Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia bajeti ya mwaka 2020/2022 na 2020/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mimi nimchangiaji wa kwanza kabisa katika bajeti hii ya mwaka nilioutaja, ambayo inakadiliwa kuwa na thamani ya pesa za Kitanzania shilingi trilioni 41, naomba nichukuwe nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na niseme rasmi kwamba sasa naliamsha dude. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda moja kwa moja kwenye suala la kilimo. Suala la kilimo niseme kwamba sasa kimepata Waziri ambaye anaendana na kasi ya sasa ya kwenda kufungamanisha masuala ya kilimo na viwanda. Ni matumaini yangu kwamba akipewa bajeti itakayotosha, basi atakwenda kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge hili naomba niwajulishe Watanzania kwamba wasiwe na hofu kuhusiana na suala la kilimo, tayari linakwenda kupata tiba na ndugu zangu wa Mkoa wa Ruvuma sasa wanakwenda kupata tiba ya kile kilio cha mbolea kwa maana ya bei kubwa ya pembejeo zilizokuwa zimewekwa. Kwa mujibu wa taarifa ambayo juzi imetolewa na Waziri mwenye dhamana, anasema kwamba ana uhakika wa kuweka ruzuku kwenye mbolea na hatimaye mbolea hii itakuja ikiwa na bei ambayo inanunulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuomba taasisi mbalimbali za fedha kujitokeza kusaidia kwenye Mkoa wa Ruvuma walete pesa za mikopo ili wananchi wa Mkoa wa Ruvuma weweze kukopa waende kuwekeza kwenye kilimo. Naomba sana taasisi hizo zitukopeshe kwa style ya single digit ili kila mkulima aweze kukopa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mkoa wa Ruvuma ni bingwa kabisa na umeshika namba moja miongo minne mfululizo kwa uzalishaji wa mazao ya nafaka nchini, ni matumaini yangu kwamba Serikali itaona umuhimu pia wa kupeleka Benki ya Kilimo ili wananchi waweze kukopa kwa ukaribu. Hata mtoto akifanya vizuri, anapewa zawadi. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Serikali kwenda kuweka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na suala la EPZ kuchukua maeneo mbalimbali na kuwafanya wananchi kuendelea kuwa masikini kwenye maeneo husika bila kuwapa riba. Miongoni mwa maeneo hayo naomba nitaje Kata ya Mwengemshindo iliyoko katika Manispaa ya Songea. Hivi ninavyozungumza, kutokana na zoezi la anuani ya makazi, Mwengemshindo imetengwa na wananchi wana tafrani, hawaelewi mwisho wao, hawaelewi mwelekeo, kwenye eneo la makazi hawajahesabiwa nyumba zao. Kwa misingi hiyo, wanapata mashaka kwamba inawezekana wanaondolewa kwenye duru ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia EPZ wamechukua eneo la Mwengemshindo tangu mwaka 2008, mpaka sasa hivi ninavyozungumza ni takribani miaka 12 wananchi hawa hawajapewa fidia na wamedumaa kiuchumi. Serikali inachukua hatua gani ya haraka ya kuwawezesha hawa wananchi ili waweze kuondoka kwenye maeneo haya na waende kwenye maeneo mengine ambayo wataweza kwenda kufanya uwekezaji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa wanayoidai mpaka sasa hivi kutokana na eneo hilo ni shilingi bilioni 3.5. Naomba Serikali iniambie ni lini watawezesha wananchi hawa wa Kata ya Mwengemshindo ili waweze kuondoka maeneo hayo na kwenda kuwekeza maeneo wanayokwenda kutarajia kufanya shughuli zao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda mrefu sasa imekuwa ikitajwa barabara ya Njombe Songea ambayo haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu na inahitaji ifanyiwe upanuzi. Naomba Serikali ije na majibu, ni lini itaanza kufanya ukarabati huo? Pia tunayo barabara ya kimkakati Likuyufusi - Mkenda inayokwenda kuunganisha Tanzania na Mozambique, ina urefu wa kilometa mia 124; ni barabara ya kimkakati. Tunaomba kujua ni lini Serikali itaanza kuijenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara ya Mtwara - Pachani kwenda Lusewa na Rasi mpaka Tunduru pia ni barabara ya mkakati, tunaomba sasa ianze kujengwa kwa kiwango cha lami. Lumecha - Londo kwenda kwa Mpepo, yaani inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro, tunataka ianzwe kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Msindo ni kituo cha muda mrefu sana. Wananchi sasa wamejitokeza kujenga jengo la upasuaji kwa kutumia pesa zao. Sasa Serikali ni lini itapeleka pesa ili iweze kuhakikisha kwamba lile jengo la upasuaji linakamilika na waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la utawala bora. