Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia nafasi ya kujadiliana na kutoa maoni yetu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge inaonesha nia njema ya kuisukuma nchi kuweza kusogea mbele kwa niaba ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nilipata maneno, nimeambiwa ni ya kiarabu, yanayosema: “Yashukurunasu lashukurullah.” Nirudie tena kwa ambao hawakusikia, Yashukurunasu lashukurullah, yaani maana yake, asiyemshukuru binadamu mwenzake kwa wema aliomtendea, hawezi hata kumshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwatendea mema sana Watanzania na kuhakikisha kwamba wanafikia katika ile nchi ya ahadi. Pili, nakushukuru na kukupongeza wewe kwa jinsi ambavyo unaliendesha Bunge letu, nasi wanafunzi wako na Wanasheria wenzako tunajivunia na kuona tulipita kwenye mikono salama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa michango yao ambayo nimesema inaonesha kabisa kuwa objective na progressive kwa nia ya kuijenga nchi. Niongeze shukurani na pongezi nyingine kwa wale ambao pengine hawakusemwa hapa; hoja zilizopo hapa zinaihusu Serikali na Serikali inayo watendaji. Siyo watendaji wote wameoza, wameharibika, hawana weledi, ni wezi. Wapo ambao ni wazuri na wanafanya yale mazuri ambayo humu tumekuwa tukimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutufanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wangu niwashukuru na niwapongeze watumishi safi wa Umma na tuendelee kuwatia moyo ili wao sasa wasihamie kwenye lile kundi la wengine ambao tunakubaliana hapa kwamba mwisho wa siku tushughulike nao kisawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kwenye maeneo matatu yaliyosemwa kwenye Wizara ya Nishati, nikikubaliana na hoja na ushauri wa maeneo mengine ambao umetolewa kwenye taarifa ya CAG na kwenye Taarifa za Kamati. Yale ambayo sitayasema kwa taarifa zilivyo, tunakubaliana na tunachukua ushauri na maoni na maelekezo yaliyotolewa kwenye taarifa hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye eneo la kwanza la Symbion. Sitakuwa na mengi sana ya kusema hapa kwenye eneo hili. Mkaguzi amekagua objectively na ametoa maoni yake na yalikuwa matatu. Ameshauri mikataba isimamiwe vyema kwa kuwashirikisha wanasheria; pia ameshauri kabla ya kuivunja, basi tuhakikishe kwamba tunaangalia mapato na hasara za sasa na za baadaye; na pia ameshauri kwamba zile pesa ambazo zimelipwa na Serikali zitizamwe namna bora ya kuziweka kwenye vitabu na hesabu za Serikali ili mikeka ikae vizuri. Hayo ndiyo maoni ya CAG, nasi tunakubaliananayo na tunayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kwenye eneo la mazuri yaliyotokana na malipo yaliyofanywa baina ya Serikali na huyo aliyekuwa Symbion. Nadhani huko panaweza pakawa panafaa zaidi. Wakati kesi inapelekwa Mahakamani, ilipelekwa ikiwa inadaiwa jumla ya kama Dola bilioni moja na milioni mia tano na zaidi kidogo. Kwa
majadiliano yaliyofanyika nje ya Mahakama, imelipwa kama ilivyosemwa, milioni 153 ambazo zinakwenda kwenye bilioni karibia mia tatu na zaidi kidogo. Kwa hiyo, kwa upande wangu naweza kusema pesa nyingi iliokolewa tofauti na kama tungeendelea Mahakamani na kuwa na mafanikio yasiyokuwa chanya, yaani mafanikio hasi, kwa maana ya kushindwa katika kesi hiyo.

Mheshimiwa Spika, ule mtambo ambao umelipiwa zile fedha, sitaki kusema tumeununua; ule mtambo ambao umelipiwa fedha ikiwa ni maelekezo ya makubaliano, thamani yake kwa wataalamu walioifanya ni karibia Dola 120. Kwa hiyo, kwa kulipa milioni 153, maana yake ni kama tumenunua mtambo. Hizo 153 ndani yake kulikuwa kuna deni la bili za kuuziwa umeme, kuna faini ya kuchelewesha yale malipo ya kulipia umeme na gharama za uwekezaji. Kwa hiyo, ukifanya hesabu ya kawaida, inaonekana kama tulichokifanya kilikuwa ni kitu ambacho ni kizuri kwa maana ya kuokoa pesa ya Serikali, ni kama tumenunua mtambo kwa gharama ambazo zilikuwa zina uhalisia.

