Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia kwenye taarifa hizi za Kamati ambazo zimewasilishwa kwetu Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni Mwanamama jasiri na shupavu kweli kweli! Na hii ni namna ambavyo miradi inaweza kutekelezwa katika maeneo yetu, nasi tumekuwa mashahidi hasa fedha za miradi zinavyokuja kwa wingi kwenye maeneo yetu kwenye Majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona fedha hizi zinavyokuja kwa wingi na taarifa ilivyokuja hapa, hii ni taarifa ambayo imewasilishwa na kamati inaonesha taarifa ya mwaka 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021 na tumeona madudu yaliyomo ndani ya taarifa hizi. Ni fedha nyingi sana ambazo zimeonekana kupotea na sijajua mwarobaini wake hasa ni nini? Hasa katika nchi zetu za kiafrika na sijajua labda ndiyo tumeumbwa tuwe hivyo sijaelewa, maana yake kila anayeweza kupata fursa ya kufanya kazi katika eneo lazima aongeze yeye anapata nini, hata kama kuna mshahara ambao utamwambia auchague yeye mwenyewe utamlipa Shilingi ngapi, lakini kwenye akili zetu tunaongeza ninapataje fursa ya kuiba zaidi ya hiki ambacho napatana na huyu mtu. Kwa hiyo, imekuwa ni dhana ambayo ipo, nafikiria hata mfumo wetu wa elimu kila siku tunataka tuungalie upya kuanzia chini nursery huko kuja Sekondari mpaka Vyuo Vikuu. Hata mtu anayesomea fani mbalimbali anasoma lakini anawaza akipata fursa abutue, akipata fursa achukue chake, sasa hii imekuwa ni gonjwa kubwa sana, ugonjwa si wa Taifa ni ugonjwa wa Afrika nzima, ndiyo maana maendeleo yanachelewa sana unaweza kushangaa nchi tulizopata uhuru miaka ya 1960 za Asia na ukichukua nchi za Afrika zilizopata uhuru miaka ya 1960 na maendeleo yaliyokuwepo kwa kipindi hicho na ukiangalia maendeleo yaliyopo sasa hivi ni vitu viwili tofauti kabisa, ni kama vile wenzetu waliwahi zamani kupata uhuru kuliko sisi, kumbe nadhani kuna mahali tumekosea ni lazima tujirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG kila mahala ni wizi, hata ukisoma taarifa ya ukaguzi wa Halmashauri zetu, unaona kuna POS ambazo zipo zenye namba za kufanana. POS za kukusanyia mapato, sasa mpaka POS zenyewe kwenye Halmashauri ziko zaidi ya 100 zina namba moja zinafanana maana yake nini hapa? Usajili wake na taarifa zake maana yake kuna wizi wa fedha za Serikali za wananchi zinapotea kwa wingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii inatupeleka kurudi nyuma, kama tunaweza tu kukuta kwa miaka hii tumepoteza kwa fedha hizi karibu Trilioni Nne, bajeti yetu kwa mapato yetu ya ndani ni Trilioni 20 kwa mwaka, Je, ni miradi mingapi ambayo fedha hizi zingedhibitiwa tungeweza kupiga hatua kubwa kama Taifa? Sasa iko haja ya kuangalia pamoja na kuwa tunachangia, tunaonesha maeneo na kumekuwepo na watumishi wanahamishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, imekuwa kama desturi, kasumba na kama tabia yetu.

