Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kujadili taarifa ya Serikali za Mita. Mimi nitajikita huko.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kilio cha Waheshimiwa Wabunge wote, kila aliyesimama analizungumzia kwa uchungu mkubwa sana suala hili. Naomba tusimalize kwa kuzungumza peke yake, tuje na maazimio makali ili Bunge hili liwe ni mfano ambao mtu mwingine yeyote aweze kufanya reference kwamba Bunge hili chini ya Mheshimiwa Spika Dkt. Tulia walisimama wakakemea na wakachukua hatua kupinga ubadhirifu unaofanywa katika halmashauri zetu. Hiyo ndiyo opening statement yangu.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye tathmini ya Mkaguzi. Ukifungua kwenye ukurasa wake wa tano, kwanza kabisa anasema, amefanya tathmini ya mifumo ya utawala ambayo tumeizungumzia na amebaini migongano ya kimajukumu kati ya wachaguliwa kwa maana ya Madiwani na watendaji. Hii migongano aliitolea mifano ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa au Madiwani kusaini Mikataba. Hapa ndipo penye matatizo na ulaji uko hapa. Ndiyo maana utakuta kwamba kwa kuwa tunafanya kazi pamoja, sioni Madiwani pamoja na sisi kuwa na political will ya kusimama na kukemea huu ubadhirifu. Kwa maana na sisi ni sehemu, si tunaitwa Madiwani na tunatoka katika halmashauri!

Mheshimiwa Spika, ukiangalia dhana nzima ya utawala bora inatuhitaji hata sasa katika Serikali za Mitaa tuwe na separation of powers. Hii dhana ambayo iko katika Serikali kuu inapaswa kushuka chini, madiwani tubakie au na kazi ya usimamizi na watendaji wafanye kazi za utendaji. Haya ndiyo matatizo, ingawa ndiyo sharti la kisheria la sasa hivi, lakini kwa miaka 38 mfumo huu haujatusaidia. Ni wakati wa kuungalia mfumo kwamba haufai.

Mheshimiwa Spika, kwa nini haufai? Hakuna ripoti ya CAG ambayo kwa mwaka mmoja itakuwa inaonesha kuna matumizi mazuri ya fedha za Serikali, hakuna. Kila mwaka kuna matatizo. Hebu chukulia mfano, fedha ambazo tunazipitisha hapa katika Bunge lako Tukufu, utakuta kati ya asilimia 60 mpaka 75 na kuendelea zinapelekwa katika Serikali za Mitaa, na kule ndipo tunapotegemea pajengwe shule, hospitali na huduma nyingine za wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ukaguzi huu haujaonesha pia pesa za COVID ambazo nazo zilikwenda kufanya kazi hiyo hiyo. Je, leo ukaguzi ungeonesha fedha za ndani zimeliwa hivi na fedha za COVID zimeliwa hivi, pangekalika humu ndani? Sasa nilikuwa nashauri kwamba kwa kuwa ukaguzi umefanyika, matokeo yametokea, ningemwomba CAG akaangalie pia fedha za COVID. Kwa sababu ukiisoma hii taarifa kuna mambo mengi sana hasa yale ya re-allocation yaliyofanyika.

Mheshimiwa Spika, fedha imeingia, inaonekana hii imekwenda kujenga shule fulani; na hii imetokea pale kwenye jimbo langu. Shilingi milioni 600 zimeletwa kwa ajili ya Secondary School Tandale, zimeondolewa zikapelekwa mahali pengine na shule haijajengwa. Haya mambo hayakubaliki. Ukiangalia haya yote ni kwamba hawa watu hawana uwoga kabisa. Wamejawa na dharau na siyo dharau tu, na jeuri, naweza kuthubutu kusema ni jeuri kwa Rais na kwa Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unawezaje kupewa maagizo na Kamati ya LAAC, Kamati ambayo ni sehemu ya Bunge; kamati ikizungumza Bunge limezungumza. Kamati inatoa maagizo, wewe huyatekelezi, kama siyo dharau maana yake ni nini? Kuna tafsiri nyingine yoyote hapo? Bunge linaelekeza ukafanye moja, mbili, tatu, nne, nawe huyafanyi, unatarajia nini? Unatarajia kwamba huna utakachofanywa. Ndiyo maana kwenye opening statement yangu nimesema na kila mtu amezungumza, kwamba lazima tuje na mfano kwamba hawa watu, hatua za kishera zianze kuchukuliwa. Kama ukaguzi huu ni sampling bases ten percent: Je, hizo asilimia 90 zingeonesha nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mengine humu yanaonesha kabisa ni uhujumu Uchumi. Unapokeaje risiti ya kugushi. Jamani Waheshimiwa Wabunge, risiti ya kugushi inatafsiri ngapi? Inatafsiri kwanza kuna makosa ya kugushi; pia kuna tafsiri ya uhujumu uchumi ndani yake. Tumewaona hapa miaka miwili, mitatu iliyopita watu wanaotiwa ndani kwa ajili ya uhujumu uchumi. Lina tafsiri gani hili suala kama siyo uhujumu uchumi? Ukiikosesha mapato Serikali na ukiyatumia mapato ya Serikali visivyokusudiwa, yote hayo ni makosa. Tukikaa kimya na hili likapita; na humu ndani naona CAG ametumia lugha nyepesi, anawaambia TAMISEMI chukueni hatua hizi; maeneo machache, TAKUKURU chukueni hatua hizi.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako liazimie kwamba wale wote wenye dalili za kijinai katika ripoti hii watambulike walipo na wachukuliwe hatua. Kila ambaye amefanya kosa la dalili za kijinai za ubadhirifu wa fedha za Serikali achukuliwe hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge hapa tumedharaulika sana wakati tunapitisha tozo, wametusema sana katika mitandao ya kijami. Uongo, kweli! Tumesemwa sana! Zile fedha tukazipata, tukazipeleka huko kwenye kujenga shule, barabara na ndiyo fedha hizi ambazo zimeliwa au hazionekani. Kama hatukuchukua hatua, leo wananchi watatuona ni watu wa namna gani?

