Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika mjadala huu unaoendelea. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye Enzi na Utukufu kwa kunisimamisha mahali hapa muda na wakati kama huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kuchangia katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali katika kipengele cha 9.2 cha Usimamizi wa Manunuzi na Mikataba. Kwa mujibu wa CAG amesema kwamba Taasisi 16 zilinunua bidhaa na huduma zenye thamani ya shilingi bilioni 77.62 bila kutumia mfumo wa TANePS

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni ya 342 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2013 kama ilivyorekebishwa mwaka 2016 imezitaka taasisi za Serikali zinazofanya manunuzi ya Umma kutumia mfumo huo wa TANePS. Pia Waraka Na. 4 wa Wizara ya Fedha umezitaka taasisi hizo kuanza haraka kufanya manunuzi ya Umma kuanzia tarehe 01 Januari, 2020. Kwa maana mpaka leo ni miaka miwili na ushei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uhakika wa taarifa zilizopo ni kwamba mfumo wenyewe wa TANePS ni shida tupu. Ukiangalia maelezo ya CAG aliyoyatoa ukurasa wa 141 akielezea umuhimu wa mfumo wa TANePS amesema kwamba kushindwa kutumia mfumo wa TANePS katika manunuzi kunakwamisha jitihada za Serikali katika kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa manunuzi na kuboresha uwazi katika manunuzi ya Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba mfumo huu bado una changamoto kubwa na kwa kiasi kikubwa hauleti uwazi uliokusudiwa, wala ufanisi uliotarajiwa. Nasema hivi kwa sababu gani? Katika mfumo huo wa TANePS kwanza mfumo wenyewe jinsi ambavyo umenunuliwa kutoka huko uliponunuliwa ni changamoto kubwa, ni aibu tupu kusema kwamba unanunua mfumo ambao haukupi full access ya kuutumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya evaluation report, nimefanya tathmini ya tender na mfumo huu lengo lake ilikuwa ni kufanya tathmini ya zabuni na kufanya usimamizi wa mradi, maana yake contract administration inafanyika ndani ya mfumo. Malipo yote unayowalipa Wazabuni uyanafanya ndani ya mfumo. Kadri unapolipa certificate namba moja, hivyo hivyo inapungua mpaka mradi wote unakamilika. Cha ajabu, mfumo huu bu hauipi PPRA wala taasisi inayofanya manunuzi ya Umma full access ya mfumo huu. Maana yake mfumo huu so far ni kimeo na kama umenunuliwa, tumenunuliwa na tumepigwa. Haiwezekani ununue mfumo ambao haukupi full access (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge kwamba mfumo huo ambao anauzungumza, TANePS ni kweli ulikuwa na changamoto lakini Serikali imeamua kujenga mfumo mpya unaoitwa NEST na upo Iringa na unajengwa na wazalendo kutokana na changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mfumo tulionao sasa utapunguza gharama na utakuwa ni wa uwazi na utakuwa unakamilisha zabuni zote kwa uhakika na kwa muda maalum.

Mheshimiwa Mwenyeki, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge, unapokea taarifa?

