Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Miradi inayohusisha fedha za umma ama fedha za Watanzania lazima itekelezwe kwa kuzingatia masuala yafuatayo; moja, lazima ichagize ufanisi; pili lazima iendane na thamani ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya mradi; tatu, lazima iwekewe ushindani; nne lazima ilete maendeleo ya kuiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya umma ni lazima zitekelezwe kwa uadilifu mithili ya matendo ya mke wa mfalme, isiwe hata ina thumni ya udanganyifu ama isiwe hata ina thumni ya ubadhirifu wa aina yoyote. Miradi inayoendeshwa kwa fedha za Watanzania ambazo ni fedha za umma lazima iendeshwe kwa uwazi, kwa sababu rushwa mwenzake ni siri. Miradi yoyote inayoendeshwa kwa usiri mkubwa bila sababu za msingi lazima ilete mianya ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima ifahamike, kwamba, wale waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ambayo inatekelezwa kwa fedha umma lazima wafahamu kuwa hawana hati miliki ya miradi hiyo. Zile fedha ni za Watanzania. na kwa sababu tumewaamini kwa majukumu hayo lazima watekeleze majukumu hayo kwa uadilifu mkubwa, kwa kuzingatia sheria na taratibu na wahakiishe fedha za umma zinatumika kwa maslahi ya Watanzania, lakini si kwa maslahi ya mtu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi hii inapambana na umasikini kwa kiasi kikubwa sana. Nchi hii mpaka leo tunapambana na kupeleka huduma za msingi kwenye jamii, tunapambana na huduma za afya, tunapambana na huduma za maji, tunapambana na huduma za umeme, barabara; ni kwa sababu wananchi hawajafikiwa. Nchi hii mpaka leo Watanzania asilimia 28 ni masikini wa kutupwa wa huduma za msingi.

Mheshimiwa Spika, katika nchi hii Mtanzania wa kawaida pato lake la kila siku ni 2,798/= na si kila Mtanzania anaweza kupata kiasi hicho cha fedha. Nchi hii bado tunapambana na Watanzania. Sasa inasikitisha, inashangaza, inahuzunisha kuona baadhi ya watu wanaweza kupandisha mabega juu wakajivika viti vya ufalme na kutumia fedha za umma kwa udanganyifu, kwa kiburi kikubwa na kwa uthubutu uliopitiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Tanga ni mojawapo ya bandari zenye umuhimu mkubwa si tu kwa Taifa letu la Tanzania bali Afrika Mashariki. Bandari hii hivi karibuni imefanyiwa maboresho kwa kuongeza kina pamoja na ujenzi wa gati ili kuweza kuongeza ufanisi katika kuhudumia mizigo kutoka tani laki saba hadi tani milioni tatu. Zoezi hili lilifanyika kwa kuongeza kina cha maji mpaka kufikia mita 13, lakini vilevile pamoja na ujenzi wa gati.

Mheshimiwa Spika, wakati wa maboresho ya bandari hii kina cha maji kilichokuwa kinaongezwa ilikuwa ni katika eneo la kuingilia baharini ambapo zamani mizigo ilikuwa inaenda kuchukuliwa baharini kwa kadiri ya kilometa 1.7, kwa hiyo maboresho ilikuwa ili ule urefu upungue mpaka kufikia mita 200. Hili lilikuwa ni jambo jema na kwa dhamira njema kwa maslahi ya taifa letu, lakini katika mchakato huu tumepigwa.

Mheshimiwa Spika, Ripoti ya CAG inasema, udanganyifu mkubwa umetokea katika zoezi hili la maboresho ya kuongeza na kufanya marekebisho katika Bandari hii ya Tanga. Tarehe 03 Agosti, 2019 Mamlaka ya Bandari Tanzania iliingia mkataba pamoja na mkandarasi mkuu kwa ajili ya kufanya maboresho katika Bandari ya Tanga. Mkandarasi huyu mkuu ni kampuni inaitwa kampuni ya CHEC.

