Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia. Kwenye bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na nitachangia Fungu 65 - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia specific kwenye eneo moja sana kwenye maendeleo ya vijana kwa sababu pamoja na kwamba tunafanya sensa mwaka huu lakini sensa ya mwisho kufanyika bado imeonesha kwamba nguvu kazi ya Taifa sehemu kubwa sana ni vijana na hatuwezi kuzungumza maendeleo ya vijana bila kuangalia mambo ambayo yanawakabili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kwamba baadhi ya Mawaziri na Mawaziri wengi sana hawapo hapa na kuna vitu ambavyo tunaongea vingine vinaingia kwao moja kwa moja. Kwa hiyo niseme hivyo, lakini kwenye kitengo na segment kuu ya maendeleo ya vijana kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye upande wa Sera ya Maendeleo ya Vijana. Mwaka 2019 vijana wa nchi waliitwa kutoka maeneo mbalimbali wakakaa wakajadili na wakapitisha kwa kutoa mapendekezo yao kuhusu namna ambavyo tunaweza tukawa na Sera ya Maendeleo ya Vijana yenye tija. Mpaka sasa ni miaka minne Sera ya Maendeleo ya Vijana ambayo kimsingi ndiyo inayotoa dira ya shughuli za vijana kwenye nchi, sera inatoa dira kwenye masuala ya Maendeleo ya Vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunafahamu wote kwamba life span yaani umri wa kuishi sera ni miaka 10. Kwa hiyo mpaka sasa hivi katika miaka 10 ya sera ya vijana tumeshakula miaka minne mpaka sasa hivi hatujui nini kitakachofuata, lakini kimsingi watu wanatakiwa wajue. Kwa hiyo wakati sera inakuja tayari imeshakula miaka minne bila kutekelezwa na kimsingi nina sera hapa ambayo kuna baadhi ya vitu tayari vimeshakuwa outdated, vimeshapitwa na wakati ambapo pia inatakiwa irudishwe ikapitiwe upya ndiyo iende tena kutekelezwa, four years. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuzungumzia Maendeleo ya Vijana bila kuzungumza uwezeshaji wa vijana kiuchumi. Kamati imetoa mapendekezo yao na nimekuwa nikisoma taarifa za Kamati miaka kadhaa ya nyuma siyo mwaka tu wa leo na leo pia wamezungumza kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Mfuko huu umekuwa ni kichomi na kimsingi nilikuwa nasoma pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi hapa kuanzia ukurasa wa 26 mpaka ukurasa wa 30 wanazungumzia masuala ya vijana, lakini mwelekeo wao umejiwekeza katika kutoa semina, kufanya warsha, kufanya makongamano na kujengea uwezo vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imetosha kujengea uwezo vijana, tunataka Mfuko usaidie vijana kujiendesha kiuchumi. Serikali haiwezi kuajiri vijana wote, soko la ajira linatoa watu wengi sana, haiwezekani, kwa hiyo lazima Mfuko huu usaidie vijana kujitegemea kujiajiri na kulipa kodi kuchangia maendeleo ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia taarifa hata Kitengo cha Ofisi ya Waziri Mkuu pia na wao wanazungumza ni semina, makongamano, warsha na kujengea uwezo, inavunja moyo kwa sababu sasa hivi kuna kitu kinaitwa startups mmekuwa mkisikia, inawezekana watu hawaelewi nitafafanua startups business ni biashara ambazo ni za Watanzania zimebuniwa humu, yaani vijana wetu wa Kitanzania wanabangua bongo zao wanaandaa biashara