Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi hii ya kuchangia hoja. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai wake na leo hii tunaweza kuhudhuria Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Rais wetu kipenzi, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake kubwa anayoifanya kwa awamu hii. Mama huyu ametoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali katika Halmashauri zetu. Ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya, ametoa fedha nyingi kwa ajili ya umaliziaji wa maboma mbalimbali, kwa ajili ya ujenzi wa shule, madarasa na mambo mengineyo. Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali kwa Halmashauri. Tumebaini udhaifu mwingi sana kwenye ripoti ya CAG kwenye halmashauri zetu. Kwanza kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa maeneo ya ununuzi na mikataba. Kama tunavyofahamu kwamba eneo la manunuzi linatumia fedha nyingi sana za Serikali, ni zaidi ya asilimia 70 ya pesa zote za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo basi, ndiyo maana Serikali ikaona ni vyema Bunge litunge sheria kwa ajili ya matumizi ya fedha hizi za manunuzi. Kuna Public Procurement Act ya 2011 pamoja na Regulation yake ya mwaka 2013. Lengo kubwa ilikuwa ni kudhibiti fedha hizi za Serikali ili zitumike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kitu cha kusikitisha na kushangaza sana kwenye halmashauri zetu hili eneo limekuwa ni bovu kweli kweli. Kuna fedha nyingi za Serikali zimetumika isivyo. Inaonekana kuna halmashauri 42 zilitumia fedha zenye thamani ya Shilingi bilioni 7.93 bila idhini ya Bodi ya Zabuni. Kwa kweli hapa nashindwa kuelewa. Hivi unafanyaje manunuzi bila kupitisha kwenye Bodi ya Zabuni? Hapa kuna question mark, huu unawezekana ukawa ni mpango wa makusudi wa kutaka kutumia vibaya na kutumia tofauti fedha ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna halmashauri 24 zilifanya ununuzi wa Shilingi bilioni 3.84 bila kuzingatia Mpango wa Manunuzi ya Mwaka. Kwenye Taasisi zote za Serikali ikiwemo halmashauri, huwa tunakaa, tunaandaa procurement plan ya mwaka husika. Unapoona kuna matumizi ya dharura yamekuja, labda kuna fedha zimekuja, mnatakiwa mwombe kibali maalum kwa matumizi hayo, na pia mnatakiwa muweke kwenye nyongeza ya mpango wenu wa manunuzi. Unapoona haya hayafanyiki, tunaanza pia kuwa na question mark kwamba fedha hizi hazikutumika kihalali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna Halmashauri 39 zilifanya ununuzi wenye thamani ya Shilingi bilioni 5.37 bila kuitisha nukuu za bei (competitive tendering/competitive quotation). Ni kitu cha kushangaza kama hujaitisha nukuu za bei, umempataje huyo mzabuni kwenda kuleta bidhaa katika halmashauri? Hapo panaonesha kuna upendeleo, rushwa na ubadhilifu wa fedha za Umma. Haiwezekani mimi kama procurement officer nimekaa ofisini kwangu nikaamua kampuni ‘X’ ije ifanye kazi ya Ujenzi, au Kampuni ‘Y’ ije ifanye kazi ya kuleta bidhaa fulani, hiyo siyo sahihi na haikubaliki. Moja kwa moja inaonesha kwamba kuna rushwa ndani yake, kuna upendeleo na ubadhirifu wa mali za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna baadhi ya halmashauri 21 zilinunua bidhaa ya Shilingi bilioni mbili, lakini cha ajabu ziliingizwa kwenye ledger bila Kamati ya Mapokezi kuzikagua bidhaa hizo. Pia hapa kuna ukakasi ndani yake. Sheria inatutaka tunaponunua bidhaa zozote au huduma yoyote accounting officer aunde Kamati Maalum kwa ajili ya Ukaguzi na mapokezi ya bidhaa hizo. Ni ajabu, inaonekana baadhi ya halmashauri wanapokea kinyemela hivyo vitu, mtu wa procurement ameagiza yeye na anapokea yeye na anaingiza kwenye ledger yeye na ana-issue yeye. Hii haikubaliki. kwanza tuna wasiwasi, inawezekana hizo bidhaa hazikufika ipasavyo au hazikufika kabisa au hizo huduma hazikufanyika na ndiyo maana Kamati ya Mapokezi na Ukaguzi haikufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna halmashauri wanafanya ununzi wa bidhaa mbalimbali au huduma mbalimbali kwa kuwatumiua wazabuni ambao hawajasajiliwa GPSA. Hili ni kosa kubwa kwa Sheria za Manunuzi. Ina maana mtu anaamka tu nyumbani kwake asubuhi anaenda kupanga, leo nitachukua Kampuni ‘Z’ ilete bidhaa fulani. Hiyo siyo sahihi, kwa sababu manunuzi haya ni ya Serikali, yana sheria na taratibu zake, siyo kama manunuzi ambayo tunayafanya majumbani kwetu.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache tu kwanza Kamati ilibaini kwamba kuna upendeleo, udanganyifu na ubadhirifu wa mali za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inashangaza pia kuna halmashauri nyingine ilionekana imenunua vitu lakini haijaingiza kwenye ledger na wala hawaja mu-issue local fundi. Kuna mizania ambayo iko tofauti kwenye hizi force account, watu wanataka kuzitumia vibaya hizi force account. Haiwezekani mimi nimenunua labda mchanga au nimenunua matofali halafu fundi anayajengea bila mimi kumkabidhi. Sidhani kama hiyo ni sahihi. Hapa pia kuna ukakasi, inaonekana kuna mambo yanaenda ndivyo sivyo kwa dhamira ya makusudi, kwa nia potofu na nia ovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachoomba Wabunge, ushauri wetu, watu wanaofanya haya mambo, wachukuliwe hatua kali kwa haraka. Tatizo linaonekana kwamba, kama mtu amefanya kosa mwaka 2022, inafika mwaka 2023, 2024, 2025 issue ni ile ile moja haijachukuliwa hatua, kwa kweli hii haikubaliki na ndiyo maana watu wengi wanaendelea kufanya mambo haya wanaona kwamba zile sheria za kinidhamu hazichukuliwi kwa haraka. Vilevile tunapendekeza kwamba ifanyike hivyo, haya mambo yatapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna uteketezaji wa dawa za binadamu katika vituo vinavyotoa huduma ya afya. Hii inasikitisha sana. Kuna vituo vya afya, zahanati na hospitali hazina dawa. Hivi inakuwaje mpaka dawa zinafikia wakati wa kuteketezwa? Kuna sheria inaruhusu, kama mimi kituo ‘X’ nina dawa za ziada/za nyongeza, nimeona labda baada ya miezi mitatu zinaweza ku- expire au miezi minne, ninaruhusiwa kuwapa zahanati ‘Y’ hizo dawa. Kwa nini wasipeane hivyo? Kwa nini kama unajua kwenye eneo fulani hayo magonjwa siyo mengi, upeleke dawa ziwe nyingi?

Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kwa sababu inaonekana kuna fedha nyingi zimetumika kununulia dawa hizo ambazo wananchi wetu wanazihitaji, lakini baadaye zinakwenda kuteketeza. Hiki nacho ni kichaka kingine, tunatakiwa tukiangalie sana, haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna maeneo manne ambayo Kamati imeyabaini ambayo ni mianya ya upotevu wa mapato ya halmashauri. Vilevile kuna ushuru wa huduma (service levy), inakusanywa bila uthibitisho wa mapato halisi ya kampuni ya mwaka (turnover). Hiki kitu siyo halali, inabidi kifuatiliwe. Kuna halmashauri nyingine zinafanya malipo bila kukata kodi la zuio (withholding tax five percent).

Mheshimiwa Spika, hii ni fedha ya Serikali ambayo inatakiwa itumike kwa ajili ya Serikali, lakini cha kushangaza, mzabuni analipwa fedha yake kama kawaida, inakuwaje halmashauri usikate hii kodi ya zuio ukairudisha TRA ili iweze kutumika na Taifa letu? Huu ni mwanya mwingine wa matumizi mabaya ya fedha ya Serikali. Pia tumebaini kuwa kuna halmashauri nyingine zinafanya malipo bila kutumia risiti ya electronic. Hiyo ni kosa kisheria.

Mheshimiwa Spika, pia inaonekana kuna halmashauri nyingine zinaendelea kutoa leseni mbalimbali za biashara nje ya mfumo. Pia hicho ni kichaka kingine. Vile vile kuna baadhi ya stahiki za watumishi kutolipwa ipasavyo. Rasilimali watu ndiyo msingi wa utendaji wa mafanikio ya taasisi yoyote, lakini rasilimali watu usipoitendea haki kuna matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inaonekana kuna watumishi wengi wa halmashauri wanadai stahiki zao; wengine wanadai malimbikizo ya mshahara baada ya kupanda cheo, lakini hawapati kwa muda mrefu. Hiyo ipo sana, na mimi mwenyewe ni mfano halisi nikiwa mtumishi wa Serikali, nilipokuwa Serikalini, nilifanya kazi, nikapanda cheo, lakini nilikaa zaidi ya miaka sita bila kulipwa arrears. Hiyo inashusha morali na ari ya kufanya kazi. Kwa sababu hiyo ni haki yao, tunaomba TAMISEMI na Serikaki kiujumla iangalie eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kuna wafanyakazi wengine wanahamishwa; kwa mfano, anahamishwa kutoka Wilaya ya Buchosha unampelewa Wilaya nyingine. Mtumishi huyu ana familia na mizigo yake, anatakiwa alipwe stahiki yake, lakini unamwambia aripoti ndani ya siku saba au siku 14 aende pale lakini fedha yake haumlipi, anaendaje kule? Hii nayo inashusha morali ya kufanya kazi vizuri. Tunaomba wafanyakazi hawa walipwe stahiki zao vizuri ili waweze kufanya kazi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)