Mheshimiwa Spika, wakati mkataba huu unaingia kazi iliyotakiwa ifanyike pale ilikuwa ni ya thamani ya bilioni 176.36 ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari iliiingia na Kampuni ya CHEC ambaye ndiye mkandarasi mkuu kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hii. Kampuni hii ilipewa kazi na Mamlaka ya Bandari kwa kazi kuu tatu; moja kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli katika bandari ya Tanga; mbili kufanya tathmini ya athari ya kimazingira; tatu kununua vifaa kwa ajili ya shughuli za bandari.

Mheshimiwa Spika, mkataba huu walioingia kati ya hawa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari pamoja na Kampuni ya CHEC ulikuwa ufanyike kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka tarehe 03 Agosti, 219 mpaka Agosti, 2020. Japo baadaye sasa kutokana na changamoto walizoelezea mkataba ulikuwa extended kwa mwaka mmoja kwa sababu haukuweza kumalizika mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, Mkataba ule ambao ni kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na mkandarasi mkuu, Kampuni ya CHEC, ulikuwa una mapungufu makubwa sana. Moja, Kampuni ya CHEC ambaye alikuwa ni mkandarasi mkuu kabla hajapewa mkataba na bandari alikuwa ameshaingia mkataba na mkandarasi ubia kwa ajili ya kumpa kazi ile ambayo alikuwa anaenda kufanya na usimamizi wa bandari. Yani kazi yake aliyokuwa anapewa alikuwa ameshaenda kumpa third part aifanye, na aliingia mkataba huo na kampuni ubia ya Kitanzania tarehe 01 Agosti, 2019 kabla hajapewa mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.

Mheshimiwa Spika, baada ya siku mbili ndipo mkandarasi mkuu Kampuni ya CHEC akaenda kupewa kazi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. Katika mkataba aliousaini, Kifungu kidogo cha (4.4) kinasema, hairuhusiwi mkandarasi mkuu kwenda kugawa kazi ambazo amepewa kwenye mkataba, labda kama ni ulazima lazima atoe notice ya kabla ya siku 28 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, kama hiyo kazi ina umuhimu wa kwenda kuitoa. Cha kushangaza masharti hayo hayakufuatwa kwa sababu, mkandarasi mkuu tayari alikuwa ameshaingia mkataba na mkandarasi mbia wa kumpa kazi hata kabla hajasaini mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi mkandarasi mkuu, Kampuni ya CHEC baada ya kusaini mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, mkataba wa bilioni 176 akaenda kuigawa kazi ile kwa mkandarasi mbia kwa gharama za chini. Kazi aliyompa mkandarasi mbia ilikuwa ni ile kazi moja ya kuongeza kina na ujenzi wa gati, kazi ambayo ilikuwa inagharimu takribani asilimia 60 ya fedha yote bilioni 176, ile kazi ni ya bilioni 104 kwa ajili ya ile kazi ya kwanza ndiyo akampa mkandarasi mbia. Lakini badala ya kumpa kwa bilioni 104 aliyoichukua Serikalini akampa kwa bilioni 40. Kwa hiyo, mkandarasi mkuu hakufanya kazi, kazi akampa mkandarasi mbia kwa bilioni 40, bilioni 64 akaweka mfukoni.

