Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kujadili hoja muhimu ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa ambayo kimsingi ina mambo makuu matatu.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, mikopo inayotolewa inatosha? Watu wanalalamika kwamba mikopo haitoshi, kuna watu wanashindwa kupata mkopo. La pili, mikopo hii, hata kama haitoshi, inatolewa kwa haki? Kwamba watu ambao kwa vigezo vilivyowekwa walitakiwa wapewe mikopo, wanapewa hiyo mikopo? Wako watu ambao hawakidhi hivyo vigezo wanapewa na ambao wanakidhi wanakosa mikopo? La tatu; Serikali ina mpango na mkakati gani?

Mheshimiwa Spika, naomba nijaribu kujadili hoja hii kwa kutoa maelezo kadhaa. La kwanza, tuanze na ugawaji wa mikopo kwa haki. Na Mheshimiwa Eng. Ezra ameeleza na ametoa mfano wa mtu ambaye ukimuangalia kabisa na wazazi wake inaonekana kwa vigezo hivi angetakiwa kupata mkopo lakini hakupata.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mikopo imeweka vigezo na viko wazi, viko kwenye tovuti vya nani anaweza akapata mkopo kwa hali ya kiifamilia, aina ya masomo unayosoma na kuna clusters za masomo; la kwanza, la pili, la tatu. Viko wazi.

Mheshimiwa Spika, wakati tunajadili bajeti ya elimu hapa Bungeni, Waheshimiwa Wabunge kadhaa walitaka Serikali ipitie kuhakiki kwamba tunapogawa hii mikopo vile vigezo ambavyo tumewaambia waombaji wa mikopo kweli tunavizingatia. Na kulikuwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa wanasema tunafahamu watu wengine ni yatima na vigezo vinasema kama wewe ni yatima utapata mkopo labda asilimia mia moja usome. Je, linafanyika hilo?

Mheshimiwa Spika, kwenye hilo nimeunda kamati ya watu makini kwelikweli, wataalam wa mifumo wanaoweza wakaingia kwenye kompyuta, huwadanganyi chochote, kutoka Mzumbe University, University of Dar es Salaam na kutoka Zanzibar kukagua, moja tu, vigezo hivyo whether ni vizuri au vibaya, vipo; tunavifuata?

Mheshimiwa Spika, mimi nilichogundua baada ya kuunda hii kamati, resistance ambayo ilikuwepo ya kuzuia isifanye kazi imenishawishi kwamba huenda kuna madudu makubwa sana katika bodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mbinu mbalimbali zinatumika kuvujisha information, kutoa barua kwenye mitandao, kumtumia Kigogo, kuzunguka kuchafua, kuweka ukabila na vitu kama hivyo. Na hiyo kwa hakika inaonesha kwamba huu ukaguzi ni muhimu, unafanyika, utakamilika, na utafanyika kwa muda mfupi sana kwa sababu wanaingia kwenye mfumo, watacheki tutajua nini kinaendelea. Hicho Waheshimiwa Wabunge, tutawaletea taarifa. La pili; mkopo unatosha? Kwa sababu hata kama vigezo hivyo kweli vikifuatwa, unatosha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tuangalie historia ya mikopo; tulianza, na nadhani Mheshimiwa Mnzava ametoa takwimu vizuri sana. Tulianza wakati fulani mwaka wa kwanza tunadahili wanafunzi 34,000. Kwa kila tunapoongeza bajeti ya mikopo tunaongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Na nitaeleza baadaye changamoto ya sasa hivi imetokana na nini na hatua gani tunazichukua.

