Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia na ninaunga mkono hoja zote tatu za Kamati. Vilevile nakushukuru wewe kwa kutuongoza vizuri Wabunge na kutuwezesha kufanya kazi zetu vizuri na kwa weledi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako lina mchanganyiko wa Wabunge wazuri wenye weledi mkubwa sana. Pia naomba nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifungua nchi kuitafutia fedha na pia kubwa, ku-control uchumi wa nchi yetu ambao umeweza kuhimili mfumuko (inflations rate) ambao upo duniani kwa sasa hivi. Nchi yetu imeweza ku-control, kwa mfano tu wa haraka haraka, duniani huko nchi iliyotutawala, Uingereza mpaka Septemba inflations rate yao, wao wali-target 2% ya infations rate, lakini mpaka Septemba, 2022 wamekuwa na inflations rate ya 10.1 percent kwa maana ya two digits.

Mheshimiwa Spika, kwa uwezo wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa ku-control uchumi wetu, sisi tumeendelea kuwa katika single digit ya uchumi wetu kwa maana ya kudhibiti kwa mfano mafuta, kupeleka ruzuku, pia lingine kubwa kuweka ruzuku ya mbolea kwa wakulima. Kwa hiyo, tunamshukuru sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, wetu.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye hili la mbolea kabla sijaenda kwenye mada, tunaishukuru sana Serikali baada ya kuiomba kuweka kituo cha ununuzi wa mbolea Namtumbo ambacho kilikuwa Songea Mjini. Watu wa Namtumbo walikuwa wanatembea kilometa nyingi kwenda kufuata mbolea. Serikali ilisikia na imefungua kituo Namtumbo Mjini. Hata hivyo, bado haitoshi, tunaomba mbolea za ruzuku ziende vijijini kwa wakulima kama ilivyokuwa hapo nyuma. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itafakari ione jinsi gani inaweza ikasaidia kwenye hili.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein Bashe.

T A A R I F A

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Vita na Wabunge wote, siyo rahisi kwa Serikali kufungua vituo vya kuuzia mbolea katika kila kijiji katika nchi yetu. Vituo vya kuuzia mbolea ya ruzuku vitafunguliwa katika centers ambazo hapo awali biashara ya mbolea ilikuwa inafanyika na kwa Wakala ambaye atafikia vigezo tunavyoviweka vya udhibiti ili tusirudie matatizo yaliyotokea 2014, 2015, 2016 ambapo ruzuku haikumsaidia mkulima, bali iliwasaidia Mawakala na Wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge waelewe kwamba kama una concern ya eneo, wasiliana na Wizara, tutali-evaluate eneo hilo, kwa sababu unaweza ukapeleka kijijini gharama ya kusafirisha na ku-supply mbolea kule kijijini, mantiki yote ya ruzuku ikawa imekufa na wala isiwepo bila sababu yoyote. Kwa hiyo, tutafungua katika maeneo ambayo awali mbolea ilikuwa inauziwa na distribution tutendelea kuiongeza kadri ambavyo inawezekana.

SPIKA: Mheshimiwa, kabla sijamwuliza Mheshimiwa Vita Kawawa kama anaipokea taarifa hiyo, nadhani jambo la msingi ni kwamba mbolea isogezwe kwa wakulima. Hilo ndilo jambo la msingi. Sasa hoja ya kila Kijiji ni namna Mheshimiwa Mbunge anavyojenga hoja yake, lakini hoja ni kwamba maeneo ambayo wakulima ni wengi, mashamba ni makubwa, mbolea isogee kwao ili kuwapunguzia mzigo wa kusafiri umbali mrefu kwenda kufuata mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Vita Kawawa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, kuipokea ni ngumu kweli. Napokea maelekezo yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sasa nirudi kwenye hoja. Taarifa ya CAG imetueleza kwamba baada ya kufanya tathmini, fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 185, kulikuwa na Shilingi bilioni 838 hazikupelekwa kwenye miradi ya maendeleo na pia matumizi ya kawaida. Pia imejitokeza taarifa ya CAG inasema, kuna Halmashauri 39 zilipokea fedha za makisio ya bajeti zilizohidhinishwa ziada Shilingi bilioni 74.38 kama 8% ya makisio yaliyoidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, hapa utakuta kwamba kuna halmashauri zimepata zaidi ya makisio yao ya bajeti ambayo yaliidhinishwa na Bunge lako Tukufu, lakini kuna halmashauri ambazo zimepata upungufu. Sasa ushauri wangu hapa ni kwamba, siyo vyema kwa Watumishi wa Serikali ambao wana disburse fedha hizi wakazigawa halmashauri. Halmashauri nyingine zinapendelewa, nyingine zinanyimwa fedha. Tutoe kulingana na tulivyoidhinisha kwenye Bunge letu Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa Kamati unasema katika ukurasa wa nane wa kwenye kishikwambi kwamba, Kamati imeona kuwa dosari hizo hazikutokea kwa bahati mbaya na ishara ya mkakati maalum unaoratibiwa na baadhi ya Watumishi wa Umma wasiokuwa na uadilifu kwa lengo la kuwa na upendeleo, udanganyifu na ubadhirifu. Katika hili, naomba Serikali na sisi Bunge katika maazimio yetu tusimamie ili Wizara ya Fedha ihakikishe inatoa fedha sawa kwa wote kama walivyoidhinishiwa na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Wizara ya Fedha itueleze katika eneo hili ambalo kuna baadhi ya halmashauri zimeongezewa fedha za ziada nje ya bajeti iliyoidhinishwa imelifuatitia kama kweli fedha hizo za ziada zilizotoka nje ya bajeti zilifanya kazi gani huko katika halmashauri zilikopelekwa? Suala la tatu, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe azimio lake kwamba, Bunge lifanye uchunguzi ili kubaini iwapo fedha zilizotolewa zaidi, au nje ya bajeti haikuwa na viashiria vyovyote vya upendeleo, udanganyifu au ubadhirifu.

