Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia. Kabla ya yote nipongeze taarifa zote za Kamati Tatu na niwapongeze Wajumbe kwa namna ambavyo walijitoa kuchakaka na kujadili kwa kina taarifa hizi.

Mheshimiwa Spika, kulingana na umuhimu wetu kama Muhimili wa Bunge, kuna sehemu pekee ambayo sisi tumepewa hiyo neema ya kuisimamia Serikali. Kama kuna eneo Taifa letu linapata hasara na kupoteza fedha ni eneo la mikataba, nami nitajikita eneo hilo la mikataba.

Mheshimiwa Spika, wakati tunajadili hapa taarifa iliyopita ya Kamati yetu ya PAC, ilijadili kuhusu mkataba ambao ulikuwa unahusiana na NFRA wa ujenzi wa vihenge, mpaka leo nazungumza hakuna kitu kimefanyika, kwa namna nyingine alizungumza Mheshimiwa Getere hapa kwamba tunamwambia nani? Unaweza usimuelewe, lakini kama tunazungumza tunaleta taarifa kama Kamati ya Bunge ili Bunge lipitishe na Bunge likapitisha tunakuja kutoa taarifa kwa mara nyingine jambo lile halijatekelezwa, inatia uchungu wakati mwingine.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, yule Mkandarasi hatujui anafikiri nini mpaka leo, lakini wakati Wabunge wanajadili yale matrekta mabovu, ndiyo huyo huyo msumbufu Mkandarasi ambae hakuna maamuzi yoyote yamefanyika mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nazungumzia suala la mikataba nilikuwa najiuliza machache sana, kwa nini tunaingia mikataba mibovu? Je, nchi yetu inashida ya Wanasheria? Je, ni kweli nchi yetu imeshindwa kuwashirikisha kikamilifu wanasheria wetu washauri vizuri tunapoingia mikataba? Ni kweli Wanasheria wanapitia hiyo mikataba kabla hatujaingia kwenye hiyo mikataba? Na ni kweli wanatoa usahuri wa kina? Je, huo ushauri ni kweli Wizara inazingatia?

Mheshimiwa Spika, ukianza kutazama hasara hizo ambazo tunazipata kama Taifa kupita mikataba, utapata maswali mengi ambayo hayana majibu. Aidha, Wanasheria wetu wanatumika kuhujumu nchi yetu, kwamba wanajua kwamba mkataba huu tumwambia yule mtu apite uchochoro ambao anaweza kutokea. Ninatoa mfano tu wa vitu vichache kwa sababu ni vitu vingi ambavyo tunapata hasara kama Taifa. Ukitazama Shirika letu la Umeme TANESCO, Symbion namna walivyoingia huo mkataba na hasara ambayo tumeipata kama Taifa ya malipo ya Dola za Kimarekani Milioni 153.43.

Mheshimiwa Spika, ni huzuni na inaumiza sana, yaani wameshaingia mkataba, umeanza kutekelezeka, wanafika katikati wanagundua kuna makosa, wanaamua sasa ngoja tujiondoe kwenye huo mkataba. Hawajui madhara yanayoweza kutokea baada ya wao kujiondoa, ndiyo hapo ninaposema, Je, ni kweli Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inashirikishwa kwenye mikataba hii? Hasara hii ya Dola za Kimarekani, Milioni 153 ingesaidia Watanzania wangapi huku kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri watu wawe wanaangalia ikitokea mkataba kama huu umeingiza hasara kwenye Serikali yetu, ni watu gani wameshiriki, wakiwa wanachukuliwa maamuzi mapema inawezekana tukaokoa fedha zingine kwenye mikataba mingine inayokuja na wengine wakajifunza, kwamba kwa kupelekea hasara kwenye Taifa, yeye mwenyewe anaweza akatolewa pale kama mfano, lakini unaona mambo yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya tumewahi kushauri Bunge lililopita, kwamba ni vizuri Bunge lishirikishwe kwenye mikataba hii, kwa sababu hasara inayotokea kwenye Taifa ni wananchi wetu wanaoenda kuumia. Ni vizuri kama Bunge litashiriki yawezekana tukashauri mambo kadhaa kabla ya kupata hasara kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano wa pili ambazo zinaingiza hasara pia kupitia mikataba ni TANROADS. Kwa hali ya kawaida, siamini kwamba TANROADS wanaweza kukosa Wanasheria makini wa kushauri kuingia kwenye mikataba. Mara nyingi tunapata hasara kwenye TANROADS sehemu gani? Ni pale ambapo, TANROADS inashindwa kuwalipa Wakandarasi kwa wakati. Wanasheria kama wameshirikishwa ni lazima washauri. Ukitazama kila Bunge hili jambo litazungumzwa. Sasa kama linazungumzwa kila Bunge halafu tunakuja tena tunazungumza, ndiyo maana tunarudi kulekule kwa Mheshimiwa Getere, tunasema nini na tunamshauri nani? Lakini kwa sababu ni wajibu wetu tutaendelea kushauri.