Mheshimiwa Spika, kuna fedha nyingine zinapelekwa katika uwekezaji wa mitaji ambayo haina faida. CAG anazungumza na ametoa mifano kwamba Halmashauri sasa zinaigana katika kutengeneza miradi ya kuwekeza na wengine walikwenda kuwekeza hata katika mabenki. Kuna benki moja waliwekeza karibu share 24,000 ambazo zina thamani ya Shilingi bilioni nne. Sasa hivi shares zile zimepungua zimekuwa za Shilingi bilioni moja. Hakuna faida kwa fedha za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kama kuna sheria ambayo inasimamia mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda kuwekeza, tuilete hapa Bungeni tuifanyie marekebisho. Yawezekana kuna mambo mengine yanafanyika hatuyajui na hii ni sehemu ya asilimia kumi ya ukaguzi. Je, tungekwenda kwenye kila Halmashauri kuona wanawekeza wapi; wanafanya nini? Ni dhahiri kabisa tutakuta kuna fedha nyingi zimepotea.

Mheshimiwa Spika, kuna dharau nyingine. Mkaguzi anakuja anagundua kuna hoja 10,824; zimetekelezwa 3,511 tu ambayo ni asilimia 32. Asilimia 35 hazikuguswa kabisa. Hii ndiyo ninayosema kama siyo dharau ni nini? Wanajua kama hukutekeleza mwaka wa kwanza, wa pili, wa tatu, kama vile tutakavyobadilisha Bunge, Wabunge wakiondoka wanaopiga kelele kama akina Tarimba hawatakuwepo, yatapita. Haya ndiyo mazoea ambayo tumeyajenga. Bunge hili lisikubali. Kwa hali hiyo, tufanyeje?

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nilikuwa nashauri, mfumo mzima wa Serikali ya Mitaa Sheria ile sasa imechoka, inahitaji kuangaliwa. Sheria lazima tuifumue, hata Rais mwenyewe amesema, ameona udhaifu alipokuwa amepokea hii ripoti, akawataka TAMISEMI waangalie. Tuangalie mifumo iliyopo haitusaidii, itupeleke kwenye separation of powers ikiwezekana, kila mtu afanye lake, usimamizi uwepo.

Mheshimiwa Spika, sisi Waheshimiwa Wabunge sioni sababu ya kuwemo katika Halmashauri. Kama hali yenyewe ndiyo hii, maana yake na sisi tunajumuishwa. Wewe sio Mbunge; Mbunge ni Mbunge na Mbunge ni Diwani, leo tutakataa vipi ule uozo ambao umefanyika kule kama sisi sio sehemu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye kamati za fedha sisi ni Wajumbe, ndiyo yanayofanyika humo. Wanafanya vikao sisi hatupo, na muda mwingi sana tuko Dodoma, halmashauri zinakutana katika mabaraza sisi hatupo. Tunaandikwa pale hakuhudhuria kwa taarifa, lakini maana yake ni sehemu ya maamuzi yanayofanyika. Sasa maamuzi yale kama yanatisha kiasi hiki na sisi tumo mle ndani, naomba kati ya mambo ambayo tuangalie, ni Wabunge tusiwe Madiwani ili tuweze kuisimamia na kuishauri vizuri Serikali, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)