Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii. Naomba nichangie kwenye taarifa zetu mbili hasa hii taarifa ya LAAC. Nikiwa sehemu ya Madiwani kule kule ninapotoka, nianze na eneo moja la Mwenendo wa Bajeti na Kiwango cha Utegemezi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, nitambue ukweli kwamba halmashauri nyingi nchini kwa kweli zinajitahidi sana kukusanya mapato kwa kuzingatia makadirio ambayo imejiwekea.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ukiangalia huu mwaka wa fedha ambao CAG ameufanyia audit, 2020/2021, Halmashauri zilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 822.38 na zimekusanya bilioni 799.42, sawa na asilimia 94. Kwa hiyo, zinafanya vizuri na kwa nini? Uki- bench mark na Serikali Kuu TRA ilipanga kukusanya trilioni
20.326 ikakusanya trilioni 17.599 sawa na asilimia 86.6. Kwa hivyo, tukilinganisha kiufanisi na kitakwimu halmashauri zetu zilifanya vizuri kuliko Serikali Kuu. Hili ni vizuri tukaliona kwa sababu huwa tunaona tu ule upande wa udhaifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukweli ni kwamba, changamoto za halmashauri zetu sio uwezo wa kukusanya, changamoto kubwa ni ufinyu wa vyanzo vya mapato, hii ndio changamoto kubwa ambayo inatukabili. Ndio maana katika shilingi trilioni zaidi ya 34 kwenye bajeti ambayo tunaijadili, halmashauri zote ukikusanya kwa pamoja hata trilioni moja haziwezi kukusanya, kwa hiyo, ni changamoto kubwa. Tunategemea tu leseni za biashara, service levy, leseni za vileo, vibali vya ujenzi na vibali vya sherehe kwa wale wanaokaa kwenye manispaa na mijini, ukienda vijijini huko wanategemea ushuru wa mazao na kadhalika. Sasa hivi vyanzo ni vidogo ni vifinyu, haviwezi kuifanya halmashauri itekeleze jukumu lake sawasawa kama ambavyo imewekwa katika Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chanzo kingine tunafahamu ruzuku, lakini CAG anasema nini kuhusu ruzuku ambazo zinapelekwa kwenye Halmashauri? Mambo matatu; moja kuna halmashauri kama 19 ambazo zenyewe zimepokea ruzuku zaidi ya bajeti yao, kiwango cha shilingi 47.19 na ipo kwenye taarifa ya Kamati yetu. Pili, kuna halmashauri 163 zenyewe zimepokea ruzuku chini ya bajeti yao, yaani imepungua kwa shilingi bilioni 312, lakini tunazo halmashauri 144 ambazo zenyewe hazikupokea kabisa ruzuku ya matumizi ya kawaida. Hii maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ruzuku kimsingi ni hisani, hakuna formula inayotoka Hazina inayotumika kugawa ruzuku, inategemea pengine bidii ya Mkurugenzi mwenyewe, inategemea Meya anaongea vipi na Hazina, ndio maelezo pekee, lakini kwa nini tuwe na variable ya ugawaji wa ruzuku? Hii ni hisani. Je, ni sahihi sisi kama Bunge hili tuendelee kutegemea hisani ya ruzuku? Au tuweke utaratibu mzuri ambao kuna formula inaeleweka na nchi nyingi zimeshaweka, nchi nyingi zimeweka vizuri kabisa kwamba, kila jimbo linapata shilingi ngapi kwa utaratibu upi? Wamefanya hiyo South Africa, wamefanya hivyo Nigeria, wamefanya hivyo juzi wenzetu Kenya kupitia Sera yao ya Devolution. Kwa hiyo nataka niiweke hiyo observation ambayo nadhani ni muhimu sana sisi kama Bunge tukaelewa na tukaizingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nipendekeze kutatua hili tatizo kwa sababu tuko kwenye kikao hiki cha hili Bunge hili na hapa hatuishauri Serikali, tunataka kuweka maazimio ili tukasimamie utekelezaji. Naomba nipendekeze mambo matatu na naomba Mwenyekiti wa Kamati kama itampendeza achukue haya mapendekezo, kama ninavyosoma kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa Halmashauri zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha, mapato kwa ajili ya uendeshaji na miradi ya maendeleo;

Na kwa kuwa ruzuku kutoka Serikali Kuu imekuwa haiendani na bajeti za halmashauri na mara nyingi haipatikani kwa muda muafaka.