Mheshimiwa Spika, TANROADS pekee yake, wameingiza hasara ya Bilioni 68.73 kwa kuchelewa kuwalipa Wakandarasi. Hizi fedha ambazo Mheshimiwa Rais anazunguka kutafuta, kwamba watoto wasihangaike kwa ajili ya madarasa, lakini kuna nyingine hasara za ajabu na za kizembe tu zinafanyika kwenye Taifa letu. Kuna haja ya kuangalia vizuri mikataba yote kuna shida gani, nani anakubaliana na hili jambo, nani yuko nyuma ya haya mambo yanayofanyika. Mimi siamini kama Wanasheria wanashirikishwa kikamilimu na kama wanashirikishwa wao wenyewe wanahusika kutuhujumu kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la vihenge nimkwishalizungumzia. Yule mkanadarasi hatujui mpaka leo anawaza nini na fedha alishalipwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 33, yuko huko na hatujui nini kitaendelea mpaka leo; kwa sababu yeye alikuwa ametishia kupeleka mahakamani lakini sisi kama taifa tupo tu na kuna vihenge havijamalizika mpaka leo. Kwa hiyo kuna haja sasa ya kufanya maamuzi kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Spika, nataka nishauri kwenye jambo hili. Ninashauri Serikali ichukue hatua za makusudi kwa watendaji wote waliosababisha hasara hizo kwa makosa ya uzembe au kwa makosa ya kuruhusu kuingia mikataba kama hiyo ambayo inaleta hasara kwa taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanapokuwa wanasikia kuna mkataba umesainiwa, wanaambiwa tu hivyo; lakini baadaye ukija kukuta mambo yaliyopo; lile kundi ambalo linakuwepo pale wakati mkataba unasainiwa; sisi tunaamini kabla ya kusaini kuna watu wameshakaa, jopo la wataalamu mbalimbali likapitia ule mkataba, unamaslahi kwa taifa? Je, ni hasara gani ambayo tunaenda kuipata kama taifa? Je, hakuna eneo lingine ambalo tunaweza tukapata fedha mpaka kuingia kwenye mkataba mbovu?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba hatua zichukuliwe, pia zichukuliwe kwa wakandarasi wote ambao wanafanya makusudi na uzembe wakiamini kuna uchochoro wa kutokea; kwamba kuna sehemu watatokea tu. Ndiyo maana nasema na wanasheria wanakuwa wanahusika kwa wakati mwingine. Kwa sababu kama mkataba wameupitia na wanajua lazima washauri vizuri, wakiwashauri vizuri tutajua kwamba shida ipo kwa wataalamu wetu na hatua zichukuliwe kwa watumishi hao.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimezungumzia kwenye suala la mikataba, narudia tena kusema. Kuna haja ya uchunguzi wa kina tunapokuwa tunaingia kwenye hii mikataba kama wanasheria wetu au Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashirikishwa kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, naomba nihame hapo kidogo, niende kwenye kamati ya LAAC. Katika miradi ambayo inaendelea hivi sasa kwenye halmashauri zetu, ikiwemo ujenzi wa madarasa; ni jambo jema sana ambalo analifanya Mheshimiwa Rais. Ukitazama jambo hilo jema, tuna ma-engineer wachache sana; wamezungumzia changamoto ya watumishi.

Mheshimiwa Spika, leo walimu wameingizwa kusimamia ujenzi wa hiyo miradi kwenye halmashauri zetu. Mwalimu anajua taaluma yake ni kufundisha, unampeleka akasimamie jengo ambalo, tena ni la pressure. Ukitazama zile fefdha za COVID, wote mnajua presha iliyiokuwepo kwenye ujenzi wa yale madarasa. Umemuweka mwalimu, tena kwa bahati mbaya zile kamati zote nne walimu wapo. Kwa hiyo walimu zile siku 90 zote badala ya kufikiri kuwafundisha wanafunzi wetu wanafikiri kuhusu miradi ya ujenzi. Kwa bahati mbaya zaidi, yeye kwa sababu si taaluma yake, ukitazama yale madarasa ya COVID, nafikiri Waheshimiwa Wabunge wote wameshapita kwenye maeneo yao wameona. Mimi sijajua kama ni lile jina, au ni nini.