Mheshimiwa Spika, mtambo huu wataalamu wameuhakiki na kuukagua kuona unaweza kufanya kazi kwa miaka 15 ijayo mpaka 30 bila kuhitaji matengenezo makubwa. Kwa hiyo, bado ni mtambo ambao uko vizuri na unaweza ukatusaidia kwenye kazi zetu za kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Spika, tangu ulipoanza kufanya kazi mwezi wa pili baada ya kuwa umelipiwa mpaka huu mwezi Oktoba mwishoni umeshaizalishia Serikali jumla ya Shilingi bilioni 73 kwa kufanya kazi za kuuza umeme katika muda mfupi huu ambao umefanya kazi. Kwa hiyo kwa hesabu hizo ndani ya miaka kama minne kuanzia tulipolipa ile pesa bilioni 153 za dollar ambazo zimelipwa juzi zitakuwa zimerudi kwenye Serikali na Serikali itaendelea kutumia mtambo huu kwa faida zake.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa tunayo chaangamoto ya upungufu wa maji kwenye vyanzo vyetu vya maji mtambo huu wa Symbion unatumia gesi na hivyo sisi kama Serikali kwa kutumia gesi tuliyokuwa nayo na mtambo wetu tuliyoupata baada ya kumaliza ile kesi nje ya mahakama, tunautumia kupunguza gap la upatikanaji umeme kwa takriban megawatt 112 ambazo zinatoka kwenye mtambo huu. Kwa hiyo kwa ushauri wangu na kwa mchango wangu, nadhani yapo mazuri mengi ambayo mtambo huu unatupatia sisi kama Serikali na ni wa kwetu tunaumiliki sisi wenyewe. Kwa maoni na hoja ya CAG nadhani sasa itoshe tuachane na hii habari tuannze kusonga mbele kwa yale mazuri ambayo yamepatikana kwenye hili eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye eneo lingine la Mradi wa Mwalimu Nyerere. Kwa Nchi yetu ya Tanzania katika miradi mikubwa ambayo tunayo na tuliwahi kuwa nayo mmojawapo ni huu wa trilioni sita na bilioni 500 na zaidi. Ni faraja kubwa sana kwa nchi kuwa na mradi kama huu tunaoutekeleza kwa pesa zetu za ndani. Katika hili lazima tuipongeze Serikali.

Mheshimiwa Spika, pesa hizi zinapatikana kwa wakati katika yale maeneo ambapo Serikali ya Awamu ya Sita imehakikisha inalipa pesa kwa wakati bila kuchelewa hata siku moja madai yanapokuwa yamehakikiwa ni katika eneo hili la Mradi wa Mwalimu Nyerere. CAG alipokagua ameona mambo ya kushauri na kusonga mbele na tunayachukua kwa sababu ni ya kuboresha. Nisemee mambo mawili tu kwa haraka haraka kwa sababu naona kengele ya kwanza tayari imegonga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo mawili makubwa ambayo naona nichangie kidogo ni kuhusu muda wa kukamilisha mradi. Ni kweli mradi ulianza 2018 na ulitakiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu ambayo ilikuwa ni Juni mwaka jana. Juni ilipofika mradi ulikuwa haujakamilika kwa sababu ambazo zinafahamika na zinavutana kati ya pande mbili ya Serikali na mtekelezaji wa mradi. Tulikuwa na options mbili sisi kama wasimamizi, tu-abandon mradi kwa sababu muda umeisha au tuwe weledi na wazalendo tuendelee na mradi kwa ku-extend muda huku tukiendelea kuvutana na kubishana kuhusiana na nani mwenye haki, kwenye nini nani kamchelewesha nani na nani kafanya nini? Busara zilituonyesha tutoe kitu kinachoitwa ex-gratia grants of extra time ya kufanya kazi extension of time wakati tukiendelea na majadiliano mengine, nani amechelewesha nini? Nani anamdai nani nini? Nani anatakiwa kumlipa nani?

