Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi uliyonipatia, lakini nianze kuunga hoja taarifa hizi tatu ambazo zimeletwa na Kamati zetu hapa Bungeni. Sisi tunaamini kwamba, Kamati ya PAC, PIC na LAAC, CAG ndiye jicho letu, maana yake ndiye jicho la Bunge. Kwa hiyo, tunapokuwa humu ndani sasa hivi leo, tunafanya kazi sisi wenyewe kama CAG. Kwa hiyo, tunapoona kuna watu wanateteatetea haya mambo tunajiuliza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana mchangiaji wa mwisho hapa, Profesa Kitila, amesema CAG ameshaleta mapendekezo mengi, lakini hayafanyiwi kazi. Hayafanyiwi kazi kwa sababu, sisi wenyewe humu tena tunawateteatetea hawa ambao wamesemwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Bunge ni kutunga sheria. Tunapotunga sheria miongoni mwetu humu kuna Mawaziri wanakwenda kutunga kanuni ili kuiwezesha sheria kufanya kazi. Wanapokwenda kufanya kazi tumepitisha bajeti hapa ya miradi, wao ndio wanaoandaa Bill of Quantity, makadirio ya mradi. Wao ndio wanaoandaa taasisi hiyo, inaandaa mikataba; ikiandaa mikataba inaweka vigezo mbalimbali. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Taasisi ya TANROADS…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Maganga.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumpa Taarifa mchangiaji. Kwa kweli, wanaojaribu kuteteatetea kuhusiana na hii ripoti, nataka nimwongezee tu mchangiaji, yeye atiririke tu asiwe na wasiwasi tutafikia hitimisho na nawaandika hapa wale wanaotetea, tutakuja kumalizana mwishoni. (Kicheko/Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga unapokea Taarifa?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na miradi ya bilioni 664 ya ujenzi wa barabara. Bilioni 600 hizi wakandarasi walicheleweshewa kulipwa na kufanya Serikali kuingia hasara ya jumla ya bilioni 68.7. Huu ni udhaifu wa usimamizi wa mikataba. Kama ambavyo nilisema sisi ndio tunaandaa makadirio, sisi ndio tunaandaa mikataba, halafu tunashindwa kusimamia mikataba, kulipa kwa wakati mkandarasi akiwa amemaliza kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki kwenye dunia hii. Hatuwezi kukubaliana na jambo hili. Nchi hii ni tajiri, lakini inataka kufilisiwa na watu ambao kimsingi wanaangalia maslahi yao. Inaingiaje akilini kwamba, tuliweka sheria ya siku 28, tukaweka sheria ya siku 56 ili mkandarasi awe ameshamaliza kulipwa, jumla ni siku themanini na ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuangalie, tuwafuate mmoja mmoja ambaye amesababisha hasara hizi, kwamba, mkandarasi alipo-raise certificate ilikaa kwake siku ngapi ili tumwone nani ameingiza hasara hizi. Haya yamekuwa ni mazoea, huu ni mradi mmoja tu wa taasisi moja ya TANROADS; miradi mingi ya Serikali yote ina riba, kwa nini tuwe na riba? Kwa nini tuwe na riba wakati kuna wataalam waliobobea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewapa ofisi nzuri, tumewapa magari, tumewapa kila linalowezekana ili wafanye kazi hizi, haiwezekani hata siku moja. Kwa hiyo, Bunge tuangalie ni nani aliyesababisha hasara hizi, awe ni mtoto wa shangazi, awe ni mjomba, awe ni mke wangu, wote wachukuliwe hatua. Haiwezekani nchi hii watu wakatengeneza kichaka cha kupigia kwenye miradi na sisi tupo, haiwezekani. Tumekuja hapa Bungeni kufanya kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tulikuwa tunajadili kuleta Muswada hapa wa bima na Wabunge tunalalamika kwamba, wananchi hawana uwezo wa kuchangia, kumbe fedha ambazo zingeweza kulipa zimekwenda kulipa riba na sisi tupo, haiwezekani! (Makofi)

