Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kidogo kuhusu taarifa ya Kamati za PAC, PIC na LAAC. Nianze kwa kuunga mkono hoja ya taarifa hizi, nami ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC nashukuru Wajumbe wamechangia, nami naweza kuongeza kidogo kwa sababu tumesikiliza namna gani mnavyounga mkono kazi yetu tuliyoifanya na inafurahisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kiswaga ameuliza swali bado wapo? Bado wapo kwa sababu nchi hii imelea mfumo wa wizi! Narudia nchi hii imelea mfumo wa wizi, tumelea kizazi sisi wenyewe! Mfumo huu umebadilika sasa umekuwa utamaduni, tumeuchukua kama sehemu ya maisha yetu. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mdogo tu ndani ya Halmashauri ya Longido, wengine wanasema mambo ya Serikali Kuu ngoja sisi turudi huku chini, msije mkafikiri kwamba uchafu huu mnaousema Serikali Kuu, kwa sababu ni mahela makubwa, ngoja niwapeleke Longido mjue kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la TANESCO walilipa pesa za fidia kwa Halmashauri ya Longido 341,820,000 na walikuwa wanalipa vijiji ile njia iliyopitisha umeme kutoka Longido kwenda mpaka kuvuka kwenda Kenya. Pesa hizo, ziliwekwa katika Halmashauri ya Longido. Afisa Masuuli alichukua 251,320,000 akapeleka kwenye akaunti ya Vijiji, alikuwa anapeleka asubuhi pesa zinatolewa baada ya masaa mawili kama zile za EPA. Alivyoona afanye nini akachukua milioni 90 akampa Mkuu wa Wilaya ili kumkata ngebe! Yaani Mkuu wa Wilaya anafungwa zipu mdomoni! nafikiri alimuona kwamba ana maneno maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa hizi zilichukuliwa zikapotea na Afisa Masuuli huyo akasema zilikwenda kwenye uchaguzi. CAG alipokwenda kufuatilia Tume ya Uchaguzi ikasema haijui hizo pesa. Pesa hizi zimepotea na hazijawahi kupatikana na hazina kielelezo. Afisa Masuuli huyu yupo kazini! Mkuu wa Wilaya yupo kazini!

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ndiyo mtiririko wa malalamiko ya Waheshimwa Wabunge, kwamba mtu anafanya kitu cha namna hii bado anaendelea kukaa kazini, huu ni mfumo tumeulea unapendeza sana! Je, tutawezaje kuurekebisha? Kama wote tunaheshimiana na tunahurumiana? Tunaona kwamba hakuna sababu ya kusemana, yaani mtu anabeba fedha zote hizo viongozi wapo wanaona, kinachofanyika kwa watu kama hawa wanahamishwa anatoka kwenye Halmashauri moja kwenda nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukaguzi wetu kama LAAC tumegundua hilo, wakipewa taarifa kwamba Kamati ya LAAC itakuita kwenye Halmashauri wanamhamisha the next day, unapata Mkurugenzi ambaye amekaa kwenye Halmashauri mwezi mmoja atajibu nini, wakati manyanga yalifanywa na Mkurugenzi ambaye alihamishwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba sana, jambo hili tusichukulie mzaha hii nchi inapoteza pesa nyingi na wapigaji kama nilivyosema ni wengi na wanaoshiriki pia. Mimi najiuliza Je, huu mfumo tumeulea unaanzia wapi, ukatiririka wapi mpaka kwenye Kijiji? there is something wrong somewhere! Naomba niishie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kuhusu ukosefu wa Watumishi katika Halmashauri. Halmashauri zetu na hasa zile za pembezoni hazina watumishi kabisa. Majuzi ni kweli tumepitishwa na TAMISEMI katika mfumo wa TAUSI na wameenda mbali wameonesha watakavyoweza kutoa mikopo ile ya asilimia Kumi kwa njia ya kielektroniki. Sasa nikajiuliza hawa wamefanya hapa TAMISEMI je, wapo wataalam huku chini? Hakuna wataalam wa TEHAMA katika Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Maendeleo ya Jamii hawawezi hiki kitu, zipo Halmashauri ambazo zina pesa nyingi kama Maafisa Maendeleo wangeweza kusimamia mikopo hii lakini hawana magari, hawana hata pesa. Tuliuliza kwa nini Mkurugenzi hatoi pesa za usimamizi wa mikopo hii? TAMISEMI wakatuambia kwamba wanapanga kwamba kwenye