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na wachangiaji wengi hapa Wabunge ambao wamechangia, kuna suala ambalo tunaliona labda kama huyu mkandarasi alikuwa anamaliza Mwezi Juni na amechelewesha mradi na kimsingi yule anaye chelewesha mradi ndiye anaetakiwa kuomba Serikali au kuomba aongezewe muda. Sasa hoja iliyokuja ni kwamba mtu amechelewesha mradi halafu ameongezewa muda, ameongezewa na fedha na wataalam wetu mahiri kabisa waliofanya ule mkataba walikuwepo, Watanzania kabisa wazalendo wamefanya ile mikataba, wakakubaliana kwa ngazi yeyote kwamba mradi utaisha mwezi Juni, sasa hii ya kuongeza muda na kuongeza fedha ufafanuzi wake ukoje labda inakuaje hii? (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, unaipokea taarifa hiyo?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mchangiaji hajatoa taarifa, lakini katika mchango wangu sijasema tumeongeza gharama za mradi na nimesema kuhusu kuongezeka kwa muda wa utekelezaji. Kwa hiyo sijasemea kuhusu kuhusu kuongezeka kwa gharama za mradi.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, nadhani nia ni kwamba kwa sababu hii mikataba ambayo tunaingia kwa maana ya Serikali pamoja na hawa wenzetu ambao tunaingia nao mikataba kwa kutoa huduma mbalimbali, upande wa Serikali inaonekana kwenye mikataba pengine si yote, lakini mingi kuwa inalipa ile pesa ya riba kwa kuchelewesha malipo. Sasa huyu mwingine anapochelewesha yeye, Serikali kwa sababu wataalam wapo na mikataba ipo na yeye upande wake analipa? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, mkandarasi ana madai yake kwa Serikali na Serikali ina madai yake kwa mkandarasi na kama tungekaa kwenye kuvutana na kubishana tu-establish nani mwenye haki gani kwanza ndio tuendelee na mradi mpaka sasa mradi ungekuwa umesimama. Kwa hiyo alipoomba extension of time kwa sababu alizozileta na akiomba kuongezewa pesa, tumekataa kumwongezea pesa, tumemwambia kwa sababu tuna madai yetu kwako na wewe una ya kwako kwetu hatuja-resolve. Sasa tutakuongezea muda usiokuwa na hayo masharti ya kuongezewa pesa au kuongezeka kwa kitu kingine, tuendelee kutekeleza mradi kwa sababu pesa tunazo na wakati huo tukiendelea kujadiliana nani mwenye haki ya kupata nini.? Kwa hiyo hakuna ambaye mpaka sasa amemdai na kufanikiwa kwa mwenzake kulipa hela ya ziada na sisi tunachokisema ni kwamba hatutalipa pesa ya ziada kwa sababu tunayo madai yetu kwake tukionyesha yeye ndiyo kachelewesha mradi. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge wawili mmesimama, hiyo taarifa inahusu ufafanuzi aliotoa? Maana ndicho kinachoendelea sasa. Mheshimiwa Mpina.

T A A R I F A

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ndiyo. Mkataba wetu uko very clear, juu ya mkandarasi kuchelewesha mradi anatakiwa kufanya nini? La pili Waziri hapa anatueleza kwamba Mkandarasi ameomba extension of time na Serikali ika-grant extension of time, base ya extension of time waliipata wapi? Kama hawajafanya tathmini ya kazi iliyofanywa na changamoto zilizopo? Utaipata wapi base of extension of time kama ujafanya tathmini?

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, sasa nimeshawaanbia anayeruhusiwa kuuliza maswali ni mimi. Mheshimiwa Naibu Waziri hoja yako imeeleweka, sasa haya maswali ya Mheshimiwa Mbunge, ni maswali, kwa hivyo siyo taariafa. Kwa hiyo endelea na mchango wako wako.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna taarifa nyingine nyuma yako. Mheshimiwa Kigwangalla.

T A A R I F A

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nilipenda kumpa taarifa mchangiaji anayezunguza kwamba wametoa extensions ya muda ex-gratia kwa favor, kwa huruma, lakini kule kucheleweshwa kwa utekelezaji wa Mradi kwa zaidi ya miaka miwili kumesababisha mazingira ya utekelezaji wa mradi huo yabadilike. Kwa mfano; kuchelesha tu tayari kunabadilisha exchange rate ya kati ya dollar na shilingi na hatimaye leo hii wanapomlipa pesa nyingine za kukamilisha huo mradi wanamlipa kwa exchange rate ya sasa na hasara ambayo imeingia ni zaidi ya bilioni 110 kwa kuchelewesha tu. (Makofi)

SPIKA: Haya, ahsante sana. Waheshimiwa Wabunge, hili jambo nilikuwa najaribu kuangalia hapa kwenye hivi vitabu vya Kamati wameandika azimio kwa namna gani, lakini hoja hii imeshawahi kufafanuliwa hapa na Mheshimiwa Waziri na kueleza ule mradi umechelewa kwa sababu zipi? Alitoa maelezo, lakini sasa kwa maelezo anayotoa hapa Mheshimiwa Naibu Waziri ni maelezo ambayo ni mahususi kwa zile hoja ambazo zimejitokeza hapa, lakini kwa maana ya yale maelezo ya jumla kukusu mradi Mheshimiwa Waziri wa Nishati alishawahi kusimama hapa Bungeni na akaeleza sababu.