Na kwa kuwa vyanzo vingi vya mapato vya kodi vipo kwa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii niifafanue, vyanzo vingi vya mapato katika halmashauri vilienda TRA. Tulikuwa tunategemea sana property tax ilienda na juzijuzi tumenyang’anywa ushuru wa mabango na wenyewe hatukusanyi tena na haieleweki sasa hivi anakusanya TANROADS au TRA, lakini halmashauri zimenyang’anywa kukusanya hiyo. Na kwa kuwa kwa hali hii imekuwa ikiathiri uwezo wa halmashauri katika kutekeleza wajibu wake wa kisheria na Kikatiba;

Hivyo basi, Bunge linaazimia kuwa: -

(1) Bunge liweke utaratibu wa kisheria na kikanuni wa kugawana mapato ili kwamba, sehemu ya mapato ya kodi yarudi katika halmashauri. Kama Serikali Kuu tumekubali kwamba, TRA ndio Professional Tax Collectors, lakini TRA hawezi kufanya makusanyo ya property tax bila kushirikisha halmashauri, hivyo tukubaliane kwamba, sehemu ya kodi hiyo irudi halmashauri kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika halmashauri ili utaratibu wa kupata hizi fedha uwe ni wa haki, ni wa kisheria kuliko kusubiri hisani ya Hazina.

(2) Kwa kuanzia katika mwaka wa fedha ujao, asilimia 40 ya mapato ya kodi ya majengo na ushuru wa mabango irudi kwenye halmashauri husika; na

(3) Serikali iweke utaratibu na vigezo vya wazi vinavyotumika katika kugawa ruzuku kwa halmashauri ambazo hazina vyanzo vya uhakika vya mapato kwa ajili ya uendeshaji na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mapendekezo matatu ambayo nayatoa katika kuboresha jambo hili ili halmashauri zetu ziwe na uhakika wa mapato na kwamba, utolewaji wa ruzuku ufanyike kwa mujibu wa sheria kuliko ilivyo sasa ambapo tunaona kabisa halmashauri hii inapata na nyingine haipati. Hilo ni eneo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ambalo limeibuka kwenye Taarifa ya CAG na bahati mbaya sijaliona kwenye Kamati zetu ni suala la mfumo wa udhibiti wa ndani. Usimamizi wa vihatarishi na mfumo wa utawala bora. CAG katika ripoti yake ameibua jambo kubwa sana, ukurasa wa 8-13 anasema, changamoto za mfumo wa uendeshaji wa Serikali za Mitaa amehoji kile ambacho wanaita mwingiliano kati ya Madiwani na mamlaka za utendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amebainisha kwamba, Madiwani wamekuwa wakishiriki katika shughuli za kiutendaji za mamlaka ikiwemo kwa mfano Wenyeviti na mameya kusaini mikataba na ameona hili jambo sio zuri. Sasa hili tumrejeshe CAG kwenye Ibara ya 145 na Ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumrejeshe CAG kwenye sera ya ugatuaji decentralization by devolution ambayo tuliipitisha mwaka 1996. Tumrejeshe pia kwenye Sheria mbili ambazo zinaongoza Local Government Authority.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Serikali kamili na zipo chini ya Madiwani. Kwa hiyo, ni jambo la muhimu likaeleweka na Waheshimiwa Wabunge hapa sisi ni Madiwani na zile lawama zote ambazo tunazitupa halmashauri ni za kwetu. Sisi ndio wasimamizi, sio tu wasimamizi, sisi ni waendeshaji wa halmashauri tofauti na Serikali hapa, tunaweza tukalaumu Serikali Kuu hapa kwa sababu sisi ni washauri tu, lakini sisi ndio waendeshaji na wasimamizi wa halmashauri kisheria. Sasa kiuhalisia hiyo tutajadili siku nyingine kwamba, kweli sisi tuna nafasi kiasi gani? Hivi kati ya DC na Mkurugenzi, Mkurugenzi akiagizwa akipewa maelekezo na DC anafuata ya nani? Hili tulijadili siku nyingine, lakini kwa sasa tuseme kwamba, Waheshimiwa Wabunge sisi ni Madiwani zile halmashauri zipo chini yetu na kwa jambo hili CAG sio sahihi. Kwa hiyo, azimio hapa liwe ni kwamba:

