Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi. Nina masuala kama matatu; la kwanza ni sakata la KADCO na Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro; la pili, suala la TIC kwa maana kwenye Muswada wa Uwekezaji; na la mwisho, suala nguvu za Kamati zako za Bunge ambazo sisi tunazitumikia dhidi ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mtumishi mstaafu, nilibahatika kufanya kazi Wizara na Maliasili na Utalii. Kipindi changu nikiwa Wizarani nilishiriki katika shughuli za kufanya utafiti wa hali ya utalii nchini na bahati nzuri nilikuwa napangwa Kiwanja wa Ndege cha Kilimanjaro kwa miaka takribani mitano mfulululizo. Utafiti huo tulikuwa tunafanya watu wa Idara ya Utalii ya Wizara ya Maliasili, Commission ya Utalii ya Zanzibar, Idara ya Uhamiaji Tanzania pamoja na Benki Kuu.

Mheshimiwa Spika, kipindi chote sehemu yangu nilipangiwa Kilimanjaro ndipo nilipata kuufahamu ule uwanja na kuifahamu KADCO. Kwa bahati mbaya sikubahatika kipindi kile kuifahamu KADCO vizuri mpaka juzi baada ya kuisoma taarifa ya CAG na baada ya kualikwa kwenye Kamati ya PIC kuweza kusikiliza haya masuala yanakwendaje.

Mheshimiwa Spika, kimsingi KADCO kwa sasa ni kama kigenge au kibubu cha watu kufanyia maisha nje ya mfumo wa Serikali. Kinachonisikitisha sikuona kama Katibu Mkuu wa Wizara ile au watu wa Wizara kama wanaumwa na hali hii. Sinema zinazoendelea KADCO wao wako comfortable kabisa, wanapumua vizuri na wanaendelea kula vizuri kana kwamba hakuna kinachoendelea mpaka CAG, Wabunge na wadau ndio wanakuja kuona matatizo ya mle ndani, jambo ambalo linasikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, katika ushirki wangu wa kikao, tunamhoji Katibu Mkuu na watu wake ambao walikuja jopo zima pale, Waraka wa Baraza la Mawaziri Na.5 wa mwaka 2009, ulitoa maelekezo kuwa tutanunua hisa zote za KADCO kutoka kwa wale wabia ambao walikuwa wajanja wajanja. Tutanunua kwa 100% baada ya kumaliza zile hisa, umiliki uende kwa TAA. Aidha, iendelee ku-operate kama kampuni tanzu ya TAA au KADCO ifariki kabisa uwanja uendeshwe direct na TAA kama wanavyofanya Kiwanja cha Dar es Salaam na viwanja vingine, lakini jambo hilo halikufanyika.

Mheshimiwa Spika, tunawauliza watu wa Wizara kwa nini hamjatekeleza maagizo haya? Wanajibu, Waheshimiwa mnajua tulikuwa na mchakato wa kutafuta mbia mpya wa kuendesha. Tukawaambia KADCO nani anawapa mamlaka ya kutafuta mbia, nadhani lilipaswa liwe ni jambo la Wizara na Mkuu wa masurufu (Accounting Officer) wa Wizara ni Katibu Mkuu pengine wangefanya wao. Hata hivyo wanasema kwamba huu mchakato tulikuwa tunafikiria kutafuta mtu. Hali ambayo inaonesha kabisa mashaka na kuna nia ovu ya wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliwahoji, kama kuna mchakato wa kutafuta mtu mpya, sasa hivi ni miaka 12, maana ni mwaka 2010 ndio tulinunua hisa zote, hivyo kampuni imekuwa ya Serikali kwa 100%. Hadi leo tunazungumza mwaka 2022 ni miaka 12, mnachakata kwa miaka mingapi kumtafuta mtu wa kuendesha? Hawana majibu yaliyonyooka, wanaongea vitu ambavyo havieleweki. Nilitamani kumshawishi Mwenyekiti tuwafukuze kwenye kikao. Kwa hekima ya Mheshimiwa Hasunga, alisema tuwasikilize mpaka mwisho, tuone inakuwaje?

Mheshimiwa Spika, tukasema kama kweli huo mchakato ulikuwepo, mmetangaza wapi kwamba jamani tunatoa tangazo, tunatafuta mbia, tunatafuta mtu wa kuendesha Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, mna tangazo ambalo mmelitoa juu ya hili? Halipo. Katika mazingira yoyote inaonekana kabisa kuna nia ovu, hawa watu hawana nia nzuri na ni mchongo tu, wanataka watupige na waendelee kutupiga zaidi.