Mheshimiwa Spika, kabla hayajakamilika, yana ufa. Unaanza kuwaza ni jina hili lenyewe COVID ndilo limeendana na hii kasi inayokwenda ya madarasa kuharibika au kuna nini?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kunakuwa na masharti mengi, ni vizuri tujue, tuko hapa leo kuna madarasa ambayo yalijengwa na wazazi wetu yapo imara; lakini madarasa ya sasahivi yanajengwa, yaani ni kama watu hawawi na mtazamo kwamba hivi tunajenga hili darasa tukitazamia miaka mingapi mbele? Wanatazama kumaliza, ukifika pale utaona rangi inapendeza, ndani ya miezi mitatu ufa umetokea pale, yaani mambo hayaeleweki.

Mheshimiwa Spika, na kama ni wajibu wetu sisi kama Bunge, kuisimamia Serikali, kuna haja ya kuona kwamba mikopo tunayokopa, tunalenga nini? Tunataka kua-achieve nini? Tunataka ku-achieve kwa muda gani ambao tunafikiri kwamba angalau lile lengo ambalo tumelenga litaonekana kwa muda fulani.

Mheshimiwa Spika, leo tunamaliza ndani ya mwaka mmoja hali ni mbaya; kuanzia kwenye sakafu, ukuta na unaanza kujiuliza ni kwanini? Ni kwa sababu ya pressure tuliyokuwa nayo ya kujenga madarasa au shida ni kwa sababu wataalamu wetu hawakutosha. Tulitumia walimu wenye taaluma nyingine kuwapeleka kwenye taaluma ambayo si ya kwao labda ndiyo maana hayo mambo yametokea.

Mheshimiwa Spika, hapo nataka nizungumze kidogo kwenye suala la hawa watu ambao wanaitwa maafisa manunuzi kwenye halmashauri zetu. Yaani kama unavyoona changamoto hizi zingine, ukienda kwenye halmashauri, yaani kila mradi ukienda lazima utakuta kuna madudu tu kwa hawa watu wanaitwa maafisa manunuzi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, kuna haja ya kufuatilia kwa kina, je, wale maafisa manunuzi waliopo kule ni kweli wana taaluma hiyo? Kwa sababu fedha hizi zote ambazo tunapeleka, mabilioni na mabilioni, wasimamizi ndio hawa wanaoenda kuhusika na manunuzi. Ni kweli wanayo elimu ya kuweza kusimamia hizo fedha? Kama sivyo kuna haja sasa ya kuendelea kupitia upya, kwenda kuwatazama, halmashauri kwa halmashauri ili kama shida ni maafisa manunuzi kwamba hawapo wenye sifa, Serikali ifanye kazi ya ziada ya kuwaajiri hao kwanza kwa kuwa wao ndiyo wanaokwenda kuhusika na manunuzi ya kila kitu.

Mheshimiwa Spika, kuna wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema hapa, kwamba ni vizuri yale mabaraza na kamati za fedha wanapokutana na Wabunge wahusike. Muda mwingi tupo hapa Bungeni. Ulipokuwa unazungumza asubuhi, kwamba na ninyi Wabunge muone huko mnakotokea, kiukweli hali ni mbaya, na ukifika huwezi kuwaambia mlikopita hapa hamkufanya vizuri watakushangaa. Kwa hiyo kwa sababu wewe unaingia automatically kwenye kamati hiyo inabidi uliache tu lipite, liende, eeh!

Mheshimiwa Spika, na kwa mazingira ya kawaida huwezi kusimama mle ukaanza kukosoa, wanasema wewe ni mjumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango, lakini hukuwepo wakati hilo jambo linafanyika.

Mheshimiwa Spika, naomba na hilo jambo mliangalie tena, kwa sababu tukipunguza hayo mambo wenyewe kule hapa tuatapunguza mambo mengine ambayo hayana sababu. Wabunge tutakwenda huko sisi wenyewe kwenda kusaidia haya badala ya kuja kuleta hoja nyingine ambazo hazina sababu ya kuwepo hapa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)