Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Afya. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. Napenda vilevile kuwapongeza Mawaziri wetu kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na nataka tu kuwapa moyo wazidi kufanya kazi, Wizara hii changamoto ni nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuwapongeza watumishi wetu wa afya. Kwa kweli wanafanya kazi ngumu kwenye mazingira magumu, hospitali zetu nyingi hazina vifaa tiba, hazina dawa, hazina vitendea kazi na bado wanapata lawama nyingi kutoka kwa wananchi kitu ambacho kwa kweli si sawa. Nadhani kama Wabunge na wananchi tungejitahidi kuwapa moyo waendelee kufanya kazi kwa bidii katika mazingira hayo na tuwape moyo kwamba Serikali ya sasa hivi ya Awamu ya Tano ipo makini na changamoto zote zitatatuliwa, ni suala la muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wamechangia suala la vifo vya akinamama na takwimu zimeonyesha wanawake 42 wanakufa kila siku. Hili ni suala la kushtua na inabidi lifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la hospitali na vituo vyetu vya afya. Unakwenda kwenye vituo vya afya unakuta hakuna maji na umeme. Inafika mahali kuna watu wanaogopa kwenda hospitali kwa sababu anajua akienda hospitali atatoka na magonjwa mengine ambayo yanaambukizwa kutokana na mazingira mabovu ya hospitali zetu. Suala la maji na umeme kwenye hospitali zetu ni mambo muhimu kabisa ambayo inabidi yaanze kufanyiwa kazi kwenye hivi vituo ambavyo viko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu population growth, ongezeko la watu hasa nchini kwetu. Tatizo hili ni kubwa, ni changamoto kwetu na nashangaa ni kwa nini watu wengi hawaliongelei suala hili. Tutakaa hapa tutaongelea suala la umaskini lakini ni vigumu sana kwa rate ya ukuaji wetu wa asilimia 2.7 tukatoka kwenye hali hii tuliyopo, ukuaji wetu ni mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano mdogo tu wa mwaka 1961 wakati tunapata uhuru nchi yetu ilikuwa ina watu milioni tisa, nchi kama Norway walikuwa na watu milioni 3.6, leo hii sisi tuna watu karibia milioni 50, nchi ya Norway ina watu milioni 5.6. Kwa hiyo, tukiendelea kuongelea suala la shule za kata itaendelea kuwa changamoto kama rate ya kuongezeka inazidi kukua kwa kiasi hiki, changamoto hizi ni vigumu sana kwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ya Afya tujitahidi kuelekeza nguvu kwenye uzazi wa mpango (family planning). Hili siyo kwa Wizara tu, nadhani ni changamoto yetu sote na bila kujali vyama wala itikadi zetu, tunapokwenda majimboni, tunapofanya mikutano yetu tuongelee suala la uzazi wa mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uzazi wa mpango ni changamoto na inabidi tulizungumzie watu wajue. Kuna maeneo unakwenda, mfano Mwanza huko kwetu, unaongea na akinamama hawajui haya mambo, hawajui kama kuna contraceptive pills, hawajui kama kuna njia za kuweza kutumia ili usipate watoto wengi, anakwambia mimi nitazaa mpaka watakapokwisha, sasa wataishia wangapi? Kwa hiyo, nadhani hili suala tungelipa kipaumbele kama tunavyofanya upande wa diabetes, ugonjwa wa moyo, cancer, family planning pia iwe priority. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine baadhi ya wachangiaji wameliongelea nami naomba nitoe msisitizo kidogo kwenye hilo, ni suala la afya ya akili (mental illness). Hili suala ni changamoto na kwa nchi yetu nadhani ni kitu ambacho kimekuwa kama ni aibu, hakitakiwi kuongelewa na mtu akionekana ni mgonjwa inakuwa kama ni laana au umerogwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tunatakiwa kuwa na uelewa na kampeni ifanyike kuhusu hili suala la ugonjwa wa akili. Nchi zilizoendelea tafiti zimefanyika, nchi kama Marekani wanasema kila watu watano kuna mtu mmoja ambaye ni mgonjwa wa akili. Nchi kama Uingereza wamefanya research wanasema kila walipo watu wanne mmoja ana ugonjwa wa akili. Nchi kama Australia vilevile wamefanya utafiti wanasema kila walipo watu watano mtu mmoja ana ugonjwa wa akili. Hili suala siyo la kulifumbia macho na inabidi tusiwe na aibu tuliongelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na research ya WHO ya mwaka 2014 inasema, 25% of the population worldwide will suffer mental illness. Around four hundred and fifty million people currently suffer from such condition, placing mental disorder among the leading causes of ill-health and disability worldwide. Nina imani kabisa hata hapa kwetu ikifanyika assessment, ukifanyika utafiti wagonjwa ni wengi na siyo suala la kulifumbia macho. Tusione aibu majimboni kwetu na kwenye familia zetu kuliongelea suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala lipo na mmoja wetu hapa anaweza akaugua, ni vitu vya kawaida kabisa na wanasema, there is no physical health without mental health likewise there is no mental illness without physical health. Kwa hiyo, hivi vitu vinakwenda pamoja. Naomba tusichukulie hiki kitu kama ni mzaha kwa sababu ni kitu ambacho ni serious kabisa na tukiongelee na ikiwezekana kama kuna uwezekano tutafute Madaktari waje watupime hata humu ndani ni kitu muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka kuongelea kuhusu suala la damu. Suala la damu ni janga la Kitaifa. Kule kwetu Mwanza kuna watu wanakufa, wajawazito wanakufa, watu wanapata ajali wanatakiwa kuongezewa damu lakini damu safi na salama haipo. Hili suala ni jukumu letu sote siyo la Serikali peke yake, tuhamasishe watu, sisi pia wenyewe kama kuna uwezekano twende tujitolee damu. Leo linaweza likampata mtu mwingine lakini kesho na kesho kutwa inaweza ikawa miongoni mwetu au miongoni mwa familia zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili suala ni la kuhamasishana, damu ni ya muhimu sana na upungufu wa damu upo na siyo tu Dodoma. Kwanza napenda kumpongeza Makamu wa Rais, mwanamke mwenzetu juzi amejitokeza akatoa damu na akahamasisha, hili jambo inabidi tulifanye sisi sote kwa sababu linahusu watu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.