Mheshimiwa Spika, tufike hatua tubadilike, wenzetu China ukikutwa na hatia ya kukamatwa na rushwa unanyongwa, wengine wanapigwa risasi unauawa, sisi huku tuna roho za kibinadamu, aah! muache, msamehe, sheria iko wazi lakini hatua hazichukuliwi, hizo ni sheria za nchi za watu. (Makofi) [Neno China Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

SPIKA: Mheshimiwa Gulamali, hiyo habari ya China hapo kwenye mchango wako hebu iondoe wewe mwenyewe halafu uendelee kumalizia hoja yako.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naondoa neno ‘China’ ni nchi zingine hatua kama hizo zinachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, sasa nchi yetu tunawalea hawa watu na tuko zaidi ya milioni 61. Ukiangalia idadi ya wasomi sasa hivi Watanzania imekuwa ni kubwa, kwa nini kusiwe na utaratibu wa hawa wanaokosea, hata wale vyeti vyao vinaingia kwenye dosari na kuondolewa kazini, hata kama akienda kuomba tena nafasi nyingine ndani ya Serikali, alama inakuwepo ya kum-identify kwamba huyo alishawahi kuharibu sehemu fulani hapaswi kupewa nafasi tena sehemu nyingine. Hasa hii ya kumhamisha, ameharibu Igunga unampeleka Musoma, anaharibu Musoma unampeleka Dar es Salaam, anaharibu Dar es Salaam as if nchi hii haina wasomi, tunao wasomi wengi?

Mheshimiwa Spika, ifike mahala mtu anapoharibu na kazi yake inakuwa imekoma hapohapo, siyo hadithi ya kusema unamhamisha akajirekebishe sehemu nyingine, kama tu mwizi wa kuku anapelekwa mahakamani, kuku ni shilingi ngapi? Kuku ananunuliwa shilingi ngapi? Shilingi 5,000, shilingi 7,000 mtu anaenda kuhukumiwa miezi Sita. Leo ni mabilioni ya fedha kwenye ripoti za CAG yamepotea, yanapotea au yataendelea kupotea lakini je adhabu wanazozipata hawa watu zinafanana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nikuambie Wabunge tunalalamika hapa lakini wananchi wanaenda kuwalaumu akina nani? Atalaumiwa Rais, atalaumiwa Waziri, atalaumiwa Mbunge, atalaumiwa Diwani, lakini wezi wapo kwenye mfumo na Mbunge ataondoka atakuja Mbunge mwingine, Rais ataondoka atakuja Rais mwingine, Waziri ataondoka atakuja Waziri mwingine, mfumo bado unawabeba wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wezi wanahama phase tu wanatoka phase ya Mheshimiwa Jakaya anakuja phase ya Mheshimiwa Hayati Magufuli, mwizi yupo tu, anatoka mwizi huyo phase ya Hayati Magufuli anaingia Mheshimiwa Mama Samia mwizi yupo tu anaendelea kwenye mfumo, anaendelea kunyonya Taifa. Kwa nini huu mfumo tusiufumue uende sawa? Kama tunatumbuliwa na wananchi wakati wa kura, kwa nini na sisi tusiwatumbue hawa watu kwenye ajira zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ifike hatua tuwaonee huruma Watanzania, fedha hizi zilizoainishwa humu na Kamati imechambua kwa kina, kuna haja gani ya kukaa tunabembelezana kwamba huyu mtu tumuache aende sehemu nyingine, umeshaharibu hata kama ni kidogo umeharibu pisha kazi aingie mtu mwingine italeta heshima. Hizi taarifa za CAG zitapungua kuja na makosa makubwa ambayo leo tunayaona. Kila siku hasara inaongezeka hazipungui yaani taarifa za fedha zinazokuja kutokana na hasara kutokana na fedha zinazopelekwa kwenye miradi na zinazopotea hazipungui bali zinaongezeka siku hadi siku.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana ilikuwa Trilioni Mbili, mwaka huu utaambiwa ilikuwa Trilioni Sita, mwakani itakuja Trilioni 15, ndiyo tunakusanya tunafanikiwa kukusanya lakini bado mianya ya kupotea kwa fedha zetu umekuwa ni mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimewasikiliza Wabunge wenzangu hapa kila mmoja analia, zimezungumzwa zile taasisi, zimezungumzwa Halmashauri zimetajwa na majina; Je, hatua tunazoenda kuzichukua zinaenda sambamba na taarifa zilizoletwa humu ndani? Ifike hatua wakati mwingine walikuwa wanawajibishwa Mawaziri hapa, lakini ndiyo solution kwa sababu bado hata ukimwondoa anayekuja mfumo ule wa wizi upo tu unaendelea, kwa hiyo lazima tuangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni Sheria ya Manunuzi ya Umma, hii Sheria imekuwa tunailalamikia kila siku tunasema inashida, alikuwepo Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alizungumza sana juu ya Sheria hii ya Manunuzi, amekuja Mheshimiwa Mama Samia anazungumza juu ya hii Sheria ya Manunuzi, hivi kuna ugumu gani hii Sheria kuletwa humu Bungeni tukaibadilisha? Tumekwama wapi? Ni nani ambaye anatakiwa ailete hii Sheria humu ndani tuiboreshe? Maana imekuwa ndiyo gonjwa na limekuwa eneo ambako majizi yamejificha huko, sasa tumekwama wapi?