mkopo humohumo kutoke na pesa ya kusimamia mikopo, hatukukubaliana na jambo hilo. Tulisema Mkurugenzi maana yake mikopo hii Waheshimiwa Wabunge haina riba hairudishwi na haina riba. Sasa kama hakuna riba na siamini kwamba huo mfuko uko too political. Hata kama ungekuwa wa kisiasa hauna riba? Yule anayekusanya mikopo anatumia nyenzo gani kuweza kufuatilia hiyo mikopo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ndani ya Halmashauri kuna upungufu mkubwa wa Engineers tumesema hapa tena kwenye miradi ile ya force account, wasiwasi wangu nafikiria kwamba kule mbele tutakuwa na crisis ya miradi hii ambayo inayo pesa kubwa lakani haina msimamizi. Darasa linajengwa leo kesho nyufa! Nani anasimamia? Tumetoa ushauri kwamba kwa sisi ambao ni vijana wa zamani tulimwona Rais Hayati Mwalimu Nyerere wakati ule anahangaika na Walimu ali-introduce kitu kinaitwa Universal Primary Education aka-train Walimu kwa misingi aliyoiona yeye. Ni kwa nini Halmashauri, TAMISEMI, VETA na sehemu nyingine msikae kwa pamoja mkatengeneza technician? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako vijana wengi ambao wamemaliza Form Six na Halmashauri inaweza kusomesha watu hawa. Halmashauri kusomesha mtoto VETA akawa technichian wa ujenzi ni gharama ndogo sana, ni lazima Serikali mtoke ndani ya box, lazima Serikali iyaone haya, kama tunakosa Engineers basi tutengeneze watu hapa ambao watasimamia ujenzi, tutengeneze sisi wenyewe watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zinaweza kabisa kusomesha watoto mafunzo ya TEHAMA vijana wapo, Halmashauri wanaweza kusomesha Technicians kama siyo Engineers ambao wanaweza kwenda kule vijijni wakasimamia ujenzi kwa sababu hii miradi imechukua pesa nyingi lakini haikujengwa imara. Inawezekana baada ya miaka fulani miradi hii yote madarasa yakaanguka, japo wengine wanajitahidi, lakini iliyomingi haitekelezwi kwenye viwango vinavyotakiwa. Kwa hiyo, naomba Serikali, TAMISEMI na Halmashauri tuje na idea ya kusomesha Watoto. Wanao uwezo Halmashauri kama wanapoteza pesa namna hiyo, mtu anampa Mkuu wa Wilaya anamfunga mdomo kwamba usiseme chukua Ninety Million na wewe uweke hapa halafu ukae kushoto! Kwa nini pesa kama hizo zisiende kusomesha watoto na Halmashauri ikawawekea mikataba fanyaeni hapa miaka mitatu mtusaidie hiki, hiki na hiki halafu baadae uondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kidogo kuhusu kupeleka bajeti kubwa na ndogo katika miradi ya maendeleo katika Halmashauri. Aliongea vizuri Mheshimiwa Kitila lakini wasiwasi wangu ni kwamba, haya mambo ya kupeleka pesa pungufu yanaumiza Halmashauri maskini. Hebu fikiria Halmashauri kama ya Bumbuli ina mapato yasiyozidi Milioni 800 kwa mwaka. Kama Halmashauri inakusanya Milioni Mia Saba au Milioni 800 what do you expect? Hivi hawa wanaweza kuchangia nini hata hiyo 40 percent ya maendeleo, watachangia alafu hamupeleki hela, mnawapelekea 33, 34 percent na ukitazama Halmashauri zote za Tanga huko zimekaa mkao huo, sijui mnafikiria nini, sijui mna agenda gani huko, hakuna pesa zinazokwenda kwenye Halmashauri zote Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili mlitazame kwa maana kuna Halmashauri ambazo uwezo wake ni mdogo. Halmashauri ya Bumbuli ilikuwa na Kiwanda kimoja tu cha Chai na sasa hakifanyi kazi miaka mingapi, sijui wanatoza ushuru kwa nani? Zipo nyingine ambazo hata kutoka kwenye Halmashauri kwenda kununua mafuta kama ile ya Momba unatembea karibu Kilometa mia moja na kitu, sasa Mkurugenzi anakwenda kununua mafuta Kilometa mia moja halafu akirudi mafuta yameisha. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho CAG anakagua siyo tu mambo ya pesa peke yake, ametuambia kuhusu elimu, kwamba kuna drop out kubwa sana kwa watoto ambao wako darasa la…

(Hapa Kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)