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa taarifa hiyo, lakini naomba kama Serikali tusirudie makosa hayo kila kukicha. Kwa nini tununue mfumo kwa fedha nyingi halafu baadaye tuje tutafute mfumo mwingine kwa ndani, zile pesa value for money yake tunaisemaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni vizuri umetoa taarifa hiyo kaka yangu Mheshimiwa Naibu Waziri Chande, nimeipokea vizuri kabisa, lakini je, tumefanya tathmini ya kina ya kuangalia ni hasara kiasi gani tumeingia? Mfumo unaokuja mtuhakikishe kwamba utakwenda kutatua changamoto zifuatazo: Mfumo huu wa TANePS kwanza kabisa ukimaliza evaluation report ulikuwa hautoi full detailed evaluation report; ulikuwa unatoa taarifa ambayo inatoka kama mtindo wa excel. Wakati tulipokuwa tukifanya manunuzi na zile zabuni, tulikuwa tunapata taarifa kamili (full detail) ya mchakato mzima wa zabuni, lakini mfumo huu wa TANePS umekuwa haufanyi hivyo. Hata baada ya hapo, unapoingia tena ukitaka kufanya mwendelezo wa mradi kwa maana ya usimamizi, haukupi access kwa maana ya mpaka ulipe tena fedha. Kwa nini tumeingia kwenye mifumo ya aina hii? Ina maana kweli hatuna weledi wa kutosha wa kujua mifumo inakuaje? Kwa nini tupewe mifumo ambayo haitupi full access? Kwa nini huwezi ku-edit report baada ya kuingiza katika TANePS? Hii siyo sawa, tunafanya makosa yanayojirudia kila siku. Ina maana ndiyo Tanzania kweli ni kichwa cha wenda wazimu? Kwa nini tuje na mifumo ya aina hii? Tumesema lengo ni kupata ufanisi na uwazi lakini TANePS hautoi ufanisi na uwazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa hatua ambazo mmezichukua. Tunawapongeza sana na hili, lakini ukweli lazima tuuseme kwamba kuna hasara tumeingia ili jambo hili tulichukulie very serious, manunuzi ya Umma ni suala kubwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nichangie sura ya tisa kwa maana ya ukurasa wa 139 unaozungumzia hasara ya Shilingi bilioni 68.73 zimepatikana kwa Serikali kulipa riba kwa wakandarasi. Naomba nisirudie sana, kaka yangu Mheshimiwa Ndulane amezungumza vizuri, amekuwa kwenye utendaji huko TANROADS, ameelezea vizuri kabisa jinsi malipo yanavyofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba CAG ameonesha kidole kwa mtu ambaye siyo stahiki. Kama kweli tunatafuta solution, kama kweli tunataka kuondoa changamoto hizi, CAG anyooshe kidole kwa mtu anayestahili. Kumtaja TANROADS kama ndiyo chanzo cha riba hizi au upotevu huu, nafikiri kuna shida, sielewi labda utendaji wa CAG ukoje? Kwa sababu namwini CAG katika uzoefu wake wa usimamiaji wa miradi, lakini anaponyoosha kidole kwa mtu asiyestahili sifikiri kama ni sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ndulane amezungumza vizuri sana, kule Wizara ya Fedha na Mipango unapeleka certificate ya malipo, watu 10 wote wale ni wa nini? Halafu hawaendi site, wanakaa nazo tu ofisini. Certificate inakutaka uende site ukafanyea measurement ya kazi iliyofanyika. Mnakaazo kule siku 10 nzima Wizara ya Fedha na Mipango, zinafanya nini? (Makofi)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa wapi? Mheshimiwa Mtemvu.

T A A R I F A

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nilitaka nimpe taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Engineer Mwanaisha ya kwamba CAG, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anachokifanya, akienda kwa implementer wa mradi anamhoji juu ya kutokamilika kwa mradi husika bila kuangalia alitakiwa kupokea hiyo hela kwa nani? Pia ana jukumu la kwenda kwenye Wizara ya Fedha chini ya fedha ambazo zinatokea kwenye GoT - Government of Tanzania; na kule pia mtoaji fedha anahojiwa vilevile, mbona wewe una jukumu la kutoa fedha kwenye taasisi kadhaa na hujazitoa kwa wakati? Kwa hiyo, nilitaka kumwambia, hiyo ndiyo kazi ya CAG, ameifanya sahihi kwa yule anaye- implement mradi na pia kwa mtoaji wa fedha. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge, unapokea taarifa?

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa elimu, lakini nimkumbushe kaka yangu Mheshimiwa Issa Mtemvu, kwamba yeye ni mhasibu kweli, lakini hapa hasimami kwa CAG. Hapa tunatafuta solution, kwa nini miradi inaleta riba nyingi? Kwa hiyo, sisi kama tunataka kutoa maazimio na kuishauri Serikali, inabidi kuangalia mambo in wide perspective, hatusimami upande wa CAG. Kama Wizara ya Fedha haijapeleka pesa kwa wakati, miradi yote ya DEVO ni kimeo nchini humu. Mkandarasi yeyote akipata mradi wa DEVO, siku zote sisi tunajua atapata shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni miradi ya mantainance pekee ambayo inatokana na fedha za fuel levy ndiyo yenye uhakika wa malipo. Miradi ya development hailipwi kwa wakati yote. Chanzo cha fedha cha miradi ya DEVO ni Serikali, fedha zinatoka Hazina.kwa hiyo, ni lazima tuyaseme haya ili tuije na mapendekezo sahihi na maelekezo sahihi kwa Serikali. Sasa hapa Mheshimiwa Mtemvu, uzoefu wako kwenye auditing na uhasibu lakini wewe sio CAG hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi Shilingi bilioni 68.73 kwa uhakika ni kwamba ni riba peke yake, lakini hasara ni kubwa zaidi ya hii. Kwa maana gani? Hapa bado hatujaingiza fedha. Kama una Mwandisi Mshauri kwa mfano, anasimamia mradi huu, unapochelewa kumlipa mkandarasi, maana yake unaongeza na muda wa usimamizi wa mradi. Kwa hiyo, na mwandishi mshauri naye anaongeza malipo yake. Kwa hiyo, cost and time over run nazo ni thamani kubwa katika mradi. Achia wafanyakazi ambao ni client ambao wana supervised miradi kila siku na kufuatilia kila siku kule site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni fedha nyingi sana kiukweli za Watanzania walalahoi zinapotea. Tangu nimekaa kwenye Serikali zaidi ya miaka kumi kabla ya kuja huku, miradi yote ya DEVO pesa haziji kwa wakati, haziji at all, shida ni nini?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)