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, Taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nampa taarifa mzungumzaji kwamba, hata hizi riba ambazo zimelipwa bilioni 68 hazikulipwa kwa wakandarasi wazawa, zimelipwa kwa kampuni za nje. Hakuna mkandarasi mzawa anayedai fidia kwenye Serikali, maana yake riba na mimi nikiwemo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga unapokea Taarifa?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo maana yake nini? Ni kwamba, hawa wataalam wetu walioko ofisini wanakaa wanazungumza na hizi kampuni, tukucheleweshee certificate, tukulipe riba, halafu na mimi uje unipe cha kwangu, ndivyo inavyoonekana. Halafu Serikali imeshindwa kuweka utaratibu wa kisheria wa kuteua bodi, Executive Board, inateua bodi ya ushauri ilimradi iwe na mkono wake na yenyewe au kuna namna gani humo ndani, Serikali watueleze haya maneno haya? Kwa hiyo, Bunge tuchukue hatua kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili nakwenda kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Imezungumzwa hapa, bahati nzuri Mheshimiwa Songe jana alizungumza kwamba, kuna watu wanapewa mikopo ambao hawana sifa, ni zaidi ya bilioni mbili, ngoja niangalie hapa. Ni zaidi ya bilioni 2.5 hivi, bilioni 2.255, hawana sifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wataalam wamebobea wako kule ofisini wanatoa kwa watu ambao hawana vigezo, watoto wa walalahoi wanakosa hela hizi. Nilimsikia Mheshimiwa Spika, jana anasema hawa wataitwa, hivi bado wapo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata Mheshimiwa Waziri mwenyewe wa Elimu alipouona huu uozo akateua Kamati, Kamati ikaenda kukwamishwa maana yake nini? Unajua Sheria haina mbadala na sisi ndiyo watunga Sheria, akikwamishwa Waziri Kamati yake maana yake Serikali imekwamishwa kufanya kazi, hao bado wapo? Waziri, tena Profesa mbona tunataka kuchelewa nchi hii, hao hawana mjadala, hao anzeni kuchukua hatua mara moja. Haiwezekani Serikali inakwamishwa na taasisi ambayo imeiweka yenyewe, halafu Bunge tuko hapa, CAG leo sasa anafanya kazi yake lazima tuamue, haiwezekani! Tuliomba Ubunge ili tuwasaidie wananchi, Hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine mmetupa Kamati ngumu kweli! Kamati ya PAC ya kuangalia wezi, usiku na mchana wezi! tena Kamati hii inamaliza vikao kila siku usiku Saa Mbili, hizi Kamati ni nzito kweli halafu tuache hawa,tumeumia migongo hawa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio letu tuchukue hatua iwezekanavyo hawa hawapaswi hata kukawia kama ni Jumamosi wangeitwa, sijui waitwe lini, sijui kesho asubuhi ili kwanza Kamati iwanyonge, halafu sasa azimio letu nalo Jumamosi tukamalizie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, PAC ilipendekeza Bodi za Wakurugenzi kwamba zikimaliza muda wake ziendelee, hili nalo siyo sawa kwa sababu inafahamika bodi hii inamaliza muda wake lini, kama inafahamika wale wanaopendekeza majina kwenda kwa mamlaka ya uteuzi wanaweza wakawa wanachelewesha, kwa sababu yupo mtoto wa Shangazi, Mjomba, yupo mate wangu, wanachelewesha hata kama bodi hii haitoi matokeo chanya, Hapana! Wale wanaopendekeza majina kama tutabaini wanachelewesha kupeleka kwa mamlaka ya uteuzi tuchukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu, Bodi hizi…… samahani niongeze muda kidogo. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya dakika moja hitimisha hoja yako.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Bodi siyo mahala pakwenda kupumzikia. Kuna utaratibu wa kuchagua watu ambao wanaelekea kustaafu sikatai, lakini kuna wengine ukiwaona wakitoka PAC wengine PIC pale, unaona wamechoka, unaweza kutafakari sijui wanaomba msaada huyo au namna gani! Lakini nataka niwaeleze Bodi hizi ni za kwenda kuweka akili ili Shirika au Taasisi iendelee. Haiwezekani tunao vijana wazuri wa miaka 30 au 45 wanashindwa kuteuliwa kwenye Bodi tunateua watu ambao kimsingi wanapaswa kupumzika, tusifanye hisani kwenye Mashirika yetu na Taasisi zetu tupelekeni akili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)