Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema; lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Taarifa ya Kamati ya LAAC na taarifa zingine.

Mheshimiwa Spika, sitakuwa na shukrani kama sitaanza kwa kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu shupavu jemedari Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kipekee nimpongeze yeye mwenyewe binafsi. Hii ni kwa sababu ya utashi wake na dhamira yake aliyokuwa nayo katika kutekeleza au kutatua changamoto za wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Samia Hassan anafanya kazi kubwa sana, kazi ambayo hakuna mwananchi wa nchi hii hazioni. Amekuwa na dhamira njema kabisa ya kuhakikisha kwamba kila palipokuwa na changamoto, changamoto hiyo inatatuliwa. Pamoja na dhamira hii njema kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo zinazoweza kupelekea matarajio haya ya Mheshimiwa Spika yasifikiwe.

Mheshimiwa Spika, kumeripotiwa makosa, changamoto mbalimbali au dosari mbalimbali na Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika ripoti zake. Dosari hizi zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara, mwaka hadi mwaka hali ambayo imesababisha baadhi yetu kufikiri kwamba ripoti hizi hazina majibu au hazina suluhisho, jambo ambalo sio kweli.

Mheshimiwa Spika, changamoto hizi ukiziangalia kwa umakini kabisa unaweza ukakuta kwamba zinatatulika. Nataka niziangalie changamoto chache tu kama mfano.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto zilizokuwa zikiripotiwa mara kwa mara na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni kama ifuatavyo: -

Kumekuwa na matumizi mabaya kwenye akaunti ya amana. Hapa pamekuwa na kizungumkuti kwa sababu akaunti ya amana si akaunti ya halmashauri. Akaunti hii ni imewekwa kwa ajili ya kutatua migogoro ya kimkataba wakati panapotokea changamoto; kwa hiyo pesa zinazowekwa kwenye akaunti hii zinaweza kutumika kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na manunuzi yasiyozingatia taratibu. Hiki ni kichaka kikubwa sana kinachotumika kupoteza fedha za wananchi kwa makusudi kabisa. Hapa kuna mambo mengi sana. Kunakuwa na kutokushindanisha kandarasi, hali kadhalika kunaweza kukawa na mtu mmoja amekusanya document zote, akitaka kutengeneza kandarasi anajitengenezea mwenyewe lakini mtu huyu akapewa tender. Kwa maana hiyo mara zote yeye atakuwa ndio mpataji wa tender hizo. jambo hili limekuwa ni gumu sana hususan kwa watu ambao wako makini katika suala zima la manunuzi.

Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na changamoto katika uwekezaji wa mitaji ya umma. Fedha nyingi zimewekwa katika maeneo ambayo hayana tija. Mara nyingi watu wamekuwa wakijiamulia kutengeneza mradi pasipokufata taratibu kama vile kufanya visibility study; pia bila kujua hata breakeven point itafanyika kwa wakati gani au itatokea lini. Mambo mengine ni kama vile halmashauri kushindwa kukusanya madeni ya mikopo ya vikundi ambavyo imevikopesha. Kuna pesa nyingi sana zimekopeshwa na halmashauri kwenye vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu lakini imekuwa ni shida sana urejeshaji wake.

Mheshimiwa Spika, kuna vitu vingine ambavyo vinaweza vikakushangaza zaidi, kama vile ujazaji wa fomu. Kama suala la kujaza fomu tu limekuwa ni changamoto ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa sana upotevu wa fedha katika halmashauri. Fedha nyingi sana zimekuwa hazipewi halmashauri kwa kisingizio hiki. Pia kuna tatizo hili la uteketezaji wa dawa. Nchi kama Tanzania yenye mahitaji makubwa sana ya dawa inashangaza sana inapofika wakati kwamba dawa zinateketezwa eti kwamba zime-expire.