kwa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kuitikia mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani, lakini kuitikia maendeleo ya viwanda yaani mapinduzi ya nne ya viwanda. Sasa vijana hawa kuna vitu wanahitaji kufanyiwa hawahitaji warsha na makongamano, walishatoka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, startups za Tanzania kuna kitu kinaitwa Tanzania Startups Association ambayo ndiyo imeunganisha startups za Tanzania ambazo zipo 587. Waheshimiwa wana vishikwambi, wachukue tabulates zao, wa-google Tanzania Startups Association wataona jinsi ambavyo vijana wetu wanabuni vitu vikubwa ambavyo wengine wanashinda mpaka tuzo Afrika. Kuna startup inaitwa Agree Info wameshinda katika nchi 19 Afrika, lakini sisi tunajadili warsha na makongamano yaani irrelevant kabisa, yaani tunakuwa hatulingani na jinsi vijana wanataka twende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa wanabuni vitu ambavyo ni vya kielektroniki, wengine wanahitaji vitu vidogo vidogo kwa mfano, badala ya kujadili warsha na makongamano, tujadili ni namna gani tunatunga sheria kwa ajili ya kuzilinda startup business. Tutunge sheria, sasa hivi ninavyozungumza nilikuwa napitia Kenya, Kenya mwaka 2020 mwezi wa Tisa wamepeleka Bungeni Muswada wa startups Kenya kwa ajili ya kuzilinda biashara za kiteknolojia ndogo ambazo zinaanzishwa na vijana wa Kenya. Sasa si kitu kibaya kuiga kwa wenzetu kama kuna kitu kizuri kinafanyika, si mpaka tuchelewe sana, tuje mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kitu kingine mfano mzuri wa startup ya Tanzania ni ile gari ya juzi ya Masoud Kipanya ile ni ya ndani, Masoud ameanzisha kile kitu from the scratch ameagiza mitambo kutoka nje. Sasa kama vijana wetu wapo wengine ambao wanaagiza mitambo kutoka nchi mbalimbali kwa maana ya kuja kuhakikisha wanakuja kutengeneza vifaa vyao vya kielektroniki basi tuwaondolee VAT kwa ajili ya kuwa-support na kuhakikisha kwamba tunakuza ubunifu katika nchi yetu. Sasa haiwezekani Wizara ambayo ita-deal na masuala ya Vijana inajadili warsha na makongamano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo ninawe nikazungumza, sasa hivi ni miaka saba tangu Bunge hili litunge Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa, na ni miezi saba tangu Mheshimiwa Rais aongee na Vijana wa Tanzania kupitia Jukwaa la Vijana wa Tanzania kupitia jukwaa la Vijana wa Mkoa wa Mwanza kutoa maelekezo tuunde Baraza la Vijana wa Taifa. Sasa sitazungumza faida yake lakini nataka tu muone double standard, Zanzibar kuna Baraza la Vijana la Taifa, hawawezi kupata kitu chochote kwenye kuiwakilisha nchi kwa sababu Zanzibar siyo nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumza kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki wameanza mchakato wa kuanzisha Baraza la Vijana la Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini Vijana wa Tanzania hawatashiriki kwa sababu sisi tunaendekeza siasa mpaka kwenye mambo ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fursa mbalimbali ambazo Vijana wa Tanzania wanaweza kuzipata, sasa labda tuulize Serikali hivi ni kweli mnataka kuwanyima vijana wa Tanzania fursa za kushirika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Vijana wenzao?