“Serikali iongeze kasi katika utekelezaji wa sera ya ugatuaji na kuwajengea uwezo wa kutosha Madiwani. Na kwamba, irudishe mamlaka ya Madiwani dhidi ya watumishi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la msingi kwa sababu, sasa hivi Madiwani kwa kweli mamlaka dhidi ya watumisi ni madogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kwa sababu ya muda nilisikia kengele hapo. Hili ni la wananchi wa Ubungo kule.

MWENYEKITI: Nimekuongeza dakika mbili Profesa.

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ubarikiwe. Ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, tunao Mradi wa DART Dar-es- Salaam, mradi muhimu na unatusaidia sana na tunaupenda, lakini naomba katika suala la kutwaa maeneo ya wananchi wazingatie sheria ya fidia wala wasifanye vinginevyo. Zoezi hili liwe la wazi, liwe shirikishi kama sheria inavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna mgogoro pale Ubungo Kisiwani kaya 91 zinataka kuondolewa. Uthamini ulifanyika katika utaratibu ambao haueleweki, wananchi wamelalamika, Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 7.8 kwa ajili ya fidia, lakini watu wa DART wameshindwa kusimamia utaratibu mzuri wa kuweka utaratibu pale kwa ajili ya fidia. Mheshimiwa Waziri tumelizungumza hili naomba alifuatilie ili wananchi wale watendewe haki, wapishe mradi, fidia ilipwe kwa mujibu wa sheria. Hili ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika moja iliyobaki nichukue nafasi hii kuzipongeza sana Kamati zetu mbili kwa kazi kubwa, ripoti zao ni nzuri sana. Tupongeze vilevile halmashauri zetu kwa sababu, kwa mara ya kwanza wamepata hati inayoridhisha asilimia 96. Ukiangalia kwa miaka mitano hiyo record haijawahi kuvunjwa, kwa hiyo, ni jambo jema, halmashauri zetu zinafanya kazi katika mazingira magumu, tuwatie moyo, tuwasimamie wafanye vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale wanapofanya vizuri tuweze kuwatia moyo, kwa hiyo, hili ni jambo zuri ambalo nadhani kwamba, ni muhimu likazungumzwa. Hii ni sawa na waliopata kwenye upande wa Serikali Kuu, lakini la mwisho, bahati mbaya mapendekezo mengi hayatekelezwi yale ya CAG na CAG analalamika kwamba, mapendekezo mengi yamekaa bila kutekelezwa. Azimio moja tupendekeze hapa ni kwamba, pengine kuanzia mwaka ujao wa fedha pale ambapo Mamlaka ya Serikali za Mitaa au Mamlaka ya Serikali Kuu haijatekeleza angalau asilimia 50 ya mapendekezo ya CAG, watu hawa waitwe kwenye Kamati yetu ya Haki na Maadili wajieleze na hatua stahiki zichukuliwe ili tuokoe fedha za wananchi wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya malalamiko mengi ambayo tunayatoa hapa CAG ametoa mapendekezo namna ya kuyashughulikia, watu hawatekelezi. Bahati mbaya hawajachukuliwa hatua yoyote criminal kwa sababu, CAG report sio criminal document ni jambo nadhani kwamba, sisi kama Bunge tutake watu hawa waitwe. Kama mtu anaweza akaitwa kwenye Kamati kwa kosa dogo, kama amefuja fedha za wananchi aitwe kwenye Kamati yetu ya Haki na Maadili ili ajieleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)