Mheshimiwa Spika, kitu kikubwa ambacho kimefanywa na Serikali, na kwa kweli hii ni credit kwa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa sababu alivyoingia madarakani mnakumbuka, kwa sababu bajeti inapitishwa humuhumu Bungeni, alikuta mikopo ya elimu ya juu ikiwa ni bilioni 464 na akafanya maamuzi matatu. kwanza iongezwe kutoka 464 kwenda 570, na ni nyongeza kubwa sana kwa mkupuo. Pili, akaondoa zile tozo, kuna moja ilikuwa asilimia 10 na nyingine asilimia sita, kuna retention na nyingine kama hujawahi kurudisha unakuwa punished. Kwa hiyo hivyo vyote vilikuwa vinasababisha mzigo kwa wanafunzi kurudisha mkopo kuwa mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maamuzi hayo tumerahisisha mzigo kwa waliochukua mikopo ili waweze kurudisha, lakini vilevile udahili uliongezeka, nafikiri wanafunzi 70 kwa mwaka wa kwanza, kwa mara ya kwanza katika historia tangu tuanze Bodi ya Mikopo. Huo ni umamuzi uliofanyika baada ya Mheshimiwa Rais kuingia madarakani, ile bajeti ya kwanza ilisomwa hapa na mtangulizi wangu, Mheshimiwa Prof. Ndalichako, ndivyo tulivyokwenda huko.

Mheshimiwa Spika, sasa kabla sijaeleza chimbuko la changamoto hii tuliyonayo sasa hivi nieleze na hatua nyingine ambazo zinachukuliwa. Ukiacha mkopo kwamba bajeti sasa hivi imeongezwa kutoka bilioni 464 iliyopitishwa na Bunge kwenda bilioni 570, ilipitishwa na Bunge bajeti iliyopita na mwaka huu ilipitishwa kwenye Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, hatua za ziada ambazo zimechukuliwa, kabla sijaenda kwenye changamoto, ni pamoja na kwa mara ya kwanza Serikali kuanza kutoa scholarship, yaani kusomesha wanafunzi bila mkopo, unasomeshwa moja kwa moja. Na hii ilipitishwa na Bunge lako Tukufu, na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulivyoleta proposal hiyo kuanzisha kuhimiza watoto wanaotaka kusoma science na wanaofaulu vizuri sana, wao wapewe scholarship, wasomeshwe kama tulivyosoma sisi wengine moja kwa moja mpaka wamalize. Na wadau wengi wakasema hii iitwe Samia Scholarship.

Mheshimiwa Spika, tulipewa mapendekezo mengi sana, sisi tumeamua tu sasa inaitwa Samia Scholarship. Kuna wanafunzi 640, kwa kufaulu, na ufaulu huo ni wa wazi, hakuna upendeleo. Unaonekana kuanzia wa kwanza mpaka wa 640. Kama umefaulu vizuri kwenye science kama tulivyosema hapa Bungeni na ukaamua kwenda kusoma science, ama engineering au tiba, utasomeshwa na Serikali moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Serikali ime-engage private sector kuhakikisha kwamba tunaongeza fursa za mikopo. Kwa mfano NMB, na tulisema wakati tunasema bajeti hapa, tukawapongeza. Tumeongea nao, wametenga bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya elimu.