Mheshimiwa Spika, kituko kingine, wanajibu sasa hivi tuko kwenye mchakato wa ku-renew mkataba wa uendeshaji, ile concession agreement. Awali ile concession agreement ilikuwa baina ya wale wawekezaji na Serikali. Sasa hivi wawekezaji hawapo uwanja ni wetu tangu awali na KADCO imekuja kwetu kwa 100%, Mkataba Serikali inataka isaini na nani? Maana yake wanajadili Serikali kuingia makubaliano ya kuendesha uwanja na jini au hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna muda huwa nawaambia wenzangu tukiwa tunazungumza, muda mwingine Mungu akikusaidia ukiwa huna akili unaishi kwa amani sana, lakini ukiwa na akili utapata stress. Maana upeo wako ukiwa mfupi unaona kila kitu sawa tu, nyeupe na nyekundu ni sare, ndefu na fupi unaona ni sawa tu. Kwa hiyo wenzetu ambao hawana akili wanaishi sawa kuliko sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nakishangaa, kwa maana baada ya sisik kuinunua ile kwa 100% nilitarajia Katibu Mkuu wa Wizara ndiye Mkuu wa Masurufu na watu wake waiagize moja kwa moja KADCO iende TAA, maana, KADCO pamoja na kwamba tumeinunua haiwezi kujipeleka yenyewe na watendaji ambao wako pale wananufaika na KADCO, hawawezi kujipeleka na kusema tumekuja TAA. Ni Katibu Mkuu wa Wizara (KM) anatakiwa aiagize iende, lakini hafanyi hivyo, hakufanya hivyo na anapumua na ana amani tele kabisa, ni kituko. Kwa hiyo, mambo haya yanakera na ni mambo ya wazi kabisa, inaonesha kuna nia ovu, kitu ambacho sisi sote hatukukubaliana.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, kwa hekima za Mheshimiwa Hasunga ambaye alikuwa anakaimu Uenyekiti katika kile kikao alisema, Waheshimiwa hebu tuwape muda kidogo, maana wenyewe waliomba walisema, tunahitaji muda tukajadiliane tutaleta majibu. Tukasema kwa nini mlete majibu mkishajadiliana, mnajadiliana na nani? Katibu Mkuu wa Wizara tuko naye hapo mbele, Mwenyekiti wa Bodi na Bodi yake ya KADCO yuko pale, Mkurugenzi wa KADCO yuko pale, Mwanasheria wa KADCO yuko pale, timu nzima ambayo wanayojua hili sakata wako pale. Pembeni mnaenda kujadiliana na nani ili mtuletee majibu baada ya wiki moja? Ni vitu ambavyo havieleweki. Bahati nzuri kwa hekima za Mwenyekiti, Mheshimiwa Hasunga alisema tuwavumilie kwa wiki moja, Ijumaa inayofuata watuletee majibu. Akasema pia Mheshimiwa Mgungusi tutakualika tena, uje ushiriki na hicho usione kwamba leo tunakwepesha. Hata hivyo, mpaka kesho, mpaka mwakani, hawakuleta majibu.

Mheshimiwa Spika, hapa kuna picha mbili, nia ovu ya moja kwa moja, kwamba wanapiga mchongo, lakini pia ni dharau kwa Kamati yako ya Bunge. Kwa hiyo, pamoja na mambo hayo yote, nashauri kwenye sakata hili tuagize ukaguzi maalum ukafanyike kuhusu KADCO kuanzia mwaka 2010 tangu tumenunua hisa kwa 100%.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu KADCO hawakuwa na Mwanasheria. Kituko kingine wana-hire huduma mtaani kwa maana wana Mwanasheria wao private mtaani na wanalipa. Ukiangalia zile legal services za kila mwezi unaweza ukazimia, bora usijue. Kwa hiyo, siwezi nikasema mengi, naomba tukubaliane ukaguzi maalum ukafanyike kule KADCO, wanaweza wakaona vituko vya hatari.

