Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kutoa mchango wangu katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha vyema Hotuba yake lakini pia, nawapongeza Mawaziri wote walio katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge na Waziri wa Nchi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, nawapongeza sana. Nchi yetu imekuwa ikifanya vizuri katika hatua za maendeleo pamoja na changamoto zinazotukabili za ndani ya nchi na nje ya nchi. Lakini bajeti hii iliyowasilishwa leo naamini itatuvusha na kutufikisha mahali pazuri. Kuna maeneo ya huduma za jamii tumepiga hatua nzuri, lakini napenda kutoa ushauri pia kuna maeneo tunahitaji kuongeza juhudi za kutosha, ili kuweza kusaidia mahitaji ya kufanikisha kwa ufanisi maendeleo ya huduma za jamii kwa wananchi wetu kama tulivyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dunia imebadilika inakabiliana sasa hivi na changamoto kubwa ambazo na sisi zinatuathiri kiuchumi na kijamii. Hivyo, sisi kama nchi hatuna budi na sisi kukaza mkanda ili tuendelee kuwaendeleza wananchi wetu kiuchumi na kijamii. Katika kipindi hiki cha Serikali ya CCM Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tumeona Serikali ikifanya mambo makubwa ya kuendeleza hasa miradi ile mkakati iliyoanzishwa, lakini kuanzisha miradi mipya ya huduma za jamii. Shule zimeejengwa, vituo vya afya vimejengwa, hospitali za wilaya na mikoa zimejengwa na zinaendelea kujengwa. Miradi ya maji inaendelea kujengwa na kazi zingine zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii pia pamoja na miradi hiyo inayojengwa inahitaji watu wa kwenda kuifanya kazi. Kwa hiyo, naomba niishukuru Serikali kwa kauli yake leo iliyotoa hapa Bungeni kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama ya kuwa Serikali inategemea kutangaza ajira 32,000. Hii ni taarifa njema ni taarifa muhimu na yenye afya, kwani katika maeneo ya afya na elimu sasa hivi tunahitaji sana watumishi. Kama nilivyoeleza hapo awali tumejenga majengo ya afya, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya tunahitaji watu wa kwenda kutoa huduma na hili likikamilika dhamira ya Serikali ya kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo haya ya elimu na afya itakuwa imetimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya afya ina unyeti wake inahitaji pia kufanyika uchambuzi wa kina ili kuangalia madaktari na madaktari bingwa, manesi na manesi bingwa wa maeneo yote, tunahitaji wangapi katika hospitali zetu na kwa sasa tunao wangapi? Ili kukidhi mahitaji hayo inatubidi tuchukue muda gani kuwapata hao wapya. Tukishajua hilo, tutaweza kupanga mkakati mahususi kabisa kwa ajili ya kuwatafuta na kuwapata hawa wataalam wetu. Wiki iliyopita nilisoma kwenye gazeti la Uhuru Mheshimiwa Waziri wa Afya alikuwa anaeleza kwamba tuna wataalam wa ubongo na wa mishipa ya fahamu 16 tu, lakini kwa population tuliyonayo sisi nchini takribani milioni 60 tunahitaji wataalam hao wawe kama 600. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna upungufu wa wataalam bingwa huo ni mfano tu. Kwa hiyo, hatuna budi tuweke mkakati mahususi wa kuona tunapataje wataalam bingwa kwa ajili ya kwenda kuhudumia wananchi wetu. Leo tumenunua vifaa vya kwenda katika hospitali za mikoa, hospitali za wilaya, tunahitaji watumishi ambao wataweza kuhudumia katika vifaa tiba hivyo. Pamoja na ajira mpya Serikali imetangaza leo, naomba iangalie pia na replacement za ajira za watu wanaokufa, wanaostaafu, wanaoacha kazi wenyewe, wanaofukuzwa kazi na replacement haiathiri wage bill. Kwa hiyo, Serikali iendelee kuangalia tunafanya replacement na eneo hili ndio tunalolipoteza sana la wataalam bingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali iangalie sana. Jana Profesa hapa wakati anauliza swali alitoa na pendekezo kwamba, wale wataalam/Madaktari Bingwa tuwaongezee muda na tuna pengo kubwa la wataalam bingwa kama nilivyoeleza awali. Kwa sababu, pia tulisahau hii replacement. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali iangalie kundi hili pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la uzalishaji. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali hatuna budi kuedelea kuliangalia kwa karibu sana na kuliwezesha na kulipa fursa zaidi eneo la uzalishaji. Eneo hili tukiliangalia kwa karibu wananchi/wawekezaji watapata fedha na Serikali itapata fedha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilitoa ushauri kwamba tunajenga SGR Standard Gauge Railway, lakini huko njiani kuna eneo kubwa sana ni porini. Nikasema sekta ya kilimo, sekta ya maliasili na sekta za viwanda zianze kufanya utafiti kuangalia maeneo gani inakopita hii reli kwenye mapori tunaweza tukapanda mazao ya miti. Pia, tunaweza tukaweka eneo la utafiti la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)