Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye taarifa hizi za Kamati ambazo zimewasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu. Kabla sijachangia, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu. Sisi wananchi wa Jimbo la Hai kwa kweli tuna msemo wetu, ‘Mama ametuletea miradi kedekede na tunamshukuru sana’. Kila eneo limeguswa na tuna miradi mingi inatekelezwa ndani ya Jimbo la Hai, jambo ambao halijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze wasaidizi wake wote, nikianza na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote na Wakuu wa Mikoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakuu wa Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Wakurugezi na Watendaji wote, Wenyeviti wa Halmsahauri na Madiwani mpaka Mwenyekiti wa Kitongoji, kwa kweli wote tunashirikiana kuijenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo makubwa anayoyafanya Mheshimiwa Rais, nimesoma taarifa hizi, lakini natokea Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, hiki kinachoendelea kuhusu Matumizi ya Fedha za Serikali, kimenistua, na kikanifanya nijiulize sana. Dhamira ya hawa wasaidizi wa Mheshimiwa Rais ni ipi, ikiwa Mheshimiwa Rais anahangaika huko kutafuta fedha, anazileta hapa hiki kinachoendelea huku ni kitu gani, leo tumeona namna amehangaika ameleta hela za UVIKO. Watu wameenda kujificha, yale mapato ya ndani ambayo yalipaswa kutekeleza miradi hayafanyi kazi iliyokusudiwa, maana yake wanajifika kwenye UVIKO na vitu vinavyofanana na hivyo.

Mheshimiwa Spika, ukisoma taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, ukurasa wa sita, utaona mambo yalivyo magumu sasa hivi. Kwanza wamesema ununuzi wa bidhaa za thamani ya shilingi bilioni 7.9 ulifanyika bila idhini ya Bodi, kwamba taasisi zinajiendesha zinavyotaka, mamlaka imeteua Mwenyekiti wa Bodi pale ambaye ni Mteule wa Rais, lakini wao wanaenda kufanya matumizi bila kushirikisha bodi. Hii ni hatari kama tutaiacha.

Mheshimwa Spika, wameenda mbali zaidi, hapa kuna bilioni 3.84, hizi ni ununuzi wa bidhaa ambazo zimenunuliwa bila kuwa kwenye mpango. Hapa halmashauri 24 zimehusika. Ukisogea tena kuna bilioni 5.34 katika halmashauri 39, wamefanya manunuzi bila ushindanishi wa bei. Hizi zote ninazotaja ni fedha, lakini ukienda kuna bilioni 1.2 zimetumika bila kuwa na hati ya kuagiza vifaa (LPO) kwenye halmashauri 14. Wamesogea mbali, ununuzi wa thamani ya bilioni mbili bila kushindanisha wazabuni.

Mheshimiwa Spika, hii ni hatari kama tutaacha jambo hili. Niliombe sasa Bunge lako Tukufu, kwa kweli tuone namna ya kuchukua hatua, kama hatutachukua hatua hii ni hatari, tutakuwa hatumsaidii Mheshimiwa Rais. Hawa wote ambao wamehusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria, ili iwe fundisho. Naomba kabisa Bunge lako hili Tukufu, safari hii tusiache kuchukua hatua kwa hawa watu. Tutoe maelekezo thabiti ya kuhakikisha Serikali inafanya kazi yake ya kuwawajibisha hawa ambao wamehusika na vitu hivyo.

Mheshimiwa Spika, pia, mambo yanayofanana na hayo hayo yapo ukurasa wa 11 kuhusu asilimia 10 ambayo inatengwa kutokana na mapato ya halmashauri. Kimsingi fedha hizi kanuni zinaeleza wazi, sheria inatamka wazi kwamba ukishakusanya mapato yasiyolindwa, asilimia kumi nenda kakopeshe kwa akina mama, vijana na watu wenye ulemavu. Kanuni inasema kakopeshe 4:4:2 ambaye hatumii formular hii, huyu ana jambo baya na sisi, hamtakii Mheshimiwa Rais mema. Sisi kwenye Kamati yetu ya USEMI, tumesema sana na hizi halmashauri, lakini hawatekelezi kwa sababu wana jambo lao na jambo lao ni hili, halmashauri 154 zimeshindwa kukusanya bilioni 47.01 ambazo zilipaswa kurejeshwa kwenye vikundi.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni nyingi, sisi tumepiga hesabu kwenye Kamati yetu tumebaini karibu bilioni 65 kila mwaka zinatengwa kwenda kukopeshwa. Hizi fedha ni mtaji wa kuanzisha benki kabisa, lakini fedha hizi haziendi kama ambavyo kanuni inataka na hazikopeshwi kwa kuzingatia utaratibu. Sasa naomba, kwa sababu Kamati yako ya USEMI tumekuwa wabobezi sana kwenye eneo hili. Tupe fursa twende ndani tupate muda wa kutosha, tukuletee taarifa sahihi kwenye asilimia hii 10 tu; kwa sababu hizi ni fedha nyingi ambazo kusudio la Serikali ni fedha hizi zikasaidie kule chini: pamoja na kwamba tumeshashauri hapa, sheria hiyo iletwe, ifanyiwe marekebisho ili kundi la wanaume nao wanufaike. Sasa kama kundi hili linapokwenda kunufaika kama hatuna mechanism ya kusimamia na tunaletewa na CAG taarifa hii, hii sio sawa, hatumsaidii Mheshimiwa Rais kwa namna hii.

