Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie kwenye ripoti hizi ambazo zimewasilishwa ndani ya Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitasema kidogo kwenye ripoti ya PAC katika eneo ni moja tu la usimamizi wa mikataba na athari zake katika matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamejadili katika eneo hili kwa kugusia jinsi gani mikataba kwenye nchi yetu haiheshimiwi; jinsi gani mikataba ambayo imefungwa vizuri pasiposhaka na wataalamu wetu, kwa maana ya wanasheria wabobezi (land lawyers) ikija katika usimamizi wake inaleta shida katika nchi yetu. Mifano iko mingi, michache tutaisema lakini mingine imesemwa na wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ripoti ya CAG ametoa mifano mingi sana ya jinsi mikataba ilivyoshindwa kusimamiwa vizuri mpaka fedha za umma zimepotea nyingi sana. Nitasema mifano kama miwili;

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na mikopo mingi sana ambayo imekuwa inakuja baada ya makubaliano ya nchi yetu na mashirika ya kimataifa. Pamekuwa na mradi mikubwa ambao ulikuwa unaendeshwa chini ya TANROAD, Mradi wa Uwezeshaji wa Biashara na Uchukuzi Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni huzuni sana, fedha tunazikopa nje, nyingi sana. Kama ambavyo tunaendelea kukopa fedha nyingi, na mimi nakubaliana kabisa na taratibu za kukopa, na hasa hii mikopo ambayo Mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa awamu ya sita ambaye tunaenenda naye. Mikopo mizuri yenye tija na isiyo na riba kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo masharti ya kimkataba ambayo pale ambapo tunakubaliana kuchukua mikopo mikubwa kwa ajili ya kufanya miradi hasa ya barabara ambayo imetolewa na CAG; katika mradi huu niliotamka, Mradi wa Uwezeshaji wa Biashara na Uchukuzi Kusini mwa Afrika, palitokea malipo ya ada isiyo na tija ya ada ya huduma ya kifedha ya zaidi ya dola za kimarekani laki moja na ishirini na tisa mia tisa na sitini na nane. Hizi ni takriban milioni mia tatu na hamsini, zilipotea tu, na tulifikia tukalizilipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tulizilipa? Tulipewa mkopo fulani mkubwa ambao ulituambia mpaka kufikia tarehe 30 Julai, 2013, miaka kadhaa, zaidi ya kumi ilitakiwa tuwe tumekamilisha miradi husika. Lakini kwa sababu ambazo, inawezekana design ya mradi ilikuwa na changamoto, na sababu zingine ambazo hazina mantiki kabisa tunashindwa ku-meet yale masharti ya kimkataba. Matokeo yake nini; hii ilitokea, bakaa ya fedha ambayo imekopwa; katika bakaa yoyote ambayo ulitakiwa uitumie kwa kipindi fulani na ukashindwa kukitumia makubaliano ya mkataba ni kwamba utakatwa robo ya tatu ya asilimia moja ya kiasi ulichoshindwa kutumia. Hii ni aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikabaki Dola za kimarekani milioni kumi na saba laki tatu ishirini na tisa mia moja themanini na nne na nukta kama ishirini, na taarifa ya Kamati inatuambia hivyo. Ukitafuta robo tatu ya aslimia moja ya fedha hizo dola milioni 17 unapata dola 129,698.90, zaidi ya milioni mia tatu na hamsini; na tukazilipa, tunalipa tu halafu tumetulia. Aliyesababisha damage hii kama nchi hakuna chochote alichofanyiwa na hakuna lolote lililoendelea, business as usual.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu; mfano mwingine CAG anatuambia wa kushindwa kusimamia mikataba yetu ambayo wenyewe tumeiingia, kulikuwa kuna ongezeko la gharama za fidia ya kiasi cha shilingi bilioni 22.35, na hii ni kutokana na kutolipwa kwa kaya 1,125.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1997 Wizara iliyokuwa ya Uchukuzi na Mawasiliano Iliingia na Mkandarasi Mshauri kuhusu jinsi gani ya kuongeza Airport yetu Julius Nyerere International Airport. Katika ule mchakato wa kuongeza kulikuwa na kaya nyingi sana zilitakiwa zilipwe mabilioni. Kiukweli niishukuru Serikali yangu Sikivu, kwa kiasi fulani ilifanikiwa kulipa.

Mheshimiwa Spika, lakini ni ukweli pia katika mwaka ule kwa sababu za kibajeti hatukufanikiwa kuwalipa wote au kulipa fidia zote, tukabakiza wananchi 1,125, ripoti ya CAG inatuambia hivyo. Wale wananchi walitakiwa kulipwa bilioni saba za Kitanzania; lakini tangu mwaka huo hadi tathimini ya mwisho inafanyika mwaka 2020 unaweza ukaona hakuna chochote kilicholipwa wakati wote. Msimamizi wa mkataba hayupo na hajui kama kuna watu aliwaacha pending hajamalizana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kanuni ya 13 (3) ya Kanuni za Ardhi, Uhakiki na Thamani ya Fidia na Ardhi ilibidi wajielekeze kwenye kufanya tathimini upya ili kujua bilioni saba zimeongezeka kiasi gani, zile za wale watu wetu 1,125 ambalo ni jambo jema, ni takwa la kikanuni. Tulipoenda wakasema riba ni asilimia sita, tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2019, lakini ilibidi riba iongezeke, ikatupeleka mpaka wakafanya uthamini wa mara kwa mara. Ilikuwa jambo jema sana ili wananchi wetu wasionewe, ikatufikisha kwenye 29,768.029,951 zaidi ya bilioni 22; nataka kusema jambo hapo. Si sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tumefika wakati tunasema tuna mradi X tunataka kuutekeleza kama nchi, huu wa kufungua airport yetu wakati huo tulifikiri ni jambo jema. Maana yake mhandisi mshauri alishasema pana idadi ya watu hawa, tunajua maeneo ya pale, lakini hawa watu wanatakiwa walipwe kiasi hiki. Kama tunakwenda maana yake tuko tayari kwa fedha za ndani na fedha za nje. Sasa kama tumekaa kutoka bilioni saba hadi bilioni 29, tunaambiwa na CAG, bilioni ishirini na mbili nukta kadhaa ni deni mpaka sasa tunavyoongea, sio sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamesema hapa, hii ni kiashiria kibaya sana. Wataalamu wetu wanakaa wanajua kuwa wanatakiwa wasimamie mikataba ile lakini hawaisimamii kwa wakati lakini wanaacha. Je, wanaacha kusudi ili riba iongezeke? Au wanakuwa na sababu zipi? Sasa tumetoka billion saba hadi bilioni 29. Bilioni 22 linakuwa deni.

Mheshimiwa mwenyekiti, hii sio sawa; fedha za Watanzania zinapotea. Bilioni 22 tungezipeleka kwenye Jimbo la Kibamba. Leo mimi ninalia maji hayatimii, barabara hazipo chini ya kilomita tano za TARURA na TANROAD hakuna. Huduma nyingine ni changamoto sana. nimpongeze sana Mama Samia anatusaidia sana, tunaona huduma nyingine za afya na elimu zinakuja, lakini tunashida kubwa bado. Maji hatuyaoni maeneo mengi, na ninasema kila siku, barabara bado sana, idadi ya watu Dar es salaam ni zaidi ya milioni nne na nusu. Sasa, hivi tunafanyaje? Sio sawa, lazima tuiseme.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hizo sababu mbili za kushindwa kusimamia mikataba ya nchi yetu vizuri. Ahsante.