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana kipenzi chetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, mwanamke shupavu ambaye amejipambanua ndani ya nchi na nje ya nchi, anafanya vizuri sana; na kwamba anafanya kazi zake kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na anakwenda vizuri mno. Tuna imani naye, hatuna mashaka naye, mama yetu atatuvusha vizuri sana. Tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie kila la kheri na kila atakapoona kwamba kuna jambo ambalo linakuwa ni kikwazo katika kutimiza majukumu yake kupitia masuala ya sheria, shime atuletee sheria hapa Bungeni tuzirekebishe na mambo yake yasikwame. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kuhusiana na suala la utawala bora. Mheshimiwa Mama Samia anakwenda mwendo kasi, lakini wako baadhi ya watendaji wanamkwamisha. Tunaomba watendaji wote wa nchi hii wafanye kazi kwa uadilifu na uaminifu ili mama yetu asikwame mahali popote pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nizungumzie suala la LATRA. Nchi yetu ni nchi ambayo hiko katika hali ya usalama kabisa, lakini pia tunatakiwa tuweke mazingira mazuri ya wananchi kufanya shughuli zao ikiwemo wajasiliamali waweze kusafiri muda wote, wasafiri mchana, wasafiri usiku. LATRA wana mpango gani wa kuhakikisha jambo hili linatekelezeka ili wananchi waweze kusafiri?

Mheshimiwa Naibu Spika, wako baadhi ya Watendaji Wakuu ambao ni tatizo kuhusiana na suala hili hili la utawala bora. Unampigia simu Mtendaji Mkuu unajitambulisha kwamba mimi ni fulani bin fulani. Sasa kama mimi kiongozi ninaweza nikajitambulisha na bado asirudi kwangu, asijibu message, hao ni watu ambao ni majipu yanatakiwa yatumbuliwe haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii pasipo shaka yoyote na nina ushahidi wa kutosha, ninaomba kama kanuni inaruhusu nimtaje Mtendaji wa LATRA ni jipu. Mtendaji Mkuu wa LATRA ni jipu. Hapokea simu, hajibu message, watu wanapata ajali maeneo mbalimbali, wafanyabiashara wana shida mbalimbali ya kujua ABCD, maeelekezo mengi anapata lakini hawezi kuyatekeleza. Sasa huyu ni mtu wa aina gani? Ingekuwa ni amri yangu ningesema apishe uchunguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niende kwenye suala la mpango mzima unahusiana na masuala ya vijana. Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia bajeti yake, ameeleza namna ambavyo vijana wamewezeshwa kwenye maeneo mbalimbali na tumeona vijana, mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo, tumeona vijana wamewezeshwa vitalu nyumba kwenye maeneo yao, lakini je mrejesho ukoje? Tathmini ikoje? Hawa vijana kupitia hivyo vitalu nyumba vimewasaidia kwa kiasi gani? Wame-achieve nini? Kwa hiyo, tunataka kujua.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata taarifa maeneo mengine unakuta Madiwani wanaingilia kati, wanapoka vile vitalunyumba vya vijana. Kwa hiyo, naomba sana Serikali yangu iende kule, Wakurugenzi wa maeneo husika waende wakakague na tupate majibu, vimesaidia kwa kiasi gani na vijana wamenufaika kiasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho, naomba sana wanawake wa Mkoa wa Ruvuma wana uhitaji sana wa kuwekeza katika kilimo. Naomba sana uwepo mpango mzuri; wakati mwingine unaweza kuwakopesha vikundi mbalimbali wakafanya biashara, lakini hawana utaalamu wa mambo ya biashara, lakini tukiangalia maeneo mbalimbali kulingana na jiografia zao na mila zilizopo, unaweza kuwasaidia vikundi hivyo ukawapa mbegu, ukawawezesha katika masuala ya kilimo na wakafanya vizuri zaidi na wakawa na tija zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, naomba kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi)