Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, mimi leo nitaongea kwa kifupi, kwanza nianze kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi, nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Kwanza wa Rais, Waziri Mkuu pamoja na Baraza la Mawaziri lote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maendeleo ya nchi yanaletwa na Serikali pamoja na wananchi. Naomba niseme kwamba, kwa kipindi hiki cha Awamu ya Sita mwaka wa kwanza, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya kazi kwa bidii zote sana na sisi tulioko huko Majimboni wananchi wanaendelea kufarijika. Mpaka hapo nafikiri nimeanza kwa kifupi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niingie kwenye jambo ambalo nataka kulichangia kwenye hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba nichangie jambo moja tu, sekta ya uzalishaji, Fungu Namba 37 - Kilimo.

Mheshimiwa Spika, nikiongea kilimo kama Mbunge wa Same Mashariki, zaidi ninakwenda kugusa kilimo cha tangawizi. Nagusa kilimo cha tangawizi kwa sababu, ndani ya Jimbo langu mimi Tarafa mbili zote, Tarafa ya Mambavunda na Tarafa ya Gonja, wananchi wanategemea kilimo cha tangawizi, lakini nikizungumza kwa Tanzania, Tanzania kuna Mikoa ambayo inalima tangawizi sana, Ruvuma inalima tangawizi, ukija Mbeya wanalima tangawizi, Morogoro wanalima tangawizi na Mikoa mingine imeanza kulima tangawizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba kwa Tanzania niachie hapo, sasa nije kwenye tangawizi ulimwenguni.

Mheshimiwa Spika, hili zao sisi watanzania, zao la tangawizi, tunaliona kama ni zao ambalo halihitaji kipaumbele kabisa, naweza nikasema tunalipuuza. Twendeni duniani huko, tuanze na India. India kwa ulimwenguni ni Taifa la kwanza kwa kulima tangawizi, nakiri kwamba, wao hawa- export zaidi kwa sababu wao wenyewe kama India wanakula sana tangawizi, lakini ukiangalia India kwenye soko la dunia anapeleka asilimia 43.81 karibu anafikia asilimia 50. Na hizi data ninazizungumza nazipata August mwaka 2021, mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi ya pili ni Nigeria. Nigeria ni Taifa liko Afrika, lakini Nigeria ni namba mbili duniani kwa kupeleka tangawizi kwa wingi kwenye soko la dunia. Anapeleka asilimia 16.94 ni nchi ya Afrika hiyo. Nchi ya tatu ni Uchina.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi leo niongee kwa wivu, roho inaniuma. Ukiamuangalia Nigeria vizuri, naomba ndugu zangu mum-google vizuri, Nigeria analima tangawizi vizuri sana anapeleka kwenye mfuko wake wa Taifa, GDP anapeleka kutoka kwenye tangawizi anapeleka asilimia 23, siyo ndogo. Asilimia 23 kwenye GDP itoke kwenye tangawizi, siyo kidogo, ina maana Nigeria wanafanya kazi kwa bidii kuliangalia zao la tangawizi.

Mheshimiwa Spika, ukija ukimuangalia Nigeria huwezi kumtofautisha sana na sisi. Mimi nimeangalia kwa nini yeye anapeleka asilimia 23 kwenye GDP ya Taifa lake, ni kwamba Serikali imesimama imara sana kwenye kilimo cha tangawizi kwenye nchi ya Nigeria, imesimama imara kwa kuboresha miundombinu ya kilimo cha tangawizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi kwa nini naongea kwa wivu? Serikali ya Tanzania inashindwaje?

Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2000 niko humu ndani ninaongelea tangawizi, ninazungumzia tangawizi, ninazungumzia tangawizi. Serikali inasema hivi, inasema vile, naomba kipindi hiki, nazungumza kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini Waziri wa Kilimo asimame awajibu Watanzania wanaolima tangawizi kwa nini hili zao tunaliweka kama ni zao si kipaumbele?