Mheshimiwa Spika, sasa hiyo inakuwa na masharti yake tofauti kidogo na Bodi ya Mikopo. Kwa sababu anayeweza kupata huo mkopo ni mtu ambaye ana miamala inayopita kwenye NMB. Kwa hiyo hilo tumelifanya, bilioni 200 ina interest rate ya asilimia tisa, lakini ni mzazi ambaye anapokea mshahara kwenye NMB kumsomesha mwanao au wewe mwenyewe unataka kwenda kusoma unaweza ukaitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tuna-engage private sector kwa ajili ya kutoa mikopo. Vodacom kwa mfano, sasa hivi wanatoa scholarships, siyo mikopo, wanatoa scholarships moja kwa moja na tunaendelea ku-engage wadau mbalimbali. Na sisi tunapambana kuhakikisha kwamba tunarudisha fedha nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo sasa hivi; baada ya mchakato wa bajeti, maana yake bajeti hiyo ni moja ya Serikali. Humu ndani vuta nikuvute, budget ceiling ikoje, inaongezwa au haiongezwi, mkimaliza tunakuja humu. Bajeti ya mikopo ilikuwa ni bilioni 550, ilikuwa ni ileile ambayo iliongezwa with a big jump kutoka 464 kwenda 570. Sasa kwa ku-maintain constant budget ile maana yake ni kwamba wale wanafunzi ambao udahili uliongezeka wakaingia mwaka wa kwanza, wanakwenda mwaka wa pili wanastahili kupata mikopo. Bila kuongeza hizo bilioni 570 zikaongezeka zaidi, udahili wa mwaka wa kwanza hauwezi kuwa sawa na wale ambao tulikuwa na wanafunzi 70 kwa hiyo momentum ile itakuwa maintained tu endapo bajeti ingekuwa zaidi ya bilioni 570.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tayari tuna-engage na Hazina na tumezungumza sana na Waziri wa Fedha kuangalia kwamba udahili huu ambao kwa mwaka wa kwanza ume-drop lakini mwaka wa pili umeongezeka sana kwa sababu wale wa mwaka wa kwanza wameendelea na mwaka wa pili, idadi ya wanafunzi wanaopata mkopo mwaka wa pili sasa hivi ni kubwa kuliko ambavyo imewahi kutokea. Sasa kwa sababu wamechukua zile fedha wanaoingia mwaka wa kwanza idadi imepungua. Tuna-engage na Wizara ya Fedha, tuna mazungumzo naona yanakwenda vizuri kuangalia namna ya ku-rescue hii situation, kwamba at least ile status quo ya vigezo vilivyotumika wakati ule tuhakikishe kwamba tunaweza tuka-retain wale wanafunzi wakaendelea kupata mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli mapendekezo hapa ni ya muda mfupi kama hili nililosema. Lakini kuna mapendekezo ya muda mrefu. Moja wapo ni kupitia upya Bodi ya Mikopo, lingine ni ku-engage zaidi private sector na la mwisho ni kuona tunaangaliaje mambo ya kibajeti; haya yote ni ya kwetu. Kwa sababu hata bajeti hii ya 570 tulileta hapa Bungeni Waheshimiwa Wabunge mkaturidhia, tukashukuru, tukasonga mbele. Crisis tumeiona wote, tunazungumza tunaamini baadaye tutajua cha kufanya kwenye short term na long term lazima tutakuja na mkakati kama ambavyo imependekezwa hapa kuhakikisha kwamba tunajaribu kuipunguza hii changamoto kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa muda wako. (Makofi)

SPIKA: Sasa Mheshimiwa Waziri nakushukuru. Nilisita kukukatisha, nilitaka umalizie mtiririko wako. Nisaidie jambo moja tu; katika hizi Samia Scholarship ambazo umesema ni watoto ambao wanakuwa na ufaulu mzuri kwenye masomo ya sayansi, kwa hiyo wanaokwenda kusoma udaktari ama tiba ni miongoni mwao. Huyu aliyesomwa hapa amekosaje hiyo Samia Scholarship? Hebu tusaidie au ile 1.7 haijafikia vile vigezo vya kupata hiyo Samia Scholarship?

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwanza udaktari uko kwenye cluster ya kwanza ya watu wanapewa upendeleo kwenye mikopo. Lakini ili uweze kupata scholarship tunaangalia waliofaulu vizuri kuanzia wa kwanza, wa pili, wa tatu, wa nne, wa tano, bajeti yetu imeisha tulivyofikia 640. Wako wenye first class lakini wako chini ya 640. Na ninapenda kusema waliopewa scholarship ni nje kabisa ya hawa wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, lakini nitapenda kupata hizo details kwa sababu ndiyo maana tumeamua kui-audit Bodi ya Mikopo. Na inashangaza kupata resistance kwenye taasisi ya Serikali kama hii, kwamba usiguse mkopo, unahangaika, umeajiri watu wako, ndugu zako, na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hao wanaosoma udaktari kama alivyosema Mheshimiwa Eng. Ezra pale, kwa alivyofaulu nitapenda kwenda kuangalia. Ni sehemu ya ukaguzi ambao tutauhakiki kuhakikisha kwamba kweli watu wanapata mkopo kwa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.