Mheshimiwa Spika, nafikiri katika maazimio yetu moja wapo iwe katika kuboresha hii Sheria ya Manunuzi ya Umma, inawezekana tukiboresha hii italeta ufanisi wa miradi yetu lakini ufanisi wa mapato yetu na matumizi yetu ya fedha ambazo tunazipeleka kwenye miradi mbalimbali. Inashindikana vipi hii sheria kuletwa hapa, imefeli wapi mbona sheria zingine tunazibadilisha? Mara ngapi tunabadilisha sheria hapa? Lakini hii Sheria ya Manunuzi sijaelewa sijui kuna jini gani anashindwa kuletwa hapa! Tunaomba hiyo Sheria ya Manunuzi ile tuibadilishe kwa sababu ni kichaka cha watu kula fedha za Serikali au fedha za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa fedha zinazopotea hizo mbichi kwenye Halmashauri ni jambo ambalo lipo kila maeneo, ukikagua leo utakuta, hata ukija kukagua kesho utakuta, hata sisi pale Igunga hivyohivyo fedha zinaliwa na ushahidi upo! Lakini sasa ndiyo mwisho wa siku taarifa inasomwa inaendelea na mwakani, rekebisheni, wanarekebishaje wakati tayari wanakuwa wameshaiba, yaani unamwambia mtu arekebishe au unamwambia haya rudisha taratibu, kama vile kuna mapatano kati ya mwizi na anayeibiwa, tumekubaliana turekebishe zimeshaonekana kumepotea fedha hatua zichukuliwe tu, hamna sababu ya kusema eti kwamba mnatakiwa mzifute hizi, maana yake kuna kufuta hati chafu, au kusafisha hati chafu au kurekebisha yale maazimio ambayo yametolewa aidha na CAG.

Mheshimiwa Spika, hata hili la Mwenyekiti wa Halmashauri kusaini document au mikataba na lenyewe lina ukakasi. Ni kweli Mwenyekiti wa Halmashauri ndiye mwangalizi, sasa akiingia kwenye utendaji inaleta mgongano wa kimaslahi, hili lazima tuliangalie kwa mapana yake lakini kuunda Bodi kwa ajili ya kusimamia management tena kusimamia itakuwa ni mzigo mwingine, hizo fedha tunazitoa wapi kwa sababu mnaangalia tu fedha za kuwalipa Madiwani, fedha za kulipa posho ya vikao za Madiwani hazipatikani lakini tukienda kuunda tena Bodi nyingine naona kama tunaongeza mzigo Zaidi.

Mheshimiwa Spika, tutengeneze njia ya kuboresha Sekretariati zetu za Mikoa katika kusimamia hii mikataba yetu katika level za Halmashauri, katika miradi yetu ya kwenye maeneo, lakini Mwenyekiti wa Halmshauri kusaini mikataba ya kazi za Halmashauri hii ni conflict of interest, mimi nashauri Mwenyekiti wa Halmashauri kama ni Sheria iletwe humu Bungeni tuirekebishe, Mwenyekiti wa Halmashauri aondoke kwenye sehemu ya kusaini mikataba ya kazi za Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)