Mheshimiwa Spika, wameenda mbali, wamesema bilioni 1.2 zimetolewa kwenye akaunti ya Amana bila kuzingatia utaratibu. Wamesogea mbele zaidi wamesema, halmashauri 17 zimetoa mikopo, bilioni 3.26 bila uwiano unaotakiwa kwa maana ya 4:4:2. Wanafanya hivi sio kwa bahati mbaya, siyo kweli. Kuna taarifa tulikuwa tunaletewa unaambiwa halmashauri nzima hakuna walemavu, siyo kweli, halmashauri nzima hakuna watu wenye sifa, siyo kweli. Nia ikiwa njema kukiwa na utayari wa kumsaidia Mheshimiwa Rais, hivi vitu vipo na wenye mahitaji ni wengi mno, hatuwezi kusema kwamba kuna fedha zinaweza kurudi kwamba hazikutumika.

Mheshimiwa Spika, sasa nishauri kwenye eneo hili, nafahamu Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMi amekuja vizuri na ameanza vizuri na wamezindua mfumo ambao utatusaidia kwenda ku-control, wameshauzindua mfumo wa kieletroniki ambao utajumuisha Tanzania nzima. Wale waombaji wataingia kwa NIDA zao, maombi yao na vikundi, kwa kweli umeonyesha vizuri. Hata hivyo, bado nasema kwa kuwa fedha hizi ni nyingi na hao wanaoandaa mfumo huu tuliwashauri kwenye Kamati washirikiane na e-government, ili ku-control, namna ya kudhibiti. Bado tunahitaji kutafuta proper mechanism, bilioni 65 sio ndogo, lakini lazima tutafute mechanism ya hizi fedha ambazo zimeachwa hazijakusanywa ziweze kurejea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nirejee kukuomba tena Kamati ya USEMI na LAAC ziungane pamoja ziende kwenye mambo haya ya msingi, zikatazame hizi asilimia kumi, zikatazame kuna kitu kinaitwa bakaa kwenye taarifa za halmashauri. Wanafanya mambo yao, mwishoni unakuta bakaa milioni 35, halmashauri ndogo kabisa, halafu hizi zinaenda kutumika, wakati mwingine hata Waheshimiwa Madiwani hawashiriki. Ndio maana Bunge lililopitwa Madiwani hawa tuwatazame, tuwape nguvu, tuwawezeshe ili waweze kuzisimamia vizuri halmashauri zetu. Bila kufanya hivyo hivi vitu vinapita, unakuta bakaa milioni 60, hii inaitwa bakaa, Madiwani walishamaliza kazi yao, hao wanaenda kupanga mapato na matumizi kadiri wanavyotaka.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli naomba nihamie kwenye eneo lingine ambalo lilizungumza hapo jana kuhusiana na eneo la uwekezaji, tumepitisha mabadiliko ya sheria, lakini bado kuna changamoto. Kwa halmashauri zenye mapato machache ambayo ni wanufaika na mpango wa uwekezaji. Wale wawekezaji kupitia mfumo wa EPZ, wanakuja kwenye halmashauri zetu, wanalipa centrally kwa Serikali Kuu, zile halmashauri kule chini hazinufaiki. Kwa mfano, Jimbo la Hai, asilimia 78 sisi tunategemea kilimo na ufugaji, anakuja mwekezaji kupitia mashamba ya ushirika, anachukua anaweka mashamba ya kupanda maua kama mwekezaji kupita mfumo wa EPZ, pale Halmashauri ya Hai hachangii chochote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unakuta maeneo yetu, ukienda kule kuna wawekezaji wengi wana mashamba huku na huku, lakini halmashauri haipati kitu. Naomba turejee, watakapoenda kuandika kanuni, waseme kwamba na sisi halmashauri zilIzopo kule, hawa watu wawajibike kwetu. Hata zile bodi zilizoundwa pale zimeweka level ya Kitaifa kwenye level ya ngazi ya halmashauri hakuna kitu. Hakuna mwakilishi wetu, sasa sisi ambao tunapokea ile miradi mtu anaweka shamba la maua pale, sisi ndiyo tunampa maji, sisi ndiyo tunamsaidia kila kitu lakini halipi kodi. Niombe sana hili litazamwe kwa jicho la huruma, kwa sababu halmashauri nyingi ambazo zinahusika na maeneo ya uwekezaji zinaenda kuwa maskini.

Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja nizungumze jambo ambalo lilizungumzwa jana hapa kuhusiana na KADCO. Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro ni mali ya Serikali, mwanzoni kulikuwa na wabia mbalimbali pamoja na KADCO, lakini Serikali ilinunua hisa zile na kwa mkopo wa CRDB na ikalipa. Kwa hiyo, picha iliyopo ili tusichanganye wananchi wa Jimbo la Hai ambao kule kuna suala linaendelea chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakadhani uwanja wa ndege sio mali ya Serikali, naomba tuweke sawa hapa. Ule uwanja ni mali ya Serikali, eneo lile ni mali ya Serikali, mradi unaoendelea pale ni mali ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna changamoto ya yule anayeendesha pale kwa maana ya msimamizi na anaye-run ile activity, KADCO, tuone namna ya kuutunza vizuri ili tusiwachanganye wananchi wakaona kwamba ule uwanja sio mali ya Serikali. Ni vizuri hilo likawekwa sawa, uwanja ule ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kama nakosea utanielekeza namna gani ya kufanya, lakini taarifa sahihi ni hizo ili tusiwachanganye wananchi kwa sababu kuna suala la fidia linaendela.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nisisitize tu, hiki kitu kinachoitwa bakaa, Waziri atakapokuja kusimama hapa, atutolee mwongozo kwamba, huu utaratibu wa kubakisha hela kwa makusudi fulani, maana yake ni nini na atoe maagizo sahihi kwenye jamobo hili.

Mheshimiwa Spika, lingine, kumekuwa na ubadilishwaji wa matumizi wa fedha za Serikali kwenye hizi halmashauri zetu, wanakuja hapa, wanaleta bajeti, tunaipitisha hapa, nendeni mkajenge madarasa kadhaa. Tunawapitishia kwa asilimia 100, wanaenda wanakusanya. Hili tena niseme hapa, upo ujanja sasa hivi, kila halmashauri utaambiwa imekusanya zaidi ya asilimia 100. Ukija kwenye utekelezaji wa miradi hawatekelezi, hawapeleki fedha na hizi asilimia 100 zinawekwa kimkakati, halmashauri ina uwezo wa kukusanya bilioni tatu, watakuambia tunakusanya bilioni mbili ili wafikie malengo haraka na wasifiwe, lakini hata wale walioshindwa hawapeleki fedha.

Mheshimiwa Spika, TAMISEMI iende ku-review mifumo ya kupeleka makadirio ya makusanyo kwenye halmashauri zetu. Kuwe na vipimo ambavyo ni bayana vya kupeleka haya, vinginevyo tutaumiza halmashauri nyingine ambazo zinafanya kazi na hili la bakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kubadilisha miradi pasipo kufuata utaratibu, wanafanya reallocations ya funds. Kwa mfano, sasa hivi tulikuwa tunaangalia fedha zilizokuwa zimepelekwa za UVIKO na fedha nyingine ambazo zimepelekwa kwa ajili ya kujenga zile shule za kidato cha tano na sita. TAMISEMI imepeleka fedha, kila halmashauri inasema hazitoshi, kwanza kabla hawajenga na ukiwauliza hebu tuambieni, ukiwauliza TAMISEMI hii BOQ mliopeleleka huku ndugu zetu mlikuwa mnakadiria ifanye kitu gani na sasa mnasema fedha hazitoshi, tuleteeni basi BOQ ya kusema hapa sisi tunaongeza bilioni mbili au milioni 200. Kwa mfano, Halmashauri ya Bahi, wao wamesema milioni 58, wengine 150, wengine 200, fact za ki-engineer zipo wapi na ukienda kuangalia hizo unakuta ramani inasema jambo lingine, yaani ramani inasema ina milango nane, ukienda kwenye BOQ kumi na mbili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nasema, pamoja na kwamba tulishauri kwenye Kamati nasema hapa ili Mheshimiwa Waziri akaweke mikasi mikubwa ya kuwabana hawa watu, wafanye kazi kwenye uhalisia, warudi kwenye neno lao, wanasema ni wataalam wafanye kazi kitaalam ili tuweze kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha, niombe, sote tunaijenga nchi yetu, kila mmoja aliyepo hapa, tusiposhirikiana na kupenda nchi hii na kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa dhati, hakuna mtu mwingine atatoka nje ya Tanzania kuja kufanya kazi hii, huu wajibu ni wakwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuunga hoja zote mkono na mchango wangu ndiyo huu. (Makofi)