Mheshimiwa Spika, sasa, haya yote ni matatizo ambayo kama tusipokuwa makini yataendelea kujitokeza na kuendelea kupoteza fedha za wananchi walipa kodi, wavuja jasho pasipokuwa na mafanikio yoyote wala kuwa na matumaini kwamba mambo haya yatarekebishwa.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema mwanzo, kwamba mambo haya yanaweza yakatekelezeka. Kutokana na taarifa za ripoti ya CAG kumekuwa na ushauri mara nyingi jinsi gani ya kuenenda kutatua changamoto mbalimbali nilizojaribu kuziorodhesha hapa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kama halmashauri ikijielekeza katika kujengea uwezo kamati zake zile za halmashauri hapa patakuwa na tija. Shida iliyopo kamati hizi zimekuwa dhaifu kiasi kwamba panapohitajika kwenda kukagua miradi mbalimbali haziwezi kukagua miradi hiyo. Aidha ni kutokana na uelewa wa wanakamati au wakati mwingine vitendea kazi vya Kwenda kukaguliwa miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Ikage alipendekeza na mimi naendelea kusisitiza na kukumbusha kwamba kamati za halmashauri zitumike kikamilifu. Kwanza zijengewe uwezo wa kutosha kusudi waweze kuwa na uwezo wa Kwenda kukagua vizuri. Lakini kwa sababu Kamati ya Fedha na Kamati ya Ujenzi ni kamati ambazo zinahusika au zina mahusiano ya moja kwa moja na masuala ya pesa basi kamati hizi zitambuliwe kuwa ni kamati maalum za ukaguzi wa miradi na pesa za maendeleo katika halmashauri. Halmashauri iwajibike kwa namna yoyote kutenga pesa ambayo itaiwezesha kamati hizi kufanya kazi kikamilifu. Ikitokea kamati zimeshindwa kufanya kazi kutokana na upungufu au kutokana na uzembe wa halmashauri kuitengea fedha basi halmashauri inatakiwa iwajibike.

Mheshimiwa Spika, kamati hii ipewe jukumu la kutengeneza ripoti ya miradi ya maendeleo na pesa za maendeleo. Ripoti ieleze waziwazi kiasi gani cha pesa zimepokelewa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. Kwa mfano vyanzo vya maendeleo kutoka Serikali Kuu, kutoka kwa wafadhili; lakini pia ieleze chanzo cha maendeleo kinachotokana na mapato yake yenyewe.

Mheshimiwa Spika, vilevile kamati hii katika ripoti hii iielezee waziwazi kila akaunti; kwamba akaunti hizi zilizopo zina bakaa ya kiasi gani. Hali kadhalika kamati hii ni lazima iweze kujadiliwa na Baraza la Halmashauri. Baada ya ripoti hii kujadiliwa iunganishwe pamoja na ripoti ya ukaguzi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupelekwa kwenye vikao vya LAAC kwa ajili ya kuendelea kutumika katika matumizi ya vikao hivyo. Jambo hili litakuwa limetengeneza check and balance katika maeneo yote ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linaweza likainusuru halmashauri ni suala la ajira. Mapendekezo mengi sana yametolewa mara kwa mara pamoja na Khaji akipendekeza kwamba ajira katika halmashauri husika lazima zizingatie weledi. Watendaji katika idara mbalimbali, hali kadhalika katika vitengo na Mtendaji Mkuu lazima wawe na ueledi, kwamba lazima wawe na ujuzi wa vitengo ambavyo wanavyovisimamia, pia wawe na ujuzi husika wa idara wanazozisimamia.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mtendaji Mkuu lazima apimwe kutokana na performance kwa maana ya uwezo au kwa kile alichokitimiza katika eneo lake la kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo hili litafanya kila mtu awajibike na pia awe na ajira ya mkataba pamoja na wale viongozi wa vitengo wawe na ajira za mikataba. Hii itasaidia sana kuwafanya wawajibike wakihofia kwamba kama hawatafanya vizuri watakatishiwa mkataba wao au hawatapewa mkataba mwingine.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine limejitokeza ambalo linahusiana moja kwa moja na Wizara ya TAMISEMI, halikadhalika Wizara inayoshughulika na masuala ya utoaji wa fedha. Kumekuwa na malalamiko mengi sana kwamba fedha zile za maendeleo haziendi kwa wakati. Jambo hili limeleta changamoto nyingi sana kwa sababu unakuta fedha zinaenda zikichelewa na wakati mwingine zinakuwa hazitoshi hali ambayo mipango iliyotarajiwa katika miradi ya maendeleo haifanikiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kumekuwa na changamoto kwamba pesa ile ikienda imechelewa miradi haifanikiwi. Mfano mkubwa unaonekana hata sasa hivi, fedha yetu ya Majimbo haijaenda. Kwa hali ilivyo, kama itakwenda kwa kipindi hicho cha baadaye, maana yake, kwa vyovyote vile fedha hii itakuwa imechelewa na kushindwa kutekeleza mambo yaliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoanza kuzungumza kule mbele kwamba changamoto nyingi sana zinazoonekana katika level ya Halmashauri ni zile ambazo zinaweza zikatekelezeka lakini zikatibika pia. Hivyo tunayo kila sababu ya kumsaidia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza yale anayodhamiria yatokee.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)