Mheshimiwa Spika, wakati haya yanatokea Mamlaka ya Bandari ipo, Katibu Mkuu yupo, Naibu Katibu Mkuu yupo, Mkurugenzi wa Bandari yupo na Waziri yupo. Ubadhirifu kama huu unafanyika mbele ya macho yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili halikubaliki, bilioni 64 ingeweza kujenga madarasa 3,200, lakini kampuni, tena ya kigeni, bila ya woga wa aina yoyote, inaenda kinyume na masharti ya mkataba, anagawa kazi hata chini ya nusu ya bei ya fedha ya Watanzania aliyopewa. Zaidi ya nusu ya fedha, bilioni 64 kati ya bilioni 104 ya kazi moja tu anaweka mfukoni; inawezekana vipi? Kwenye nchi hii ya masikini asilimia 28 ya Watanzania inawezekana vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachonishangaza zaidi ni kwamba, Kamati hawakuliona? Mbona haipo kwenye ripoti yao? Imekuwaje? Hawakupata maelezo kutoka Serikalini? Wakati wanafanya majumuisho watuambie kwa nini hawakuliweka jambo kubwa kama hili linalogusa maslahi ya Watanzania na fedha za umma kwenye ripoti ya kamati? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haikubaliki.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nilikuwa nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Kapinga; ukisoma Ripoti ya CAG na kile ambacho Kamati imeleta, hawaku-cover maeneo yote, it is hardly like 10 percent tu. Sasa labda kama Bunge na wewe Mheshimiwa Spika, nampa tu taarifa lakini, tuangalie uwezekano labda wa ku-extend muda ili kamati iweze kupata muda mwingi wa ku-cover ripoti nzima, lakini as it stands haija-cover maeneo yote.

SPIKA: Sasa hiyo ni taarifa kuhusu hoja gani? Au ni pendekezo? Mheshimiwa Judith endelea na mchango wako, nadhani yeye ametoa mapendekezo.

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, hii imetoka kwenye Ripoti ya CAG kuhusiana na ukaguzi wa mashirika ya umma. Suala kama hili hata kama kamati ilikuwa ina muda mchache it can’t go under looked ni suala liko obvious na ubadhirifu wa wazi. Yaani hata ukipima yale masuala makuu yaliyoletwa na Kamati hili lilitakiwa liwepo ndani ya ripoti ya Kamati. Kwa hiyo, Kamati ya PAC itakapokuja kujumuisha watuambie ilikuwaje hapa hili halikuwekwa hata katika yale au wali- discuss nini? Serikali ilitoa majibu gani; ili tuweze kupata, kwa sababu huu ni wizi wa wazi kabisa; ni udanganyifu wa wazi kabisa, yaani hauna konakona. Kwa hiyo, kamati inavyokuja kufanya majumuisho watuambie.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile naomba kupendekeza; kwa sababu fedha za umma ni fedha ambazo zinakusanywa kwa Watanzania kwa jasho, mpaka leo tunahangaika na mikopo ya watoto wetu vyuo vikuu, tunahangaika na vituo vya afya, tunahangaika na barabara, tunahangaika na TASAF, halafu anakuja mtu anachukua bilioni 64 kiurahisi namna hii. Imeshapita miaka miwili, vyombo vya ulinzi na usalama viko wapi? TAKUKURU iko wapi? Kuna mtu hapa hafanyi majukumu yake inavyotakiwa. Tunaomba maelezo ya kina (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashindwa hata kusema maazimio kwa sababu, sijui kamati wali-discuss ama hawaku-discuss ama ilikuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kama kutakuwa kuna maelezo naomba tuazimie kwamba hatua za haraka zichukuliwe kwenye jambo hili na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya ulinzi na uaslama.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, kengele ya pili ilishagonga, lakini nakuongeza dakika tatu umalizie hoja yako. (Makofi)

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuhitimisha.

Mheshimiwa Spika, sisi kama taifa. Sisi kama Wabunge tuliopewa dhamana tuna haki ya kuwa vinara kwenye kulinda fedha za umma. Tuna haki ya kuwa vinara kwenye kulinda fedha za umma. Kama kuna watu waliambiwa walete taarifa, hawakuleta, wanapaswa kuwajibishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupelekana kwenye vyombo vya usalama ni end result. Tangu mchakato unaanza wahusika walikuwepo wapi? Sheria na taratibu zinaonesha, yaani kila siku tutakuwa tunashikana mashati mwishoni?

Mheshimiwa Spika, lazima kama Taifa tuhakikishe fedha za umma ambazo ni fedha za Watanzania zinatumika kwa maslahi ya Watanzania kwa ujumla. Nashukuru sana. (Makofi)