Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa heshima hii, nami niweze kuchangia uwasilishaji wa taarifa za kamati tatu za oversite. Nami nichukue nafasi hii kuanza kuzipongeza hizi Kamati zimefanya kazi zake vizuri kwa mujibu wa taarifa ambazo wamewaslisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kulizungumza, kabla ya kuanza kujadili taarifa ya CAG mimi binafsi nilikuwa natamani kamati zetu zingejadili taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa siku ya tarehe 30/03/2022 alipopokea taarifa ya CAG na taarifa ya TAKUKURU. Mheshimiwa Rais baada ya kupokea taarifa hizo, alibainisha na kutoa maagizo na maelekezo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza alisema, kupitia ripoti hizo mbili, kwamba kuna udhaifu katika uratibu wa Serikali kwa ujumla (Government coordination) ikiwemo kuchelewa kutoa maamuzi hasa kwenye miradi ya maendeleo. Kutokana na tatizo hilo, akaelekeza Katibu Mkuu Kiongozi achukue hatua mahususi kurekebisha udhaifu huo. Kwa hiyo, nilitegemea wapate taarifa ya utekelezaji kwa hii miezi tangu agizo hili litolewe. Hali ya utekelezaji wa agizo hili ikoje Serikalini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Rais alisema, kuna udhaifu kwenye ufuatiliaji wa tathmini ikiwemo utaalamu hafifu na nyenzo hafifu. Akaagiza Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) ifanye uchambuzi na kuishauri Serikali ipasavyo. Kwa hiyo, nilitegema Kamati zetu nazo zifuatilie status ya utekelezaji wa agizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Mheshimiwa Rais akasema, kuna udhaifu Serikalini wa kuwa na mifumo mingi sana ya utoaji wa taarifa ambapo mifumo hiyo haiwasiliani, yaani haiongei. Akaagiza mifumo yote ya mawasiliano Serikalini na kupeana taarifa iangaliwe ili ikiwezekana kuwe na mfumo mkubwa mmoja unaoongea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitegemea kwa sababu haya ni mambo ya msingi ambayo kama yatarekebishwa, yataweza kuondoa yale matatizo ambayo yanaonekana kwenye taarifa za CAG angalau kwa robo tatu yake. Sasa haya mambo ni muhimu sana. Nilikuwa napendelea sana hata kama hawakuyajadili, basi siku zijazo waweze kukaa na kupata status ya utekelezaji kwa sababu haya yalikuwa ni maelekezo ya kisera ambayo yana umuhimu wa kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye taarifa ya CAG. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 143 (1)(a) na (b) inampa mamlaka mdhibiti au CAG afanye kazi ya kudhibiti. Udhibiti (control); yaani controller anapewa mamlaka na hivyo vipengele viwili, (a) na (b). Sasa katika taarifa ya CAG mimi sijaiona taarifa ya CAG inayoelezea jinsi alivyotimiza jukumu lake la udhibiti kwenye taarifa hiyo. Nilitegemea aeleze. Tatizo ni nini? Tatizo kuu, usimamizi wa jukumu hilo umewekwa kwenye Mahakama, ndiyo maana amekuwa hatoi taarifa kuhusu udhibiti kwa Bunge au hata kwa Rais kwa sababu usimamizi wake umewekwa kwenye Mahakama, kupitia kipengele gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ibara ya 143 (6), nanukuu, inasema hivi: “Katika kutekeleza madaraka yake, kwa mujibu wa ibara ndogo za (2), (3) na (4) za ibara hii, CAG hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo haya ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili kuchunguza kama CAG ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.” Mwisho wa kunukuu. Kwa hiyo, kama usimamizi wake umewekwa kwenye Mahakama, kwa hiyo, inategemea malalamiko. Ni nani alalamike Mahakamani ili CAG aweze kusimamia ipasavyo katika utelezaji wa jukumu hili la control?