Sasa sisi sasa hivi ili tujielekeze vizuri tuko kwenye hoja hizi hapa za Kamati na tunataka tufike mahali ambapo mchango wa Serikali kwa sasa na wao wanachangia kama Wabunge, lakini utatusaidia Bunge kuazimia kwenye yale mambo ambayo Serikali hatujaweza kujiridhisha na kile ambacho wanasema. Kwa hiyo anachoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri ni kile ambacho kimeibuliwa kama hoja, lakini yale mengine ya jumla hayajaletwa bado na CAG na kwa sababu mradi unaendelea CAG atakuja atuambie tu, halafu kwenye ngazi hiyo ndiyo tutashughulika nayo kama haya tunayoshughulika nayo kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Waziri, malizia mchango wako.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Eneo lingine ambalo naona nilisemee kidogo ni kwenye gharama za mradi zinazohusiana na mabadiliko ya fedha. Miradi mikubwa kama hii inapotengenezewa mikataba inawekewa component mbili, mara nyingi local component na foreign component kulingana na kile ambacho kitatekelezwa kitatumia gharama zipi kubwa? Kwa ilivyofanyika katika mkataba huu gharama kubwa ya utekelezaji wa mradi huu ni mambo yanayotoka nje ya nchi. Kwa hiyo ilikubaliwa kwamba itakuwa ni asilimia sabini ya malipo yatafanywa kwa dollar na asilimia thelathini yatafanywa kwa shilingi ya Kitanzania, kwa sababu supply na mambo makubwa yanapatikana nje ya nchi. Hivyo wataalam walitafuta njia nzuri na namna bora ya kufanya haya. Walijaribu kuhakikisha haifikii sabini ili tuweze kuokoa exchange rate, lakini kwa mazingira na uhalisia ulivyokuwa na wote mnaufahamu mradi huu hatuna haja ya kurudi huko sana ilionekana ibaki sabini kwa thelathini kwa sababu ya uhalisia.

Mheshimiwa Spika, suala pia la kufanya utaratibu wa aging ni kama ku-secure kufanya insurance ya malipo ya baadaye kwenye exchange rate yalitazamwa yote lakini hesabu hazikuleta faida. Kwa hiyo ilikubaliwa kwamba twende na utaratibu huu. Pia kipindi tunaingia mkataba exchange rate tuliyoi-commit ilikuwa na shilingi 2,224.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimwa kengele ya pili hiyo, dakika mbili malizia mchango wako.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniongezea muda. Ilikuwa ni shilingi 2,224 kwa dollar moja. Tangu tumeanza kazi dollar imekuwa ikipanda na kuna muda fulani imefikia mpaka shi2,310.93. Sasa hii pesa bilioni 113 iliyowekwa nilihakikishie Bunge lako na Watanzania haijaliwa wala haijapigwa mtu, ni gharama halisia za mabadiliko ya pesa ambayo hata kwenye biashara zetu za kawaida yanatokea.

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho kwa haraka haraka, ukwasi wa taasisi zetu ya TPDC na TANESCO, naomba nipende kutoa mchango wangu katika hili.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunti Majala.

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na yote anayotueleza, pamoja na ucheleweshaji, pamoja na hizo exchanging rate lakini ikumbukwe kuwa mradi huu ulitakiwa pia utoe CSSR kwa jamii inayozunguka ule mradi, lakini mpaka leo zaidi ya bilioni 190 na hazijalipwa mpaka leo. Kwa hiyo hilo nalo waweze kuliona kama Serikali kwa namna gani mradi huu unavyoendelea kudidimiza Taifa letu kwenye suala hilo la mradi na mradi kutokuwa na tija kwa Watanzania.

SPIKA: Ungelikuwa umeishia hapo kabla ya swali lako ungekuwa umetoa taarifa, sasa umeuliza swali. Haya mchangiaji malizia mchango wako.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia mchango wangu kwa kuzungumzia ukwasi wa TPDC na TANESCO. Kwa mara ya kwanza katika historia chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania TANESCO imepewa shilingi trilioni 2.4 kama mtaji na wenzetu wa TPDC wamepewa shilingi trilioni karibia 2.8 kama mtaji kwa ajili ya kuweza kujiendesha. Pesa hizi zimetoka wapi? Serikali imeamua kuchukua jitihada za makusudi za kubadilisha deni lake kwenye Taasisi hizi sasa ibadilike kuwa mitaji. Kwa hiyo yale madeni ambayo Serikali ilikuwa imezikopesha hizi taasisi, lakini inaendelea kulipa yenyewe imezibadilisha sasa ili ziweze kuwa mitaji katika taasisi hizi na hivyo zitakuwa na uwezo wa kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.