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa!

T A A R I F A

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa ndugu yangu Nusrat Hanje, kwa kusema kwamba Zanzibar siyo nchi. Kwa hiyo naomba atufafanulie hapa. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Hebu zungumza tena hoja yako.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Hoja yangu nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Nusrat Hanje kwamba Zanzibar ni nchi, kwa hiyo naomba aipokee hiyo taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru na ninaelewa concern ya ndugu yangu hapa, lakini katika representation katika uwakilishi wa nchi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki haiwi-considered kama nchi, sitazungumza hapo zaidi lakini ninajua concern yake na ninafahamu na ninaheshimu masuala yote ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hatuna Baraza ambalo lingeweza kuwa chombo kiunganishi, kimsingi hata Mheshimiwa Rais anajua hilo Ndiyo maana hata yeye ndiye aliyezindua Baraza la Vijana la Zanzibar akiwa Makamu wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Nne ambayo ndiyo ya mwisho nitazungumza leo ni katika maendeleo ya vijana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kuna kitu kinaitwa Mbio za Mwenge wa Kitaifa.

Ninafahamu, ninaheshimu na ninatambua umuhimu wa mbio za Mwenge za Kitaifa kwa maana ya Mwenge wa Uhuru. Ni kitu ambacho tumeki-respect na tunakiheshimu sana, ni kitu ambacho kimefanya vitu vikubwa kwenye hii nchi. Lakini kama Mfuko wa Vijana kwa mwaka unatengewa bilioni moja haipelekwi kwa sababu hakuna pesa na tunakimbiza Mwenge nchi nzima kwa ajili ya kumulikia umoja, amani, upendo na mshikamano, tunaviheshimu sana na tunavihitaji sana kwenye nchi, lakini mimi nafikiri tufikiri kuna haja ya kuendelea kutumia gharama kubwa ambayo kimsingi hatuzijui, kwa sababu labda mimi ni mgeni, lakini sijawahi kuona Bungeni inajadiliwa Bajeti ya mbio za Mwenge za Kitaifa, hatujui wala sijawahi kusoma ripoti ya CAG imejadili kuhusiana na gharama za Mwenge na tunaheshimu na naomba ieleweke hivyo. Lakini hivi hatuwezi kutumia ubunifu mwingine kwa ajili ya kuenzi na kuheshimu Mwenge huu ambao kimsingi Luteni Kanali Alexander Nyerenda alianza yeye kwa kwenda kuweka pale juu na tunaheshimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaweza kukosa Bima za Afya kwa wote kwenye nchi lakini tusikose pesa ya kukimbiza Mwenge tunakuwa hatutendei haki Vijana wa Taifa hili. Ninasema hivi ili Vijana waelewe mbio za Mwenge kwenye Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu zipo upande wa maendeleo ya Vijana. Kwa hiyo, vijana wajue kwamba kama kuna mambo yanashindikana maana yake ni kwa sababu tunakimbiza Mwenge! Yaani haijawahi kukosekana pesa ya kukimbiza Mwenge kwenye nchi hii. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa!

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba katika hoja yake ameeleza kwamba ameshangaa kuona Mfuko wa Vijana haujatengewa fedha. Mfuko wa vijana ulitengewa Bilioni Moja na fedha zote Bilioni Moja zilipatikana kwenye Mfuko wa Vijana, isipokuwa Vijana wengine hawakukidhi vigezo, Milioni Mia Mbili na Tano zilishatolewa kwa ajili ya Vijana hao na fedha zilizobaki zinawasubiri Vijana kuziomba kwa kuzingatia vigezo.(Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru na ni ufafanuzi mzuri lakini kwa vijana kule hazifiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda hoja yangu hajanielewa, yaani hivi hakuna namna ambazo sisi kama nchi na machinery zote ambazo tunazo, Ma-Professor, Waatalam, hivi hatuwezi kufikiri namna bora tunaweza tukauenzi na kuuheshimu huu Mwenge zaidi ya kuuzungusha kutumia gharama ambazo hatuzijui? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Mbuge hili, labda ifike muda tuletewe bajeti ili tuone value for money. Mwenge unaweza ukakimbizwa kwa Shilingi Bilioni Mia Tisa ukaenda kukagua miradi ya Shilingi Milioni Mia Nne au Shilingi Bilioni Moja, yaani value for money katika kujenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu sisi hii ni awamu ya kwanza kuna watu wana awamu nyingi humu, labda tusaidiane na ni katika kujenga tusaidine hivi hamna namna nyingine tunaweza tukafanya. Kwa sababu kama Vijana wanakosa pesa, Vijana wenyewe kazi yao ni kwenda kufunga majukwaa, tunahitaji pesa tuende tukafanye miradi ya maendeleo, tunahitaji pesa kwa ajili ya kwenda kujenge barabara. Waheshimiwa Wabunge jana walikuwa wanadai vituo vya Polisi hapa.

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa!

T A A R I F A

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba Mwenge wa Uhuru ni nembo ya nchi, tunapokuwa tunapozungumzia nembo tunazungumzia culture kwa maana ya utamaduni wa Taifa huwa hatuwezi kuangalia value for money kwenye mambo yanayohusu utamaduni na alama ya nchi. Utamaduni huu wa National Torch siyo kwa Tanzania peke yake, Mataifa mengi yana tamaduni zao na wanatumia mbio za Mwenge kwa ajili ya kuhamasisha, kutia ari na kuweka nguvu katika kuhamasisha shughuli za maendeleo ya nchi husika. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 tuliahirisha sherehe za Uhuru, Mwenge ulikuja baada ya kupata Uhuru kwa hiyo sidhani kama kuna kitu ni muhimu kuliko uhuru wa nchi. Kama tuliweza kuahirisha sherehe za uhuru tukapeleka pesa na Mheshimiwa Rais wa kipindi hiko alitoa maelekezo zifanyiwe nini. (Makofi)