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitarajia CAG atueleze kwamba katika mwaka wa fedha huu alioukagua, yeye katika jukumu lake la udhibiti, tarehe fulani alitoa approval Serikali itumie kiasi kadhaa; tarehe nyingine akatoa approval Serikali itumie kiasi kadhaa; na tarehe nyingine akatoa approval Serikali itumie kiasi kadhaa. Hilo ni jukumu lake ambalo ni not delegated, yaani haliwezi kuwa delegated kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa tu ni CAG mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu taarifa hizi huwa hatoi, nilikuwa napendekeza, utakapofika wakati wa kurekebisha Katiba, tuzingatie kwamba lazima CAG apewe chombo ambacho kitamsimamia kwenye jukumu hili la control kama siyo Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la tatu ambalo ningependa kulizungumzia kwa mujibu wa taarifa yake, huyu CAG amejipambanua kutekeleza vizuri sana jukumu lake la pili ambalo ni ukaguzi. Kafanya ukaguzi vizuri na taarifa yake imeeleza kwa asilimia 100 kuhusu jukumu lake hila la ukaguzi wa mahesabu. Amekagua vizuri na taarifa ziko vizuri. Tatizo lipo kwenye hatua za kuchukua baada ya taarifa zake. Hatua za kuchukua zimekuwa ndogo ndogo sana na kuoneana aibu, labda na kuheshimiana, vitu kama hivyo. Ndiyo maana kila mwaka amekuwa analeta kwenye taarifa zake matatizo yale yale yanayofanana, kwa sababu hatua hazichukuliwi. Matatizo gani ambayo yamekuwa yanaonekana kila mwaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kutokupatikana kwa nyaraka za mapato na matumizi ili azikague kwa wakati; la pili, nyaraka kutokuwa halali; la tatu, kutokutekelezwa kwa mikataba kwa wakati na mapungufu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokutekelezwa kwa mikataba ni tatizo kuu la msingi katika utekelezaji wa miradi. Kwa sababu utekelezaji wa mikatana ili uwe mzuri, kuna mambo mawili; sheria ya ununuzi imeelekeza kwamba kila Afisa Masuuli kule ambako mradi unatekelezwa, anatakiwa ateue wataalamu wawili, watatu au zaidi kadri atakavyoona yeye inafaa, wa kusimamia mradi siku kwa siku. Kwa hiyo, kila idara ya Serikali, kila Wizara, kila halmashauri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako ulikuwa umekwisha.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona nimetumia kama dakika tano hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila taasisi inatakiwa itekeleze hili jukumu, lakini wamekuwa wanalifanya nusunusu na ndiyo maana kunakuwa na matatizo. Sehemu nyingine hata hao wasimamizi hawateuliwi na hatua hazichukuliwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu lingine ili mradi utekelezwe vizuri, lazima kuwe na maafisa mahususi kwa ajili ya ufuatiliaji na tathmini. Nao vile vile wamekuwa hawatekelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ambalo limeonekana, ni kutokutekelezwa kwa ushauri na mapendekezo ya CAG kwa wakati. Hilo nalo ni tatizo. Sheria imeweka muda maalumu kwamba taarifa ya CAG baada ya kutoka, anatakiwa Afisa Masuuli aandae program au mpango mkakati wa namna atakavyotekeleza mapendekezo ya CAG. Wamekuwa hawafanyi hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mapendekezo yamekuwa yakijitokeza miaka yote na maafisa wetu wa Serikali wala hawaogopi chochote kwa sababu hatua zimekuwa hazichukuliwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na ushauri katika maeneo kama mawili au matatu hivi. La kwanza, sheria zipo na zinajitosheleza na zinaweza kutumika kuwachukulia hatua watu ambao wanakosea, lakini zimekuwa hazitumiki. Hawa watu siyo kwamba hawazijui sheria, wanazijua. Wanajua sheria ya ununuzi, wanajua Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma, wanazijua vizuri, lakini makosa mengi yanafanyika kwa makusudi. Naomba sana hatua zile zinazoeleweka ziwe zinachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Kamati za Oversight naomba ziongeze ukali wa mapendekezo yao, ikiwa ni pamoja na kulishauri Bunge kuhusu maazimio ya kuchukua. Nimemsikia Mheshimiwa aliyekuwa anatoa mapendekezo ya maazimio ya Bunge, yeye mwenyewe, lakini yeye mwenyewe ni Mjumbe wa Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiri kule kwenye kamati ndiyo wangeshauri Bunge kwamba Bunge kwamba tunaazimia, ili Bunge liazimie kuchukua hatua moja, mbili, tatu. Hiyo ingelisaidia Bunge kufanya maazimio ambayo yangeisaidia Serikali kuweza kurekebisha maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu naona muda umekwisha, naomba niishie hapo. Naomba sana tujipambanue katika utekelezaji wetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. Ahsante.