Mheshimiwa Spika, nirudi tena niongee kwa uzito na ninyi mtani-support. Mwaka 2019 tulipata Covid 19, tangawizi ndiyo iliyotusaidia sana. Kila Daktari akisimama kuleni tangawizi, kila Dakrati akisimama tumieni tangawizi, lakini zao hili Serikali naomba nizungumze kwa uchungu, sikufurahi sana hakuna Waziri wa Kilimo, lakini hakuna hata Naibu Waziri wa Kilimo, anyway atasoma kwenye mitandao, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuliangalia hili zao vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa huu ni mwaka wa 22 nikisimama ni tangawizi mpaka wengine wananiita tangawizi, lakini it is fine. Naomba Serikali kipindi hiki izungumze inaiangaliaje tangawizi kwenye nchi hii?

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Same Mashariki wanaongoza kwa kile kilimo, lakini mioundombinu ya kilimo cha tangawizi Same Mashariki inaumiza roho. Wananchi wanatengeneza wenyewe hakuna wataalam, lakini bado wanaongoza kwa kulima kilimo hiki. Serikali iseme kwa nini haipeleki wataalam wa tangawizi, zile sehemu zinazolimwa tangawizi?

Mheshimiwa Spika, nimekwenda Madaba nikalima tangawizi eka 20, nimelima kule, miundombinu ni hivyohivyo kama Same Mashariki, hapana! Upande wa kilimo, Serikali nazungumza kwa malalamiko hamjawa serious. Upande wa zao hili la tangawizi wala hamlijali, lakini tulipopata Covid…

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Anne Kilango Malecela kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge.

T A A R I F A

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nampa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Anne Kilango Malecela kwamba, anayoyazungumza ni sahihi kabisa, Serikali yetu siyo tu haijalipa kipaumbele zao la tangawizi, lakini haijatoa kipaumbele kwa mazao yote ya viungo nchini Tanzania ambayo yanaingiza fedha nyingi nchi za jirani. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Anne Kilango Malecela unapokea taarifa hiyo?

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, napokea na ninamshukuru sana Mheshimiwa.

Mheshimiwa Spika, wakati namalizia nikwambie ukweli kabisa Serikali isimame imara kuangalia haya mazao. Inachagua mazao kidogo inayafanyia kazi, haya ambayo inayapuuza kwenye nchi nyingine kama Nigeria yamepeleka asilimia 23 kwenye GDP ya nchi. Sasa ninajiuliza aah! kwani hawa wa-Nigeria wao wakoje, sisi tukoje?

Mheshimiwa Spika, ukiangalia hali ya hewa ya Jimbo la Kaduna kule Nigeria ndiyo hali ya hewa iliyopo Ruvuma, ndiyo hali ya hewa iliyopo Kilimanjaro. Serikali imechukua serious sana mazao ya viungo, lakini sisi tunayapuuza, hapana. Serikali katika hili mimi sitakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimejitahidi nilipoingia mwaka 2005 Jimbo la Same Mashariki, nilipoona wale wananchi wanalima sana tangawizi, nilianzisha ujenzi wa kile kiwanda. Naishukuru sana Serikali, nashukuru mbia aliyekuja kutuunga mkono kujenga kile kiwanda cha tangawizi pale Same Mashariki. Ukweli sasa tunagawana sisi pamoja na mshirika mwenzetu, lakini bado sasa hivi nazungumza tena nikiwa ninajivuna, Tanzania, Mamba Miamba tuna kiwanda cha kusindika tangawizi ambacho Afrika Mashariki hakipo, lakini Serikali inatusaidiaje? Tuna kiwanda, kilimo kiko wapi?

Mheshimiwa Spika, kile kiwanda ni kikubwa mno, kinahitaji tangawizi nyingi sana. Serikali isipokuwa imara kuboresha kilimo cha tangawizi hata kile kiwanda kitakuwa hakina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nasema ahsante sana. (Makofi)