabiliana na hii hali. Sasa kule Caltex wana 49 na huku BP wana 49 hizo ni sehemu ambazo mafuta yetu sisi yangeweza kupitia katika angle hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini huyu TPDC anazalisha gesi pia. Si kwamba hana mtaji lakini pamoja na kuwa anazalisha gesi anaidai TANESCO. Mpaka Januari mwaka huu TPDC peke yake anaidai TANESCO bilioni 502. Ukichukua mwezi huu wa Februari ukachukua na Machi na sasa hivi huu mwezi huu wa Aprili utakapoisha TPDC atakuwa anaidai TANESCO bilioni 652. Huyu TPDC ni kwamba anayo kampuni tanzu inaitwa TANOIL ambayo imetengenezwa kwa ajili ya ku-supply mafuta kwa nchi kama hali ya nchi inakuwa mbaya. Tumekwenda kuanzisha TANOIL wakati tayari sisi kule PUMA tuna asilimia 51. Tumekwenda kuanzisha kule kwenye Tipper kule kuna CALTEX ambako kuna storage kubwa ya kuhifadhi mafuta; zaidi ya lita milioni 300 tunaweza tukahifadhi pale Tipper. Pia, bado tungeweza kujenga uwezo pale Tipper tukaweza kuhifadhi mafuta yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa leo TPDC anadai bilioni 652 na hana mtaji; sasa hili linakuwa ni tatizo kubwa sana. Mimi ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba wamlipe, waje hapa wanatueleza kwamba wanamlipa lini TPDC apate pesa ya kuagiza mafuta. Mashirika kama haya yako nchi zote duniani. Ukienda Algeria, Misri nan chi nyingine zote zinazotuzunguka ina nguvu kubwa, isipokuwa sisi Tanzania hili Shirika limekuja kuonekana mfu kama halina kazi. Lakini kama tungekuwa tumeagiza mafuta yetu ikitokea shida tunafungulia mafuta yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa nakupa mfano, TPDC ameshinda tenda ya Januari kwa premium ya kuagiza mafuta bei ya gharama ya mafuta kuyaleta hapa Tanzania kwa dola 26, amekuja kuomba mwezi wa pili amenyimwa kazi, amekuja kuomba mwezi wa tatu huu amenyimwa kazi. Uzalendo hakuna huko PPBA.

Mheshimiwa Spika, tunamuomba Mheshimiwa Rais tunamuomba aiangalie PPBA kwa haraka mno hawa ni watu ambao watamletea tatizo kubwa kwenye nchi hii. Vilevile Mheshimiwa Rais aiangalie EWURA; hatuwezi kukubali. Tarehe 22 imekuja meli ina mafuta, hii meli ilikuwa inaitwa MTSL Falcon, ilikuwa na tani 39. Watu wa TBS wamekwenda kuipima wakasema kwamba asilimia 90 ya vyumba vingine mafuta yake yako bora asilimia 10 mafuta si mazuri. Hawa Adax ambao ndiyo walikuwa wamepewa tender wakaondoa ile meli wakaipeleka Beira.

Mheshimiwa Spika, kuagiza yale mafuta tayari Serikali imepoteza bilioni sita, sawa na bilioni 14 ilhali yale mafuta asilimia 90 yangeshushwa na asilimia 10 iliyobakia yale ndiyo yakarudishwa; lakini yale mafuta yakaachwa yote yakaondoka yakaletwa mafuta mengine na zile LC zilizokuwa zimefunguliwa zikabadilishwa. Uzalendo! Uzalendo ni bidhaa adimu sana katika nchi hii. Huyu Mheshimiwa Rais tutamsaidiaje kwenye hali kama hii? Hili ni tatizo kubwa sana mfumo wa tender wa PPBA uangaliwe.

Mheshimiwa Spika, na hivi tunavyozungumza na wewe leo kuna kampuni ambazo tayari zimeshinda tender ya kuja kuua wananchi. Leo kuna kampuni iko hapa, naangalia Adax huu mzigo uliokuja alikuwa na dola 28 kwa premium kwa usafiri wake, kuna hawa Vitol Bahrain wakapewa dola 72. Yaani kuna mtu amepewa tender ya dola 28, kuna mtu amepewa tender ya dola 72 kwa tani. sasa dakika hizi na jambo hili ni kubwa sijui nifanyeje nakuomba sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja malizia, unaweza ukachangia kwa maandishi mchango utafika tu, dakika moja malizia.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Amepewa Agusta kwa dola 53, amepewa traffic Gula kwa dola 44,000, akapewa TPDC kwa dola 26 inauma sana. Leo huyu TPDC ana kosa tender yuko PUMA ndiyo mwenye hisa na sisi anakosa tender. Nchi hii naomba mengine yaliyobakia niyaache kwa usalama wa Taifa ahsanteni sana. (Makofi/Kicheko)