Mheshimiwa Spika, kingine niseme tu, kama ikiwapendeza, naomba Katibu Mkuu wa Wizara ajitafakari kwa maana ya sehemu ya Uchukuzi, Mwenyekiti wa Bodi ya KADCO ajitafakari, maana ni nje ya mamlaka yangu, lakini nashauri tu wajitafakari, Mkurugenzi wa KADCO na safu yake, Menejimenti nzima ijitafakari. Kwa suala la KADCO naomba niishie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kwenye Muswada wa Uwekezaji. Suala la TIC- Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Kwenye ule Muswada ambao tulipitia Wizara ya Viwanda na Biashara katika kipengele cha Board Members, Wajumbe wa Bodi ya TIC tulipendekeza kuwepo na Wizara ya Mambo ya Nje kama moja ya member wa ile Bodi ya TIC. Kwa sasa kuna Wizara zimetajwa, Wizara ya Fedha ipo, Wizara ya Ardhi, TAMISEMI ipo lakini Wizara ya Mambo ya Nje haipo kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya TIC. Kwa hiyo, sisi tulipendekeza, lakini sasa Serikali nadhani hawakuichukua hii, wakaacha kama ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Spika, naona haja ya Wizara ya Mambo ya Nje kuwepo TIC kwa sababu gani? Tunapozunguzma Uwekezaji mkubwa leo Foreign direct investment zinatoka nje, makampuni makubwa yanatoka nje na leo hii mnajua sera yetu sisi ya kimataifa ni diplomasia ya uchumi. Tunawataka Mabalozi wapambane kuacha siasa bali watafute wawekezaji kuja Tanzania. Wawekezaji wanakuja na mitaji yao au pengine wanakopa lakini wanaingia hapa nchini, wangependa kuona mwenyeji wao yupo kwenye huduma zao. Mwenyeji wao ni Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Mabalozi. Inawezekanaje katika Bodi ya Wakurugenzi ya TIC hakuna mtu wa Wizara ya Mambo ya Nje, lakini kuna TAMISEMi? Nawaza sijui kwa nini kuna TAMISEMI au kwa sababu ya ardhi, wanamiliki maeneo, lakini Wizara ya Ardhi ipo!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tulipendekeza aidha, iongezeke Wizara ya Mambo ya Nje kwenye Bodi au apunguzwe mmoja, apunguzwe hata TAMISEMI, Wizara ya Ardhi anamwakilisha, lakini hakuna sababu ya msingi ya kufanya Foreign Affairs asiwepo kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya TIC, maana hata wawekezaji wanapoona wanalalamika au hawahudumiwi vizuri mwenyeji wao yupo wanabanana naye pale inapendeza, kuliko mtu wa Mambo ya Nje akienda kulalamikiwa na wawekezaji wake ambao amewaleta na yeye aanze kuuliza pembeni hai-make sense kwa hali ya kawaida. Hivyo, napenda kushawishi Bunge kama litakubaliana Wizara ya Mambo ya Nje iongezwe kwenye Bodi ya Wakurugenzi pamoja na ile Kamati ya Kitaifa ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni suala la nguvu za Kamati zako za Bunge ambazo tunazihudumia dhidi ya watendaji wa Serikali. Nimekuwa na uzoefu mdogo tangu nimekuwa nikifanya kazi za Kamati miaka hii miwili ya Ubunge, watendaji wa Serikali mara nyingi hawako serious. Wanakuja kwenye Kamati tunakaa nao, unaona kabisa hawako serious. Kuna watu ni Maprofesa na elimu kubwa lakini wengi unakuta hawa-own taarifa ambazo zinazokuja. Tunauliza maswali ya kawaida kabisa very obvious, hawawezi kusema mpaka unabaki unashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatoa maelekezo kwa mfano Bunge la Bajeti, tunawaambia Bunge lijalo mje na taarifa fulani, fulani wanaitikia ndio Waheshimiwa. Session inayokuja mnakutana hawaleti, yaani kama wametuzoea au wanatuweza hivi. Muda mwingine watendaji wanaambiana kwamba wewe peleka tu taarifa hata zikiwa kubwa, Waheshimiwa Wabunge huwa hawasomi. Waambie tu Mheshimiwa, Mheshimiwa huwa hawasomi. Sasa bahati mbaya wanakosea njia, siku hizi watu wanasoma sana na hata kukesha inapolazimu watu tunakesha, we read between lines, hata wakileta vitabu vikubwa tunasoma na tunafuatilia.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa Wabunge wenzangu ambao ni Mawaziri na Naibu Mawaziri, sisi ni wenzenu. Tupo kuwasaidieni kuhakikisha kwamba tunasaidia hii nchi na inakwenda mbele, there is nothing personal. Mara nyingi utakuta Mawaziri au Naibu Waziri, hawatumii muda mwingi kubanana na watendaji wao. Sijui wanazoeana? Baadaye unakuta Kaibu Mkuu anamwingiza chaka, Waziri anakuja kukaangwa kwa ajili ya mambo ya watendaji wake. Naibu Waziri anakaangwa kwa ajili ya Mkurugenzi fulani aliye chini ya Taasisi zao, kwa nini? Wasiwachekee, sisi tukija kwenye Kamati tunakaza, wakitulaumu sawa, mahusiano yetu ya urafiki yakivunjika sawa, lakini you need to be serious kuwasimamia watendaji.

Mheshimiwa Spika, naomba uwatie moyo Wabunge wako kwenye Kamati kwamba waendelee kufanya kazi seriously. Mtu anashindwa kujibu halafu baadaye wanaongea pembeni kwamba hili suala ni zito sana, msilijadili sana maana huwezi kujua kwa nini halitatuliwi kwa miezi yote halitatuliwi, kutakuwa kuna kit utu. Wanataka kama kuanza kutishatisha watu, lionekane jambo sijui ni la nani? Halipo. kinachokuja kwenye Kamati tunajadili na tunakaza na watalifanyia kazi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa leo nashukuru sana, lakini nasisitiza Katibu Mkuu wa Uchukuzi na timu yake wajitafakari. Ahsante sana. (Makofi)