Mheshimiwa Spika, vilevile Kamati iliendelea kusema halmashauri nyingi hufanya manunuzi kwa dharura bila kuzingatia mipango ya manunuzi kwa mradi wa mwaka. Wote tunafahamu kuna Sheria ya Manunuzi, lakini ukitazama shida iliyojitokeza hapa kubwa ni kwa sababu mfumo huu wa force account, ni mzuri lakini lazima tukubaliane kuwe na kiwango maalum cha fedha za miradi itakayofanyika kwa huu mfumo wa force account. Tukiacha mradi wa fedha, Shilingi milioni 800, Shilingi bilioni moja, Shilingi bilioni mbili, ukaendeshwa kwa mfumo huu wa force account peke yake, ndiyo shida hizi zitaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini kinatokea? Kinachotokea ni kwa kwamba Watumishi wa Halmashauri ndio wanaonunua vifaa na wanatafuta fundi. Sasa hapa kwenye ununuzi wa vifaa mradi unaanza; wakati ukiwa kwenye msingi, Watumishi wa Halmashauri, Idara ya Manunuzi inanunua vifaa vyote vya mwanzo mpaka msumari wa bati, mpaka rangi inanunuliwa kwa mara moja. Ukitazama kiuhalisia kwenye tender au kwa Wakandarasi wanaofanya kazi hizi, huwa wanapewa fedha kulingana na kazi waliyoaifanya. Sasa pale wanaponunua vifaa vyote kwa mara moja, kwa maana nyingine wanaweza wakanunua vifaa vile kwa interest yao ya ten percent au wapate ziada, wana-inflate rate za bei na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaponunua vifaa vyote vile kwa pamoja, inapofika mradi umefikia mwishoni, fedha zimekwisha na kuna vitu vya msingi vinatakiwa, wanakosa fedha za kuzifanya. Kwa mfano, kwangu Namtumbo yaliyotokea Waziri Mkuu alipokuja kuangalia na kuona milango iliyokuwa chini ya kiwango, kwa sababu fedha zote zimekwisha, hawana fedha za milango, wanaenda kuchukua fundi wa Mwembeni kutengeneza mlango, ndiyo yaliyotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile siyo hayo tu, ukiondoa hiyo, baadaye wameingia tena kula hata mbegu yenyewe. Kwangu Namtumbo kule kuna mradi ulikuwa wa kutengeneza vyoo vya zahanati zetu tano. Wameenda kununua cement 1,200 lakini zilizoshushwa ni cement 600, na 600 nyingine zimeshuka huko njiani. Pia wameenda ku-order milunda 800 ya kutengenezea vyoo. Unatengeneza vyoo vya shimo ili uweke milunda ufunike! Milunda ya nini kwenye vyoo? Milunda haikuletwa, fedha zimelipwa toka mwaka 2021. Waziri Mkuu anakuja ndiyo wamestuka, wameenda kuleta milunda 800 wameilundika. Waziri Mkuu akastukia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala la force account nalo tunasema lazima tuliangalie. Hayo makosa yataendelea kuwepo, lazima tuwe na limit ya fedha kwa ajili ya Miradi ya force account. Miradi mikubwa ya fedha nyingi lazima itumike na Wakandarasi. Tukubali, tusikatae, mradi wa bilioni na zaidi hauwezi kutumiwa tu na fundi. Lazima tuangalie hilo pia. Vilevile kuepusha gharama. Kwa mfano, yaliyotokea kwangu Namtumbo kwenye hospitali ya Wilaya, fundi yule kashamaliza kazi yake, hakuna fedha za kuweza kurekebisha ile milango. Tunamlazimisha sasa technician aliyesimamia atengeneze kwa gharama yake. Ingelikuwa kazi ile inafanywa na Mkandarasi, kuna fedha zinabakizwa pale, hapewi miezi sita. Kama kuna dosari, anarekebisha.

Mheshimiwa Spika, sasa hili la force account ndiyo hasara yake hiyo. Pia force account fundi hela zote zile hazilipiwi kodi. Anapopewa Mkandarasi, analipa kodi;0 analipa service levy kwenye Halmashauri na pia analipa TRA. Hela nyingi kwa ajili ya force account kwa fundi tu hailipwi, Serikali hai-collect, inatoa tu, lakini ikimpa Mkandarasi, Serikali pale inatoa na inakusanya kodi.

Mheshimiwa Spika, leo hii mradi wa bilioni nne kwangu unajengwa na shule ya wasichana wanapewa mafundi wa kawaida. Pale Serikali haitakusanya na halmashauri haikusanyi, lakini on top of that wana-inflate rate ya vifaa vile.

SPIKA: Sekunde 30, malizia.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wana-inflate rate ya vifaa, gharama inakuwa kubwa, matokeo yake CAG anakuja kuona hayo, kwa hiyo, haya yataendelea kuonekana kutokana na watumishi wasiokuwa waadilifu. Nakubaliana kabisa watumshi wote ambao pia, hawakuwepo, shida wanayoipata Kamati zetu hizi wakiwaita, unakuta waliokuwepo sasa hivi wanakwambia mimi nina miezi miwili sikulifahamu hili. Kwa hiyo, tunaomba wale wote waliokuwepo mwaka huo 2021, waitwe watoe majibu kutokana na hoja za CAG na hatua zichukuliwe.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)